Tatizo la matapeli wa uwekezaji

Egypt's Dar Al-Ifta

Tatizo la matapeli wa uwekezaji

Question

Hivi karibuni kumeenea kwa kiwango kikubwa mifano mipya ya watu wanaopewa jina la "Al-Mustarih" (Tapeli wa uwekezaji), hususan katika maeneo ya vijijini na Kusini mwa Misri kwa lengo la kufanya biashara. Kwa mfano, kuna mtu ananunua mifugo kwa bei ya juu kuliko ya soko, na pengine hata mara mbili ya thamani yake, lakini hamkabidhi muuzaji pesa zote bali anampa kiasi kidogo cha awali kwa muda wa siku 20. Kisha anaiuza mifugo hiyo kwa bei ya chini kuliko ya soko na kurudisha fedha hizo. Anafanya jambo hili na idadi kubwa ya watu, hadi watu wakaanza kumpa fedha zao ili awafanyie biashara. Je, nini hukumu ya miamala hii? Na nini hukumu ya anayempa mali yake kwa lengo la biashara?

Answer

Jambo la "Al-Mustarih"(Tapeli wa uwekezaji),  ni hila miongoni mwa hila za kukusanya fedha kutoka kwa watu, na lina picha nyingi kupitia njia mbalimbali, iwe katika biashara ya mifugo, magari, matunda na mbogamboga, n.k. Jambo hili linajumuisha jumla ya makatazo ya kisharia na ukiukaji wa kisharia; ambapo mbinu nyingi zimebainika kutumiwa na "Al-Mustarih" au mlaghai ili kunasa wahanga, kama vile kutumia uongo na udanganyifu. Kufanya muamala na watu hawa wanaoitwa "Al-Mustarih" ni miongoni mwa kupoteza mali ambayo imeamriwa ilindwe na kuhifadhiwa.

Maelezo

"Al-Mustarih" ni jina la kidesturi linalokusudiwa kumtaja mtu anayekusanya fedha kutoka kwa "wawekaji amana" kwa lengo la "kuzizuia kwa uwekezaji", na kuwadanganya kuwa watapata faida kubwa ya kifedha, hasa ikilinganishwa na viwango vya riba katika benki za Misri, kwa kudai kuwa anamiliki miradi ya uongo inayendeshwa kupitia mwonekano wa nje wa kihalali.

Huyu "Al-Mustarih" hununua bidhaa kwa bei ghali kuliko ya soko, kisha anaiuza kwa bei ya chini, ikiwa ni hila mpya ya kukusanya fedha za watu. na lina picha nyingi kupitia njia mbalimbali, iwe katika biashara ya mifugo, magari, matunda na mbogamboga, n.k.

Kwa mtazamo wa kisheria tu, miamala inayofanywa na "mtapeli" katika kununua na kuuza imeonekana kuwa na makatazo na ukiukaji kadhaa wa kisheria na kidini. Baadhi ya tafiti zimebainisha mbinu kadhaa zinazotumiwa na "mtapeli" au mlaghai kuwanasa waathiriwa wake, kama vile kutumia uongo na udanganyifu kuwapotosha waathiriwa. Uongo ndio kiini cha mbinu za ulaghai, na kwa kweli, ndio msingi wa mchakato wa ulaghai kwa ujumla. Uongo huo unaimarishwa na mwonekano wa nje unaoimarisha uwongo na kuwafanya wengine waamini katika uhalali wake, kama jaribio la kujenga uaminifu kwa wahanga, na pia kumpotosha na kuwanasa wahanga.

Miongoni mwa makatazo na ukiukaji huu ni:

Kwanza: Miamala hii inahusisha udanganyifu, uongo, na ulaghai, ambavyo vimekatazwa na kulaaniwa vikali na Sharia ya Kiislamu. Muslim amepokea kutoka kwa Abu Hurairah (R.A) kwamba Mtume (S.A.W) amesema: ((Anayetudanganya hayuko pamoja nasi)). Na katika mapokezi mengine: ((Anayedanganya hayuko pamoja nami)).

