Hukumu ya kuamkiana na asiyekuwa mw...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya kuamkiana na asiyekuwa mwislamu

Question

Nini hukumu ya kuamkiana kati ya mwislamu na asiyekuwa mwislamu kwa kuanza salamu au kuijibu. Kwa mujibu wa maamkizi ya kiislamu au mengineyo?

Answer

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehema na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:
Neno (Maamkizi) katika lugha ya kiarabu ni (Tahiyah), maana yake ni: Dua kwa ajli ya kuishi, kama vile (Attahiyatu Lillahi) yaani: kubaki, au kumiliki. Lakini matumizi haya yameongezeka mpaka yakawa yanatumiwa katika maamkizi kwa ujumla n.k.
Maamkizi ambayo Mwenyezi Mungu ameyajaalia kwa waja waumini duniani na akhera ni Salamu. Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu amewawekea sheria, wakikutana, wakitaka kuombeana dua wenyewe kwa wenyewe waseme: (Assalaamu Alaikum Warahmatu Allahi Wwabarakatuh). [Lisaan Al-Arab, 14/216, Ch. ya Dar Sader, na Al-Misbaah Al-Muniir, Kidahizo (Hayya), 1/160, Ch. ya Al-Maktabah Al-Elmiyah, na Tafsiir Al-Qurtubiy, 5/297-98, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Masriyah].
Kimsingi, kutoa salamu ni sunna, na kuijibu salamu ni fardhi kifaya (ya kutoshelezeana), ikiwa salamu hiyo itatolewa kwa kundi la watu. Lakini ikitolewa kwa mtu mmoja, basi kujibu wakati ule ni wajibu. Na hali hii inahusu waislamu wenyewe kwa wenyewe, kama alivyosema hayo Imam Al-Nawawiy katika kitabu chake (Al-Rawdah): "kutoa salamu ni Sunna iliyotiliwa mkazo, kama akiitoa mtu mmoja salamu kwa mtu mwingine, basi inalazimika kumjibu. Akitoa salamu kwa kundi la watu, basi kuijibu ni fardhi kifaya (ya kutoshelezeana). Akiijibu mmoja wao, basi jibu lake linatosha kwa niaba ya wengine. Kama wakijibu wote, basi watakuwa wanatekeleza fardhi, ni sawa sawa wakijibu wote kwa pamoja, au mmoja mmoja. Kama hawajajibu wote, basi watapata dhambi. Akijibu salamu asiyekusudiwa, basi haitoshelezi kwa wale waliosalimiwa. Kuanza kutoa salamu kunakuwa ni sunna ya kutoshelezeana kwa walio wengi. Watu wengi wakikutana na wengine, na mmoja wao akitoa salamu kwa hao wengine, basi inatosha katika utekelezaji wa Asili ya sunna". [Rawdatu Al-talibiin, na Al-Nawawiy, Ch. ya Al-Maktab Al-Islamiy].
Kuhusu asiyekuwa mwislamu, pana masuala mawili: Kwanza ni kujibu salamu, Pili ni kutoa salamu.
Kuhusu kujibu salamu ya asiyekuwa mwislamu, salamu hiyo iwe salamu ya kawaida (maamkizi ya kawaida), au kwa kutumia salamu ya kiislamu, nayo ni (Assalaamu Alaikum). Ikiwa ametoa salamu ya kawaida, sheria inalazimisha kumjibu, kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na mnapoamkiwa kwa maamkizi yo yote yale, basi itikieni kwa yaliyo bora kuliko hayo, au rejesheni hayo hayo}. [AN NISAA: 86].
