Hukumu ya kutembelea (kuzuru) makab...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya kutembelea (kuzuru) makaburi siku ya Idi

Question

Ni ipi hukumu ya kutembelea (kuzuru) makaburi siku ya Idi? Na ni ipi hukumu ya mwanamke mwenye hedhi kwenda makaburini?

Answer

Kuzuru makaburi ni jambo linalopendekeza kisharia katika nyakati zote, na ubora wake huongezeka katika siku zenye baraka ambazo mtu hutafuta ziada ya thawabu na ujira kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, zikiwemo siku za Idi mbili; kwa kuwa ndani yake inapatikana hisia maana za kuendeleza uhusiano na wema, na kuwaombea rehema na msamaha waliokufa miongoni mwa jamaa na ndugu.

Hata hivyo, anayezuru makaburi anapaswa kuepuka kufanya jambo lolote linalomkasirisha  Mwenyezi Mungu Mtukufu kama vile kuomboleza kwa vilio na kutamka maneno yanayoonesha kupinga kudura za  Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Kwa upande wa sharia, inafaa kwa mwanamke mwenye hedhi kwenda kuzuru makaburi ikiwa ameshikamana na hijabu yake, kwa sharti asifanye lolote katika matendo ya kijahili kama kuomboleza, kujipiga usoni, na kutamka maneno yasiyokubaliwa na sharia tukufu.

Maelezo

Sharia tukufu imependekeza kuzuru makaburi na imehimiza jambo hilo; kwa kuwa katika kuyazuru kuna kukumbuka akhera, kujiepusha na dunia inayopita, na kulainisha nyoyo. Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira R.A kwamba Mtume (S.A.W) amesema: “Zuruni makaburi; kwani yanawakumbusha Akhera.[1]” Na kutoka kwa Abdullah bin Mas‘ud R.A, kwamba Mtume (S.A.W)  amesema: “Nilikuwa nimewakataza kuzuru makaburi; basi yazuruni, kwani yanazifanya nyoyo zijitenge na dunia na yakumbusha Akhera.”[2]

Hadithi inaonesha kwamba kukataza kwa Mtume (S.A.W) kuzuru makaburi mwanzoni mwa ulinganio wa Kiislamu kulikuwa kwa sababu watu walikuwa na desturi ya kuomboleza[3] na kutamka maneno yasiyokubalika kisharia wanapoyazuru; na Uislamu ulipoimarika katika nyoyo zao na desturi hizo mbaya kuondoka, Mtume (S.A.W) akawaamuru kuyazuru na akawahimiza hilo.

Ama kauli ya kukataza kuzuru makaburi katika siku za Idi kwa kuwa ni siku za furaha na bashasha, na kwamba kuzuru makaburi ni sababu ya kuhuisha huzuni, basi kauli hiyo si sahihi kwa sababu zifuatazo:

Kwanza: Amri ya kuzuru makaburi imekuja kwa ujumla bila kufungamanishwa na wakati maalumu wala hali maalumu; Kuweka siku maalum za kutembelea makaburi hakuvunji sharia tukufu za Kiislamu[4]. Isipokuwa inapendekezwa kuyazuru katika baadhi ya siku ambazo Mwenyezi Mungu Mtukufu amezipa ubora zaidi; kwa kuwa ndani yake kuna kuongezeka kwa thawabu na kukubaliwa dua, kama siku ya Ijumaa, mwanzo wa mwaka wa Hijria, na msimu wa Hijja[5].

Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira R.A kwamba Mtume (S.A.W)  amesema: “Atakayezuru kaburi la wazazi wake au mmoja wao kila Ijumaa atasamehewa na ataandikiwa kuwa mwema.”[6].

