Athari ya kuwekwa bomba la kuondoa ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Athari ya kuwekwa bomba la kuondoa usaha kwenye udhu na Swala

Question

Mtu amefanyiwa upasuaji na ikahitajika kuwekwa bomba la kuondoa usaha na damu na kubaki nalo kwa siku kadhaa, je, kutoka damu kwenye jeraha na kushuka kwake kwenye bomba hili kunabatilisha udhu? Na je, kubeba bomba hili na yaliyomo ndani yake kwa muda wote kunathiri usahihi wa Swala yake?

Answer

Mtu aliyefanyiwa upasuaji na akawekewa bomba[1] la kuondoa usaha na damu ambalo damu na majimaji ya jeraha yanakusanyika humo, na daktari akamwamuru abaki nalo kwa siku kadhaa, udhu wake hautenguki kwa damu hii inayotoka iwe kidogo au nyingi, na hakuna tatizo kwake kisharia. Anaweza kuswali akiwa nalo, na hakuna tatizo kwake kwa kuwa hawezi kuliondoa au kulimwaga, na kubeba kwake hakuharibu usahihi wa Swala yake, wala halazimiki kuirudia Swala alizoswali akiwa amelibeba.

Maelezo

Swala ni nguzo kati ya nguzo za Uislamu. Mwenyezi Mungu amemwamuru kila mtu aliye timamu aisimamishe katika hali yoyote awe mzima au mgonjwa, wala haimuondoki kamwe mradi tu masharti ya wajibu yamekamilika. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na simamisheni Swala} [Al-Baqara: 43], na amesema tena: {Hifadhini Swala na Swala ya katikati na simameni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hali ya unyenyekevu} [Al-Baqara: 238]

Na kutoka kwa Imran bin Huswayn (R.A) amesema: Nilikuwa na bawasiri, nikamuuliza Mtume (S.A.W) kuhusu Swala, akasema: (Swali ukiwa umesimama, kama huwezi basi kaa, na kama huwezi basi Swali kiubavu) Ameitoa Al-Bukhari katika “Sahih” yake.

Na Wanazuoni wengi wameweka sharti la usahihi wa Swala kuwa ni twahara ya nguo, mwili na mahali, na imepokewa Ijmaa juu ya hilo[2]. Na damu nyingi inayotoka mwilini mwa mtu inahesabiwa kuwa ni najisi kwa makubaliano ya Wanazuoni. Kwa hiyo mgonjwa mwenye kubeba “bomba la kuondoa usaha” anapotaka kuswali, ni lazima awe na udhu na awe twahara na najisi (kwa kuondoa damu najisi) ili Swala yake iwe sahihi.

Ama twahara kutokana na Hadathi: Wanazuoni –pamoja na kukubaliana kwao kuwa damu ni najisi– wametofautiana kuhusu damu inayotoka katika isiyo katika njia mbili (tupu ndogo na tupu kubwa) kama miongoni mwa yanayobatilisha udhu au la. Kauli iliyochaguliwa kwa ajili ya Fatwa: Ni kwamba haibatilishi udhu, iwe damu hiyo ni kidogo au ni nyingi. Hii ndiyo kauli ya Madhehebu ya Maliki na Shafi, na imepokelewa kutoka kwa Mama wa Waumini Bi Aisha, na Abdullah bin Umar, na Ibn Abbas, na Ibn Abi Awfa, na Jabir, na Abu Hurairah  na Said bin Al-Musayyib, na Salim bin Abdullah bin Umar, na Al-Qasim bin Muhammad, na Tawus, na Ata, na Mak’hul, na Rabiah, na Abu Thawr

Kutoka kwa Ibn Abbas (R.A) amesema: “Osheni athari za chukwu juu yenu na hiyo inakutosheni.”

 Na kutoka kwa Al-Qasim bin Muhammad amesema: “Hana ulazima wa kutia udhu mwenye kupiga chukwu.” amezipokea zote Imamu Al-Bayhaqi katika “As-Sunan Al-Kubra.”

 Na amepokea Imamu Malik katika “Al-Muwatta” kutoka kwa Abdurrahman bin Harmalah Al-Aslami kwamba amesema: “Nilimuona Said bin Al-Musayyib anatokwa na damu puani, mpaka vidole vyake vimepakwa na damu inayotoka puani mwake, kisha anaswali bila ya kutia udhu.”

Na kutoka kwa Tawus amesema: “Mtu akitokwa na damu puani kwake na yupo katika Swala, na aondoke, kisha aioshe damu, kisha arejee na akamilishe kilichobaki kwa yale yaliyopita ikiwa hakuzungumza, na wala hakuna udhu juu yake.” Ameipokea Imamu Abdurrazzaq As-San’ani katika “Al-Musannaf.”

