Uhuru wa mke katika kutumia mshahara wake na umiliki wa mali binafsi wa kila mmoja wa wanandoa.
Question
Je, mke wangu ana haki kwa kiwango gani katika mshahara wake binafsi? Na je, ana umiliki wa mali binafsi unaojitegemea?
Answer
Msingi wa uhusiano wa ndoa ni kuheshimiana, na familia za Kimisri kwa kawaida zimekuwa zikitegemea ushirikiano kati ya wanandoa, ambao umekuwa sehemu muhimu ya mahusiano ya kijamii ndani ya mfumo wa maisha ya ndoa. Hili linapongezwa kwa uhalisia wa Misri, ambapo maadili yamekita mizizi sana, na hatujaona jambo hili la kisheria likiibuliwa isipokuwa katika kesi za migogoro. Kwa hivyo, jambo hilo linahitaji ufafanuzi, kwa sababu mke ana umuliki wa mali tofauti kabisa na umiliki wa mali wa mume, na mkataba wa ndoa wenyewe hauathiri umuliki wa mali wa wanandoa kwa ujumuishaji kamili au sehemu yake, isipokuwa katika haki au masharti yanayotokana na mkataba wa ndoa. Ikiwa mke anafanya kazi halali kwa ruhusa ya wazi au isiyo wazi ya mumewe, basi mume hana haki ya kuchukua sehemu yeyote ya mshahara wake bila idhini yake, mume hawezi kudai haki ya sehemu yeyote ya mshahara wake kwa misingi kwamba anafanya kazi na anapokea mshahara kwa kazi hii. Kwa sababu ndoa si mkataba wa umiliki, na mume hana haki ya mali za mke wake, iwe alizipata kabla au baada ya mkataba wa ndoa. Yote haya yalikuwa tu katika kipengele cha kutekeleza haki zilizowekwa na Sharia.
Maelezo
Mahusiano kati ya wanandoa katika Uislamu yanategemea upendo, huruma, wema, na maelewano, kwani mmoja hupata faraja na utulivu kwa mwenzake, na kuhisi amani kwa uwepo wa mwenzake, kila mmoja humwambia mwenzake siri zote, akishiriki kile ambacho kimekatazwa kabisa kwa wengine kukiona. Hivyo, wanakuwa kama mtu mmoja, mume hujitolea kila kitu chenye thamani ili kumfurahisha mkewe na kutunza familia yake, na mke hutoa upendo, juhudi, na utajiri wake ili kuisaidia familia yake. Mwenyezi Mungu Anasema: “Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao”[Ar-Roum: 21].
Uislamu pia umeweka uhusiano huu juu ya msingi wa ushirikiano na usaidizi kati ya wanandoa katika kukabiliana na mizigo ya maisha na kutimiza mahitaji ya watoto wao. yote haya yanaambatana na wema na urafiki mzuri, ambayo ni moja ya sababu muhimu zaidi za kuanzishwa kwa ndoa, Mwenyezi Mungu Ameamuru wema kati ya mume na mke, hata katika hali ya kuachana kabla ya kuingiliana, amependekeza kila mmoja wao kufanya jambo ambalo litaondosha madhara na maumivu yanayosababishwa kwa mwenzake kwa kushindwa kukamilisha mkataba wa ndoa, na hii ni kwa kufariji mioyo yao na kurekebisha roho zao zilizovunjika, Mwenyezi Mungu Anasema: “Wala msisahau fadhila baina yenu.” [Al Baqara:237].
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu Ameamrisha kuoneshwe wema kati ya wanandoa iwapo talaka itatokea, inafaa zaidi kwamba wema uoneshwe kati ya mume na mke baada ya kumuingilia na kujenga ndoa imara, hii ni kwa sababu huhifadhi utulivu wa maisha ya ndoa, hujenga familia yenye afya na furaha, na huepuka chochote kinachoweza kuvuruga amani yake, kama vile tofauti na magaomvi, na kujipamba kwa maadili mema na sifa nzuri, pamoja na sifa nzuri na moyo safi, Miongoni mwa wema ambao mwanamume humwonesha mkewe ni uvumilivu wake kwake na ruhusa yake kwa mke wake kwenda kazini, Mwanamke hutoka kwenda kazini kwa ruhusa yake ya wazi au isiyo wazi, kwa sababu haki za ndoa ni za pande zote mbili, Mwanamume ana jukumu la kumtunza, na mwanamke ana jukumu la kuzingatia majukumu ya ndoa kwa mume, kama Mungu Mwenyezi Alivyosema: {Nao wanawake wanayo haki kwa Sharia kama ile haki iliyo juu yao}[Al-Baqarah: 228].
