Sifa" /> Sifa" /> Sifa" /> Egypt's Dar Al-Ifta | Malaika wa Mauti Kutoa Roho Nyingi ...

Malaika wa Mauti Kutoa Roho Nyingi ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Malaika wa Mauti Kutoa Roho Nyingi Kwa Wakati Mmoja

Question

Vipi Malaika wa Mauti hutoa roho za watu wengi katika wakati mmoja licha ya watu hawa kuwepo sehemu mbalimbali?

Answer

Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na waliomfuata.Ama baada ya hayo:

Neno mauti (kifo) katika lugha ni kinyume cha uhai, na maiti (mfu) kinyume chake ni hai (mwenye kuishi) [Al–Kamuus Al-Muhiyt Ju.1, uk. 160.ch. Mu’assasat Al Risaala].

Na maana ya mauti katika istilahi ni: Roho kutengana na mwili. [Al-Majmou’ Sharh Al Muhadhab, 5/105, ch.Dar Alfikr].

Abu Hamid Al-Ghazali anasema: “kutoa roho mwilini, maana yake ni kukata mahusiano kati ya roho na mwili, maana mwili haujaifuata roho” [Ihyaa’ Uluum Al-Diin Ju.4, Uk. 477, ch. Mustafa Al - Halabi].

Anayefisha bila shaka ni Allah S.W -Aliyetakasika na kutukuka- Allah S.W. amesema: {Sema “Enyi watu! Ikiwa mna shaka kutokana na Dini yangu, basi (mimi) siabudu ambavyo mnaviabudu badala ya Allah; lakini namwabudu Allah Ambaye Anakufisheni. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa Waumini”}. [YUNUS 104]. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na Mwenyezi Mungu amekuumbeni kisha anakufisheni} [AN NAHL 70]. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliyefisha. Kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu alimwumba Malaika wa mauti na akamjaalia awe mwakilishi wa kutoa roho za watu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Sema: “Atakufisheni Malaika wa mauti ambaye amewakilishwa kwenu, kisha kwa Mola wenu mtarejeshwa.”} [AS-SAJDAH 11]. Abdulrazzak na Ahmed wamenukuu katika kitabu cha Alzuhd, na vilevile Ibn-Jarir, Ibn-Almunzir, Abi-Hatim,Ibn-Abi Shaiba, na Abu-Sheikh kutoka kwa Mujahid alisema: “Kila mtu anayeishi mjini, kijijini, au jangwani Malaika wa mauti, humzunguka mara mbili kila siku.”

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu Aliwaumba wasaidizi wa Malaika wa mauti, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {hata yanapomfikia mmoja wenu mauti, Wajumbe Wetu humfisha} [Al AN-AM 61]. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Basi itakuwa vipi (pale) Malaika watakapowafisha (huku) wakiwapiga nyuso zao na migongo yao?} [MUHAMMAD 27]. Pia Allah S.W anasema: {Na kama ungewaona madhalimu watakapokuwa katika mahangaiko ya mauti, na Malaika wamewanyoshea mikono yao (na kuwaambia) “Zitoeni roho zenu!} [AL AN-AM 93]. Na Abdulrazzak, na Ahmed wamenukuu katika kitabu cha “Alzuhd”, na vilevile Ibn Jarir, Ibn-Almunzir, na Abu-Sheikh katika kitabu cha “Al-Adhama”, na Abu-Naiim katika kitabu cha “Al-Hilya” kutoka kwa Mujahid alisema: “Ardhi imejaaliwa kama ni bakuli, na Malaika huchukua kutoka mahali popote apendapo na Malaika huyu ana wasaidizi ambao wanazifisha nafsi, kisha Malaika anazitoa roho za nafsi hizi”. Na Ibn-Jarir na Abu-Sheikh wamepokea kutoka kwa Al-Rabii Ibn-Anas anasema: “Yeye aliulizwa kuhusu Malaika wa mauti: Je, yeye peke yake anafisha roho? Alijibu: Yeye anatawala mambo ya roho na ana wasaidizi wanaomsaidia, lakini Malaika huyu ni kama kiongozi anayetoa amri kwa wasaidizi kutoa roho kutoka mashariki hadi magharibi". Ibn Abi Shaiba, Ibn jarir, Ibn Almunzir, Ibn Abi-Hatim, na Abu-Sheikh wamenukuu katika kitabu “AL Tafsir” kutoka kwa Ibn Abaas alisema kuhusu kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wajumbe wetu humfisha} [Al AN-AM 61], maana yake wao ni wasaidizi wa Malaika wa mauti”. Na Abdu Ibn Humaid, Ibn-Almunzir, na Abu Al Sheikh katika kitabu “AL Tafsir”, wamepokea kutoka kwa Ibrahim Al Nakh’I kuhusu kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {wajumbe wetu humfisha} [Al AN-AM 61] alisema: “Malaika wanatoa roho, kisha Malaika wa mauti anazitoa baada yao”. Abdulrazzak, Ibn Jarir, na Abu Sheikh katika kitabu cha “AL’Adhama” wamepokea kutoka kwa Katadah alisema kuhusu kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu {wajumbe wetu humfisha} [Al AN-AM 61]: “Hakika Malaika wa mauti ana wajumbe wanaozitoa roho kisha wanazituma kwa Malaika wa mauti” Abu Sheikh katika kitabu cha (Al Adhama) amepokea kutoka kwa Wahb Ibn Munabbih alisema: Malaika ambao wanaambatana na watu ndio wanaowafisha na wanaandika umri wao, na wanapozifisha roho zao wanazituma kwa Malaika wa mauti”.