Na ameipokea Imamu Al-Bukhari katika “Sahihi” yake kwa maelezo, amesema: Wamesema Tawus, na Muhammad bin Ali, na Ata, na Watu wa Hijaz: “Hakuna udhu kwa damu.” Na Ibn Umar (RA) Ibn ‘Umar alikamua jipu, damu ikatoka, lakini hakutawadha.. Na Ibn Abi Awfa (RA) alitema damu na akaendelea na Swala yake. Na amesema Ibn Umar L na Al-Hasan kuhusu mwenye kupiga chukwu (hijama): “Hana wajibu ila kuosha maeneo ya chukwu yake.”

Na kauli ya kutobatilika udhu kwa kutoka damu katika zisizo njia mbili ndio inayolingana zaidi na sifa ya kupunguza uzito na kuwepesisha na kuondoa dhiki kwa wanaokalifishwa na Sharia ya Kiislamu; kwa kuenea wa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Mwenyezi Mungu anataka kukupunguzieni (mashaka), na mwanadamu ameumbwa dhaifu} [An-Nisaa: 28], na kauli yake Mtukufu: {Wala hakukuwekea katika dini dhiki} [Al-Hajj: 78].

Na ameipokea Imamu Ahmad katika “Musnad” yake kutoka katika Hadithi ya Abu Umamah (R.A) kwamba Mtume (S.A.W) amesema: “Nimetumwa kwa dini ya unyofu na wepesi.”

 

Basi ikiongezwa pamoja na hilo kuwa mwenye kukalifishwa ni mgonjwa, na ugonjwa unahesabiwa miongoni mwa sababu za kwanza za kulegezewa masharti katika Sharia tukufu, mpaka Mwenyezi Mungu akamhusisha mgonjwa kwa kutajwa kuondolewa dhiki, akasema: {Wala si dhambi juu ya mgonjwa} [An-Nur: 61], na mgonjwa aliyepata mtihani kwa kutoka damu kwenye jeraha na kushuka kwake katika kinachojulikana kama “bommba la upasuaji” ndiye mwenye kuhitajia zaidi kulegezewa huku na kupungiziwa mashaka; kwani inamshughulisha mno kujiepusha na kutoka damu, na kanuni za kisharia zinahukumu kwamba: “Mashaka huleta wepesi” na “Panapokuwa na dhiki jambo hupanuka.”
Na kwa mujibu wa hayo: Udhu wa mtu huyu hautenguki kwa kutoka damu kwenye jeraha na kushuka kwake katika kinachojulikana kama “bomba la upasuaji,” iwe damu hiyo ni kidogo au ni nyingi, na hakuna dhiki juu yake katika hilo kisharia.

Na ama kuondoa najisi kwa kuacha kubeba damu na najisi nyingine katika bomba wakati wa kuswali, inagawanywa katika mambo mawili:

La kwanza: Ikiwa mgonjwa anaweza kuondosha bomba la kutoa uchafu huu au kuimwaga yote iliyomo humo kabisa kiasi kwamba ataswali bila kuwa na najisi, bila madhara yoyote, basi inampasa kufanya hivyo na Swala yake itakuwa sahihi.

La pili: Ikiwa hawezi kuiondoa wala kuimwaga au inamshughulisha sana, na damu pamoja na najisi nyingine zinaendelea kutoka – kama ilivyo katika suala letu – kwa kuogopa kucheleweshwa kupona, au kuongezeka ugonjwa, au kuharibika kwa jeraha, na mfano wa hayo, au akawa amezuiwa kufanya jambo hilo ila kwa ruhusa ya daktari na kupitia yeye au mhudumu wa afya, basi husameheka wakati huo kutokana na najisi hii, na swala yake inasihi pamoja na kulibeba, na halazimiki kuirudia, hasa kwa kuwa kulibeba kunachukua muda wote wa swala, hivyo kuamrishwa kuiondoa huku akikwepa najisi ni mashaka makubwa, na kumletea madhara nafsi yake, na imekubaliwa kisharia kuwa mwenye utimamu amekatazwa kuidhuru nafsi yake; kwa ujumla wa kauli ya Mwenyezi Mungu: {wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo.} [Al-Baqara: 195], na kauli yake Mtukufu: { Wala msijiuwe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwarehemuni} [An-Nisa: 29], na kauli ya Nabii (rehema na amani zimshukie): (Usidhuru wala usijidhuru). Imetolewa na Maimamu wawili, Imamu Ibn Majah katika “Sunan” na lafudhi hii ni yake, na Tabarani katika “Al-Mu’jam Al-Kabir” na “Al-Mu’jam Al-Awsat”, kutokana na Hadithi ya Abdullah bin Abbas (RA) na wameitoa Maimamu: Al-Hakim katika “Al-Mustadrak” na akaisahihisha, Ad-Daraqutni na Al-Bayhaqi katika “Sunan” zao, kutokana na hadithi ya Abu Sa’id Al-Khudri (R.A).

