Anaeswali Swala ya faradhi Kumfuata Imamu Anayeswali Sunna
Question
Niliingia msikitini kuswali Isha na nikawakuta watu wakiswali jamaa, nikaswali pamoja nao. Baada ya jamaa kumalizika, nikashangaa Imamu wa Swala akiniambia kuwa wao walikuwa wanaswali Sunna na si Swala ya Isha. Je, swala yangu ni sahihi?
Answer
Kuswali Swala ya faradhi nyuma ya Imamu anayeswali Sunna ni sahihi. Inajuzu maamuma anayeswali faradhi kumfuata Imamu anayeswali Sunna, vivyo hivyo anayeswali Sunna kumfuata anayeswali faradhi; kwani si sharti nia ya maamuma iendane na nia ya Imamu kwa kauli iliyochaguliwa kwa ajili ya Fatwa.
Maelezo
Sharia Tukufu imehimiza kuswali Swala za faradhi kwa jamaa na imeweka thawabu kubwa juu yake. Kumepokelewa hadithi nyingi kuhusu hilo, miongoni mwazo: Hadithi iliyopokelewa na Imamu Bukhari katika "Sahihi" yake kutoka kwa Abdullah bin Umar (R.A) kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) amesema: (Swala ya jamaa inazidi Swala ya mtu mmoja kwa daraja ishirini na saba)).
Na ni lazima kwa maamuma kumfuata Imamu wake, kama ilivyopokelewa na Imamu Bukhari katika "Sahihi" yake kutoka kwa Abu Huraira (R.A): (Hakika Imamu amewekwa ili afuatwe, basi msikhitalifiane naye)).
Na Wanavyuoni wamekhitalifiana kuhusu maamuma anayeswali faradhi kumfuata Imamu anayeswali sunna, Imamu Hanafi, Maliki na Hanbal katika moja ya riwaya wameona kuwa haijuzu; kwa sababu Swala ya Imamu na ya maamuma si moja[1].
Lakini Imamu Shafi na Hanabilah katika riwaya nyingine – walioyaona sahihi zaidi baadhi yao, kama Ibn Qudamah na Ibn Taymiyyah – na Dhahiriyah, wameona kuwa si sharti Swala mbili ziwe sawa, na inajuzu mwenye kuswali faradhi kumfuata anayeswali Sunna, na anayeswali Sunna kumfuata anayeswali faradhi, na anayeswali faradhi kumfuata mwenye kuswali faradhi nyingine[2].
Na hii ni kauli ya baadhi ya Salaf, miongoni mwao: Ata bin Abi Rabah, Tawus, Sulaiman bin Harb, Abu Thawr, na Al-Awza’i.
Na kauli iliyochaguliwa kwa ajili ya kutoa Fatwa: Ni ile waliyoisema Imamu Shafi na waliowafuata kwamba Swala ya mwenye kuswali faradhi nyuma ya anayeswali Sunna ni sahihi; kwa sababu ya yaliyokuja katika Hadithi ya Mu’adh (R.A): (Kwamba alikuwa akiswali pamoja na Mtume S.A.W), kisha anarudi na kuwaongoza kaumu yake) imepokewa na Bukhari.
Na katika riwaya nyingine: (Mu’adh alikuwa akiswali pamoja na Mtume (S.A.W) Swala ya Isha, kisha anaenda kwa kaumu yake na kuwaswalisha; nayo kwake ni Sunna na kwao ni Swala ya faradhi ya Isha)) imepokewa na Imamu Shafi katika "Al-Musnad", na Al-Bayhaqi katika "Ma’rifat As-Sunan wal-Athar".
Ama Hadithi: (Hakika Imamu amewekwa ili afuatwe, basi msikhitalifiane naye)) haina dalili ya kutaka kufanana nia ya maamuma na Imamu katika kubainisha aina ya Swala; kwa kuwa kinachokusudiwa ni kumfuata katika vitendo vya nje, kama vile: takbira, rukuu, sujudu, kusimama na kukaa, si katika vitendo vya ndani kama nia.
Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:
Sharia Tukufu imehimiza kuswali Swala za faradhi kwa jamaa na imeweka thawabu kubwa juu yake.
Swala ya mwenye kuswali faradhi nyuma ya anayeswali Sunna ni sahihi kwa mujibu wa kauli iliyochaguliwa kwa ajili ya kutoa Fatwa.
[1] Kitabu Al-Hidāyah (juzuu ya 1, uk. 59, chapa ya Dār Iḥyā’ at-Turāth al-‘Arabī), Sharḥ al-Kharshī ʿalā Mukhtaṣar Khalīl (juzuu ya 2, uk. 38, chapa ya Dār al-Fikr), na Al-Mughnī (juzuu ya 2, uk. 166, chapa ya Maktabat al-Qāhira)."
[2] "Kitabu Al-Majmū‘ (juzuu ya 4, uk. 271, chapa ya Dār al-Fikr), Al-Mughnī (juzuu ya 2, uk. 166), na Al-Muḥallā bi al-Āthār (juzuu ya 3, uk. 140, chapa ya Dār al-Fikr)."
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
