Kusoma kwa kuangalia kwenye Msahafu...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kusoma kwa kuangalia kwenye Msahafu katika Swala ya Tarawihe

Question

Ninataka kukamilisha (kuhitimisha) usomaji wa Qur'ani Tukufu katika Swala ya Tarawih ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, lakini sijahifadhi Qur'ani yote. Je, inaruhusiwa kwangu kusoma kwa kuangalia kwenye msahafu katika Swala?

Answer

Kusoma Qur'ani Tukufu yote katika Swala ya Tarawihe ni jambo zuri, kitendo kinachotakiwa, na Sunna iliyofuatwa. Inaruhusiwa kwako kutumia msaada wa kusoma kutoka kwenye msahafu ili kufikia jambo hilo, na hakuna dhambi juu yako kwa kufanya hivyo.

Maelezo

Wanachuoni wote wamekubaliana kuwa Swala ya Tarawihe ni Sunna iliyokokotezwa (Mu'akkadah) kwa wanaume na wanawake. Nabii Muhammad (S.A.W) aliihimiza katika Hadithi nyingi, akisema:

"Mwenye kusimama (kuswali) Ramadhani kwa imani na kutarajia malipo, husamehewa dhambi zake zote zilizotangulia." (Imepokewa na Bukhari na Muslim).

Imepokelewa kutoka kwa Abdurrahman Ibn Auf kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Hakika Mwenyezi Mungu ameifanya Saumu ya Ramadhani kuwa Faradhi juu yenu, na mimi nimewatengenezea (nimeweka Sunna) kwa ajili yenu Swala ya usiku wake (Tarawihe). Basi atakayefunga na kusimama (kuswali) kwa imani na kutarajia malipo, hutoka katika dhambi zake kama siku aliyozaliwa na mama yake." (Imepokewa na Imam An-Nasa'i).

Usomaji wa Qur'ani Tukufu una fadhila kubwa na thawabu za kuikamilisha (kuihitimisha) ni kubwa. Hadithi ya Abdullah ibn Mas'ud, ambapo Mtume  (S.A.W)  amesema: "Mwenye kusoma herufi moja ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu, ana malipo (hasana) moja, na malipo moja ni sawa na kumi mfano wake. Sisemi {Alif laam Meem} ni herufi moja, lakini Alif ni herufi, Lam ni herufi, na Mim ni herufi." (Imepokewa na Imam At-Tirmidhi).

Hizi ni thawabu kwa mwenye kusoma Qur'ani Tukufu nje ya Ramadhani, na inapokuwa ndani ya Ramadhani, thawabu yake huwa kubwa zaidi.

Salman Al-Farsi (R.A) amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu  (S.A.W)  alituhutubia siku ya mwisho ya Shaban na akasema: “Enyi watu! Hakika mwezi mtukufu umekukaribieni; mwezi wenye baraka; mwezi wenye usiku ulio bora kuliko miezi elfu moja. Allah amejaalia kufunga kwake kuwa ni wajibu, na kusimama kwake usiku (kwa ajili ya Swala) kuwa ni Sunna. Atakayejikurubisha kwa jambo jema (sunna) ndani yake ni kama mtu aliyefanya wajibu (faradhi) katika miezi mingine, na anayefanya wajibu (faradhi) ndani yake ni kama mtu aliyefanya wajibu sabini (faradhi) katika miezi mingine”. Imesimuliwa na Maimamu wawili: Ibn Khuzaymah katika Sahih yake na al-Bayhaqi katika Shu'ab Al-Iman.

Imethibitika katika Sharia za Kiislamu kwamba usomaji bora kabisa wa Qur’ani Tukufu ni ule unaofanywa wakati wa Swala. Kwa mujibu wa Hadithi ya Mama wa Waumini, Aisha (R.A), Mtume  (S.A.W)  amesema: “Kusoma Qur’ani Tukufu wakati wa Swala ni bora kuliko kuisoma nje ya Swala, na kusoma Qur’ani Tukufu nje ya Swala ni bora kuliko kusema ‘Allahu Akbar’ na ‘Subhanallah’ na Tasbihi ni bora kuliko kutoa sadaka, na sadaka ni bora kuliko kufunga (Sunna), na kufunga ni ngao dhidi ya moto wa Jahannam” Imesimuliwa na Imam Al-Bayhaqi katika Shu’ab Al-Iman.

Imepokewa kutoka kwa Amirul-Muuminina Ali Ibn Abi Talib (R.A) kwamba amesema: “Mwenye kusoma Qur’ani Tukufu hali ya kuwa amesimama katika Swala atapata mema mia kwa kila herufi, mwenye kusoma akiwa amekaa katika Swala atapata mema hamsini kwa kila herufi, mwenye kusoma nje ya Swala hali ya kuwa na udhu atapata mema ishirini na tano na mwenye kuisoma hali ya kuwa hana udhu atapat mema kumi." Hili lilitajwa na Hujjat Al-Islam Al-Ghazali katika “Ihya’ ‘Ulum Al-Din” na Imam Abu Al-Qasim Tamam alilijumuisha katika “Fawa’id” yake kwa urefu kutoka kwa Al-Baraa Ibn Azib (R.A).