Na Abu Dawud na wengineo wamepokea kutoka kwa Sufyan Ibn Asid Al-Hadrami (R.A) akisema: Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) akisema: ((Ni khiana kubwa kumhadithia ndugu yako hadithi ambayo yeye anakuamini ilhali wewe unamwambia uongo)).

Na Muslim amepokea kutoka kwa Abdullah Ibn Mas'ud (R.A) kwamba Mtume (S.A.W) amesema: ((Shikamaneni na ukweli; kwani ukweli huongoza kwenye wema, na wema huongoza Peponi. Na mtu hataacha kusema ukweli na kuufuatilia ukweli mpaka aandikwe mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa ni mkweli (Siddiq). Na tahadharini na uongo; kwani uongo huongoza kwenye uovu, na uovu huongoza Motoni. Na mtu hataacha kusema uongo na kuufuatilia uongo mpaka aandikwe mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa ni mwongo).

Miongoni mwa upotoshaji na uongo wa anayefanya hivi ni kujiita "Al-Mustarih"; ili kuwaghilibu watu waamini watapata nafuu ya kiuchumi wakimpa fedha zao kwa ajili ya uwekezaji katika miamala hii ya biashara, jambo ambalo linapelekea kuvutia idadi kubwa ya wateja, na hiyo ni kuita vitu majina yasiyostahiki. Na kanuni kuwa kubadilisha jina hakubadilishi uhalisia wa kitu wala hakuondoi hukumu yake; kwani hukumu huzingatia maana na uhalisia, si majina na majengo yake.

Hila na hadaa kwa kutumia majina ya kupotosha ili kuhalalisha mali za watu huongeza dhambi, na hakumuondolei mtu uwajibikaji wa kisheria na kikanuni.

Sheria imekataza hila zinazokusudia kugeuza ukweli na kuvisha haramu vazi la halali kwa kuonesha mkataba wa halali ilhali unakusudia haramu, ikiwa ni udanganyifu na njia ya kufanya yale aliyokataza Mwenyezi Mungu, au kuacha wajibu, au kuzuia haki.

Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurairah (R.A) amesema: Mtume (S.A.W) amesema: ((Msifanye mliyoyafanya Mayahudi, mkahalalisha haramu za Mwenyezi Mungu kwa hila ndogo kabisa)). Imepokelewa kutoka kwa Ibn Battah katika kitabu cha "Ibtal al-Hiyal", na akasema Al-Hafiz Ibn Kathir: "Isnad yake ni nzuri".

Miongoni mwa mifano ya matumizi ya hayo katika Sunna: Aliyoyapokea Al-Bukhari na Muslim kutoka kwa Jabir Ibn Abdullah (R.A): Kwamba alimsikia Mtume (S.A.W) akisema mwaka wa kukombolewa Makka: ((Hakika Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wameharamisha biashara ya pombe, mizoga, nguruwe na masanamu)). Ikasemwa: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, unaonaje mafuta ya mizoga, kwani hupakwa katika meli, hupakwa ngozi, na watu huyatumia kwa ajili ya taa? Akasema: ((Hapana, ni haramu)). Kisha akasema Mtume (S.A.W): ((Mwenyezi Mungu awaangamize Mayahudi! Mwenyezi Mungu alipowaharamishia mafuta yake, waliyayeyusha kisha wakayauza na kula thamani yake)).

