Swala ya Sunna kuswaliwa sehemu tof...

Egypt's Dar Al-Ifta

Swala ya Sunna kuswaliwa sehemu tofauti na ile iliyoswaliwa Faradhi

Question

Je, ni Sunna kuswali Swala za sunna sehemu tofauti na pale niliposwali Faradhi?

Answer

Inapendeza (ni Sunna) kwa mwenye kuswali —awe ni Imamu au maamuma—kusogea kutoka pale aliposwali Faradhi kadiri atakavyoweza, ili kutofautisha kati ya Swala ya Faradhi na ile ya Sunna, na pia ili sehemu nyingi zaidi za kusujudu na kuabudu zishuhudie ibada yake. Vilevile, inapendeza kwake kubadilisha sehemu kwa kila Swala anayofungua miongoni mwa Sunna. Iwapo hatofanya hivyo, basi ni vyema atenganishe kati ya Swala hizo kwa kutamka maneno yasiyo na dhambi, na inapendekezwa zaidi maneno hayo yawe ni dhikri ya Mwenyezi Mungu (S.W.).

Maelezo

Kisharia imebainishwa kwamba Swala za Sunna zenye kuthibitishwa (zile zenye kusisitizwa) zimegawanyika katika aina mbili: zipo ambazo hazihusiani na faradhi, na zipo ambazo zinafuata Faradhi au zina wakati maalumu ulio nje ya Faradhi. Swala hizi zinazoambatana na Faradhi huitwa “Rawatib”.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) alitupangia Swala hizi za Sunna Rawatib, kabla na baada ya Swala za Faradhi, na akazihusisha na ahadi ya pepo.

Akasema (S.A.W.): “Yeyote atakayekuwa daima akiswali rakaa kumi na mbili (12) kila siku na usiku ataingia peponi: nne (4) kabla ya adhuhuri, mbili (2) baada yake, mbili (2) baada ya magharibi, mbili (2) baada ya isha, na mbili (2) kabla ya Alfajiri.” (Hadithi hii imesimuliwa na An-Nasa’i kupitia Mama wa Waumini Aisha [R.A.]).

 

Vilevile, kuendelea kuswali Sunna mara kwa mara humpeleka mja katika hali ya kupendwa na Mwenyezi Mungu na kuwa miongoni mwa wapenzi Wake.
Abu Hurayra (R.A.) amesimulia kwamba Mtume (S.A.W.) alisema katika hadithi ya Qudsiy: “Mwenyezi Mungu amesema: Yeyote anayempiga vita rafiki (mpenzi) wangu, mimi humtangazia vita. Mja wangu hakaribii kwangu kwa jambo lolote nipendalo zaidi kuliko yale niliyomfaradhishia. Na mja wangu anaendelea kunikaribia kwa kufanya ibada za Sunna hadi ninampenda. Nikiisha kumpenda, huwa masikio yake anayoyasikia, macho yake anayoyaona, mkono wake anaoutumia, na mguu wake anaotembea. Akinisihi, nitampa; na akinseekea hifadhi, nitamkinga.” (Hadithi hii imepokelewa na Imam Bukhari katika Sahih yake).

Imependekezwa (ni Sunna) kutenganisha kati ya Swala ya Faradhi na Swala ya sunna kwa maneno kama vile dhikri au kusoma sehemu ya Qur’ani Tukufu, au kwa kitendo kama kusogea kutoka mahali uliposwali Faradhi kwenda sehemu nyingine. Hali hii inahusu pia kila swala ya Sunna ambayo mtu anaianza binafsi.

Kwa msingi huo, Wanazuoni wameafikiana kuwa inapendeza kubadilisha sehemu ya kuswali ili kutenganisha kati ya Faradhi na Sunna, na pia kuongeza idadi ya sehemu ambazo mtu amesujudia na kumuabudu Mwenyezi Mungu. Sehemu hizo zote zitakuwa mashahidi kwa mja Siku ya Kiyama, zikithibitisha ibada zake na utiifu wake kwa Mola wake.

Imepokewa kutoka kwa Al-Mughira bin Shu‘ba (R.A.) kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) alisema: “Imamu asiswali sehemu ile ile aliyoswalia swala ya faradhi mpaka aiondokee (asogee mbali kidogo).” (Hadithi hii imepokewa na Ibn Majah katika Sunan yake na wengineo).

Vilevile, Abu Hurayra (R.A.) amesimulia kuwa Mtume (S.A.W.) alisema:

“Je, mmoja wenu hawezi, baada ya kuswali, kusogea mbele au nyuma, au kulia au kushoto?” Yaani kwa ajili ya “as-subbhah” — ambayo ni swala ya sunnah baada ya Faradhi. (Hadithi hii pia imepokewa na Ibn Majah katika Sunan yake).

Hadithi hizi mbili zinathibitisha uhalali na kupendeza kwa mswali kusogea kutoka sehemu aliyoswalia Faradhi ili kuswali sunna, au kwa kila Swala ya Sunna anayoanza binafsi. Sababu ya hilo ni kuongeza idadi ya sehemu za ibada, kwa kuwa maeneo ambayo mtu amesujudia yatashuhudia kwake Siku ya Kiyama. Imepokelewa katika tafsiri ya kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Basi mbingu na ardhi havikulilia wao.” [Ad-Dukhan: 29]) kwamba, mja mwaminifu anapofariki, mahali alipokuwa akiswali duniani na njia ambamo amali zake zilikuwa zikipanda mbinguni humlilia.

Hivyo basi, hekima hii pia inaashiria kwamba inapendeza mtu kubadilisha sehemu kati ya Swala ya Sunna na Faradhi, na vilevile kwa kila Swala ya Sunna anayoianza. Na iwapo hatosogea, basi anashauriwa kutenganisha kati ya Swala hizo kwa maneno mema, ikiwezekana kwa dhikr au kusoma Qur’ani Tukufu.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Inapendeza (ni Sunna) kwa mwenye kuswali — awe ni Imamu au maamuma — kusogea kutoka pale aliposwali Faradhi kadiri awezavyo, ili kutofautisha kati ya swala ya faradhi na sunnah, na pia kupata ushuhuda wa maeneo mengi ya kusujudia na kuabudu ambayo yatamshuhudia Siku ya Kiyama.

Inashauriwa pia kwa mswali kubadilisha sehemu kwa kila Swala ya sunnah anayoiendeleza binafsi; na ikiwa hatofanya hivyo, basi anatakiwa kutenganisha kati ya swala hizo kwa maneno yasiyo na dhambi, na inapendekezwa zaidi maneno hayo yawe dhikri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Share this:

Related Fatwas