Swala ya Tasbihi
Question
Ni ipi hukumu ya Swala ya Tasbihi? Na ni upi usahihi wa Hadithi yake? Kwani baadhi ya watu wanadai kuwa ni uzushi na upotofu, na kwamba Hadithi yake ni ya uongo na ya kutungwa, basi ni nini hukumu ya Sharia katika hilo?
Answer
Swala ya Tasbihi imethibiti na ni ya kisharia (imehalalishwa), kwani imepokewa katika vitabu vya Sunna kwa njia mbalimbali zinazokamilishana na kuimarishana. Na rai yenye nguvu kwa Wanazuoni wa Hadithi ni kwamba Hadithi za Swala ya Tasbihi ni sahihi, si kama wanavyodai baadhi kuwa ni za kubuniwa na za uongo.
Hivyo, kutofautiana kwa Swala ya Tasbihi na namna za Swala za Faradhi hakumaanishi kuwa haijathibiti. Kwani zipo baadhi ya Swala zilizothibiti kisharia ambazo zinatofautiana katika namna yake na Swala za Faradhi, kama vile Swala ya Idi mbili na Swala ya kupatwa kwa jua na mwezi.
Haifai kabisa kuikuhumu Swala ya Tasbihi kuwa ni uzushi na upotofu, hasa kwa vile imethibitishwa usahihi wa Hadithi zilizokuja kwayo, na wameitekeleza Swala ya Tasbihi idadi kubwa ya wema waliotangulia (Salaf), na jamhuri ya mafakihi wamekubaliana juu ya uhalali wa swala ya Tasbihi, na haikunukuliwa kutoka kwa yeyote miongoni mwao kauli ya kuiharamisha au kuibatilisha.
Maelezo
Imethibitishwa kisharia kwamba Swala za Sunna ni miongoni mwa matendo yanayopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu Mtukufu, imepokelewa kutoka kwa Abu Hurairah (R.A) amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W): ((Mwenyezi Mungu amesema: Mwenye kumfanyia uadui walii wangu basi nimemtangazia vita, na mja wangu hajanikurubia kwa kitu nikipendacho zaidi kuliko kile nilichomfaradhishia, na mja wangu haachi kunikurubia kwa Sunna mpaka nimpende)) . [1]Na miongoni mwa Sunna ambazo mja hujikurubisha kwazo kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni swala ya Tasbihi; na namna yake imekuja katika Hadithi za Mtume; imepokelewa kutoka kwa Abdullah Ibn Abbas (R.A), kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) alimwambia Al-Abbas Ibn Abdul-Muttalib (R.A): ((Ewe Abbas, ewe ami yangu, je, nikupe (elimu)? Je, nikuzawadie? Je, nikupandishe daraja? Je, nikufanyie mambo kumi, ukiyatenda Mwenyezi Mungu atakusamehe dhambi zako, za mwanzo na za mwisho, za zamani na mpya, za kukosea na za makusudi, ndogo na kubwa, za siri na za dhahiri, mambo kumi:
Uswali rakaa nne, usome katika kila rakaa Fatiha ya Kitabu na Sura, utakapomaliza kusoma katika rakaa ya kwanza nawe umesimama, utasema: Subhanallah, wal-Hamdulillah, wala ilaha illa Allah, wallahu Akbar, mara kumi na tano, kisha utarukuu, nawe utasema ukiwa umerukuu mara kumi, kisha utainua kichwa chako kutoka kwenye rukuu, utasema mara kumi, kisha utaporomoka kusujudu, utasema ukiwa umesujudu mara kumi, kisha utainua kichwa chako kutoka kwenye kusujudu utasema mara kumi, kisha utasujudu, utasema mara kumi, kisha utainua kichwa chako (kikao cha mapumziko), utasema mara kumi, hizo ni sabini na tano katika kila rakaa, utafanya hivyo katika rakaa nne. Ukiweza kuiswali kila siku mara moja, basi iswali, usipoweza basi kila Ijumaa mara moja, usipoweza basi kila mwezi mara moja, usipoweza basi kila mwaka mara moja, usipoweza basi katika umri wako mara moja))[2].
Wanazuoni wametofautiana kuhusu uhalali wa kuitekeleza Swala ya Tasbihi katika rai kadhaa; kwa sababu ya tofauti yao juu ya usahihi wa Hadithi zilizokuja katika kuitaja, na hiyo ni kama ifuatavyo:
Rai ya Kwanza: kutokuwepo na uhalali wa Swala ya Tasbihi na kwamba ni uzushi na upotofu; kwa sababu Hadithi zilizokuja katika kuitaja ni za kutungwa na hazikuthibitishwa katika Hadithi sahihi za Mtume.
Rai ya Pili: Inaona uhalali wa Swala ya Tasbihi; kwa sababu Hadithi zilizokuja katika kuitaja ni dhaifu[3], na imethibitishwa kuwa kufanyia kazi Hadithi dhaifu katika fadhila za matendo ni jambo linalojuzu kisharia; kwa hivyo kuitekeleza Swala ya Tasbihi haina ubaya kisharia.