Na kutoka kwa Muhammad bin Ibrahim At-Taymi R.A amesema: Mtume (S.A.W) alikuwa akiyazuru makaburi ya mashahidi kila mwaka[7], na kusema: “Amani iwe juu yenu kwa yale mliyoyavumilia; basi uzuri ulioje wa malipo ya nyumba ya Akhera.” amesema: Na Abu Bakr, Umar na Uthman walikuwa wakifanya hivyo[8].

Na kutoka kwa Ibrahim An-Nakha‘i kwamba Mtume (S.A.W)  alitoka yeye na Maswahaba wake katika Hijja ya kuaga kuelekea makaburini, akapita kati ya makaburi hayo hadi akaketi karibu na kaburi moja, kisha akasimama hali ya kulia na kusema: “Hili ni kaburi la mama yangu Amina …[9]”

Pili: Si kila kuhuisha huzuni kunakatazwa; bali Mtume (S.A.W) amehimiza kukumbuka baadhi ya misiba ikiwa ndani yake kuna mawaidha, mazingatio na kulainisha nyoyo; kwani kukumbuka kifo cha Mtume (S.A.W) humfanya mtu aone misiba mingine kuwa midogo. Imepokewa kutoka kwa Abdullah bin Abbas (R.A) kwamba Mtume (S.A.W) amesema: “Anapopatwa mmoja wenu na msiba, basi akumbuke msiba wake kwa kunipoteza mimi, kwani huo ni miongoni mwa misiba mikubwa.[10]”

Tatu: Kukatazwa kuhuisha huzuni kunakusudiwa pale kunapopelekea kupinga kudura ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; ama ikiwa kunaambatana na kukubali, kusubiri na kutaraji thawabu, basi mwenye kufanya hivyo hulipwa thawabu na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Imepokewa kutoka kwa Fatima bint Al-Husayn, kutoka kwa baba yake, kwamba Mtume (S.A.W) amesema: “Anayepatwa na msiba, kisha akaukumbuka msiba wake na akasema ‘Inna lillahi wa inna ilayhi raji‘un[11]’ hata kama umepita muda mrefu, Mwenyezi Mungu humwandikia ujira kama ule wa siku aliyopatwa nao.”[12].

Nne: Mtume (S.A.W) alizuru makaburi katika baadhi ya siku za ushindi, nazo ni siku za furaha na bashasha; imepokewa kwamba alizuru kaburi la mama yake Bi Amina bint Wahb R.A alipokuwa akirudi kutoka vita vya Tabuk. Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas R.A: “Mtume (S.A.W) aliporudi kutoka vita vya Tabuk na akafanya Umra, aliposhuka katika mlima wa ‘Usfan aliwaamuru Maswahaba wake wabaki mpaka atakaporudi kwao; akaenda akasimama kwenye kaburi la mama yake na akamwomba Mola wake kwa muda mrefu …”[13].

Tano: Siku za Idi ni wakati wa watu kukutana na kutembeleana; na jambo linalomfurahisha zaidi mtu ni kukutana na anayempenda na iwapo ampedae amefariki, basi mahali alipozikwa na kaburi lake ndiko mahali pa kumzuru na kumpa salamu.

Sita: Ilikuwa katika Sunna yake (S.A.W) kwenda kuswali Idi kwa njia moja na kurudi kwa njia nyingine; na wanazuoni wamefasiri miongoni mwa sababu za kufanya hivyo kuwa ni kuzuru makaburi ya jamaa zake na kuwaombea watu wa makaburini[14]. Imepokewa kutoka kwa Ibn Umar R.A: “Mtume (S.A.W) alikuwa akichukua njia moja siku ya Idi kisha akirudi kwa njia nyingine.”[15]