Hata hivyo, usaidizi ambao mwanamke hutoa kwa familia yake ni sababu ya moja kwa moja ya kuimarisha vifungo vya upendo na mapenzi kati ya wanandoa. Mwanamke ana haki ya kutumia mali zake kama mwanamume, na mwanamume anaweza kuchukua katika mali za mkewe kile anachompa kwa hiari. Sharia imemruhusu mke kumpa mumewe chochote anachotaka kutoka katika mali zake, na kumpa sadaka.
Yote haya yanaendana na kanuni ya kuheshimiana kati ya wanandoa, ambayo ndiyo njia bora na inayofaa zaidi ya kudumisha uhusiano imara wa ndoa unaohifadhi utulivu wa jamii.
Hata hivyo, ikiwa baadhi ya waume na wake hawafuati misingi ya kusaidiana na kuitanguliza kati yao, baadhi ya Wanazuoni wa Fiqhi wamempa mume haki ya kuifuta ruhusa hii na kumzuia mke kuendelea kufanya kazi, isipokuwa kama kuna wajibu alioufanya katika kazi hii kabla ya ndoa, katika hali hiyo, mume hana haki ya kumzuia kufanya hivyo.
Hii ndiyo maana ambayo sharia iliitumia ilipoweka mipaka ya haki hii kwa mume na kufanya ruhusa ya mume kwa mkewe kufanya kazi nje ya nyumba kuwa ruhusa ya lazima kwa mume inayodumu, muda wa kuwepo uhusiano wa ndoa kati yao, haki iliyohakikishwa kwake. Ikiwa atamtaka aache kufanya kazi na mke hakutii, hachukuliwi kama mkaidi na matunzo yake hayatapotea, kwa sababu alikubali aina hii ya kifungo na akaondoa haki yake ya zaidi ya hayo, isipokuwa kama kazi yake itakuwa ni kinyume na masilahi ya familia yake au anaitumia vibaya haki hiyo, kama Aya ya tano ya Kifungu cha Kwanza cha Sheria (ya Misri) Nambari 25 ya 1920, iliyorekebishwa na Sheria Nambari 100 ya 1985, ilivyoeleza yafuatayo: "Kuondoka kwake nyumbani bila ruhusa ya mumewe katika hali ambazo inaruhusiwa kwa hukumu ya Sharia, katika yale ambayo yameelezwa kwa maandishi, au yaliyokuwa katika desturi, au kumesababishwa na jambo la lazima, haitachukuliwa kuwa sababu ya matunzo ya mke kuondoka, wala kuondoka kwake kwa ajili ya kazi halali, ikitoonekena kwamba matumizi yake ya haki hii iliyowekewa masharti imetumika vibaya au kinyume na masilahi ya familia, na mume anamtaka kuachana nayo."
Na hili ndilo linalofanyiwa kazi na idara ya Fatwa na Mahakama, na inajulikana kwamba hukumu ya hakimu inaondoa tofauti.
Kuhusu uhuru wa kifedha wa mke: Imethibitishwa katika sheria ya Kiislamu kwamba mume ana dhima ya kifedha inayojitegemea mbali na mke wake, na kwamba mke pia ana dhima ya kifedha inayojitegemea mbali na mumewe. Saeed bin Mansur, Al-Daraqutni, na Al-Bayhaqi wamepokea kutoka kwa Hibban bin Abi Jablah kutoka kwa Al-Hasan, katika Hadithi mursal, kwamba Mtume S.A.W. amesema: "Kila mtu ana haki zaidi ya mali zake kuliko baba yake, mwanawe, na watu wote." Hadithi hii inaweka kanuni ya haki kamili ya mtu ya kutumia pesa zake.
Katika sheria ya Kiislamu, ndoa haimaanishi kuunganishwa kwa dhima ya kifedha ya mmoja ya wanandoa na ile ya mwingine, na hakuna mwanandoa yeyote aliye na haki, chini ya mkataba huu, ya kutumia pesa za mwingine isipokuwa kwa idhini yake.
Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:
Uhusiano kati ya wanandoa katika Uislamu unategemea upendo, huruma, wema, na maelewano, Mwanamke ana haki sawa ya kusimamia pesa zake mwenyewe kama mwanamume.
Mume anaweza kupokea mali kutoka kwa mkewe kama zawadi yeyote ambayo amempa kwa hiari.
Sheria ya Kiislamu inaruhusu mke kumpa mumewe chochote anachotaka katika mali yake na kumpa sadaka.
Ndoa katika sheria ya Kiislamu haipelekei kuunganishwa kwa mali za mmoja wa wanandoa wawili na mwingine, na hakuna hata mmoja wao, kwa mujibu wa mkataba huu, mwenye haki ya kutumia mali ya mwingine bila ruhusa yake.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
