Kurefusha rukuu kwa ajili ya kumsub...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kurefusha rukuu kwa ajili ya kumsubiri anayetaka kuswali

Question

Watu hunitanguliza mbele wakati Imamu rasmi anapokosekana ili niwaswalishe, kwa kuwa mimi nimehifadhi kiasi kikubwa cha Qur’ani Tukufu. Huenda nikasikia sauti ya mtu akiingia akitaka kupata rakaa kabla sijainuka kutoka kwenye rukuu, basi humsubiri kwa muda kidogo hadi aipate rakaa. Je, kitendo hiki ni halali kisharia?

Answer

Iwapo Imamu atarefusha rukuu akisubiri anayetaka kuswali, kwa sharti kwamba anaeyemsubiri awe tayari yumo ndani ya msikiti wakati wa kusubiri, na asirefushe mno, na akusudie kwa hilo kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu wala si kujipendekeza kwa aliyeingia na kumtukuza, na pia wasidhurike watu kwa kurefusha huko – basi amefanya vizuri. Na akiacha kabisa kusubiri hakuna ubaya juu yake. Jambo hili liko wazi kutokana na tofauti ya Wanazuoni.

Maelezo

Sharia Tukufu imehimiza kuhudhuria Swala za jamaa na kuwahi mapema kuindea. Imenukuliwa kutoka kwa Abu Hurayrah (R.A) kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu  (S.A.W)  amesema: (Lau watu wangelijua yaliyomo katika adhana na safu ya mwanzo, kisha wasingepata ila kwa kupiga kura, basi wangelipiga kura. Na lau wangelijua yaliyomo katika kuwahi  Swala, wangeliharakia kwenda. Na lau wangelijua yaliyomo katika Isha na Alfajiri, wangehudhuria hata kwa kutambaa.)) Wameipokea Bukhary na Muslim “Tahjiir” ni kwenda mapema kwenye Swala, iwe Swala yeyote ile.

Wanazuoni wametofautiana katika hukumu ya kurefusha Imamu rukuu akisubiri anayetaka kuswali ili aipate rakaa – na hii ndiyo hoja yetu:

Imamu Hanafi na Maliki wameona kwamba inachukiza kurefusha rukuu kwa ajili ya kumsubiri anayetaka kuswali. Ni kuchukizwa kwa haramu kwa upande wa Imamu Hanafi iwapo anamjua anayeingia. Na kama hamjui basi hakuna chukizo. Ama Imamu Maliki, kuchukizwa kunathibiti kwao kwa yule anayeongoza jamaa iwapo kutokurefusha hakutazua madhara, kama vile kuogopa kupata madhara yeye mwenyewe kutoka kwa aliyeingia au kuharibika kwa Swala yake kwa kuhesabu rakaa hiyo. Lakini kama ataswali peke yake, basi hakuna chukizo kabisa.

Wakati huo huo, Imamu Sahnun na Qadhi ‘Iyadh katika wafuasi wa Madhehebu ya  Imamu Maliki, na Shafi katika sahihi, na Imamu Ahmad katika riwaya, wameona kuwa inapendeza Imamu kurefusha rukuu akisubiri anayetaka kuswali. Hii ni kwa sharti kwamba huyo aliyekawia awe tayari yumo ndani ya msikiti wakati wa kusubiri, na asirefushe mno, na akusudie kwa hilo kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu wala si kujipendekeza kwa aliyeingia na kumpendelea.

Wametolea dalili katika hilo, miongoni mwazo: yaliyopokewa na Anas bin Malik (R.A), amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu  (S.A.W) amesema: (Hakika mimi huingia katika Swala nikiwa nataka kuirefusha, lakini husikia kilio cha mtoto, basi huifupisha kutokana na dhiki ya mama yake kwake.) Ameipokea Muslim.

Hadithi hii ni dalili kwamba Imamu akiwa kwenye rukuu na akahisi mtu anataka kuswali pamoja naye, basi anaweza kumsubiri katika rukuu ili aipate fadhila ya rakaa pamoja na jamaa. Kwa kuwa kama Imamu amepewa ruhusa ya kufupisha Swala kwa haja ya kidunia, basi ana ruhusa zaidi ya kuongeza kwa ajili ya ibada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, bali hili lina haki zaidi.

Na imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullah bin Shaddad kutoka kwa baba yake, amesema: Alitujia Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) katika moja ya Swala mbili za Alasiri: Adhuhuri au Alasiri, naye akiwa amembeba Hassan au Hussein. Kisha akatangulia Mtume (S.A.W), akamweka chini, kisha akasoma Takbira kwa ajili ya Swala. Akaswali. Kisha akasujudu katikati ya Swala yake sajda ndefu. Nikainua kichwa changu, nikamwona mtoto yuko juu ya mgongo wa Mtume (S.A.W) naye yuko katika sajda. Nikarudi katika sajda yangu. Alipomaliza Mtume  (S.A.W) Swala, watu wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, umesujudu katikati ya Swala yako sajda ndefu, tukadhani kuwa jambo limetokea au unateremshiwa Wahyi. Akasema: (Hakuna chochote kati ya hivyo, bali mwanangu alinipanda, nikachukia kumharakisha mpaka akamaliza haja yake.)) Ameipokea Ahmad katika “Musnad” yake.

Hili linaonesha kwamba mwenye kufanya mfano wa hivyo ndani ya Swala yake kwa haja iliyomjia au dharura iliyompata, basi hilo halibatilishi Swala yake wala halichukizi kwake ndani yake. Vivyo hivyo kwa anayemsubiri mwenzake aingie ili apate kutoka kwenye fadhila za jamaa alizotoka ili kuzipata kwa kuja kwake: hatakuwa kwa kitendo chake hicho amebatilisha Swala yake.

Na Imamu Shafi katika kauli moja na Hanbali katika riwaya wameona kwamba inachukiza kwa ujumla.

Basi, iwapo Imamu atarefusha rukuu akisubiri anayetaka kuswali akizingatia yale masharti yaliyotajwa awali na bila ya kudhurika watu kwa urefu huo, au akafupisha kwa kuwa anajua watu wataudhika iwapo atarefusha, basi amefanya vyema katika hali zote mbili. Na akiacha kabisa kusubiri basi hakuna ubaya juu yake. Jambo hili ni pana kutokana na tofauti za Wanazuoni.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Kwamba Imamu ana ruhusa ya kurefusha rukuu akisubiri anayetaka kuswali kwa sharti awe tayari ndani ya Msikiti wakati wa kusubiri, na asirefushe mno kiasi cha kuwasumbua waumini, na akusudie kwa kusubiri kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu wala si kujipendekeza kwa aliyeingia na kumpendelea.

Share this:

Related Fatwas