Daktari kufichua siri ya mgonjwa

Egypt's Dar Al-Ifta

Daktari kufichua siri ya mgonjwa

Question

Je, inafaa kwa daktari kufichua siri ya mgonjwa iwapo ataogopa kutokea madhara kwa watu wengine?

Answer

Kufichua siri ni katika khiyana ya amana, ambayo ni miongoni mwa sifa za wanafiki. Inampasa yule anayekabithiwa siri za watu kwa sababu ya kazi au nafasi yake, kama daktari, awajibike kuhifadhi siri za wagonjwa wake, na ni haramu kwake kuzifichua; kwa kuwa kuzifichua kunahusisha kuangukia katika kusengenya jambo lililoharamishwa, na kuvunja heshima na sitara ya wengine. Hata hivyo, huweza kutokea baadhi ya matukio katika hali fulani ambapo inajuzu kwa daktari kusema siri za mgonjwa bila ya kuwa amevunja wajibu wa kuzihifadhi siri hizo, kama pale ambapo kufichua huko kunapelekea kupatikana kwa maslahi au kuzuia janga  (uharibifu). Miongoni mwa hali hizo ni pale panapokuwepo hofu ya madhara kwa wengine, au pale mgonjwa anapokuwa ameathiriwa na ugonjwa wa mlipuko unaohofiwa kuenea kwa watu wengine na kusambaa katika jamii. Katika hali hiyo, daktari analazimika kuwataarifu mamlaka husika ili kuondoa madhara hayo, na kwa kufanya hivyo hatakuwa amevunja uaminifu wa kuhifadhi siri za wagonjwa wake.

Maelezo

 

Miongoni mwa maadili makuu yaliyomo katika Sharia ya Kiislamu ni uaminifu. Kwa uaminifu, haki za Mwenyezi Mungu Mtukufu na haki za waja wake hulindwa. Mtume (S/A.W) kabla ya kutumwa alijulikana kwa jina la Mkweli Muaminifu. Mwenyezi Mungu amewasifu waja wake waumini kwa kuhifadhi kwao amana; anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{Na wale ambao wanazihifadhi amana zao na ahadi zao} [Al-Mu’minun: 8].

 

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amekataza khiyana ya amana, akasema:
{Enyi mlioamini! Msimsaliti Mwenyezi Mungu na Mtume, wala msisaliti amana zenu hali mnajua} [Al-Anfal: 27].

Dhana ya amana inajumuisha kila kitu kinachopasa kuhifadhiwa na kutekelezwa. Inajumuisha kuhifadhi amana zilizowekwa, uaminifu katika kazi, na kuhifadhi siri, nayo ndiyo yenye uzito mkubwa na daraja ya juu zaidi. Kila jambo alilofaradhisha Mwenyezi Mungu kwa waja ni amana, kama vile Swala, Zaka, Funga, na kulipa deni. Amana zilizo na mkazo zaidi ni amana zilizowekwa, na amana iliyo na mkazo mkubwa zaidi ni kuficha siri.

Siri ni jambo linalofichwa na kuhifadhiwa. Miongoni mwa dalili zake ni kauli ya Mwenyezi Mungu: {Na ukisema kwa sauti kubwa, basi Yeye anajua siri na kilicho fichika zaidi} [Taha: 7], yaani anajua siri za waja, na hata kilicho fichika zaidi kuliko siri.

Kuhifadhi siri ya mwingine ni amana ya lazima, na thawabu yake ni sawa na thawabu ya kuficha aibu. Imepokewa kutoka kwa Abdullah bin Umar (R.A) kwamba Mtume (S/A.W) amesema:v“Muislamu ni ndugu wa Muislamu; hamdhulumu wala hamtelekezi… na yeyote anayemsitiri Muislamu, Mwenyezi Mungu atamsitiri siku ya Kiyama” (Imepokelewa na Bukhariy na Muslim).

Kama ambavyo, kufichua siri ni khiyana ya amana, nayo ni miongoni mwa sifa za wanafiki. Imepokewa kutoka kwa Abdullah bin Amr kwamba Mtume (S/A.W) amesema: “Sifa nne zikimkusanyika mtu huwa mnafiki kamili, na yeyote mwenye sifa mojawapo miongoni mwa hizo huwa na sifa ya unafiki mpaka aache: anapoaminiwa husaliti, anapozungumza hudanganya, anapo ahadi huvunja, na anapogombana hupitiliza mipaka” Imepokewa na Bukgari na Muslim.

