Subira juu ya Mitihani
Question
Ni yapi malipo ya kusubiri juu ya mitihani?
Answer
Subira ni miongoni mwa tabia adhimu ambazo Muislamu anapaswa kujipamba nazo, na kuizoeza nafsi yake juu yake. Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: {Enyi mlio amini! Subirini, na shindaneni kusubiri, na kuweni macho, na mcheni Mwenyezi Mungu, ili mpate kufanikiwa.} [Al-Imran: 200]. Mtume (S.A.W) alikuwa kielelezo bora katika kujipamba na subira; alisema wakati wa kifo cha mwanawe Ibrahim: ((Hakika jicho linatoa machozi, na moyo unahuzunika, na wala hatusemi isipokuwa kile kinachomridhisha Mola wetu, na sisi kwa kufarikiana nawe ewe Ibrahim ni wenye kuhuzunika)). Subira, kama walivyosema baadhi ya Wanazuoni, ipo katika sura nne nazo ni:
Subira juu ya mitihani: Nako ni kuizuia nafsi kutokana na machukizo (kunung'unika).
Subira juu ya neema: Nako ni kuzifunga kwa shukrani na kutovuka mpaka.
Subira juu ya utiifu: Nako ni kudumu kwayo.
Subira dhidi ya maasia: Nako ni kuizuia nafsi kwayo.
Mtume (S.A.W) amebainisha fadhila ya kusubiri juu ya mitihani kwa kusema kwake: ((Ajabu ni jambo la Muumini, hakika jambo lake lote ni kheri, na hilo si kwa yeyote isipokuwa kwa Muumini, akifikwa na kheri hushukuru ikawa ni kheri kwake, na akifikwa na dhara husubiri ikawa ni kheri kwake)); kwa hiyo Mwenyezi Mungu amewabashiria wenye kusubiri malipo makubwa kutoka Kwake; Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: {Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu.} [Az-Zumar: 10].
Maelezo
Subira ni miongoni mwa tabia njema na adhimu ambazo Muislamu anapaswa kujipamba nazo, na kuizoeza nafsi yake juu yake, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu amebainisha kuwa subira ni njia ya mafanikio; Mwenyezi Mungu Mtukufu Akasema: {Enyi mlio amini! Subirini, na shindaneni kusubiri, na kuweni macho, na mcheni Mwenyezi Mungu, ili mpate kufanikiwa.} [Al-Imran: 200]. Mtume (S.A.W) alikuwa mfano bora na kielelezo katika kujipamba na subira, na kuvumilia shida kwa nafsi iliyoridhika na azma isiyolegea; kutoka kwa Anas Ibn Malik (R.A), kwamba Mtume (S.A.W) alisema wakati wa kifo cha mwanawe Ibrahim: ((Hakika jicho linatoa machozi, na moyo unahuzunika, na wala hatusemi isipokuwa kile kinachomridhisha Mola wetu, na sisi kwa kufarikiana nawe ewe Ibrahim ni wenye kuhuzunika)) imepokelewa na Al-Bukhari.
Na katika Hadithi kutoka kwa Suhaib Ibn Sinan (R.A), amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W): ((Ajabu ni jambo la Muumini, hakika jambo lake lote ni kheri, na hilo si kwa yeyote isipokuwa kwa Muumini, akifikwa na kheri hushukuru ikawa ni kheri kwake, na akifikwa na dhara husubiri ikawa ni kheri kwake)) imepokelewa na Muslim.
