Kuwa na nafasi ya juu…Uzuri wa kuitikiwa; Kubadili kibla ni mfano wa hilo.
Question
Tunaweza kuangalia nafasi ya Mtume S.A.W. kwa Mola wake katika Aya za Qur’ani Tukufu na matukio ya Kisharia, miongoni mwa matukio hayo tukio la kubadilishwa kibla ambalo lilikuwa kutokea kwake ni kuitikia matamanio ya Mtume S.A.W., katika hili Mwenyezi Mungu Ameshusha Aya isemayo
Answer
Tunaweza kuangalia nafasi ya Mtume S.A.W. kwa Mola wake katika Aya za Qur’ani Tukufu na matukio ya Kisharia, miongoni mwa matukio hayo tukio la kubadilishwa kibla ambalo lilikuwa kutokea kwake ni kuitikia matamanio ya Mtume S.A.W., katika hili Mwenyezi Mungu Ameshusha Aya isemayo: (Kwa yakini tukiona unavyo geuza geuza uso wako mbinguni. Basi tutakuelekeza kwenye Kibla ukipendacho. Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu; na popote mnapokuwa zielekezeni nyuso zenu upande huo; na hakika wale walio pewa Kitabu wanajua kwamba hiyo ni haki itokayo kwa Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale wanayo yatenda) [Baqarah:144].
Waislamu kipindi chote walichokua Makkah walikuwa wanaelekea Msikiti wa Aqsaa; kwa kufuata amri ya Mwenyezi Mungu ambaye Amewaamrisha waelekee huko na kuufanya kuwa kibla cha Swala, Pamoja na Mtume S.A.W. kufuata kwake amri ya Mola wake lakini moyo wake ulikuwa unamuomba aelekee Al-Kaaba Tukufu; ambacho ndio kibla cha baba yake Ibrahim Amani imshukie, na Mtume S.A.W. ni mbora zaidi wa watu kwa hilo, pia ndiyo nyumba ya kwanza ya ibada kujengwa kwa watu, pamoja na haya Mtume S.A.W. alikuwa mwenye kuujali sana umma wake kama ilivyoeleza Qur’ani Tukufu: (Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma) [Al-Tawbah:128} na katika kuujali kwake umma wake ni kwamba aliutakia Ibada zake na mambo yake yote yawe tofauti na Umma nyingine katika umma za daawa nyingine ambazo ziliongezewa mambo na kubadilishwa na kuyanasibisha mambao waliyobadilisha kwa Mwenyezi Mungu kwa uzushi.
Uthibisho wa hilo ni Hadithi iliyopokelewa na bwana Al-Baraa bin Azb R.A amesema: Mtume S.A.W. alikuwa akiswali akielekea upande wa Msikiti wa Bayt Al-Maqdis miezi kumi na sita au kumi na saba, na Mtume S.A.W. alikuwa anapenda kulekea Al-Kaaba” ([1]). Na Mtume hawezi kupinga amri ya Mola wake, naye anajulikana kwa kufuata amri kikamilifu na kujisalimisha moja kwa moja katika amri ya Mola wake, isipokuwa yeye ameweza kukusanya kati ya mapenzi katika kuelekea Al-kaaba na kutopinga amri ya Mola wake kwa kuelekea Msikiti wa Aqsaa akisali mbele ya Alkaaba lakini akielekea kaskazini, kama inavyothibitisha hili Hadithi ambayo umepokelewa na Ibn Abbas R.A aliposema: “Mtume S.A.W. alikuwa anaswali akiwa Makkah akielekea msikiti wa Aqsaa na Alkaaba ipo mbele yake” ([2]).
Kisha Mtume S.A.W. akahama akiwa bado na matumaini yake, lakini kwa kufuata amri akawa anaelekea Msiki wa Maqdis, akaendele hivyo kwa miezi kumi na sita au kumi na saba, kama ilivyo kuja katika sahihi mbili katika Hadithi ya Baraa bin Aazib amesema: “Tumeswali na Mtume S.A.W. tukielekea Msikti wa Maqdis miezi kumi na sita au kumi na saba, kisha tukabadilishiwa kibla” ([3]).