Ingawa maandiko ya dini yako wazi katika kusisitiza kuhifadhi amana, ikiwa ni pamoja na kuhifadhi siri za wengine, wajibu huu unakuwa na mkazo zaidi kwa wale wanaokuwa na siri za watu kwa sababu ya kazi zao, kama ilivyo kwa daktari, ambalo ndilo suala linaloulizwa hapa. Kazi ya udaktari humlazimu daktari kufahamu hali za mgonjwa wakati wa uchunguzi na utambuzi wa maradhi.

Kwa hiyo, ni lazima kwa daktari kuhifadhi siri za wagonjwa wake, na ni haramu kwake kuzifichua; kwa kuwa katika kuzifichua kuna kuangukia katika kusingizia kilichoharamishwa. Mwenyezi Mungu anasema:  {wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anaye penda kuila nyama ya nduguye aliye kufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.} [Al-Hujurat: 12].

Dalili ya hilo ni kwamba kufichua siri ya mgonjwa — jambo ambalo hapendi mtu mwingine alijue — ni aina ya kusengenya, kwa kuwa humo kuna kumtaja mgonjwa kwa jambo analolichukia, na huo ndio uhalisia wa usengenyaji ulioharamishwa.

Na kauli ya Mwenyezi Mungu: {Enyi mlioamini! Msimsaliti Mwenyezi Mungu na Mtume, wala msisaliti amana zenu hali mnajua} [Al-Anfal: 27].

Mahusiano ya mtu yapo ima na Mola wake, au na waja wengine, au na nafsi yake. Ni lazima uaminifu uzingatiwe katika aina zote tatu. Kuhusu uaminifu kwa Mola, ni kutekeleza yaliyoamrishwa na kuepuka yaliyokatazwa. Na uaminifu kwa viumbe wengine unajumuisha kurejesha amana, kutopunguza katika vipimo na mizani, na kutofichua aibu za watu.

Amri ya kutekeleza amana inajumuisha kila jambo ambalo mtu anaaminishwa nalo. Daktari ameaminishwa yale anayoyajua miongoni mwa siri za wagonjwa wake. Kuzihifadhi ni katika kutekeleza amana, na ni haramu kuzifichua au kuzisambaza isipokuwa pale panapokuwepo dharura. Akifanya hivyo bila dharura, atahesabiwa kuwa msaliti wa amana na aliyeipoteza.

Na kwa kuwa kufichua siri kunahusisha kuvunja sitara ya mwingine, na maandiko ya dini yanaamuru kusitiri aibu za Muislamu kwa ndugu yake. Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira (R.A) kwamba Mtume (S/A.W)  amesema: “Hakuna mja ambaye Mwenyezi Mungu humsitiri aibu zake duniani isipokuwa Mwenyezi Mungu atamsitiri Siku ya Kiyama” (Imepokewa na Muslim). Ikimaanisha, kuficha aibu na madhambi yake ili yasitangazwe mbele ya watu, na huenda pia ikawa ni kutohojiwa juu yake au kutokumbushwa.

Kwa hiyo, daktari anatakiwa awe muaminifu na mwenye kuficha siri za wagonjwa, asifichue chochote kuhusu maradhi yao, wala asimjulishwe mtu mwingine yale aliyoyasema mgonjwa, kwani mgonjwa hakumpa ruhusa ya kumshirikisha mtu mwingine. Hata kama angeidhinisha, ni vyema daktari asifanye hivyo.

Kwa ajili hiyo, si halali kwa daktari na aliye katika nafasi yake kufichua siri za mgonjwa, la sivyo atahesabiwa kuwa msaliti wa amana na mwenye dhambi. Huu ndio msingi wa jumla. Hata hivyo, huweza kutokea baadhi ya matukio katika hali fulani ambapo inajuzu kwa daktari kufichua siri za mgonjwa bila kuvunja wajibu wa kuzihifadhi siri hizo, pale ambapo kunapatikana maslahi au kuondolewa ufisadi. Miongoni mwa hali hizo ni pale panapokuwepo hofu ya madhara kwa wengine, ambalo ndilo linaloulizwa hapa, kama vile mgonjwa kuwa na ugonjwa wa mlipuko unaohofiwa kuambukiza wengine na kusambaa katika jamii, au mgonjwa amefanya kosa la jinai na akaumia wakati wa kulifanya na akamkimbilia daktari ili atibiwe, na hali nyinginezo ambazo zinahakikisha uwepo wa madhara kwa wengine. Katika hali kama hizi, daktari atalazimika kuwajulisha mamlaka husika ili zichukue hatua stahiki za kuzuia madhara kwa wengine. Kufanya hivyo hakuhesabiwi kuwa ni kuvunja uaminifu wa kuhifadhi siri za wagonjwa.

