Kusoma Qur'ani Tukufu kwa Jamaa

Egypt's Dar Al-Ifta

Kusoma Qur'ani Tukufu kwa Jamaa

Question

Nimehifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na nina kituo cha kuhifadhisha Qur'ani Tukufu. Moja ya njia za kuhifadhisha watoto ni kuwaelekeza kusoma Aya kadhaa kwa pamoja kwa sauti moja; kwani inachochea bidii na inafaa zaidi kwa kuhifadhi. Pia nina nia ya kurekebisha njia hii kwa mfumo wa usomaji wa wasomaji mashuhuri, lakini mmoja wa marafiki zangu alinikataza kufanya hivyo akidai ni bidaa (uzushi). Je, hukumu ya kile ninachokifanya ni ipi?      

Answer

Inajuzu kukusanyika kwa ajili ya kusoma Qur'ani Tukufu kwa sauti moja; kwani kupendeza kukusanyika kwa kusoma Qur'ani Tukufu na kuifundisha kumekuja kwa ujumla, hivyo kunabaki kwa ujumla wake kunakokusanya aina mbalimbali za mkusanyiko katika kusoma na kuifundisha, kwa sharti njia hiyo isiharibu utukufu wa Qur'ani Tukufu na isisababishe usumbufu kwa wengine, kama vile mwenye kuswali, msomaji wa Qur'ani Tukufu, msomaji wa kitabu, au aliyelala.

Maelezo:

Sharia Tukufu imehimiza kujifunza Qur'ani Tukufu na kuifundisha, na Mtume (S.A.W) amemfanya mwanafunzi wa Qur'ani Tukufu na mwalimu wake kuwa ndio watu bora zaidi wa umma. Imepokelewa kutoka kwa Uthman Ibn Affan (R.A) kwamba Mtume (S.A.W) amesema: (Mbora wenu ni yule anayefundisha Qur'ani na akaifundisha) Imepokelewa kutoka kwa Al-Bukhari. Kusoma Qur'ani Tukufu ndio bora zaidi ya matendo yote ya wema; kwa sababu yule anayejifunza au kufundisha Qur'ani Tukufu anakuwa mbora na mwema zaidi ya watu, hii inaonesha kwamba kusoma Qur'ani Tukufu ndiyo bora zaidi ya matendo ya wema; na kwa sababu fadhila na ubora kwa mwanafunzi na mwalimu wa Qur'ani Tukufu, na kwa sababu hii imekuwa wajibu kwa anayejifunza kusoma na anayefundisha Qur'ani Tukufu kuwa bora na kupata fadhila kwa ajii ya Qur'ani Tukufu, na fadhila ya kufundisha inaendelea maadamu kila aliyefundishwa anasoma. Kujifunza na kufundisha Qur'ani Tukufu ni mambo yanayotakiwa kwa kusisitiza katika Sharia tukufu, kwa ngazi ya umma na kwa kiwango cha mtu mmoja mmoja.

Ama kwa ngazi ya umma: Wanazuoni wamekubaliana kwamba ni wajibu kwa Waislamu kushikamana na Qur'ani Tukufu kwa kuhifadhi, kuisambaza, kuijifunza, na kuifundisha. Na kwamba kuihifadhi Qur'ani yote na kuidhibiti ni Fardh Kifaayah (wajibu wa kutosheleza) kwa ujumla wa Waislamu, ikiwa baadhi yao watahifadhi, dhambi zinaondoka kwa waliobaki, na ikiwa wote wakiiacha, wote watapata dhambi.

Ama kwa ngazi ya mtu mmoja mmoja: Wanazuoni wamekubaliana kwamba inamlazimu kwa aliyekalifishwa na Sharia kuhifadhi Qur'ani Tukufu kile anachosimamisha kwacho Swala yake na faradhi yake.

Na kwa kuwa kujifunza na kufundisha Qur'ani Tukufu kunatakiwa na Sharia Tukufu, basi njia zote zinazopelekea kwenye kuijifunza na kuifundisha zinaruhusiwa kwa sababu hiyo, na miongoni mwa hizo ni kusoma Qur'ani Tukufu kwa jamaa, isipokuwa ikiwa njia yenyewe ni haramu; kwa sababu imethibitishwa kisharia kwamba njia hufuata hukumu za malengo.

Na jumhuri ya Wanazuoni wametoa dalili juu ya uhalali wa kusoma Qur'ani Tukufu kwa jamaa kwa sauti moja, bali wameitaja kuwa ni jambo linalopendelewa na lenye kupendeza. [1]

Imepokelewa kutoka kwa Imamu Malik kuchukiza kukusanyika kwa wasomaji wanaosoma Sura moja kwa pamoja, na hiyo ni kwa ajili ya kudhibiti baadhi ya njia zisizoruhusiwa za kusoma, kama vile kuwa pamoja na usomaji huo kwa kujaribu kuboresha sauti kwa baadhi yao kuongeza sauti yao kwa njia inayoondoa usomaji kutoka katika kanuni za tajwiid, au kwa sababu baadhi ya wanaofanya hivyo wanajitokeza katika mashindano ya kuhifadhi na kujionesha kwa kujitokeza mbele.

