Kuomba idhini kabla ya kuingia katika nyumba kwa ajili ya ziara
Question
Kuna adabu gani za kuomba idhini kabla ya kuingia katika nyumba kwa ziara?
Answer
Mgeni ana wajibu wa kuomba ruhusa kabla ya kumtembelea jamaa au rafiki, na awajulishe kabla ya kwenda kwa njia yeyote, kama vile simu au njia nyingine za kisasa, ili watu wa nyumbani waweze kujiandaa kwa ajili ya ziara. Mwenyezi Mungu Anasema: {Enyi mlio amini! Msiingie nyumba zisio nyumba zenu mpaka mwombe ruhusa, na mwatolee salamu wenyewe. Hayo ni bora kwenu mpate kukumbuka} [An-Nur: 27].
Mgeni hapaswi kuirefusha ziara au kuirudia mara kwa mara, ili watu wa nyumbani wasimchoke. Abu Hurairah amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) amesema: "Fanya ziara mara chache, na utapendwa."
Kunapasa kujitambulisha na kutaja jina lake ili waenyeji waruhusu kuingia. Pia ni muhimu kuchagua wakati mwafaka wa kutembelea, ili isiwe wakati familia inapumzika au ina shughuli nyingi, na kadhalika. Ikiwa familia haitaruhusu ziara, mgeni anapaswa kuondoka. Imepokewa kutoka kwa Abu Musa Al-Ash'ari (R.A) kwamba Mtume amesema (S.A.W): "Kubisha hodi mara tatu, na ukiruhusiwa, ingia; la rudi."
Maelezo
Inapendekeza kisharia mtu atembelee jamaa, marafiki, na wapendwa wake, awapongeze katika furaha zao, awafariji katika majonzi yao, na kuwaunga mkono wakati wa magonjwa yao. Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira (R.A) kwamba Mtume (S.A.W) amesema: (Mtu mmoja alimtembelea ndugu yake katika kijiji kingine, basi Mwenyezi Mungu Akamtuma Malaika kumfuatilia njiani, Alipomjia, akamwambia: Unaelekea wapi? Akasema: Ninaenda kumtembelea ndugu yangu katika kijiji hiki. Akamwambia: Je, unawahi kumlipa wema wowote? Akasema, 'Hapana, lakini ninampenda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ' Akasema, 'Mimi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwako, kwamba Mwenyezi Mungu Anakupenda kama ulivyompenda.'" Imepokelewa na Muslim.
Imepokewa kutoka kwa Abu Hurairah (R.A) amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) amesema: "Yeyote atakayemtembelea mgonjwa au kumtembelea ndugu yake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, muitaji atamwita, akisema, 'Uwe salama, hatua zako zibarikiwe, na upate sehemu Peponi.” Imepokewa na Bukhari.
Uislamu umeweka adabu za kutembeleana zinazopaswa kuzingatiwa, ikiwemo:
Kuomba ruhusa kabla ya kufanya ziara, kwa kuwajulisha familia ili waweze kujiandaa kumkaribisha mgeni. Mwenyezi Mungu Anasema: { Enyi mlio amini! Msiingie nyumba zisio nyumba zenu mpaka mwombe ruhusa, na mwatolee salamu wenyewe. Hayo ni bora kwenu mpate kukumbuka } [An-Nur: 27]. Kinachomaanishwa na kuomba idhini ni kuomba ruhusa ya kutembelea kabla ya kwenda na kupanga muda wa ziara, kupitia simu au njia nyingine za kisasa za mawasiliano.
Kuacha kufanya ziara na kughairisha ikiwa kuna mazingira yanayozuia familia kupokea wageni. Mwenyezi Mungu Anasema: {Na msipo mkuta mtu humo basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na mkiambiwa: Rudini! Basi rudini. Hivi ni usafi zaidi kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayo yatenda} [An-Nur: 28]. Imepokewa kutoka kwa Abu Musa Al-Ash'ari (R.A) kwamba Mtume (S.A.W) amesema: "Kuomba ruhusa mara tatu. Ukipewa ruhusa, ingia; kama la, basi rudi." Imepokewa na Muslim.
Mgeni anapaswa kuwasalimia wenyeji anapoomba ruhusa ya kuingia. imepokelewa kutoka kwa Rabiah kwamba mtu kutoka Bani Amir aliomba ruhusa ya kuingia kwa Mtume (S.A.W). alipokuwa nyumbani kwake, akasema, "Naomba kuingia?" Mtume (S.A.W) akamwambia mtumishi wake, "Toka mfate na umfundishe jinsi ya kuomba ruhusa Mwambie aseme, 'Amani iwe kwenu, naweza kuingia? Mtu huyo alimsikia na akasema, 'Amani iwe juu yenu, naweza kuingia?' Mtume (S.A.W.) akampa ruhusa, naye akaingia." Imepokewa na Abu Dawood.