Kwa kuwa kutoa taarifa katika hali kama hizi kunalinda usalama na utulivu wa jamii, na kuvuruga usalama huo ni madhara ya kijumla yanayopasa kuondolewa. Kufichua siri ya mgonjwa katika hali hizi ni madhara ya mtu binafsi, nayo ni madogo kuliko madhara ya kijamii. Hivyo, haihitajiki kuvumilia madhara ya kijumla kwa ajili ya kuepuka madhara binafsi.

Kutoa taarifa kuhusu hali ya mgonjwa kwa mamlaka husika katika hali hii kuna maslahi ya kisheria yanayotambulika, kwa kuwa yanahusiana na maslahi ya umma na kuzuia uharibifu. Inajuzu kutaja mabaya ya mtu mwingine ikiwa kuna kuondoa madhara makubwa au kuleta maslahi makubwa, kama pale mtu anapotoa taarifa kwamba fulani anataka kumuua yeye au familia yake au kuharibu mali yake, au anapomuarifu kiongozi au mwenye mamlaka kwamba mtu fulani anafanya jambo fulani lenye uharibifu. Hilo halihesabiwi kuwa ni kujiingiza katika usengenyaji ulioharamishwa.

Kifungu cha (5) cha Kanuni za Taaluma ya Madaktari nchini Misri za mwaka 2003, namba 238, kimeeleza kuwa: “Daktari analazimika kuwajulisha mamlaka za afya husika anaposhuku kuwepo ugonjwa wa mlipuko ili zichukue hatua za kinga kwa ajili ya kulinda jamii.”

Aidha, kifungu cha (30) cha Kanuni za Maadili ya Taaluma ya Udaktari nchini Misri, toleo namba 238 la mwaka 2003, kimeeleza: “Si halali kwa daktari kufichua siri za mgonjwa wake alizozijua kwa sababu ya taaluma yake isipokuwa kwa uamuzi wa mahakama, au pale panapokuwepo uwezekano wa madhara makubwa na ya hakika yatakayompata mtu mwingine, au katika hali nyingine zilizoainishwa na sheria.”

 

Vilevile, kifungu cha (33) cha Kanuni za Maadili ya Taaluma nchini Misri kimeeleza:
“Daktari analazimika kuwajulisha mamlaka husika kuhusu majeraha na ajali zenye dalili za jinai, kama vile majeraha ya risasi, majeraha ya kuchomwa, kukatwa, au mengineyo, pamoja na kuandika ripoti ya kitabibu iliyo kamili kuhusu hali hiyo wakati ilipowasilishwa kwake. Daktari anaweza kumwita daktari mwenzake kushiriki katika kuchunguza hali hiyo na kuandika ripoti.”

Inapaswa kuzingatiwa kwamba katika hali kama hizi na nyinginezo zinazojuzu kutoa taarifa kuhusu siri na hali ya mgonjwa, taarifa hiyo iwe kwa mamlaka husika tu bila kuvuka mpaka kwa wengine. Hii ni kwa sababu kufichua siri ya mgonjwa katika hali hii ni kwa sababu ya haja, na haja huchukuliwa kama dharura, na dharura hupimwa kwa kiwango chake. Hivyo basi, daktari akifichua siri za mgonjwa kwa wasiokuwa mamlaka husika, atahesabiwa kuwa msaliti wa amana, aliyekiuka wajibu wake wa kuhifadhi siri za wagonjwa wake, na atajiweka katika hatari ya kuwajibishwa.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Kiasili ni haramu kwa daktari kufichua siri za wagonjwa wake alizozifahamu kwa sababu ya taaluma yake, isipokuwa pale panapokuwepo dharura inayolazimisha hilo. Ikiwa dharura hiyo itapatikana kwa kuthibitika madhara makubwa yanayovuka mpaka kwa wengine, basi ni lazima daktari ataarifu wahusika ili kuondoa madhara hayo. Kwa kufanya hivyo hatakuwa amekiuka uaminifu wa kuhifadhi siri za wagonjwa wake, kwa sharti la kutovuka mipaka kwa kuwafahamisha wasiokuwa wahusika. Vinginevyo, atahesabiwa kuwa msaliti wa amana na mwenye dhambi.

Share this:

Related Fatwas