Kushindwa kutekeleza Nadhiri

Egypt's Dar Al-Ifta

Kushindwa kutekeleza Nadhiri

Question

Ni ipi hukumu ya aliyeweka nadhiri na akashindwa kuitekeleza?

Answer

Ni wajibu kwa Muislamu kutekeleza nadhiri aliyojiwajibishia mwenyewe ilimradi nadhiri hiyo iwe katika kumtii Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ama ikiwa mtu ameweka nadhiri ya kufanya maasi, basi hukumu yake ni kutotimiza nadhiri hiyo; kwa sababu kutenda maasi ni jambo haramu kisheria, na ni wajibu kwake wakati huo kutoa kafara ya kiapo. Na ikiwa mtu hawezi kutimiza nadhiri, au ameweka nadhiri bila kuitaja (bila kuainisha); basi ni wajibu kwake wakati huo kutoa kafara ya kiapo, nayo ni kama ifuatavyo:

Kwanza: Ni wajibu kwa mtu kulisha masikini kumi au kuwavisha masikini kumi. Kiasi cha chakula kwa masikini mmoja ni takriban (3.25) kilogramu ya chakula kilichozoeleka cha watu wa nchi hiyo -kama ngano au mchele kwa mfano-. Inajuzu pia kutoa thamani ya chakula au vazi kwa masikini mwenye kuhitaji.

Pili: Asiyeweza kutoa kafara kwa sura ya chakula au mavazi kwa mafakiri, ni wajibu kwake kufunga siku tatu.

Maelezo

Imethibitishwa kisharia wajibu wa kutimiza nadhiri ikiwa ni katika kumtii Mwenyezi Mungu Mtukufu; Mwenyezi Mungu anasema: {na waondoe nadhiri zao} [Al-Hajj: 29], na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wanatimiza ahadi,na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea sana} [Al-Insan: 7]. Na imepokelewa kutoka kwa Mama wa Waumini Bibi Aisha (R.A), kutoka kwa Mtume (S.A.W) amesema: ((Mwenye kuweka nadhiri kuwa atamtii Mwenyezi Mungu, basi amtii, na mwenye kuweka nadhiri kuwa atamuasi, basi asimuasi))[1]. Kunatakikana kwa Muislamu asijiwajibishie nadhiri ambayo hana uwezo wa kuitekeleza, kwa sababu kuibebesha nafsi zaidi ya uwezo wake ni jambo linalochukiza kisheria; Mwenyezi Mungu anasema: {Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyho. Faida ya iliyo yachuma ni yake, na khasara ya iliyo yachuma ni juu yake pia. (Ombeni:)Mola wetu Mlezi! Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Mola wetu Mlezi! Usitubebeshe mzigo kama ulio wabebesha wale walio kuwa kabla yetu. Mola wetu Mlezi Usitutwike tusiyo yaweza, na utusamehe, na utughufirie, na uturehemu. Wewe ndiye Mlinzi wetu. Basi tupe ushindi tuwashinde kaumu ya makafiri.} [Al-Baqarah: 286].

Hapa ni lazima kutaja baadhi ya hukumu za kisharia zinazohusiana na nadhiri, nazo ni kama ifuatavyo:

Kwanza: Ikiwa mtu ameweka nadhiri na asitekeleze, basi hukumu yake iko kati ya mambo mawili:

1- Atekeleze nadhiri hiyo ikiwa ana uwezo wa kufanya hivyo.

2- Ikiwa hana uwezo wa kutekeleza nadhiri hiyo, basi ni wajibu kwake wakati huo kutoa kafara ya kiapo.

Pili: Ikiwa mtu ameweka nadhiri ya kutenda maasi, kama aliyeweka nadhiri ya kunywa pombe, basi hukumu yake ni kutotimiza nadhiri hiyo; kwa sababu kutenda maasi ni jambo la haramu kisharia, na ni wajibu kwake wakati huo kutoa kafara ya kiapo.

Tatu: Ikiwa mtu ameweka nadhiri bila kuitaja na bila kuainisha nadhiri hiyo ni ya nini, kama kusema: "Lillahi alayya (Kwa ajili ya Mungu ni juu yangu) nadhiri ikiwa mwanangu atafaulu mtihani" na mfano wa hayo, basi ni wajibu kwake wakati huo kutoa kaffara ya kiapo; kwa sababu hakuainisha nadhiri hiyo.

Dalili ya yote yaliyotajwa hapo juu: ni Hadithi ya Abdullah Ibn Abbas (R.A), kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) amesema: ((Mwenye kuweka nadhiri asiyoitaja, basi kafara yake ni kafara ya kiapo, na mwenye kuweka nadhiri katika maasi, basi kafara yake ni kafara ya kiapo, na mwenye kuweka nadhiri asiyoiweza, basi kafara yake ni kafara ya kiapo, na mwenye kuweka nadhiri   aliyoiweza, basi aitekeleze))[2].

Kaffara ya nadhiri kama ilivyo katika Hadithi ni kama kafara ya kiapo, nayo ni ile iliyotajwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Mwenyezi Mungu hatakushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini atakushikeni kwa mnavyo apa kweli kweli kwa makusudio. Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnacho walisha ahali zenu, au kuwavisha, au kumkomboa mtumwa. Asiye pata hayo, basi afunge siku tatu. Hii ndiyo kafara ya viapo vyenu mnapo apa. Na hifadhini yamini zenu. Namna hivyo Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake ili mpate kushukuru.} [Al-Ma'idah: 89].

Inafahamika kutokana na Aya hiyo kuwa kafara ya kiapo ni kama ifuatavyo:

Kwanza: Ni wajibu kwa mtu kulisha masikini kumi au kuwavisha masikini kumi. Kadiri ya chakula kwa masikini mmoja ni takriban (3.25) kilogramu ya chakula kilichozoeleka cha watu wa nchi hiyo -kama ngano au mchele kwa mfano-. Inajuzu pia kutoa thamani ya chakula au vazi kwa fakiri.

Pili: Asiyeweza kutoa kafara kwa sura ya chakula au mavazi kwa mafakiri, ni wajibu kwake kufunga siku tatu.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Wajibu wa kutimiza nadhiri ilimradi iwe katika kumtii Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Ikiwa mtu ameweka nadhiri ya kufanya maasi, basi hukumu yake ni kutotimiza nadhiri hiyo; kwa sababu kutenda maasi ni jambo haramu kisharia, na ni wajibu kwake kutoa kafara ya kiapo.

Ikiwa mtu hawezi kutimiza nadhiri, ni wajibu kwake kutoa kafara ya kiapo.

Ikiwa mtu ameweka nadhiri asiyoitaja, ni wajibu kwake kutoa kaffara ya kiapo.

 

[1]  Imepokelewa kutoka kwa Al-Bukhari

[2]  Imepokelewa kutoka kwa Abu Daud.

Share this:

Related Fatwas