Hukumu ya kumuozesha binti ambaye b...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya kumuozesha binti ambaye bado hajafika umri wa ndoa

Question

Ni ipi hukumu ya kumuozesha binti ambaye bado hajafika umri wa ndoa?

Answer

Uislamu umeweka Sharia ya ndoa na kuitukuza nafasi yake, kwani ndani yake kuna usafi na twahara; na Sharia tukufu imejalia uhusiano wa ndoa kujengeka juu ya mapenzi, huruma, na uwiano kati ya wanandoa. Na ili uhusiano wa ndoa ufanikiwe, Uislamu umeweka sharti la kulingana kati ya mume na mke. Wanazuoni wa Sharia wamebainisha kuwa kulingana huku kunatofautiana kulingana na hali, nyakati, sehemu, mila, na tamaduni mbalimbali. Umri unachukuliwa kuwa ni miongoni mwa mambo muhimu zaidi ya kulingana kati ya mume na mke, kama ilivyoamuliwa na walio wengi miongoni mwa Wanazuoni wa Fiqhi. Hivyo basi, kitendo cha baba au msimamizi (walii) kumuozesha binti mdogo (aliye chini ya umri wa kisharia) kwa kutumia vibaya mamlaka yake juu yake ni jambo la haramu kisharia. Miongoni mwa malengo ya ndoa ni kutosheleza matamanio na kuzaa, na ndoa ya binti mdogo inapingana na malengo hayo. Kumlazimisha binti mdogo kubeba majukumu ya maisha ya ndoa, na kumtwisha mzigo unaopita uwezo wake katika umri huu mdogo, kunahesabika kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa utoto wake. Vilevile, ndani yake kuna aina ya unyonyaji wa kijinsia na manufaa ya kimali kwa gharama ya heshima ya mwanamke na haki zake; na mambo haya yote yameharamishwa na Sharia tukufu na yanaadhibiwa na sheria za nchi.

Maelezo

Uislamu umeweka Sharia ya ndoa na kuitukuza nafasi yake, kwani ndani yake kuna usafi na twahara; na Sharia tukufu imejalia uhusiano wa ndoa kujengeka juu ya mapenzi, huruma, na uwiano kati ya wanandoa. Na ili uhusiano wa ndoa ufanikiwe, Uislamu umeweka sharti la kulingana kati ya wanandoa[1], na Wanazuoni wa Fiqhi wamebainisha kuwa kulingana huku kunatofautiana kulingana na hali, nyakati, sehemu, mila, na tamaduni mbalimbali. Umri unachukuliwa kuwa ni miongoni mwa mambo muhimu zaidi ya kulingana kati ya mume na mke kama ilivyoamuliwa na walio wengi miongoni mwa Wanazuoni wa Fiqhi.

Na kumeenea katika baadhi ya mazingira ya kijamii uozeshaji wa binti mdogo kwa namna inayokosa vigezo vya chini kabisa vya kulingana, bali hata utu wa mwanamke; ambapo baba au msimamizi wa mwanamke humuozesha binti mdogo kwa kutumia vibaya mamlaka yake juu yake, kwa hoja kwamba Uislamu umemhalalishia kumuozesha.

Wanazuoni wa Fiqhi wametofautiana kuhusu hukumu ya kumuozesha binti mdogo (aliye chini ya umri wa kisharia), kama ifuatavyo:

Kwanza: Baadhi ya Wanazuoni wameruhusu baba (na si mwingineyo) kumuozesha binti yake mdogo kwa mwanamume anayelingana naye (kafuu); na hiyo ni kwa sababu ya ukamilifu wa huruma yake, upendo wake kwake, na hofu yake juu yake[2]; kwani yeye humchagulia binti yake jambo lililo bora na lenye manufaa zaidi kwa mustakabali wa maisha yake. Ama ikiwa atakusudia kumuozesha kwa mtu asiyelingana naye, basi jambo hili halijuzu kisharia; bali hiyo itakuwa ni alama ya ufasiki wa msimamizi (walii) wake[3], na binti atakuwa na haki ya kuvunja ndoa hiyo.