Kisha ikiwa shani yake Mwenyezi Mungu kugeuza kibla ni kutimiza matamainio yake, na kujibu maombi yake, wakati huohuo ni kuonesha kadari yake na kutangaza fadhila zake na utukufu wa jambo lake; Mwenyezi Mungu Ametimiza Aliyoyataka, Mwanachuoni mkubwa Ibn Hajar anasema: “Katika hili kuna kubainisha utukufu wa Mtume S.A.W. na karama zake kwa Mola wake; kwa kumpa alichokitaka pasi na kuomba waziwazi” ([4]).
Ibn Qayyim anasema: “Huyu Mtume S.A.W. ambaye Mwenyezi Mungu Amekikunjua kifua chake, na akamuondeshea madhambi yake, akanyanyua jina lake, amejaalia madhila na kudogeshwa kwa anayepinga amri yake, na akamuapia kwa uhai wake katika kitabu chake kitukufu, na akaambatanisha jina lake na jina la Mtume wake; akitajwa Mwenyezi Mungu basi anatajwa na Mtume kama ilivyo kwenye Tahiyatu na adhana, na akafaradhisha kwa waja kumtii na kumpenda na kutekeleza haki zake, na akazifunga njia zote za kumuendea yeye na katika pepo yake, hazifunguliwi kwa yeyote isipokuwa kwa kupitia kwake; yeye ndio mzani sahihi ambao kwa tabia zake na kauli zake na amali zake hupimwa tabia, kauli na amali, na kipambanuzi cha wazi ambacho kwa kukifuata kinapambanua watu wa uongofu na watu waliopotea”([5]).
Katika hili kuna dalili ukubwa ya kutukuzwa na kukirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa Mtume S.A.W., Mwenye Mungu Anasema: (Kwa yakini tukiona unavyo geuza geuza uso wako mbinguni. Basi tutakuelekeza kwenye Kibla ukipendacho. Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu; na popote mnapokuwa zielekezeni nyuso zenu upande huo; na hakika wale walio pewa Kitabu wanajua kwamba hiyo ni haki itokayo kwa Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale wanayo yatenda) [Al Baqara:144].
Mwanachuoni mkubwa Tahir bin Ashour: “Ameeleza kwamba neno {ukipendacho} dalili ya kwamba kupenda kwake Al-Kaaba ni kupenda kwa kukusudia kheri kwa kuwa Al-Kaaba ni nyumba stahiki zaidi ya Mwenyezi Mungu ya kuwa kielelezo cha Tawheed, ni nyumba stahiki zaidi ya kuelekea kuliko Msikiti wa Al-Aqsa, na kwa sababu katika kuelekea kwake ni kiashirio cha utulivu wa Dini hii kutofautisha na Dini ya watu wa Kitabu. Kwa kuwa ridhaa ni alama ya mapenzi inayotokana na kutambua, ikachaguliwa katika sehemu hii na si neno (mapenzi) au (matamanio) au mfano wa hayo, hakika nafasi ya Mtume S.A.W. inakuwa kubwa kuliko kufungamana kupenda kwake kwa lisilo na masalihi sahihi baada ya kumalizika masilahi ya mpito ya kufaradhishwa kuelekea Msikiti wa Maqdis, na taarifa na maelezo haya anaelezwa Mtume S.A.W. na amri inaelekezwa kwake kwa kuzingatiwa yaliyomo humo miongoni mwa raghaba yake, na litafuata suala la kushirikiana na umma katika jambo hili kwa kauli yake: { na popote mnapokuwa zielekezeni nyuso zenu upande huo}([6]).