Rai ya Tatu: Inaona kupendekezwa (mustahabb) kwa Swala ya Tasbihi; kwa sababu Hadithi zilizokuja katika kuitaja ni sahihi na zimethibitishwa, na imethibitishwa kuwa kila kilichosihi kutoka kwa Mtume (S.A.W) ni jambo linalopendekezwa kisharia na hupatikana thawabu kwa kulitenda.
Baada ya kuwasilisha rai hizo tunasema: Hakika rai yenye nguvu ni ya tatu na ya mwisho, na hiyo ndiyo inayofuatwa na Ofisi ya kutoa Fatwa ya Misri (Dar Al-Ifta ya Misri), na hiyo ni kwa sababu zifuatazo:
Anayedai kuwa Swala ya Tasbihi ni uzushi na upotofu, na kwamba Hadithi yake ni ya uongo na ya kutungwa, Wanazuoni wamejibu na kubainisha kosa lake; kwani Hadithi ya Swala ya Tasbihi imepokelewa kupitia njia nyingi, na kutoka kwa zaidi ya Maswahaba kumi, na kutoka kwa idadi kadhaa ya Tabi'ina, na wameitoa Hadithi yake Maimamu wa Uislamu na wahifadhi wake. Al-Hafidh Ibn Hajar amesema kuhusu Hadithi ya Swala ya Tasbihi: «Na hakika Ibn Al-Jawzi amekosea kwa kuitaja miongoni mwa Hadithi za kutungwa»[4].
Wamesahihisha Hadithi ya Swala ya Tasbihi na kuifanya kuwa ni "hasan" na kuhimiza kuifanyia kazi kundi la mahafidhi, miongoni mwao ni: Amir wa waumini katika Hadithi Ishaq Ibn Rahwayh, na Imamu wa Ahlu Al-Sunna Ahmad Ibn Hanbal, na Abu Dawood Sulayman Ibn Al-Ash'ath Al-Sijistani, na Ibn Khuzaymah, na Abu Ali Ibn al-Sakan, na Abu Hafs Umar Ibn Shahin, na Al-Daraqutni, na Ibn Mandah, na Al-Bayhaqi, na Al-Khatib Al-Baghdadi, na Muhyi al-Sunnah al-Baghawi, na Abu Sa'd al-Sam'ani, na Abu Musa al-Madini ambaye alikusanya njia zake katika kijitabu alichokiita: «Sahihisho la Swala ya Tasbihi», na wahifadhi Ibn Nasiruddin Al-Dimashqi, na Ibn Hajar Al-Asqalani, na Al-Jalal Al-Suyuti, na wengineo wengi.
Kauli ya uhalali wa Swala ya Tasbihi na kupendekezwa kwake ndiyo waliyoizingatia jamhuri ya Wanazuoni wa zamani na wa sasa, na ndivyo ilivyo kwa jamhuri ya Wanachuoni wa Fiqhi wa Madhehebu manne[5] yanayofuatwa[6].
Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:
Swala ya Tasbihi imethibitishwa na ni halali, hakika imepokelewa katika vitabu vya Sunna kupitia njia kadhaa zinazotiana nguvu.
Rai yenye nguvu kwa Wanazuoni wa Hadithi ni kwamba Hadithi za Swala ya Tasbihi ni sahihi, na si kama walivyodai baadhi ya watu kuwa ni za kutungwa na za uongo.
Kwenda tofauti tu kwa Swala ya Tasbihi kutokana na mfumo wa Swala za Fardhi hakumaanishi kuwa haikuthibitishwa, kwani kuna Swala za kisharia zilizothibitishwa ambazo zinakhalifu mifumo yake swala za fardhi; kama swala ya Eid mbili na swala ya kupatwa kwa jua na mwezi.
Haifai kabisa kuihukumu Swala ya Tasbihi kuwa ni uzushi na upotofu, hasa kwa vile imethibitishwa usahihi wa Hadithi zilizokuja kwayo, na wameitekeleza Swala ya Tasbihi idadi kubwa ya Salaf (R.A).
Jamhuri ya Wanachuoni wa Fiqhi wamekubaliana juu ya uhalali wa Swala ya Tasbihi, na haikunukuliwa kutoka kwa yeyote miongoni mwao kauli ya kuiharamisha au kuibatilisha.
[1] Imepokelewa na Al-Bukhari.
[2] Imepokelewa na Abu Daud.
[3] Hadithi dhaifu": Maana yake ni hadithi zilizopoteza sharti mojawapo miongoni mwa masharti ya kusihi (usahihi) kwa hadithi zilizopokelewa kutoka kwa Nabii (S.A.W).
[4] "Al-La’ali al-Masnu’ah fi al-Ahadith al-Maudhu’ah" cha As-Suyuti (2/ 38- 39).
[5] Madhehebu manne": Ni madhehebu ya Maimamu wanne ambayo yamekubaliwa kufanyiwa kazi, nayo ni: (Madhehebu ya Imamu Abu Hanifa, Madhehebu ya Imamu Malik, Madhehebu ya Imamu Ash-Shafi'i, na Madhehebu ya Imamu Ahmad bin Hanbal).
[6] Badai' as-Sanai'" cha Al-Kasani (1/ 216), na "Manhaj at-Tawdihi li Masaili Salatit-Tasbihi" cha Al-Allamah Al-Hashimi (uk: 51- 52), na "Al-Mughni" cha Ibn Qudamah Al-Hanbali (2/ 98).
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