Kwa hiyo, ikiwa yataepukwa makatazo hayo katika usomaji, basi inajuzu kusoma kwa jamaa wakiwa wamekusanyika kwa sauti moja; kwa sababu imepokewa kuwa wema waliotangulia walifanya hivyo. Na miongoni mwa yaliyokuja katika kitendo cha Masahaba (R.A) ni kwamba Abu Darda' (R.A) alikuwa akisoma Qur'ani Tukufu na kikundi cha watu wakisoma wote kwa pamoja, kama ilivyoelezwa katika "At-Tibyan" ya Imamu Nawawi.

Suwed Ibn Abdul Aziz amesema: Abu Darda' alipomaliza Swala ya Alfajiri katika Msikiti mkuu wa Dimashq, watu walikusanyika na kumsomea, akawagawa kumi kumi na kuweka 'arif (msimamizi) kwa kila watu kumi, naye akisimama kwenye mihrab (sehemu ya Imamu) akiwatazama kwa macho yake, na akifanya makosa mmoja wao, anamwendea kwa 'arif wake, na akifanya makosa 'arif wao, anamwendea Abu Darda' kumuuliza kuhusu hilo. Na Ibn 'Amir alikuwa 'arif juu ya kumi, ndivyo Suwed alivyosema, na alipofariki Abu Darda', Ibn 'Amir alimrithi.

Imepokelewa kutoka kwa Muslim Ibn Mishkam amesema: Abu Darda' aliniambia: Nihesabie wanaosoma Qur'ani Tukufu kwangu, niliwahesabia elfu moja na mia sita na zaidi, na kila kumi kati yao walikuwa na msomaji, na Abu Darda' alikuwa akisimama juu yao. Na mtu anapotatizika jambo, alikwenda Abu Darda' (R.A). "Ma'rifat Al-Qurra' Al-Kibar" ya Adh-Dhahabi.

Na miongoni mwa yanayotumika kama ushahidi wa uhalali pia: iliyopokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (R.A) kwamba Mtume (S.A.W) amesema: “Hakuna watu wanaokusanyika katika moja ya nyumba za Mwenyezi Mungu (Msikiti), wakisoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Qur'ani Tukufu), na wakikijifunza baina yao, isipokuwa huteremshwa juu yao utulivu, na hufunikwa na Rehma, na Malaika wanawazunguka, na Mwenyezi Mungu anawataja kwa wale walio Kwake)) Imepokelewa na Imam Muslim.

Jumhuri ya Wanazuoni walitumia Hadithi zinazoonesha kupendeza kukusanyika kwa ajili ya dhikr (kumtaja Mwenyezi Mungu) kama ushahidi wa kupendeza kukusanyika kwa ajili ya kujifunza Qur'ani Tukufu kwa ujumla, na Qur'ani Tukufu ndiyo bora zaidi ya aina zote za dhikr.

Hadithi Tukufu imekuja kuonesha kwamba kukusanyika kwa ajili ya kusoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kukijifunza ni sababu ya radhi za Mwenyezi Mungu na kuteremka kwa rehema zake, na ni matini (dalili) ya jumla, hivyo inabaki katika ujumla wake unaojumuisha aina mbalimbali za kusoma kwa pamoja na kujifunza. Kwani imethibitishwa kisharia kwamba Mwenyezi Mungu anapoamrisha jambo kwa ujumla au bila moja kwa moja, linafahamika kwa ujumla na upana wake, na hairuhusiwi kulifunga au kuliwekea mipaka kwa namna moja pasina nyingine isipokuwa kwa dalili.

Pia, aina hii ya usomaji ina malengo mengi mazuri, miongoni mwayo: kuchochea bidii, kusaidia dhaifu, kuamsha alieghafilika, na kumsaidia yule asiyesoma vizuri kuhifadhi, pia inajumuisha fadhila ya kukusanyika katika vikao vya dhikr, na Qur'ani Tukufu ndiyo dhikr bora, tukufu, na ya juu zaidi.

Ni vizuri kusema kwamba usomaji huu lazima udhibitiwe na misingi na kanuni za usomaji na utendaji, na marejeo ya hayo ni kwa wanazuoni wa Qira'at (usomaji) na Iqra' (ufundishaji wa usomaji) katika kila nchi ya Kiislamu.

Na miongoni mwa yanayofunmana na kufaa jambo hili ni: kwamba njia hiyo isiathiri utukufu wa Qur'ani Tukufu, na isisababishe usumbufu kwa wengine, kama vile mwenye kuswali, msomaji wa Qur'ani Tukufu, msomaji wa kitabu, au aliyelala.

Tunapata faida  kutokana na yaliyotangulia:

Sharia Tukufu inahimiza kuijifunza Qur'ani Tukufu na kuifundisha.

Inajuzu kukusanyika kusoma Qur'ani Tukufu kwa sauti moja.

Kupendeza kukusanyika kusoma Qur'ani Tukufu na kuijifunza umekuja kwa ujumla, hivyo unabaki katika ukamilifu wake unaojumuisha aina mbalimbali za kusoma kwa pamoja na kujifunza.

 

[1] “Al-Majmu’” (2/166, chapa ya Dar Al-Fikr), na “Kashaf Al-Qina’” (1/255, chapa ya Alam Al-Kutub).

Share this:

Related Fatwas