            Al Imam Al Tabariy alisema katika tafsiri yake kuhusu kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu {wajumbe wetu humfisha}: “kama mtu yoyote atauliza: Je anayefisha roho si Malaika wa mauti? Basi kwa sababu gani ilisemwa: {wajumbe wetu humfisha} na neno wajumbe ni wingi, ilhali Malaika wa mauti (katika kiarabu) ni mmoja? Na katika sura nyingine alisema: {Sema: Atakufisheni Malaika wa mauti aliyewakilishwa kwenu, kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu.”} [AS-SAJDAH 11]? Jibu ni kwamba inafaa kusema kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu alimpa Malaika wa mauti Malaika wasaidizi, wanaofisha watu kwa amri ya Malaika wa mauti. Kwa kuwa yeye anatoa amri basi ni kama vile yeye aliyefisha, maana bila ya amri yake hakuna kufisha. Na hali hii ni kama hali ya kitendo cha kuua na kupiga mjeledi kinachonasibishwa kwa Sultani. Sultani mwenyewe hatendi kitendo hicho lakini wasaidizi wake ndio wanaofanya kitendo. Kundi la Maulama walitoa maana hii, miongoni mwao ni Ibn Abaas, Katada, Mujahid, na Al Rabii Ibn-Anas” [Jamii Al Bayaan Fii Ta’wiil Al-Qurani, Ju.9, Uk.290, Ch. Hajr, kwa kufanya mabadiliko].

            Al Qurtubi anasema: Kuhusu kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba {Wajumbe wetu humfisha} wasaidizi wa Malaika wa mauti ambao humfisha binadamu. Hii ni kauli ya Ibn Abaas na wengine. Wasaidizi hawa hung’oa roho kutoka mwilini, inapokuwa tayari kutolewa basi malaika wa mauti huifisha kwa kuichukua. Al Kalbi anasema kwamba Malaika wa mauti huichukua roho kutoka mwilini kisha akaikabidhi kwa Malaika wa rehma iwapo aliyefishwa ni muumini au kuikabidhi kwa Malaika wa adhabu iwapo aliyefishwa ni kafiri. Na baadhi ya wakati kufisha hunasibishwa kwa Malaika wa mauti kama Alivyosema Mwenyezi Mungu {Sema: “Atakufisheni Malaika wa mauti aliyewakilishwa kwenu kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu”} [AS-SAJDA,11]. Na mara nyingine kufisha hunasibishwa kwa Malaika wasaidizi kama ilivyotajwa katika aya {Wajumbe wetu humfisha} [AL-AN-AM 61]. Na mara nyingine kufisha hunasibishwa kwa Mwenyezi Mungu ndiye mfishaji halisi wa kweli kama alivyosema Mwenyezi Mungu (Mwenyezi Mungu anafisha nafsi wakati wa mauti yao) [AZ-ZUMAR 42], {Sema: “Mwenyezi Mungu (anakuhuisheni) anakupeni uhai, kisha anakufisheni} [AL-JATHIA 26], maana kila Malaika anapopokea amri hufanya aliyoamrishwa [Tafsiir Al Qurtubi, Ju.7, Uk.7, Ch.Dar Al Kutub Al Misriya].

            Al Raazi alisema katika kitabu chake “Mafatiih Al Ghaib”: Mwenyezi Mungu alisema: {Mwenyezi Mungu anafisha nafsi wakati wa mauti yao} [AZ-ZUMAR 42], na alisema: {Ambaye ameumba mauti na uhai} [AL-MULK 2]. Aya hizi mbili zinaonesha kwamba kufishwa kwa roho hakutokei isipokuwa kutokana na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kisha anasema: {Atakufisheni Malaika wa mauti} [AS-SAJDA 11], maana yake kufishwa kwa roho hufanyika na Malaika wa mauti. Kisha anasema katika aya hii {Wajumbe wetu humfisha} [AL-AN-AM 61]. Aya hizi tatu zinaonekana kama vile zinakinzana. Lakini jawabu ni kwamba kifo ukweli wake kinatokana na kadari ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na katika ulimwengu wa nje -mazingira ya vitendo- jukumu hilo (kifo) hupewa Malaika wa mauti ambaye ana wasaidizi na watumishi ambao wanamsaidia. Kwa hivyo ilikuwa bora kunasibisha kifo kwa watatu (Mwenyezi Mungu, Malaika wa mauti, na Wajumbe wasaidizi) kwa mujibu wa mazingatio matatu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi wa hayo. [Mafatiih Al Ghaib, Al Raazi, Ju.13, Uk.15, Ch. Dar Ihyaa’ Al Turath Al Arabiy]

            Na kwa mujibu wa maelezo yaliyotangulia juu, Malaika wa mauti ndiye anayepewa jukumu la kutoa roho. Naye ana wasaidizi wake kama ilivyotanguliwa kusemwa. Si jambo la kushangaza kwamba Malaika wa mauti anachukua roho mbalimbali kwa wakati mmoja kwa kutumia wasaidizi wake Malaika. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye mjuzi wa hayo.

Share this:

Related Fatwas