Hukumu ya kutazama filamu za ngono ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya kutazama filamu za ngono ( ponografia) na jinsi ya kujikwamua kuepukana nazo

Question

Ni ipi hukumu ya kutazama filamu za ngono (ponografia) na namna gani ya kujikwamua kuepukana nazo?

Answer

Kutazama filamu hizo ni jambo lililoharamishwa kisharia, na ni njia ya kuingia katika zina, jambo ambalo lina hatari kubwa kwa ustawi wa familia, kwani linaweza kusababisha mtu mmoja wa wanandoa kutokuwa na hamu ya mwingine na kubaki tu kutazama filamu hizo mbaya, na ni jambo ambalo mwisho wake linaweza kufikia talaka.

Ama kuhusu wanandoa wote kutazama filamu hizo ni jambo lililoharamishwa zaidi na ni dhambi kubwa; kwa sababu hivyo ni kubadilisha kile kibaya ambacho Mwenyezi Mungu Mtukufu amekiharamisha kuacha kizuri ambacho Mwenyezi Mungu amekihalalisha.

Na ni wajibu kwa anayefanya dhambi ya kutazama filamu hizo kutubu  mara moja  kwa Mwenyezi Mungu, na ajutie kwa tendo hilo, na awe na nia ya kutorudia tena kutazama yaliyoharamishwa kabisa.

Maelezo

Mwenyezi Mungu Mtukufu ameweka ndoa kwa ajili ya kujikinga na kuhifadhi macho na tupu kujiepusha na kuingia katika yale aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu Mtukufu; Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na ambao wanazilinda tupu zao, Isipo kuwa kwa wake zao au kwa iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa. Lakini anaye taka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka.} [Al-Mu’minun:5–7].

Na sheria tukufu imefanya tendo la kustarehe na kutosheleza haja ya kijinsia liwe kwa njia ya muingiliano kati ya wanandoa, na imelihusisha katika uhusiano huo pekee, na ikaharamisha njia au namna yoyote isiyo ya ndoa. Imepokewa kutoka kwa Abdullah bin Masud RA kwamba Mtume (S.A.W)  amesema: “Enyi vijana, yeyote miongoni mwenu mwenye uwezo[1] wa kuoa basi na aoe; kwani hilo linainamisha zaidi macho na linahifadhi zaidi tupu. Na asiyeweza, basi na afunge, kwani hiyo ni kinga kwake[2].”[3]

Hadithi hii inaonyesha kwamba ndoa ndiyo njia pekee ya halali iliyoruhusika kisharia ya kustarehe bila ya kujihusisha na njia nyengine za haramu.

Uislamu umesisitiza heshima ya binadamu na hadhi yake, kwa hivyo Mwenyezi Mungu amekataza zinaa na kila kinachoweza kupelekea hilo; akasema: {Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya } [Al-Isra: 32].

Kutazama filamu hizo ni jambo lililoharamishwa kisharia; kwani ni njia ya kuingia katika zinaa, na linapelekea madhara kadhaa kama:

Kustahiki kuwa na makosa na kupata dhambi kwa kutazama filamu zinazoonesha uchi na kuangalia sehemu za siri, yote haya ni miongoni mwa maovu yaliyoharamishwa na sheria. Amesema Mwenyezi Mungu: {Sema: Mola Mlezi wangu ameharimisha mambo machafu ya dhaahiri na ya siri, na dhambi, na uasi bila ya haki, na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na asicho kiletea uthibitisho, na kumzulia Mwenyezi Mungu msiyo yajua } [Al-A‘raf: 33].

Kutazama filamu hizo ni ukiukaji wa heshima ya mwili wa mtu ambayo sheria imeamuru kuhifadhi. Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas (R.A): Mtume (S.A.W)  aliwahutubia watu siku ya Nahr[4] (kuchinja): “Enyie watu! Ni siku gani hii? Wakasema: Siku takatifu. akasema: Ni mji gani huu? Wakasema: Mji mtakatifu. Akasema: Ni mwezi gani huu? Wakasema: Mwezi mtukufu. Hivyo hakika damu zenu, mali zenu na heshima zenu[5] ni takatifu kama siku yenu hii, mji wenu huu, na mwezi wenu huu.” Akarudiarudia mara kadhaa, Kisha akainua kichwa chake akasema: ewe Moa wangu je nifikisha? Ewe Mola wangu je, nimefikisha?[6]

