Kupiga Punyeto «Al-Istimna»

Egypt's Dar Al-Ifta

Kupiga Punyeto «Al-Istimna»

Question

Nini hukumu ya punyeto na jinsi gani ya kujitibu na kutubu kuacha jambo hilo?

Answer

Kupiga Punyeto — kujichua kwa mkono — ni haramu kisharia; ni maasi, na mtenda maasi ana dhambi kisharia na ni lazima atubu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kutokana na kitendo hiko; Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na ambao wanazilinda tupu zao, Isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa; Lakini anaye taka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka.} [Al-Muuminun: 5-7].

Wamevuliwa katika hilo mke na mume; hivyo inajuzu kisharia kufanya kitendo hiki kati yao kwa ajili ya kustareheshana; kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu alihalalisha njia na aina zote za starehe kati ya wanandoa isipokuwa kumuingilia mke tupu ya nyuma, na kuingiliana wakati wa hedhi na nifasi; Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Wake zenu ni kama konde zenu. Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo.} [Al-Baqarah: 223]. Maana ya {mpendavyo} yaani kwa upande wowote mpendao.

Maelezo

Kupiga Punyeto — kujichua — ni haramu kisharia, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: { Na ambao wanazilinda tupu zao, Isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa; Lakini anaye taka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka.} [Al-Muuminun: 5-7].

Sharia tukufu imeweka mchakato wa starehe na kutosheleza haja ya kindoa kupitia muingiliano kati ya wanandoa, na ikaifunga katika uhusiano huo, na ikaharamisha njia au aina yeyote isiyo ya ndoa. Kutoka kwa Abdillah bin Mas'ud (R.A) amesema kuwa Mtume amesema: «Enyi mkusanyiko wa vijana! Atakayeweza miongoni mwenu kuoa[1] basi aoe, kwani hilo ni lenye kuinamisha zaidi macho, na lenye kuhifadhi zaidi tupu, na asiyeweza basi naafunge saumu, kwani hiyo kwake ni kinga[2]» (Imepokelewa na Imamu Muslim).

Hadithi inaonesha kuwa ndoa ndiyo njia halali ya kutosheleza haja ya kingono bila njia nyingine za haramu kama punyeto; ndio maana Mtume S.A.W akamuamuru yule asiyeweza kuoa afunge saumu; kwa sababu saumu hufifisha matamanio na kumkinga mwenye kufunga kutokana na kutumbukia katika fitna na haramu.

Kupiga punyeto kunasababisha yafuatayo:

Kustahili dhambi kwa kutumbukia katika kosa, na hakuna tofauti ya uharamu wake kati ya mwanaume na mwanamke.

Wajibu wa toba kwa aliyetumbukia katika hilo kwa kuacha tabia hiyo mbaya, na kujutia kwa yale aliyopuuza katika haki ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kuazimia kutorejea tena.

Kutokea kwa janaba kwa kutoa mbegu kwa matamanio, hivyo ni lazima kuoga kwa nia ya kuondosha hadathi kubwa kwa ajili ya kujisafisha.

Punyeto ni miongoni mwa vitu vinavyofunguza Saumu ikiwa itatokea mchana wa Ramadhani, hivyo ni wajibu kulipa siku hiyo, na kutubu kwa dhambi hii na kwa dhambi ya kufuturu kwa makusudi katika funga ya Ramadhani.

Ama kuhusu namna ya matibabu na toba ya punyeto ni kwa kufuata yafuatayo:

Kuinamisha macho dhidi ya mambo ya haramu.

Kutofikiria mambo yanayoamsha matamanio ya kingono.

Kuandamana na wenzako wema ambao watamsaidia mtu katika kufuata njia nyoofu.

Kukithirisha Saumu za Sunna kama ilivyokuja katika Hadithi: ((... na asiyeweza basi naafunge Saumu, kwani hiyo kwake ni kinga)).

Kuangalia mwisho wa mambo, na kuonekana  na Mwenyezi Mungu Mtukufu  katika siri na dhahiri, na kuona haya kukuona katika maasi.

Hapa ni lazima tuulize swali: Je, inajuzu kwa mume kujichua kwa mkono wa mkewe, au mke kujichua kwa mkono wa mumewe?

Jibu ni: Sharia tukufu imeruhusu kwa wanandoa kustereheshana kwa namna yeyote na wakati wowote, na ikavua katika hali mbili, nazo ni:

Ni Haramu kwa mwanaume kumuingilia mkewe katika tupu ya nyuma (sehemu ya haja kubwa).

Ni Haramu kwa mwanaume kumuingilia mkewe wakati wa hedhi na nifasi.

Hivyo, Sharia haijaharamisha punyeto kati ya wanandoa, iwe ni kwa mkono wa mke kwa mume, au kwa mkono wa mume kwa mkewe, na namna nyinginezo za starehe kati yao; Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Wake zenu ni kama konde zenu. Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo. Lakini jitangulizieni kheri nafsi zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kuwa hakika nyinyi mtakutana naye. Na wape bishara njema Waumini.} [Al-Baqarah: 223].

Maana ya {mpendavyo} yaani kwa upande wowote mpendao[3]. Inaelewaka kutokana na Aya hii tukufu kuruhusiwa starehe kati ya wanandoa kwa namna yeyote ya kisharia, na miongoni mwa hiyo ni kupiga punyeto kati yao.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Kwamba haijuzu kisharia kupiga punyeto, na mtendaji wa maasi haya ana dhambi kisharia na ni lazima atubu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Wanandoa wamevuliwa katika hili; kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu alihalalisha njia na aina zote za starehe kati ya wanandoa isipokuwa kuingilia tupu ya nyuma ya mke, na kuingiliana wakati wa hedhi na nifasi.

 

[1] «Ba'a»: Uwezo wa kimwili na mali.

[2]  «Kinga»: Kinga dhidi ya uzina.

[3] Tafsir Al-Baydhawi.(1/140)

Share this:

Related Fatwas