Anayezingatia mwenendo wa Mtume S.A.W. anagundua kuwa yale aliyompendelea Mwenyezi Mungu katika aina za ukamilifu, na aliyompa miongoni mwa matarajio, na aliyomuunga mkono katika Aya mbalimbali; ili kubainisha nafasi yake kubwa na heshima yake tukufu na Daraja yake ya juu, hili linathibitishwa na mwandishi wa Oun Al-Maaboud kwa kauli yake: “Waislamu waliposhinda na Mtume S.A.W. kutamani na akamuomba Mola wake kubadisha Kibla kutoka Msikiti wa Maqdis kuwa Al-Kaaba, Mwenyezi Mungu Akakubali dua ya Mtume S.A.W. akateremsha Aya hii “Basi tutakuelekeza kwenye Kibla ukipendacho” kwa maana tutakugeuzia upande wa kibla unachokiridhia {Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu} na makusudio ni Al-Kaaba([7]). na Mtume S.A.W. hakutamani kitu chochote isipokuwa Mwenyezi Mungu Alimtimizia.
Na kuna maelezo mafupi yanayobainisha utukufu wa heshima na utukufu wa Daraja yake kwa Mwenyezi Mungu, Imamu Al-Baydhawi anaeleza kwa ufupi sababu za kubadilishwa Kibla:
- Kumtukuza Mtume S.A.W. kwa kumtimizia mapenzi yake.
- Na Mwenyezi Mungu Amekuwa na desturi ya kila umma na Mtume kuwa na upande anaoelekea na unaoumtambulisha.
- Kuondosha hoja za wapinzani.
Pia upande wa Utukufu wa Mtume S.A.W. unathibitishwa kwa Mola wake na ukubwa wa Daraja lake kupitia kutoa baadhi ya hekima za tukio hili la kipekee na makusudio yake, ikiwemo:
Kwamba huu ni mtihani ili kutambua walio pamoja naye, na kuwajaribu Waumini katika kumtii Mwenyezi Mungu moja kwa moja na Mtume wake, na hili limeelezewa na kauli yake Mwenyezi Mungu: {Na kwa yakini hilo lilikuwa jambo gumu isipo kuwa kwa wale alio waongoa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuipoteza Imani yenu. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa watu na Mwenye kuwarehemu} [Al-Baqarah: 143] tofauti kati ya anaemuabudu Mwenyezi Mungu na mwenye kuabudia matwaka yake ni ule uharaka wa kuitikia na kufuata amri za Sharia hata kama zitapinga na matamanio ya nafsi, na zikagongana na rai za watu. Ibn Qayyim anasema: “Mwenyezi Mungu kukifanya kibla kuwa Msikiti wa Maqdis kisha kukigeuza kuwa Makkah kuna hekima kubwa, na mtihani kwa Waislamu, Washirikina na Mayahudi na Wanafiki.
Ama Waislamu wamesema tumesikia na tumetii amri, na wakasema:{Na wale wenye msingi madhubuti katika ilimu husema: Sisi tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki hayo isipo kuwa wenye akili} [Ali Imraan:7] na hawa ndio aliowaongoza Mwenyezi Mungu na jambo hili halikuwa kubwa kwao.
Ama Washirikina wakasema: Kama alivyorejea katika kibla chetu, anakaribia kurejea katika dini yetu, na hakurejea kuelekea Alkaaba isipokuwa kwamba yeye ana haki.
Ama Mayahudi wakasema: Amepingana na kibla cha Mitume walio kabla yake, lau kama angekuwa Mtume angekuwa anaswali kuelekea kibla cha Mitume.
Ama wanafiki wakasema: Muhammad hajui aelekee wapi? Ikiwa kibla cha kwanza ndio cha kweli, amekiacha! Na ikiwa kibla cha pili ndio kweli basi kiukweli alikuwa katika batili, na kauli zikawa nyingi kwa watu wapumbavu, na ikawa kama Alivyosema Mwenyezi Mungu: {Isipokuwa kwa wale alio waongoa Mwenyezi Mungu} Al-Baqarah:143], na ulikuwa ni Mtihani wa Mwenyezi Mungu anawajaribu waja wake, ili aone nani anamfuata Mtume na ani anageukageuka” ([8]).