Pili: Baadhi ya Wanazuoni wamekataza kumuozesha binti mdogo; iwe ni kumuozesha kwa mwanamume anayelingana naye au asiyelingana naye, na hiyo ni kwa sababu mbili ambazo ni:

1- Kwamba kanuni ya kisharia inaamua: «Kwamba hatua anazochukua msimamizi katika mali ya aliye chini ya umri wa kisharia imefungamana[4] na maslahi»; hivyo basi, kuzingatia maslahi katika ndoa ya binti mdogo ni jambo la kusisitizwa zaidi; kwani heshima ni kuu na tukufu zaidi kuliko mali. Na binti mdogo hajui kiasi cha kufaa kwa ndoa hii kwake au la, kwa hiyo ni katika maslahi aolewe atakapokuwa mkubwa na kubalehe ili awe na haki ya kuchagua[5].

2- Kwamba Sharia imeweka umri maalumu wa ndoa; kwani miongoni mwa malengo ya ndoa ni kutosheleza matamanio na kuzaa, na udogo wa umri unapingana na hilo. Hivyo basi, haijuzu kwa binti mdogo kuozeshwa kabla ya kufikia umri wa ndoa, na wakatoa ushahidi wa jambo hilo kwa kauli yake Aliyetukuka: {Na wafanyieni mtihani mayatima mpaka wafikie (umri wa) kuoa; mkiuona uongozi (mzuri) kwao, basi wapeni mali zao} [An-Nisa: 6]; kwani ingekuwa inajuzu kuozesha kabla ya kubalehe, basi ukomo huu usingekuwa na faida[6].

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Na baada ya ufafanuzi huu na kuwasilisha maoni hayo, maoni yenye nguvu yaliyochaguliwa na Ofisi ya kutoa Fatwa ya Misri ni uharamu wa kumuozesha binti mdogo (aliye chini ya umri wa kisharia), na hiyo ni kwa sababu kadhaa ambazo ni:

1- Miongoni mwa malengo ya ndoa ni kutosheleza matamanio na kuzaa, na ndoa ya binti mdogo inapingana na malengo hayo.

2- Kumlazimisha binti mdogo kubeba majukumu ya maisha ya ndoa na kumtwisha mzigo unaopita uwezo wake katika umri huu mdogo, kunahesabika kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa utoto wake. Vilevile, ndani yake muna aina ya unyonyaji wa kijinsia na manufaa ya kimali kwa gharama ya heshima ya mwanamke na haki zake; na mambo haya yote yameharamishwa na Sharia tukufu.

 

[1] «Kulingana katika ndoa (Kafa’ah)»: Ni usawa kati ya mume na mke katika mambo fulani, na usalama dhidi ya vilema au mapungufu yanayozuia ndoa.

[2] «Al-Kafi» cha Ibn Abd al-Barr al-Maliki (1/ 235), na «Al-Mughni» cha Ibn Qudamah al-Hanbali (7/ 49), na «Al-Hawi» cha Al-Mawardi al-Shafi’i (9/ 52).

[3] «Kashshaf al-Qina’ ‘an Matn Al-Iqna’» cha Al-Buhuti Al-Hanbali (5/ 68), na «Al-Fatawa Al-Hindiyyah» katika Fiqhi ya Mashekhe wa Kihanafi (1/ 294).

[4] «Imefungamana»: Ni sharti.

[5] «Mughni al-Muhtaj» cha Al-Khatib al-Shirbini (3/ 164- 165).

[6] «Al-Mabsut» cha Al-Sarakhsi (4/ 212), na «Bada’i al-Sana’i» cha Al-Kasani al-Hanafi (2/ 240).

Share this:

Related Fatwas