Kuvaa "Wigi" (Nywele za Bandia)
Question
Je, inajuzu kuvaa wigi?
Answer
Imethibitishwa kisharia kuwa ni haramu kuunga nywele ikiwa ni kwa madhumuni ya hadaa, udanganyifu, au upotoshaji. Ama kwa mwanamke aliyeolewa, inajuzu kwake kuunga nywele zake kwa idhini ya mumewe kwa ajili ya kujipamba kwake. Hivyo, kuvaa wigi kwa sharti la kutokuwepo madhara wala udanganyifu kunajuzu kisharia na hakuna ubaya ndani yake; kwa sababu hilo si katika uungaji nywele uliokatazwa kisharia.
Ama kuhusu mwanadamu kujitolea sehemu ya nywele za kichwa chake kwa ajili ya hospitali ya saratani ya watoto; kwa lengo la kutengeneza "wigi" litakalovaliwa na watoto hao baada ya matibabu ya kemikali (chemotherapy) kusababisha nywele zao kunyonyoka, hilo ni jambo linalojuzu kisharia, bali ni jambo linalopendekezwa (mustahabb) na mtendaji wake hupata thawabu kwa sababu ya kuingiza furaha katika nyoyo za wagonjwa hao.
Maelezo
Imethibitishwa kuwa kujipamba na kuvaa pambo ni miongoni mwa mambo yanayopendekezwa kisharia; Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: {Enyi wanaadamu! Chukueni pambo lenu kwenye kila pahala wakati wa ibada, na kuleni, na kunyweni na wala msifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye hapendi wanao fanya israfu. Sema: Ni nani aliye harimisha pambo la Mwenyezi Mungu alilo watolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki. Sema hivyo ni kwa walio amini katika uhai wa duniani, na Siku ya Kiyama vitakuwa vyao wao tu. Namna hivi tunazieleza Ishara kwa watu wanao jua (32)} [Al-A’raf: 31-32].
Hivyo, mtu anayetaka kujipamba kwa kuvaa vitu vizuri vinavyofanya muonekano wake uwe mzuri, kitendo chake ni halali, bali kinapendekezwa kisharia. Imepokelewa kutoka kwa Abdullah Ibn Mas'ud (R.A): ((Kwamba mtu mmoja alimuuliza Mtume (S.A.W) kuhusu mtu anayependa nguo yake iwe nzuri na viatu vyake viwe vizuri, Mtume (S.A.W) akasema: Hakika Mwenyezi Mungu ni Mzuri na anapenda uzuri)) [1].
Lakini kuna aina ya mapambo ambayo Sharia tukufu haikuiruhusu isipokuwa katika baadhi ya hali; kwa sababu ndani yake kuna udanganyifu na hadaa, na miongoni mwa aina hizo ni kile kinachoitwa "kuunga nywele".
Hukumu ya kuunga nywele ni kama ifuatavyo:
Kwanza: Sharia tukufu imekataza mwanadamu kuunga nywele zake kwa nywele nyingine; kwa sababu ndani yake kuna aina ya hadaa na udanganyifu, na Sharia imemfanya mtendaji wa jambo hilo kuwa ni mwenye dhambi na anayestahili laana na kuwa mbali katika rehema ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; imepokelewa kutoka kwa Abu Hurairah (R.A), kutoka kwa Mtume (S.A.W) amesema: ((Mwenyezi Mungu amemlaani mwenye kuunga nywele na mwenye kuungwa, na mwenye kuchora tatuu na mwenye kuchorwa)) imepokelewa na Muslim.
Hadithi tukufu inaonesha uharamu wa kuunga nywele; kwani laana haitokei isipokuwa kwa kitendo cha haramu.
Pili: Ikiwa kuunga nywele ni kwa madhumuni ya udanganyifu, hadaa, na hila, basi ni haramu ikiwa nywele hizo zimechukuliwa kutoka kwa mwanadamu mwingine, au kutoka kwa asiyekuwa mwanadamu kama vile sufi au baadhi ya nyuzi au hariri na vitu vingine vinavyofanana na nywele.
