Kuchanganya nia ya kuchinja (Udh-hiyya) na Akika katika mnyama mmoja
Question
Ni ipi hukumu ya kuchanganya nia ya Udh’hiya na Akika katika mnyama mmoja?
Answer
Inafaa kuchanganya Udh’hiya na Akika katika mnyama mmoja ikiwa wakati wa Akika unaafikiana na wakati wa Udh’hiya; kwa kufuata rai ya wanazuoni walioruhusu hilo, kwa sharti kwamba iwe katika wanyama wanaoruhusiwa kushirikishwa, ambao ni ng’ombe na ngamia, na isiwe sehemu ya kila moja kati ya Udh’hiya na Akika chini ya thuluthi moja ya saba ya mnyama; kwa kuwa katika hilo kuna kurahisisha kwa masikini asiyeweza kupata kitu cha kutekeleza ibada zote mbili.
Maelezo
Udh’hiya ni sunna ya Mtume (S.A.W) iliyosisitizwa kwa mwenye uwezo; kwa ajili ya kuwapa riziki jamaa, ndugu na masikini katika siku za Idi. Kutoka kwa Anas bin Malik (R.A) amesema: “Mtume (S.A.W) alichinja kondoo wawili weupe wenye madoadoa[1], wenye pembe[2]; aliwachinja kwa mkono wake, akasema Bismillah na akataja jina la Mungu (akatoa takbiri), na akaweka mguu wake juu ya mbavu zao[3].”[4]
Na katika Udh’hiya kuna thawabu kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; ndani yake kuna kufufua Sunna ya bwana wetu Ibrahim (amani iwe juu yake). Kutoka kwa Zayd bin Arqam R.A amesema: “Maswahaba wa Mtume (S.A.W) walisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni nini hii Udh’hiya? Akasema: Ni Sunna ya baba yenu Ibrahim. Wakasema: Basi tuna nini humo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema: Kwa kila unywele ni thawabu. Wakasema: Na sufi ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema: Kwa kila unywele wa sufi ni thawabu.”[5]
Ama kuhus Akika, ambayo huchinjwa kwa ajili ya mtoto aliyezaliwa, awe wa kiume au wa kike, ni sunna iliyosisitizwa aliyoifanya Mtume (S.A.W) na Maswahaba (R.A). Kutoka kwa Ibn Abbas R.A kwamba: “Mtume (S.A.W) alimfanyia Akika Hasan na Husayn, kila mmoja kwa kondoo mmoja.”[6].
Ama kuhusu masharti ya kusihi Udh’hiya na Akika ni haya yafuatayo:
1- Lazima mnyama anayechinjwa kwa ajili ya Udh’hiya au Akika awe ni ngamia, ng’ombe au kondoo; kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Ili walitaje jina la Mwenyezi Mungu juu ya alivyowaruzuku katika wanyama wa mifugo} [Al-Hajj: 34].
Mnyama kusalimika na kasoro na magonjwa; kutoka kwa Al-Baraa bin Aazib R.A amesema: “Mtume (S.A.W) alisimama akasema: Wanne hawafai katika Udh’hiya – akasema – mwenye upofu ulio wazi, mgonjwa aliye wazi ugonjwa wake, kilema aliye wazi kilema chake, na aliyevunjika mfupa asiyeweza kusimama.”[7].
Ama kwa upande wa hukumu ya kukusanya katia ya Udh’hiya na Akika katika mnyama mmoja, ni kama ifuatavyo:
Kwanza: Baadhi ya wanazuoni wanaona kuwa jambo hilo halifai; hivyo haifai kukusanya katika mnyama mmoja kwa nia mbili tofauti.
Pili: Baadhi ya wanazuoni wanaona kuwa inafaa jambo hilo[8]; kwa sababu lengo la Udh’hiya na Akika ni kuonyesha mshikamano wa kijamii kati ya watu, na katika kuruhusu kuchanganya nia mbili kuna kumrahisishia masikini asiyeweza kutekeleza ibada zote mbili kwa pamoja, na kwa hivyo katika hili kunapatikana kulinda ibada za Kiislamu. Lakini ili kusihi kukusanya na kuchinja mmnayama mmoja kwa nia mbili kumewekwa masharti, nayo ni:
Kuchanganya kuwe katika wanyama wanaoruhusiwa kushirikishwa, yaani ng’ombe au ngamia; na haifai hilo katika kondoo.
Isiwe sehemu ya kila moja kati ya Udh’hiya na Akika chini ya moja ya saba ya mnyama; ikiwa itapungua chini ya sehemu ya saba basi haifai. Kutoka kwa Jabir bin Abdullah (R.A) amesema: “Tulitoa Udh’hiya pamoja na Mtume (S.A.W) mwaka wa Hudaybiya, ngamia kwa watu saba, na ng’ombe kwa watu saba.”[9]
Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia;
Kujuzu kuchanganya Udh’hiya na Akika katika mnyama mmoja ikiwa wakati wa akika unaafikiana na wakati wa Udh’hiya; kwa kufuata rai ya wanazuoni waliojuzisha hilo, kwa sharti kwamba iwe katika wanyama wanaoruhusiwa kushirikishwa, nao ni ng’ombe na ngamia, na isiwe sehemu ya kila moja kati ya Udh’hiya na Akika chini ya moja ya saba ya mnyama; kwa kuwa katika hilo kuna kurahisisha kwa masikini asiyeweza kupata kitu cha kutekeleza ibada zote mbili.
[1] Ni mnyama mweupe pepe aliyechanganyika na kiasi fulani cha rangi nyeusi.
[2] Kila mmoja kati yao ana pembe mbili.
[3] Inamaanisha kwenye shingo, yaani upande wake.
[4] Imepokelewa na Imam Bukhari.
[5] Imepokelewa na Ibn Majah.
[6] Imepokelewa na Imam Daud.
[7] Imepokewa naImam Daud.
[8] “Nihayat al-Muhtaj ila Sharh al-Minhaj” cha Al-Ramli (8/145) na “Sharh Muntaha al-Iradat” cha Al-Bahuti (1/616).
[9] Imepokewa na Imam Muslim (2/955).
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