Baadhi ya Wanazuoni wamegawa subira katika sura nne nazo ni:
Subira juu ya mitihani: Nako ni kuizuia nafsi kutokana na kunung'unika, hofu kubwa na mfadhaiko; kutoka kwa Anas Ibn Malik (R.A), amesema: ((Mtume (S.A.W) alimkuta mwanamke mmoja akilia mbele ya kaburi, akasema: Mche Mwenyezi Mungu na usubiri, akasema: Nitokee mimi, kwani wewe hukufikwa na msiba wangu, na alikuwa hakumjua (ni nani anayezungumza naye), akaambiwa: Hakika huyo ni Mtume (S.A.W), akaja mlangoni kwa Mtume (S.A.W), na hakukuta kwake walinzi wa mlangoni, akasema: Sikukujua, akasema: Hakika subira ni wakati wa pigo la kwanza)) imepokelewa na Al-Bukhari. Yaani subira iliyokamilika kwa ujira na thawabu ni ile inayokuwa wakati wa kwanza wa kutokea msiba unaoupiga moyo ghafla.
Subira juu ya neema: Nako ni kuzifunga kwa shukrani na kutovuka mpaka na kufanya kiburi kwazo, kwa hiyo Mwenyezi Mungu amewahadharisha waja Wake kutokana na fitna ya wingi wa neema, mali na watoto, Mwenyezi Mungu Mtukufu Akasema: {Enyi mlio amini! Yasikusahaulisheni mali yenu, wala watoto wenu, kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Na wenye kufanya hayo ndio walio khasiri.} [Al-Munafiqun: 9].
Subira juu ya utiifu: Na hilo ni kwa kuuhifadhi na kudumu nao, Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: {Na waamrishe watu wako kuswali, na uendelee mwenyewe kwa hayo. Sisi hatukuombi wewe riziki, bali Sisi ndio tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni kwa mchamngu.} [Taha: 132].
Subira ya kuepukana na maasi: Na hilo ni kwa kuizuia nafsi kwayo; Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema kupitia ulimi wa Yusuf (A.S) wakati mke wa mkuu wa Misri alipotaka kumuingiza katika fitna: {Yusuf akasema: Audhubillahi! Najikinga na Mwenyezi Mungu. Huyu bwana wangu kaniweka maskani nzuri, na hakika wenye kudhulumu hawatengenekewi.} [Yusuf: 23].
Subira ina faida nyingi zinazomrudia mwenye kusubiri, miongoni mwazo:
Mwenyezi Mungu ameweka malipo makubwa kwenye Subira; Mwenyezi Mungu Mtukufu Akasema: {Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu.} [Az-Zumar: 10].
Mwenyezi Mungu anampa mwenye kusubiri malipo bora zaidi; Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: {Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu.} [Hud: 115], {Mlivyo navyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu ndivyo vitakavyo bakia. Na kwa yakini Sisi tutawapa walio subiri ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda.} [An-Nahl: 96].
Subira ni njia ya ushindi; Mwenyezi Mungu akasema: {Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri.} [Al-Anfal: 46].
Subira malipo yake ni Pepo, Mwenyezi Mungu akasema: {Na ambao wameamini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawaweka katika maghorofa ya Peponi yenye kupitiwa chini yake mito, wakidumu humo. Ni mwema ulioje huo ujira wa watendao(58) Ambao walisubiri, na wakamtegemea Mola wao Mlezi.} [Al-Ankabut: 58-59].
Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:
Subira ni tabia adhimu inayopaswa kwa Muislamu kujipamba nayo, na Mwenyezi Mungu ameweka kwa mwenye kusubiri thawabu kubwa, na Mwenyezi Mungu Mtukufu amebashiri kuwa malipo ya subira ni radhi za Mwenyezi Mungu kwa mja mwenye kusubiri na kumuingiza Peponi.
Subira kama walivyosema baadhi ya Wanazuoni ipo katika sura nne:
a) Subira juu ya mitihani nayo ni: kuizuia nafsi kutokana na kunung'unika, hofu kubwa na mfadhaiko.
b) Subira juu ya neema nayo ni: kuzifunga kwa shukrani na kutovuka mpaka na kufanya kiburi kwazo.
c) Subira juu ya utiifu nayo ni: kuuhifadhi na kudumu nao.
d) Subira dhidi ya maasia nayo ni: kuizuia nafsi kwayo.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