Madhehebu ya Imamu Shafi na wengineo ni kwamba kurefusha kisimamo katika Swala na kusoma ni bora kuliko kusujudu  na sehemu nyinginezo.

Kwa vile kusoma Qur’ani Tukufu wakati wa Swala kuna thawabu zaidi na kunufaisha zaidi kuliko kusoma nje ya Swala, Wanazuoni wamependekeza kuikamilisha Qur’ani Tukufu wakati wa Swala ili mtu apate malipo makubwa na bora kabisa ya kuikamilisha.

Kusoma Qur’ani Tukufu katika Swala ya Tarawihe ni Sunna iliyofuatwa na Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu  (S.A.W) , na wafuasi waliokuja baada yao wakafuata mfano huo. Abu Uthman al-Nahdi amesema: “Umar Ibn Al-Khattab (R.A) akawaita wasomaji watatu na akawasikiliza, akamuamrisha anayesoma haraka zaidi kati yao awasomee watu Aya thelathini, na anayesoma kwa wastani asome Aya ishirini na tano, na anayesoma taratibu zaidi kati yao asome Aya ishirini. Imesimuliwa na Maimamu wawili: Ibn Abi Shaybah katika “Al-Musannaf” na Al-Bayhaqi katika “Al-Sunan Al-Kubra.”

Kuhusu kusoma kwa kuangalia katika Msahafu katika Swala ya Tarawihe: Fatwa inayopendelewa ni kwamba inajuzu kusoma kwa kuangalia Msahafu bila ya chukizo lolote. Kwa sababu Imamu Al-Bukhari amesimulia katika Sahihi yake: “Mama wa Waumini, Aisha (R.A), aliongozwa katika Swala na mtumwa wake Dhakwan akisoma kwa kuangalia katika Msahafu. Na katika mapokezi ya Imamu Malik katika Al-Muwatta’: “Alikuwa akisimama na kumsomea wakati wa Ramadhani. Na Imamu Ibn Abi Shaybah amepokea katika Musannaf wake kutoka kwa Abu Bakr bin Abi Mulaykah akisema: “Bi. Aisha, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, alimwachia huru mmoja wa watumwa wake kwa wasia wa baada ya kifo (An dubur) na alikuwa akimswalisha katika Ramadhani kwa kuangalia katika Msahafu. Kundi la watu wema waliotangulia wameeleza kuwa inajuzu kusoma Qur-ani Tukufu  kwa kuangalia katika Msahafu wakati wa Swala ya Tarawihe, akiwemo Ibn Sirin, Al-Hasan, Al-Hakam bin Utaybah, na Ishaq Ibn Rahawayh.

Imepokewa kutoka kwa Abd al-Quddus Ibn Habib kutoka kwa Al-Hasan kwamba alimsikia akisema: “Hakuna ubaya kwa mtu kuswalisha tarawehe katika Ramadhani huku akisoma kwa kuangalia Msahafu.

‘Ayyub amesimulia kwamba Ibn Sirin alikuwa akiswali na Msahafu upo pembeni yake, na kila alipokuwa akisitasita, alikuwa akiitazama. Riwaya hizi zote mbili zimesimuliwa na Imamu‘Abd al-Razzaq katika Musannaf wake.

‘Shu‘bah amesimulia kutoka kwa Al-Hakam kwamba aliulizwa kuhusu mtu anayeongoza Swala katika Ramadhani huku akisoma kwa kuangalia katika Msahafu. Aliruhusu hilo.” Imesimuliwa na Imamu Ibn Abi Shaybah katika “Musannaf” yake.Haya ni maoni ya wanazuoni wengi wa Fiqhi kutoka Madhehebu ya Maliki, Shafi na Hanbali.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Kusoma Qur’ani Tukufu wakati wa Swala kuna thawabu na manufaa zaidi kuliko kuisoma nje ya Swala.

Kusoma Qur’ani Tukufu yote wakati wa Swala ya Tarawihe ni Sunna inayofuatwa na Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu  (S.A.W)

Kuhitimisha Qur’ani Tukufu wakati wa Swala ya Tarawihe ni kitendo chenye kusifiwa, ni kitendo cha kutamanika, na Sunna inayofuatwa. Inawezekana kusaidia kufikia hili kwa kusoma kwa kuangalia katika Msahafu, na hakuna ubaya juu yako kwa kufanya hivyo.

Share this:

Related Fatwas