Sheria imeonya vikali wenye kutazama filamu hizi kwa makemeo makali, kwani ni katakazo kubwa kumwangalia mwanamke kwa matamanio au hata kumgusa kwa matamanio. Imepokewa kutoka kwa Maqal bin Yasaar R.A kwamba Mtume (S.A.W)  amesema: “Mmoja wenu Kumchomwa kwenye kichwa kwa sindano ya chuma ni bora kuliko kumgusa mwanamke ambaye si halali yake.”[7]  Na kutoka kwa Abu Umamah RA, kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) amesema: “...Na ni afadhali kwa mwanaume kuchanganyika na nguruwe aliyejichafuka kwa matope  au uchafu unukao[8] kuliko kugonganisha bega lake na bega la mwanamke ambaye si halali kwake.”[9]

Kutazama filamu hizo ni aina ya zinaa; imepokewa kutoka kwa Abu Huraira (R.A) kwamba Mtume (S.A.W)  amesema: “Hakika macho mawili yanazini na ulimi unazini na mikono miwili inazini na miguu inazini na sehemu za siri zinathibitisha au kukanusha hilo.”[10]

Kutazama filamu hizo kwa wanandoa ni jambo lililokatazwa zaidi, kwa kuwa kunaweza kuharibu ustawi wa familia, kupelekea mmoja wa wanandoa kutokuwa na hamu na mwingine, na kubaki tu kutazama filamu hizo mbaya, jambo linaloweza kusababisha talaka. Kutoka kwa Abu Sa‘id Al-Khudri (R.A) kuhusu safari ya Isra ana Miiraj kwamba Mtume (S.A.W)  Amesema: “…na kuna watu wanafakamia nyama iliyooza yenye kunuka na kuacha nyama iliyo safi, nikasema : hao ni akina nani ewe Jibril? akasema: Hawa ni wazinzi, wanaoacha kilicho halali  na kufuata kilicho haramu…”[11].

Ama kuhusu namna ya kujiepusha na kuagalia filamu hizo ni kwa namna ifuatayo;

Ni lazima atubie mara moja kutokana na kuangalia filamu hizo zilizoharamishwa. Pia ajutie juu ya mapungufu yake na kuvunja kwake mipaka juu ya haki ya Mwenyezi Mungu. Aidha, awe na maazimio kuwa hatorudia tena kuangalia mfano wa mambo kama hayo yaliyoharamishwa.

Kufuata maelekezo ya Sharia ya kuinamisha macho na kuacha haramu. Akasema Mwenyezi Mungu: {Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao. Hili ni takaso bora kwao… Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika.} [An-Nur: 30-31].

Kuwa na marafiki wema ambao watamsaidia kwenye msimamo wa dini na kukumbuka daima kwamba Mwenyezi Mungu anaona yote ayatendayo, hivyo mtu ataona haya ya kuasi hali ya kujua kuwa anaonekana.

Kufunga kwa wingi, funga za sunna kama ilivyokuja katika hadithi: {..na asiyeweza basi ajilazimu kufunga, kwani ni kinga}

Kutafuta msaada wa wataalamu wa afya kwa ajili ya kutafuta njia ya kujiponya kuepukana na gonjwa hili.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Kutazama filamu za ngono ni haramu kisharia na ni njia ya kuingia kwenye zina.

Kuangalia filamu hizo ni hatari kwa ustawi wa familia, kwani, huweza kusababisha mmoja wa wanandoa  kutokuwa na hamu/tamaa ya mwingine na kubaki tu kutazama filamu hizo mbaya, na hali inaweza kupelekea talaka.

Kutazama filamu hizo kwa wanandoa ni kosa kubwa na ni dhambi kubwa zaidi; kwani kufanya hivyo ni kubadilisha kibaya ambacho Mwenyezi Mungu amekiharamisha na kuacha kizuri ambacho Mwenyezi Mungu amekihalalisha.

Ni wajibu kwa mtu aliyejihusisha na dhambi hii atubie mara moja kwa Mwenyezi Mungu, pia ajutie juu ya kosa hilo, na akusudie kuwa kutorudia tena kuangalia filamu zilizokatazwa.

 

[1] Uwezo wa kimwili na kifedha juu ya ndoa.

[2] Ni kujikinga na kujilinda kwa mtu asije akaangukia katika uzinifu.

[3] Imepokewa na Imam Muslim.

[4] Siku ya Nahr”: ni siku ya kumi ya mwezi wa Dhul-Hijjah.

[5] Yenye utukufu usiopasa kukiukwa au kuvunjiwa heshima

[6] Mepokea Imam Bukhari.

[7] Imepokewa na At-Tabarani katika «Al-Mu‘jam Al-Kabir» (20/ 211).

[8] Al-Hama’ah”: ni tope jeusi lenye harufu mbaya.

[9] Imepokewa na At-Tabarani katika «Al-Mu‘jam Al-Kabir» (8/ 205).

[10] Amepokea Ahmad katika Al Musnad (15/191).

[11] Musnad Al harith. (1/172.)

Share this:

Related Fatwas