Al-Bukhari na Muslim Wamepokea pia kutoka kwa Ibn Abbas (R.A) akisema: Ilimfikia Omar bin Al-Khattab (R.A) kwamba fulani ameuza pombe, akasema: Mwenyezi Mungu amuangamize fulani, je, hajui kuwa Mtume (S.A.W) amesema: ((Mwenyezi Mungu awalaani Mayahudi, waliharamishiwa mafuta, wakayayeyusha na kuyauza)); yaani waliyayeyusha ili jina la mafuta liondoke. Inachukuliwa kutoka katika Hadithi hii: Ubainifu wa ubatili wa kila hila inayofikisha kwenye haramu, na kwamba hukumu haibadiliki kwa kubadilika kwa umbo na jina.

Miongoni mwa udanganyifu na uongo ni kile kinachofichwa chini ya mwamvuli wa biashara bila kuzingatia vigezo vya mapato ya halali. Ingawa biashara haina ukomo wa faida kisheria, kuna kanuni zinazoongoza mienendo ya mfanyabiashara kama vile kuzuia udanganyifu, kuzingatia uadilifu na wema, na kuzuia madhara.

Muslim amepokea kutoka kwa Abu Hurairah (R.A): ((Kwamba Mtume (S.A.W) alipita kwenye rundo la chakula, akaingiza mkono wake ndani yake, vidole vyake vikahisi unyevu. Akasema: Ni nini hiki ewe muuzaji chakula? Akasema: Kimenyeshewa na mvua ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Akasema: Kwa nini usikiweke juu ya chakula ili watu wakione? Anayedanganya hayuko pamoja nami)). Abu Ubaidah amesema: Maana yake ni kuwa udanganyifu si katika maadili yetu. Al-Azhari amesema: "Al-Subrah" ni rundo la chakula kilichokusanywa.

Bali Mwanachuoni Ibn Hajar Al-Haytami amehesabu aina hii ya udanganyifu kuwa ni miongoni mwa madhambi makubwa. Kinachochukuliwa kwa hadaa ni kula mali ya watu kwa batili kutokana na yule mlaghai kuwadanganya wamiliki wa mali kuwa watapata utajiri mkubwa, jambo ambalo Sharia imelikataza kwa ukali: {Wala msiliane mali zenu kwa baat'ili} [Al-Baqarah: 188]. Al-Bukhari na Muslim wamepokea kutoka kwa Abu Bakrah (R.A) kwamba Mtume (S.A.W) amesema: ((Hakika damu zenu, mali zenu na heshima zenu ni haramu baina yenu kama ilivyo haramu ya siku yenu hii, katika mwezi wenu huu, katika mji wenu huu...)).

Muslim amepokea pia: ((Kila Muislamu kwa Muislamu mwenzake ni haramu: damu yake, mali yake na heshima yake)). Na Al-Bayehaqi amepokea: ((Kila mwili uliomea kutokana na haramu (Suht), basi Moto ndio unauostahiki zaidi)).

Pili: Anachokifanya "Al-Mustarih" ni unyonyaji wa mali za watu unaosababisha maumivu na madhara kwao. Mwenyezi Mungu amesema: {Na wale wanao waudhi Waumini wanaume na wanawake pasina wao kufanya kosa lolote, bila ya shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilio dhaahiri.} [Al-Ahzab: 58].

Al-Tabari amepokea kutoka kwa Qatadah kuhusu Aya hii: (Na wale wanao waudhi Waumini wanaume na wanawake) "Tahadharini na kuwaudhi waumini, kwani Mwenyezi Mungu huwalinda na huwakasirikia wanaowaudhi". Na anayemsaidia mwingine katika hili anakuwa amesaidiana katika dhambi na uadui uliokatazwa: {Na saidianeni katika wema na uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui.} [Al-Ma'idah: 2].

Tatu: Miamala ya "Al-Mustarih" haina dhamana kwa wamiliki wa mali, hivyo ni njia ya kupoteza mali wakati Sharia imekuja kulinda misingi mitano ya maisha (Dini, Nafsi, Akili, Nasaba, na Mali). Kila kinachohifadhi misingi hii ni maslahi (Maslaha), na kinachopoteza misingi hii ni uharibifu (Mafsada).

