Hukumu ya mtu aliyemgonga mbwa wa mtu mwingine kimakosa
Question
Mtu mmoja anauliza: "Nilikuwa nikiendesha gari katika barabara moja, ghafla akatokea mbwa mbele yangu akikatiza njia, sikuweza kulidhibiti gari nikamgonga kimakosa, jambo ambalo lilipelekea kifo chake. Mmiliki wake amenitaka nilipe thamani yake kwa sababu ni katika wanyama wenye manufaa, je, ni wajibu kwangu kulipa thamani yake?
Answer
Sharia tukufu imehimiza kufanyia wanyama upole na kudumisha uwepo wao wa kinyama katika mazingira na kutofuta spishi zao; lengo likiwa ni kuhifadhi usawa wa kimazingira na ukamilifu kati ya aina mbalimbali za viumbe. Na kuua mbwa kwa bahati mbaya, kama vile mtu aliyemgonga kwa gari lake kimakosa, ikiwa mbwa huyo anamilikiwa na wamiliki wake—kama vile mbwa wa shamba, wa ulinzi, na wa kuwindia aliyefundishwa—basi anahesabiwa kuwa ni mali yenye thamani inayowajibisha fidia (dhamana) kwa yule aliyemuua. Ama ikiwa mbwa huyo si miongoni mwa wenye manufaa (kama mbwa wa mitaani asiyemilikiwa), basi hakuna fidia kwa aliyemuua.
Maelezo
Sharia tukufu imehimiza kufanyia wanyama upole na kuwafanyia ihsani, na Mtume (S.A.W.) alikuwa ni kiumbe mwenye huruma zaidi kwa viumbe, na mtu mwenye huruma zaidi kwa wanyama. Sharia imechukulia huruma kwa mnyama na kumfanyia upole kuwa ni mlango wa kuingilia Peponi, kama ambavyo imechukulia ukatili dhidi yake na kumtesa kuwa ni mlango wa kuingilia Motoni. Imamu Al-Bukhari amepokea kutoka kwa Abu Huraira (R.A.) kwamba Mtume (S.A.W.) amesema: “Mwanamke mmoja mzinifu alisamehewa madhambi yake kwa sababu alipita karibu na mbwa aliyekuwa kando ya kisima akihangaika kwa kiu; kiu hiyo ilikaribia kumuua. Mwanamke huyo akavua kiatu chake, akakifunga kwa mtandio wake, kisha akamtekea maji; akasamehewa kwa tendo hilo”.
Pia imepokelewa kutoka kwa Ibn Umar (R.A) kwamba Mtume (S.A.W.) amesema: “Mwanamke mmoja aliadhibiwa kwa sababu ya paka aliyemfunga mpaka akafa, akaingia Motoni kwa sababu hiyo; hakumlisha wala kumnywesha alipomfungia, wala hakumwacha ale wadudu wa ardhini” [Imepokewa na Muslim].
Sharia tukufu imehimiza kudumisha uwepo wa wanyama katika mazingira na kutofuta spishi zao; kwa lengo la kuhifadhi usawa wa kimazingira na ukamilifu kati ya aina mbalimbali za viumbe; kwani hakuna kiumbe alichokiumba Mwenyezi Mungu isipokuwa ndani yake kuna aina fulani ya hekima na maslahi.
Kuhusu kuua mbwa kwa bahati mbaya, kama vile mtu aliyemgonga kwa gari lake kimakosa na mbwa huyo alikuwa akimilikiwa na wamiliki wake, wanazuoni wa Fiqhi wametofautiana kuhusu uwajibikaji wa kutoa fidia (dhamana) kwa aliyemuua. Wataalamu wa Fiqhi wa madhehebu ya Kihanafi na Kimaliki wanaona kuwa mbwa aliyeruhusiwa kufugwa na kumilikiwa—ambaye ni yule mwenye manufaa kama mbwa wa shamba, ulinzi, na wa kuwindia aliyefundishwa—anahesabiwa kuwa ni mali yenye thamani inayowajibisha fidia kwa yule aliyemuua. Ama ikiwa mbwa huyo si miongoni mwa wenye manufaa, basi hakuna fidia kwa aliyemuua kwa sababu hahesabiki kama mali yenye thamani.
Dalili ya jambo hilo ni kauli ya Mwenyezi Mungu (S.W.): {Wanakuuliza (ee Muhammad) ni nini walichohalalishiwa? Sema: Mmehalalishiwa vitu vizuri (vya kula), na mlichowafundisha wanyama wa kuwindia (kama mbwa) mkiwafundisha katika yale aliyowafundisheni Mwenyezi Mungu; basi kuleni katika vile walivyowakamatia na mlitajie jina la Mwenyezi Mungu} [Al-Ma'idah: 4].
Ikiwa (Mwenyezi Mungu) ametuhalalishia kile walichotuwinda, hiyo inatupa faida ya kuruhusiwa kuwatumia kwa kuwakamata, kuwauza na mengineyo. Hii ndiyo kauli ya kundi la wema waliotangulia, na imepokelewa kutoka kwa Jabir bin Abdullah na 'Ataa kwamba walijalia kuwepo kwa fidia (thamani) kwa mbwa wa kuwindia.