Aya hii imekuja kubainisha hekima za amri ya kuelekea Msikiti wa Maqdis mwanzoni mwa ulinganizi kabla ya kuja Aya iliyofutia Aya hiyo, na hekima ni ile aliyoielekeza Mwenyezi Mungu kwa kauli yake: {ili tupate kumjua yule anaye mfuata Mtume na yule anaye geuka akarejea nyuma} na maana yake hatukuweka sheria tuliyoweka kuelekea Msikiti wa Maqdis isipokuwa tujue kiuhalisia nani anamfuata Mtume, na kutekeleza amri zake kwa hali yeyote, na kupambanua ni nani ambaye Imani bado haikuingia ndani ya moyo wake, bali ameingia kwenye Dini akiwa mguu mmoja ndani mwingine nje, kwa namna anakuwa na shaka kwa jambo dogo tu, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu, lakini ametaka elimu ya yaliyojificha ishuhudiwe wazi; kwani kujua kitu kunafungamana na uhalisia wa wazi ambao inasimia hoja juu yake, na juu ya hili hupelekea thawabu na adhabu.
Mtihani huu ni aina katika aina za mafunzo ya kivitendo kwa Masahaba R.A ili kuwaimarisha na wajibu wa kumufuata Mtume S.A.W., na kutekeleza amri zake na kuitika kauli zake; hasa wanapoingia hatua mpya inayowapasa kutoa nafsi zao na mali zao za thamani, na kuvumilia tabu na kuridhia magumu, ikiwa hakuna budi kupewa mtihani kama huu; ili Mwenyezi Mungu Apambanue wazuri na wabaya, tukio la kubadilishwa Kibla likawa jaribio kwao na mtihani na uchaguzi wa kweli ili Mtume ajue nani anamfuata na nani hamfuati, kwa sababu hali ya Muumini inakuwa ni kusikiliza na kumtii Mola wake; Mwenyezi Mungu Anasema: {La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayo khitalifiana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utayo toa, na wanyenykee kabisa.} [Annisaa:65]. na Mwenyezi Mungu Anasema: {Haiwi kauli ya Waumini wanapo itwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, ila ni kusema: Tumesikia, na tumet'ii! Na hao ndio wenye kufanikiwa} [Anour:51] na Mwenyezi Mungu Anasema: {Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapo kata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi} [Al-Ahzab:36]
Na Masahaba wa Mtume wametoa funzo nadra na mfano wa kipekee katika kuitikia haraka na kufuata amri, walipoamrishwa kuelekea Msikiti wa Makkah, walifanya haraka kufuata amri; bali baadhi yao walipojuwa kugeuzwa kibla wakiwa katika Sala wakageuka na kuelekea kibla kipya katika Swala hiyohiyo; imepokewa Hadithi kutoka kwa Abdillah bin Omar ameseme: Wakati watu walipokuwa wanaswali Swala ya Alfajiri, akawajia mtu mmoja, akasema: “Hakika imeshuka Aya kwa Mtume usiku huu, na ameamrishwa kuelekea Al-Kaaba, wakaelekea Al-Kaaba, na walikuwa wameelekea Sham, wakageuka na kuelekea Al-Kaaba([9]).
Yote haya yanaelezea hekima za mtihani ambao Mwenyezi Mungu Amewajaribu Waislamu walipokuwa wanaelekea Msikiti wa Aqsa katika Swala zao, kisha akawaamrisha kuelekea Msikiti wa Makkah; wakaitikia wito huo, haya ndiyo mazoea ya Waumini wa kweli mbele ya amri za Mwenyezi Mungu, hawezi kutanguliza au kuchelewesha au kusitasita na kuwa na shaka wakifanyia kazi kauli ya Mwenyezi Mungu: (Na anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.) [Al-Hashr:7].
Imamu Al-Zajaj anasema: “Hakika Mwenyezi Mungu Anajua anayemfuata Mtume na asiyemfuata kabla ya kutokea, na elimu hii haipasi kwake kulipa thawabu au adhabu, lakini maana ni: Ili ajue hilo kutoka kwao na kuwa Ushahidi na kuwapata kwa elimu hiyo jina la watiifu na waasi, na kupasa thawabu zake na kadri ya matendo yao.
