Hukumu ya kusoma Surat Yasin kwa nia ya kutatuliwa haja fulani
Question
Ni nini hukumu ya kusoma Surat "Yasin" kwa nia ya kutatuliwa haja na kuondolewa dhiki?
Answer
Kusoma Qur`ani Tukufu ni miongoni mwa mambo yanayomletea mhusika baraka na thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na miongoni mwa Sura ambazo zimepokewa Hadithi kadhaa kuhusu fadhila zake ni Surat Yasin; kutoka kwa Ma'qil bin Yasar kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) amesema: “Yasin ni moyo wa Qur`ani, haisomi mtu anayetarajia radhi za Mwenyezi Mungu na nyumba ya Akhera ila atasamehewa, na wasomeeni maiti zenu”.
Hivyo, kusoma Surat Yasin kuna fadhila kubwa, na msomaji wake ana thawabu nyingi. Wanazuoni wamethibitisha kuwa inajuzu kusoma Surat Yasin kwa nia ya kutatuliwa haja na kuondolewa dhiki -kama vile kuongezewa riziki, kulipa deni, na mambo mengine ya kheri. Yule anayeisoma akiwa na yakini kwamba Mwenyezi Mungu (S.W.) Atamtatulia haja yake kwa baraka za kusoma Qur`ani na SuratYasin, basi atapata kile alichokikusudia kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Maelezo
Kusoma Qur`ani Tukufu kunamletea mtu baraka, malipo, na thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu; imepokelewa kutoka kwa Aisha (R.A.) amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) amesema: “Mwenye kusoma Qur’ani kwa umahiri[1] atakuwa pamoja na malaika waandishi[2] watukufu na wema[3]. Na yule anayesoma Qur`ani kwa kigugumizi[4] na hali ya kuwa inampa ugumu, atapata malipo mara mbili[5]” [Imepokelewa na Muslim].
Na miongoni mwa Sura za Qur'ani Tukufu ambazo zimepokewa Hadithi kadhaa za Mtume kuhusu fadhila za kuzisoma ni Surat Yasin; kutoka kwa Anas bin Malik (R.A.) amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) amesema: “Hakika kila kitu kina moyo, na moyo wa Qur`ani ni Yasin. Na mwenye kusoma Yasin, Mwenyezi Mungu humwandikia kwa kisomo chake hicho thawabu za kusoma Qur`ani mara kumi” [Imepokelewa na Al-Tirmidhi].
Pia kutoka kwa Anas bin Malik (R.A.) amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) amesema: “Mwenye kudumu na kusoma Yasin kila usiku, kisha akafa, basi hufa akiwa shahidi”[6].
Na kutoka kwa Ma’qil bin Yasar, kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) amesema: “...Na Yasin ni moyo wa Qur`ani; haisomi mtu anayetarajia radhi za Mwenyezi Mungu na nyumba ya Akhera ila atasamehewa, na wasomeeni maiti zenu”[7].
Hadithi hizi za Mtume zinaonesha kuwa kusoma Surat Yasin kuna fadhila kubwa, na msomaji wake ana thawabu nyingi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na kwamba yule anayeisoma kwa nia ya kutatuliwa haja na kuondolewa dhiki, hupata kile alichokusudia kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
Ama kile kinachofanywa na baadhi ya watu cha kusoma Surat Yasin kwa nia ya kumrejesha mtu aliyepotea au aliyetoweka kwa familia yake; ambapo wanapofika katika neno "Mubin" -neno ambalo limetajwa mara saba ndani ya Sura hiyo -hufunga fundo, na kudai kuwa mafundo hayo yanasababisha dunia imfanyie dhiki mtu huyo aliyepotea au aliyetoweka mpaka arejee kwa familia yake; jambo hili halijuzu kisharia. Halikupokelewa kutoka kwa yeyote miongoni mwa watu wema (Salaf) kuwa alifanya hivyo, bali jambo hilo linafanana zaidi na vitendo vya waganga na washirikina.
Tunapata faidia Kutokana na yaliyotangulia:
Kusoma Qur`ani Tukufu kunamletea msomaji thawabu, malipo, na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu (S.W.).
Kusoma Surat Yasin kwa nia ya kutatuliwa haja na kuondolewa dhiki ni jambo linalojuzu kisheria. Zimepokewa Hadithi kadhaa za Mtume (S.A.W) kuhusu fadhila za kuisoma ambazo kwa ujumla wake zinaonyesha kuwa, kupitia kisomo hicho, malengo hufanikiwa -kama vile kupata wasaa wa riziki, kulipa deni, na mambo mengine ya kheri -kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
[1] «Mwenye utofauti na umahiri»: Anayesoma Qur'ani kwa ustadi bila ugumu wala taabu.
[2] «Safarati»: Mitume au Malaika wajumbe wa Mwenyezi Mungu.
[3] «Bararati»: Wenye kutii amri za Mwenyezi Mungu Mtukufu.
[4] «Anayesoma kwa kigugumizi»: Anayesitasita katika usomaji kwa sababu ya udhaifu wa kuhifadhi.
[5] «Malipo mara mbili»: Malipo ya usomaji na malipo ya juhudi/ugumu.
[6] Imepokelewa na Al-Tabarani katika "Al-Mu'jam Al-Awsat".
[7] Imepokelewa na Ahmad katika "Musnad" yake.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