Pia yale yaliyopokelewa kutoka kwa Ibn Umar (R.A.) aliyesema: Nilimsikia Mtume (S.A.W.) akisema: “Mwenye kufuga mbwa, isipokuwa mbwa wa kuwindia au mbwa wa kulinda mifugo, basi hupungukiwa katika malipo yake (thawabu) kila siku kiasi cha qirati mbili” [Imetolewa na Al-Bukhari]. Hivyo ni kama Mtume (S.A.W.) amekataza thamani (biashara) ya mbwa isipokuwa mbwa aliyeruhusiwa kumilikiwa kwa ajili ya manufaa. Vilevile yale yaliyopokelewa kutoka kwa Sufyan bin Abi Zuhayr aliyesema: Nilimsikia Mtume (S.A.W.) akisema: “Mwenye kufuga mbwa ambaye hamfaidii katika shamba lake wala mifugo yake, hupungukiwa kila siku katika amali zake kiasi cha qirati moja”. Nikasema: Wewe uliyayasikia haya kutoka kwa Mtume (S.A.W.)? Akasema: Ndiyo, naapa kwa Mola wa msikiti huu! [Imekubaliwa na Al-Bukhari na Muslim].
Hivyo basi, kuruhusiwa kwa kuuza mbwa anayefugwa kwa ajili ya shamba, mifugo, na kuwindia; ni kwa sababu ananufaisha katika mambo hayo, inajuzu kumnunua na kumuuza, na aliyemuua analazimika kulipa thamani yake; kwani amekosesha manufaa ya ndugu yake.
Wakati huo huo, wataalamu wa Fiqhi wa madhehebu ya Shaf'i na Hanbali wameelekea kwenye msimamo kuwa mwenye kuharibu (kumuua) mbwa halazimiki kulipa thamani yake kabisa, iwe amefundishwa au hajafundishwa, mdogo au mkubwa; kwa sababu hana thamani (ya kimali), na huu ni msimamo wa baadhi ya Maswahaba na Tabiina kama Abu Huraira, Al-Hasan Al-Basriy, Al-Awza'iy, Ibn Al-Mundhir, na wengineo.
Wametoa ushahidi wa jambo hilo kwa yale aliyoyapokea Abu Mas'ud Al-Ansari (R.A.) kwamba Mtume (S.A.W.): “Alikataza thamani ya mbwa, mahari ya mzinifu, na malipo ya mpiga ramli» [Imekubaliwa na Al-Bukhari na Muslim].
Na kukatazwa kwa thamani ya mbwa kunapelekea kuharibika kwa biashara yake, na kwa msingi huo, hakuna thamani (fidia) inayowajibika kwa aliyemuua.
Rai iliyochaguliwa kwa ajili ya Fatwa: Ni ile waliyoiendea wahanafi na wamaliki kuhusu uwajibikaji wa fidia (dhamana) kwa yule aliyemuua mbwa wa mtu mwingine mwenye manufaa; kwa sababu ni mali yenye thamani. Hii ni kutokana na yale aliyoyapokea Imran bin Abi Anas: «Kwamba Uthman alimtoza mtu thamani ya mbwa aliyemuua kiasi cha ngamia ishirini» [Imetolewa na Al-Bayhaqi katika Al-Sunan Al-Kubra]. Pamoja na hayo, ni kama alivyopitisha mtungaji sheria wa Misri katika kifungu cha (163 cha Sheria ya Madai) kwamba: (Kila kosa lililosababisha madhara kwa mwingine linamlazimu aliyelitenda kutoa fidia).
Mtungaji sheria ameweka wajibu wa kutoa fidia kwa kila kosa lililosababisha madhara kwa mwingine ili kuzuia mgogoro unaoweza kutokea kati ya pande mbili kutokana na kwamba aliyemuua amemkosesha mwenye mbwa manufaa yake. Katika jambo hilo kuna kufikiwa kwa maslahi kwa kuondoa madhara kwa mmiliki wa mbwa, na ndivyo ilivyoamuliwa katika kanuni za Sharia kwamba «hakuna kudhuru wala kudhuriwa». Na makadirio ya thamani yanarejea kwenye makubaliano na ridhaa kati ya pande mbili, au kurejea kwa watu wenye uzoefu (wataalamu) katika jambo hilo, na ikiwa watashindwa kuelewana, basi suala hilo linafikishwa mahakamani ili litolewe uamuzi.
Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:
Ni kwamba yule aliyemuua mbwa kwa bahati mbaya na mbwa huyo alikuwa akimilikiwa na mmoja wa watu akitumiwa kwa ajili ya manufaa fulani miongoni mwa nyanja za manufaa—kama ulinzi au kuwindia na mfano wake—basi ni wajibu kwake kulipa thamani yake; kwa sababu ni mali yenye thamani inayowajibisha kulipwa kwa thamani yake kwa kumuua. Na makadirio ya thamani hiyo yanarejea kwenye makubaliano na ridhaa kati ya pande mbili, au kurejea kwa watu wenye uzoefu katika jambo hilo; na ikiwa pande mbili zitatofautiana, basi suala hilo linafikishwa mahakamani ili litolewe uamuzi.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