Na kwa vile imekubaliwa katika kanuni za kisharia kwamba “Madhara huondolewa”, na kwamba “Mashaka huleta wepesi”, na “Panapokuwa na dhiki jambo hupanuka.”

Na Masahaba (R.A) walikuwa wakiswali wakiwa na majeraha yao, wala hakuna aliyewakemea. Imamu Bukhari ameitoa katika “Sahih” yake akielezea akasema: Imesimuliwa kutoka kwa Jabir (RA): “Kwamba Nabii (S.A.W) alikuwa katika vita vya Dhat Ar-Riqa‘, kuna kijana akapigwa mshale, damu ikatoka, akainama, akasujudu, na akaendelea na Swala yake.” Na Al-Hasan (RA) amesema: “Waislamu wamekuwa wakiswali wakiwa na majeraha yao.”

Na Wanazuoni wa Fiqhi wamemruhusu mwenye kukalifishwa kuswali akiwa na najisi – iwe ipo juu yake au ameibeba – ikiwa hawezi kuiondoa au inamshughulisha sana, na halazimiki kuirudia Swala aliyoiswali akiwa na najisi ilivyokuwa ana udhuru wa kulazimika kuibeba – kama ilivyo suala letu – na hili ndilo walilolitaja Wanazuoni wengi wa Fiqhi miongoni mwa Madhehebu ya Imamu Hanafi, Maliki, Shafi katika kauli iliyo sahihi zaidi, na Hanbali katika kauli iliyo sahihi, isipokuwa Imamu Shafi katika kauli mpya walisema lazima kurudia Swala, lakini kauli iliyo sahihi zaidi ni ile ya kutorudia, na hii ndiyo aliyoisema Imamu Shafi katika kauli ya zamani[3].

Kwa hivyo, hakuna tatizo kwa mtu aliye fanyiwa upasuaji na akawekewa “bomba ya kutolea uchafu”, na akafahamishwa na daktari kuwa abaki nayo kwa siku kadhaa, kuswali akiwa nayo, maadamu hawezi kuiondoa au kuimwaga, na kubeba kwake hakuathiri usahihi wa swala yake, wala halazimiki kuirudia swala aliyoiswali akiwa ameibeba.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

 Damu ni najisi kwa makubaliano, lakini kutoka kwake nje ya njia mbili (tupu ndogo na tupu kubwa) hakubatilishi udhu kwa kauli iliyo chaguliwa kwa fatwa, hasa kwa mgonjwa anayelazimika kuweka bomba la upasuaji.

 Mgonjwa ataswali akiwa na bomba la kutolea uchafu la upasuaji pamoja na najisi iliyomo, maadamu hawezi kuiondoa au kuimwaga, na kubeba kwake hakuathiri usahihi wa swala yake, wala halazimiki kuirudia.

 

[1] "Darnaka (au bomba la kuondoa usaha) ni bomba linalotumika kutoa usaha, damu, au majimaji mengine kutoka kwenye jeraha. Tazama: Kamusi ya istilahi za kitiba ya Kamati ya Istilahi za Kitiba ya Majma’ wa Lugha ya Kiarabu, chini ya istilahi 'al-Munzaḥah' (Juzuu ya 2, uk. 68, chapa ya Al-Amīriyya).

[2] Kitabu At-Tamhīd (juzuu ya 22, uk. 242, chapa ya Wizarat Awqāf Al Maghrib), na Al-Istidhkār (juzuu ya 1, uk. 332, chapa ya Dār al-Kutub al-‘Ilmiyya), vyote viwili ni vya Imamu Ibn ‘Abd al-Barr. Na kitabu Al-Majmū‘ cha Imamu Nawawī (juzuu ya 3, uk. 132, chapa ya Dār al-Fikr), na Al-Mughnī cha Imamu Ibn Qudāmah (juzuu ya 2, uk. 48, chapa ya Maktabat al-Qāhira)."

[3] "Tazama: Marāqī al-Falāḥ (uk. 90, chapa ya Al-Maktaba al-‘Asriyya), Mawāhib al-Jalīl (juzuu ya 1, uk. 131, chapa ya Dār al-Fikr), na Al-Muhadhdhab (juzuu ya 1, uk. 117, chapa ya Dār al-Kutub al-‘Ilmiyya)."

Share this:

Related Fatwas