Saba: Imethibiti kwamba aliswali Idi mbili katika Baqii, nayo ni makaburi ya Madina; lau angechukia kwenda makaburini siku za Idi, angelichagua mahali pengine pa kuswali badala ya eneo lililo karibu na makaburi[16]. Imepokewa kutoka kwa Al-Bara bin Azib R.A amesema: “Mtume (S.A.W)  alitoka siku ya Adh-ha kuelekea Baqii, akaswali rakaa mbili, kisha akatuelekea kwa uso wake na kusema: ‘Hakika ibada yetu ya kwanza leo ni kuanza kwa swala, kisha turudi tukachinje; atakayefanya hivyo amefuata Sunna yetu, na atakayechinja kabla ya hapo basi hiyo ni nyama aliyoiwahisha kwa watu wake, si katika ibada (siyo sehemu ya Ibada) kwa chochote, (amepokea Al Imam Al Bohkariy”

Ama kuhusu mwanamke mwenye hedhi kuzuru makaburi: Hakuna katazo lolote katika hilo; kwa kuwa makaburi si kama misikiti. Inafaa kisharia kwake kutoka kwenda kuyazuru ikiwa ameshikamana na hijabu yake, kwa sharti asifanye lolote katika matendo ya kijahili kama kuomboleza, kujipiga na kutamka maneno yasiyokubalika na sharia tukufu.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Kuzuru makaburi ni jambo linalopendekezwa kisharia katika nyakati zote, na ubora wake huongezeka katika siku zenye baraka ambazo mtu hutafuta ziada ya thawabu na ujira kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, zikiwemo siku za Idi mbili; kwa kuwa ndani yake kuna kuhisi maana za kuendeleza uhusiano na wema, na kuwaombea rehema na msamaha waliokufa miongoni mwa jamaa na ndugu.

Anayezuru makaburi anapaswa kuepuka kufanya jambo lolote linalomghadhibisha Mwenyezi Mungu Mtukufu kama vile kuomboleza na kutamka maneno yanayoonesha kupinga kudura ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Inajuzu kisharia kwa mwanamke mwenye hedhi kwenda kuzuru makaburi ikiwa ameshikamana na hijabu yake, kwa sharti asifanye lolote katika matendo ya kijahili kama kuomboleza, kujipiga, na kutamka maneno yasiyokubaliwa na sheria tukufu.

 

[1] Ibn Majah.

[2] Ibn Majah.

[3] "AlNawah" Ni kumlilia mauti kwa sauti kubwa.

[4] “Sharh Mukhtasar Khalil” cha Al-Kharshi (2/135) na “Ash-Sharh al-Kabir li Mukhtasar Khalil” cha Ad-Dardir (1/422).

[5] “Radd al-Muhtar ‘ala ad-Durr al-Mukhtar” la Ibn ‘Abidin (2/242).

[6] “Imepokewa na At-Tabarani katika ‘Al-Mu‘jam al-Awsat’ (6/175).”

[7] Ni mwanzo wa mwaka wa Hijria.

[8] “Imepokewa na ‘Abdur-Razzaq katika ‘Al-Musannaf’ wake (3/573).”

[9] “Imepokewa na Ibn Shabbah katika ‘Taarikh al-Madina’ (1/119).”

[10] “Imepokewa na Al-Bayhaqi katika ‘Shu‘ab al-Iman’ (12/424).”

[11] yaani alisema, ‘Bila shaka sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwa Yeye tutarudi"

[12] AmepokeaIbn Majah.

[13] Imepokewa na At-Tabarani katika ‘Al-Mu‘jam al-Kabir’ (11/374).

[14] “Al-‘Aziz Sharh al-Wajiz” cha Ar-Rafi‘i (2/365), “Al-Kawakib ad-Darari fi Sharh Sahih al-Bukhari” la Al-Kurmani (6/86), “An-Najm al-Wahhaj fi Sharh al-Minhaj” cha Ad-Dimiri (2/547), na “Al-Lami‘ as-Sabih bi Sharh al-Jami‘ as-Sahih” cha Al-Barmawi (4/385).

[15] Amepokea Ibn Daudi.

[16] “Fath al-Bari” la Ibn Hajar (2/473) na “Umdat al-Qari” la Al-‘Ayni (6/306).

Share this:

Related Fatwas