Tatu: Uharamu wa kuunga nywele ikiwa ni kwa madhumuni ya udanganyifu na hadaa unawahusu wanaume na wanawake kwa usawa.
Nne: Inajuzu kisharia kwa mwanamke aliyeolewa kuunga nywele zake kwa idhini ya mumewe ili kujipamba kwake, kwa sharti kwamba nywele hizo zilizoungwa ziwe tohara ikiwa ni za asiyekuwa mwanadamu.
Baada ya ufafanuzi huu, tunaweza kusema:
Kauli yenye nguvu (Ar-Rajih) kwa Wanazuoni ni kwamba kuvaa wigi kunajuzu kisharia kwa mwanamume aliyeoa ili kujipamba kwa mkewe kama vile kuficha upara na mfano wa hayo, na vilevile mwanamke inajuzu kwake kulivaa kwa ajili ya kujipamba kwa mumewe; kwa sharti ya kutotokea udanganyifu au hadaa kwa kulivaa.
Sababu ya kuchagua maoni haya na kuyapa nguvu ni kama ifuatavyo:
Kwamba wigi ni kuweka nywele kichwani bila kuziunga, na wanazuoni wamethibitisha kuwa kuweka tu nywele kichwani bila kuziunga hakuhesabiki kuwa ni haramu, kama inavyojidhihirisha katika sura ya "wigi" inayojulikana sasa[2].
Hadithi za Mtume zinaonesha uharamu wa kuunga, na hakuna ndani yake kinachoonesha uharamu wa kuweka tu nywele kichwani.
Ruhusa inasisitizwa zaidi ikiwa mtumiaji wa "wigi" hana nywele kabisa; kama ilivyo hali ya wagonjwa wa saratani wanaotibiwa kwa kemikali, hasa watoto.
Ama kuhusu hukumu ya mtu kutoa nywele zake kwa ajili ya kutengeneza wigi kwa anayelihitaji miongoni mwa wagonjwa, hukumu yake ni:
Kwamba ni jambo linalojuzu kisharia na hakuna ubaya ndani yake, bali mtoaji anastahili thawabu na ujira kutoka kwa Mwenyezi Mungu ikiwa nia yake ni kuingiza furaha na bashasha kwa wagonjwa hao; kutoka kwa Abdullah Ibn Umar (R.A) ((Kwamba mtu mmoja alikuja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W), akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni watu gani wanaopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu? Na ni matendo gani yanayopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu? Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) akasema: Watu wanaopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu ni wenye manufaa zaidi kwa watu, na matendo yanayopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu ni furaha unayoingiza kwa Muislamu))[3].
Hivyo kujitolea kunachukuliwa kuwa ni katika kutoa kitu hali ya kuwa unakihitaji (Al-Ithar) nalo ni tabia tukufu inayohimizwa; na Mwenyezi Mungu Mtukufu amewasifu wale waliowapa ndugu zao kuliko nafsi zao; Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: {bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji.} [Al-Hashr: 9].
Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:
Ni haramu kisharia kuunga nywele ikiwa ni kwa madhumuni ya upotoshaji, udanganyifu, au hadaa.
Inajuzu kisharia kwa mwanamke aliyeolewa kuunga nywele zake kwa idhini ya mumewe ili kujipamba kwake.
Kuvaa wigi kwa sharti la kutokuwepo madhara wala udanganyifu kunajuzu kisharia na hakuna ubaya ndani yake; kwa sababu si katika uungaji uliokatazwa kisheria.
Si haramu kwa mwanadamu kutoa sehemu ya nywele za kichwa chake kwa ajili ya hospitali ya saratani ya watoto; kwa lengo la kutengeneza "wigi" litakalovaliwa na watoto hao, baada ya matibabu ya kemikali kusababisha nywele zao kunyonyoka.
[1] Imepokelewa na Muslim.
[2] "Sharhu Al-Bukhari" (9/ 172), na "Al-Fawakih ad-Dawani 'ala Risalati Ibn Abi Zayd al-Qayrawani" cha An-Nafrawi (2/ 314).
[3] Imepokelewa na At-Tabarani katika "Al-Mu'jam Al-Awsat" (6/ 139).
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