Na inakuwa inajulikana wakati wa kutuka kitendo kutoka kwao elimu ya Ushahidi kama alivyosema: (Yeye ndiye Mwenye kujua yanayo onekana na yasio onekana) kulijua kwake kabla ya kutokea ni elimu ya yaliyojificha, na kujua kwake baada ya kutokea ni elimu ya kuonekana, na kila alichokijua Mwenyezi Mungu kwa kuonekana basi kilikuwa kinajulikana kwake katika elimu ya yaliyojificha, kwa sababu anakijua kabla ya kutokea kwake, na haya yanaelezewa na yote yaliyopo ndani ya Qurani Tukufu, mfano neno lake Mwenyezi Mungu: (Na bila ya shaka tutakujaribuni mpaka tuwadhihirishe wapignao Jihadi katika nyinyi na wanao subiri. Nasi tutazifanyia mtihani khabari zenu) [Muhammad:31] ([10]).
Jinsi gani makusudio haya yamebainisha nafasi tukufu sehemu nzuri, hasa ni kwamba Mtume S.A.W. alihama kutoka Makkah Kwenda Madina; kwa ajili ya kulingania na kufikisha ujumbe wake ambao ulikuwa miongoni mwa sababu za kukwamishwa kwake ni washirikina na wanafiki na walikuwa wakifuata, Mwenyezi Mungu Akaamrisha kwenda kwenye mazingira mapya na sehemu mpya, pia tukio hili likawa ni kwa ajili ya kupambanua wabaya na wazuri, na kumuonesha Mtume S.A.W. nani yupo pamoja naye na nani hayupo naye, na nukta hii inaelezea utukufu wake na nafasi yake kubwa.
Kisha upande wa utukufu huu unadhihirika kupitia makusudio mengine ya tukio hili la kipekee nao: kuthibitisha Utume wake na kukataa kauli za wanaomkwamisha na kujibu kauli za wanaompinga; na hili linaonekena kupitia kauli ya Mwenyezi Mungu: (Wapumbavu miongoni mwa watu watasema: Nini kilicho wageuza kutoka kibla chao walicho kuwa wakikielekea? Sema: Mashariki na Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu; Yeye humwongoa amtakaye kwenye njia iliyo nyooka.) [Al-Baqarah: 142].
Upande wa Utukufu wa Mtume S.A.W. hauishii katika Miujiza aliyompa Mola wake na alama mbalimbali; bali unavuka hapo na kufikia yanayohusiana na Umma wake, na hii kwa sababu upande wa utukufu wake umeenea na kujumuisha Umma wake, kama ilivyosemwa: Hakika alama za utukufu wa mtu zinabainika katika athari zake kwa wengine, na hili limebainishwa na tukio la kubadilishwa kibla, tukio hili limedhihirisha Mwenyezi Mungu kuutukuza Umma wake, na hii kwa neema maalumu alizowaneemsha, zinazoonesha fadhila zake na ukubwa nafsi yake kwa Mwenyezi Mungu na hili linadhihirika katika mambo kadhaa kama:
Kwanza: Kuhama ujumbe na Umma wa Muhammad kurithi vitakatifu vya jumbe zilizotangulia: Kubadili Kibla kumekuja ili kutangaza kuhama Utume kutoka kwa Watoto wa Ishaq Kwenda kwa Watoto wa Ismail Amani ishuke juu yao. Na kuhama uongozi kutoka katika kizazi cha wana waizrael Kwenda kwa Waarabu; na hili ni kwamba utashi wa Mwenyezi Mungu umehukumu kuja mitume yote kutoka katika kizazi cha Ishaq, ama Ismail katika kizazi chake hakupatikana isipokuwa Mtume mmoja, naye ni Bwana wetu Muhammad, na ndio Mtume wa Mwisho; Mwenyezi Mungu Anasema: (Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu) [Al-Ahzab:40], ambapo “Msikiti wa Aqsaa ulikuwa chimbuko la jumbe za kizazi cha wana wa Izrael, Mayahudi walipopoteza utukufu wa ufunuo na kuacha hukumu za Mwenyezi Mungu ikawapata laana ya Mwenyezi Mungu, na kuamuliwa kugeuza Utume kutoka kwao moja kwa moja! Kisha ikiwa kuja ujumbe kwa Mtume S.A.W.; ni kuhama uongozi wa kiroho wa kiroho duniani kutoka kwa Umma Kwenda kwa Umma”[11].
