Kusoma Kunut kwa sauti ya kudhihir...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kusoma Kunut kwa sauti ya kudhihirisha Katika Swala ya Alfajiri

Question

Ni ipi hukumu ya kusoma Qunut kwa sauti ya kudhihirisha katika Swala ya Alfajiri?

Answer

Kusoma Qunut katika Swala ya Alfajiri ni halali na inaruhusiwa kisharia. Hii ndiyo misimamo ya Madhehebu ya Imamu  Maliki na Shafi. Ni kanuni iliyowekwa katika misingi ya Usul Al-Fiqh kwamba mambo yenye tofauti za kimadhehebu hayapaswi kukemewa, na jambo hili msingi wake ni upana (urahisi na wepesi)

Maelezo

Qunut katika Swala ya Alfajiri ni Sunna iliyopitishwa na Mtume, na imeshikiliwa na wengi wa watu wema wa mwanzo kuanzia Maswahaba na Tabi'in (wafuasi) na waliokuja baada yao katika  Wanachuoni wa Madina. Kuna Hadithi iliyopokewa kutoka kwa Anas bin Malik (R.A) inayosema: "Mtume wa Allah  (S.A.W)  hakuacha kufanya Qunut katika Swala ya Alfajiri mpaka alipoiacha dunia," na hii ni Hadithi sahihi ambayo imepokewa na kundi la Wasomi na wameithibitisha, kama alivyosema Imamu Nawawi na wengine.

Madhehebu ya Imamu Shafi na Maliki walichukua Hadithi hii na kushikilia msimamo huu, na hivyo wanaona inafaa kusoma Qunut katika Swala ya Alfajiri bila sharti lolote. Walieleza kuwa Hadithi zilizopokewa zinazosema kwamba Qunut iliachwa au kukatazwa zinalenga tu kukataa kufanya dua dhidi ya watu maalumu, sio kukataa Qunut kwa ujumla.

Kupinga Qunut katika Swala ya Alfajiri kwa kudai kuwa si sahihi ni kukataa kusiokuwa sahihi, na kumtuhumu yule anayesema inafaa kuwa haelewi maandiko au ni mjinga ni kuwakosea adabu wema waliotangulia wanaosema kuwa inafaa. Si vyema kwa Muislamu kumwita mwenzake mzushi kwa sababu tu anafanya Qunut katika Swala ya Alfajiri, kwa sababu mambo yenye tofauti za kimadhehebu hayakataliwi. Pia, "Ijtihad (ufahamu wa kisharia) haubatilishwi na Ijtihad nyingine".

Kwa mfano, wakati Sheikh Ibn Qayyim Al-Hanbali alipokubali rai kwamba Qunut inapaswa kufanyika tu wakati wa matatizo, alisema kuhusu wale wanaodumisha Qunut kila mara kwamba, "Hawapingi wale wanaoifanya, wala hachukii tendo hilo, wala hawaliiti uzushi, wala hawaoni kwamba mhusika anaenda kinyume na Sunna. Vile vile hawawapingi wale wanaokataa kuifanya wakati wa matatizo, wala hawaoni kwamba kuiacha ni uzushi, wala hawaoni kwamba aliyeacha anaenda kinyume na Sunna. Badala yake, yule anayefanya Qunut amefanya vyema, na yule anayeiacha amefanya vyema pia"[1].

Hivyo, tunaweza kuhitimisha kwamba jambo hili limejengwa juu ya ukweli kwamba yule anaesoma Qunut katika Swala ya Alfajiri anafuata Madhehebu ya mmoja wa Maimamu waliobobea katika Fiqhi ambao tumeamriwa kuwafuata. Na yule anayefuata Madhehebu nyingine inayoona kwamba ni sahihi kutofanya hivyo, hana haki ya kumkosoa yule anayefanya.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Kusoma Qunut kwa sauti ya juu katika Swala ya Alfajiri inaruhusiwa, na ni miongoni mwa masuala yenye tofauti za kimadhehebu miongoni mwa Maimamu. Haifai kumkosoa yule anaesoma Qunut akifuata mmoja wa Maimamu waliobobea.

 

[1] Zaad Al Maad , 1/226.

Share this:

Related Fatwas