Nne: Kuuza kwa bei ya chini kuliko ya soko kunaharibu usawa wa soko na kukivuruga kiuchumi. Imepokewa katika "Al-Muwatta" kutoka kwa Said Ibn Al-Musayyib (R.A) kwamba Omar Ibn Al-Khattab alimwambia mtu aliyeuza zabibu kwa bei ya chini kuliko wengine sokoni: "Aidha uongeze bei au uondoke katika soko letu". Fatwa imejengwa katika kuzuia uuzaji wa chini ya bei ya soko ikiwa utaharibu soko kwa picha tuliyoashiria.

Tano: jambo hilo linadhuru nchi na jamii kiuchumi, kisiasa na kijamii, ambapo husababisha uharibifu katika pato la taifa, kudorora kwa uchumi wa kitaifa, kuvurugika kwa miamala ya kibiashara, na kuongezeka kwa kiwango cha ukwasi wa ndani ambacho hakiendani na kiasi cha uzalishaji. Pia inadhoofisha roho ya ushindani miongoni mwa wafanyabiashara, na kusababisha kile kinachoitwa katika elimu ya uchumi (Ighraaq), pamoja na athari nyingine mbaya na matokeo mabaya, ambayo yanapingana na makusudio ya Sharia (Maqasid Al-Sharia); kwani kulinda uchumi wa nchi ni takwa la kisheria lililosisitizwa, na anayeuruhusu uharibifu huo anapata dhambi. Mwenyezi Mungu amesema: {wala msiasi katika nchi mkafanya uharibifu.} [Al-Baqarah: 60], na amesema Subhaanahu:{ Wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwisha tengenezwa.} [Al-A'raf: 56].

Na amepokea Al-Daraqutni na wengineo kutoka katika Hadithi ya Abu Said Al-Khudri (R.A) kwamba Mtume (S.A.W) amesema: ((Hakuna kudhuriana wala kulipizana madhara, na mwenye kudhuru, Mwenyezi Mungu atamdhuru, na mwenye kutia uzito, Mwenyezi Mungu atamtlia uzito)).

Pia, Sheria (ya Misri) namba 146 ya mwaka 1988 imepiga marufuku miamala ya uwekezaji inayofanywa nje ya makampuni rasmi ya hisa yaliyoidhinishwa kupokea fedha kwa ajili ya uwekezaji.

Kutokana na hayo: Miamala hii inayofanywa na watu hawa (Al-Mustarihun) ni haramu kisheria na ni jinai kikanuni, kwani imejumuisha jumla ya makatazo ya kisheria na ukiukaji wa kikanuni. Kufanya miamala na watu hawa wanaoitwa "Al-Mustarih" ni miongoni mwa kupoteza mali ambayo imeamriwa ilindwe na kuhifadhiwa.

Ofisi ya kutoa Fatwa ya Misri inawasihi raia kuwa makini na hatari ya aina hii ya miamala, na kuongeza uelewa wa kufanya kazi chini ya taasisi na makampuni rasmi ya kifedha yaliyosajiliwa, ambayo yanasimamiwa na nchi na yanatoa ulinzi unaohitajika kwa wanaofanya miamala hiyo.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Hila na hadaa kwa kutumia majina ya kupotosha ili kuhalalisha mali za watu huongeza dhambi na kosa kwa muhusika, na haimuondolei uwajibikaji wa kisheria na kikanuni.

Udanganyifu, uongo na hila huweza kufichwa chini ya mwamvuli wa biashara bila kuzingatia vigezo vya mapato ya halali.

Kuuza chini ya bei ya soko kunaharibu usawa wa soko na kulivuruga kiuchumi, jambo ambalo linadhuru nchi na jamii kiuchumi, kisiasa na kijamii, kwani husababisha uharibifu katika pato la taifa na kudorora kwa uchumi wa kitaifa.

Share this:

Related Fatwas