Mgeni anapaswa kujitambulisha kwa jina lake atakapoulizwa, ili mwenye nyumba aweze kumpa ruhusa ya kuingia. Imepokewa kutoka kwa Jabir bin Abdullah amesema: "Nilikuja kwa Mtume (S.A.W) kuhusu deni ambalo baba yangu alikuwa anadaiwa, hivyo nikagonga mlango, naye akasema, 'Nani huyo? Nikajibu, 'Ni mimi,' naye akasema, 'Ni mimi, ni mimi,' kana kwamba hakupenda." Imepokewa na Bukhari.
Hadithi hii inaashiria kuwa haipendekezi kwa anayeomba ruhusa kusema "ni mimi," kwa sababu kauli hii haimtambulishi.
Kutokuikithirisha ziara mara kadhaa, ili watu wa nyumbani wasikuchoke mgeni. Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira (R.A.) amesema: Mtume (S.A.W) amsema: "Tembelea mara chache, kwani hilo huongeza upendo." Maana ya Hadithi hii ni kwamba kutembeleana mara chache huifanya nafsi itamani kumwona mtu, kukutana naye, na kukaa naye.
Kutorefusha ziara yako kwa muda mrefu bila kuzingatia hali za watu wa nyumbani, kwani wanaweza kuwa na shughuli nyingine muhimu. Mwenyezi Mungu Anasema: {Enyi mlio amini! Msiingie nyumba za Nabii ila mpewe ruhusa kwenda kula, sio kungojea kiwive. Lakini mtakapo itwa basi ingieni, na mkisha kula tawanyikeni, wala msiweke mazungumzo. Hakika hayo yanamuudhi Nabii naye anakustahini, lakini Mwenyezi Mungu hastahi kwa jambo la haki. Na mnapo wauliza wakeze haja waulizeni nyuma ya mapazia. Hivyo ndio usafi zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao. Wala haikufalieni kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu, wala kuwaoa wake zake baada yake kabisa. Hakika jambo hilo ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu} [Al-Ahzab: 53]. Aya hii iliteremshwa kwa sababu ya kundi la watu waliokula katika nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) wakati wa karamu ya Zaynab bint Jahsh, kisha wakakaa wakiongea katika nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) alikuwa na shughuli na mahitaji ya familia yake, lakini haya yake ilimzuia kuwaamuru waondoke nyumbani kwake.
Kuchagua wakati mwafaka wa kutembelea hata kama kuwatembea wazazi, kuna nyakati ambapo si rahisi kwa familia kupokea wageni, kama vile wakati wa mapumziko na kadhalika. Mwenyezi Mungu Anasema: {Enyi mlio amini! Nawakutakeni idhini iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia na walio bado kubaalighi miongoni mwenu mara tatu - kabla ya Sala ya alfajiri, na wakati mnapo vua nguo zenu adhuhuri, na baada ya Sala ya isha. Hizi ni nyakati tatu za faragha kwenu. Si vibaya kwenu wala kwao baada ya nyakati hizi, kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kuelezeni Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima} [An-Nur: 58].
Aya hii Tukufu inaashiria kwamba hizi ni nyakati ambapo wanafamilia wako katika mapumziko na wanaweza kuwa wamevua nguo wakati wa kupumzika au kulala, Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu, Mtukufu, Aliwaamrisha wazazi kuwafundisha watoto wao adabu ya kuomba ruhusa kabla ya kuingia, kwa sababu ni kinyume cha adabu kwa watoto kuona sehemu za faragha za wazazi wao, na ni lazima wafundishwe kujistiri.
Ikiwa watoto wanatakiwa kuomba ruhusa na kuchagua wakati mwafaka wa kuingia vyumba vya wazazi wao, basi ni muhimu zaidi kwa mtu kuchagua wakati mwafaka wa kumtembelea jamaa au rafiki zake anayemtaka kumtembelea.
Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:
Tunajifunza kwamba wageni lazima waombe ruhusa kabla ya kuwatembelea jamaa zao au marafiki, na wanapaswa kuwajulisha kabla ya kuja kwa njia yoyote, kama vile simu au njia nyingine za kisasa, ili wenyeji waweze kujiandaa kwa ajili ya ziara hiyo. Mgeni hapaswi kuirefusha ziara au kuirudia mara kwa mara, ili wasiwachoshe wenyeji. Pia ni muhimu kuchagua wakati mwafaka wa ziara, isiwe wakati wa mapumziko ya wenyeji au wakati wana shughuli nyingi, na kadhalika.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