Pili: Kuelekea kibla viwili: Hekima ya Mwenyezi Mungu imehukumu kuwa Al-Kaaba kibla cha Waislamu baada ya kupata heshima ya kuelekea Msikiti wa Maqdis; ili wawe watu wa kibla mbili; na ili awajipambanue na washirikina kabla ya kuhama na Mayahudi baada ya kuhama ([12]). Na hili limeelezewa katika kauli ya Mwenyezi Mungu: (WAPUMBAVU miongoni mwa watu watasema: Nini kilicho wageuza kutoka kibla chao walicho kuwa wakikielekea? Sema: Mashariki na Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu; Yeye humwongoa amtakaye kwenye njia iliyo nyooka.) [Al-Baqarah: 142].
Tatu: Watu wote kuelekea kibla chao: Hili limebainishwa na moja ya Mashekhe wa zama hizi – Mwenyezi Mungu Amrehemu, ni Mwanachuoni mkubwa Shekhe Ghazaly aliposema: “Nilikuwa nasoma Sura hii nikasimama sana katika kauli yake (Kama tulivyo mtuma Mtume kwenu anaye tokana na nyinyi,) ni kasema katika nafsi yangu: nini maana ya {Kama} hapa? Kipi kinaunganisha na kilicho kabla yake? Nikaanza kufikiria upya Aya hii kisha maana ikabainika yote, na maana yake ni kwamba Mwenyezi Mungu Anawaambia Waarabu: Hakika mimi nimewaelekeza watu katika kibla chenu, hii ni neema yangu kwenu enyi Waarabu, lakini si neema ya kwanza kwenu, neema hii imetanguliwa na neema nyingine, nayo ni Kumtuma Mtume Muhammad S.A.W. kwenu, na hii ndiyo maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu: (Kama tulivyo mtuma Mtume kwenu anaye tokana na nyinyi, anakusomeeni Aya zetu na kukutakaseni na kukufundisheni Kitabu na hikima na kukufundisheni mliyo kuwa hamyajui. Basi nikumbukeni nitakukumbukeni, na nishukuruni wala msinikufuru}{Al-Baqarah:150-151]
Hakika karama zote hizi ambazo Mwenyezi Mungu Ameukirimu umma wa Muhammad, na tukio la kubadili kibla likawadhirishia kitu kingine kinachoongezewa katika utukufu wa Mtume S.A.W. ambao unathibitisha kuwa mkubwa usioweza kudhibitika na utukufu usioweza kutathminiwa.
([1]) Sahih Al-Bukhari: Mlango wa Sala, 1/88.
([2]) Hadithi hii imepokelewa ba Shaykhaa, Sahih Al-Bukhari.
([3]) Hadithi hii imepokelewa ba Shaykhaa, Sahih Al-Bukhari.
([4]) Fathul Bary Ibn Hajara 1/198.
([5]) Ilaam Al-Muwaqeen, Ibn Qayym.
([6]) Al-Tahreeer wa At-Tanweer, Taher bin Ashour.
([7]) Aun Al-Maaboud 2/138.
([8]) Zad Al-Maad fee Hudaa Khayr Al-Ibaad cha Ibn Qayyim 3/60
([9]) Sahih Al-Bukhary, Mlango wa Sala, 1/89.
([10]) Maany Qur’qqn wa Iraabihi 1/223.
([11]) Fiqh Al-Syra, Muhammad Al-Ghazaly. Uk, 140.
([12]) Al-Qawl Al-Mubin fee sirat Sayyid Al-Musalin, Muhammad At-Tayyib An-Najjar, uk. 205.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