Al-Mawardiy anasema katika tafsiri ya aya hii: "Salamu ni jambo lenye fadhila nyingi na liinapendeza, na kuijibu kwake ni faradhi. Na hii ina kauli mbili, kwanza ni faradhi ya kujibu na inamhusu mwislamu na kafiri, na hii pia ni kauli ya Ibn Abbas, Qatadah na Ibn Zaid. Ya pili inahusu waislamu wala si makafiri, na hii pia ni kauli ya Ataa'. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu {kwa yaliyo bora kuliko hayo}, inamaanisha kuongeza dua ". [Tafsiir Al-Mawardiy: Al-Nukat wal Uyuun, 1/513, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah].
Katika Tafsiri ya Zaad Almasiir na Ibn Aljawziy: "Qatadah anasema: maana ya (kwa yaliyo bora kuliko hayo) kwa mwislamu, na (au rejesheni yayo hayo), kwa watu wa Kitabu". [1/441, Ch. ya Dar Alkitaab Alarabiy].
Albaji anasema: "Na Abullahi Ibn Abbas anasema: hii ni kwa ujumla, kama vile mtu akikuamkia na akisema (Salamun Alaika), utajibu (Alaika Assalaamu Warahmatul Lahi) na hayo ni bora kuliko aliyoyasema. Kama ukitaka kurejesha hayo hayo, utasema (Alaika) tu. Na imepokelewa na Al-Shaa'biy kauli yake kwa yahudi mmoja (Alaika Assalaamu Warahmatul Lahi), Na alipoulizwa juu ya sababu ya kauli yake kwa Yahudi (Warahmatul Lahi), alisema: Je,Yeye haishi katika rehma ya Mwenyezi Mungu?. [Almuntaqa, Sharh Almuwatta', 7/281, Ch. ya Matbaa't Alsaa'adah].
Ama mtu asiyekuwa mwislamu akitoa salamu akisema: (assalamu alaikum), maoni ya wanachuoni wengi kuwa: inatosha kujibu kwa usemi (waalaikum), na hayo ni kutokana na Hadithi zilizopokelewa katika mlango wa salamu, miongoni mwake ni ile aliyoipokea Al-Bukhary, kutoka kwa Anas R.A. alisema: Mtume S.A.W. amesema: "Watu wa Kitabu wakikusalimieni, basi jibuni: (waalaikum), na kutoka kwa Ibn Omar R.A. kuwa Mtume S.A.W. amesema: "Mayahudi wakikusalimieni wakasema: (assaamu alaikum (yaani mauti yawe juu yenu:), basi jibuni : (waalaikum)".
Al-Ramly anasema: "Mtu wa Dhima akimsalimia Mwislamu, analazimika kumjibu (Waalaika)". [Nihayatul Muhtaaj, 8/48, Ch. ya Mustafa Al-Halabiy].
Kwa hivyo, inawezekana kusemwa kuwa: mapokezi ya pili yamebainisha sababu ya jibu hili fupi; kwa kuwa mayahudi walikuwa wakisema: (assamu) yaani (mauti). Lakini mwislamu akiwa na yakini kuwa mtu wa dhima ametoa salamu ya kweli, akisema: (assalamu alaikum), basi mwislamu amjibu (waalaika assalaam). Kwa hiyo, baadhi ya wanachuoni wamezingatia hivyo.
Ibn Al-Qayyim anasema: "hayo yote yamezingatiwa ikiwa yakini imepatikana kuwa amesema: (assamu alaikum), au ametilia shaka kwa alivyosema. Kama msikilizaji ana yakini kuwa mtu wa Dhima amesema: (salamun alaikum), Je, mwislamu anajibu: (waalaika assalam), au inatosha kusema: (waalaika)? katika jambo hili, dalili za kisheria na misingi ya Sheria zinalazimisha kusema: (waalaika assalaam). Hakika huu ni uadilifu, na Mwenyezi Mungu anaamuru kufanya uadilifu na wema. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na mnapoamkiwa kwa maamkizi yoyote yale, basi itikieni kwa yaliyo bora kuliko hayo, au rejesheni hayo hayo}, kwa hiyo, amependezesha ubora na amewajibisha uadilifu. Na hayo hayapingani hata kidogo na hadithi za mlango wa salamu. Hakika Mtume S.A.W. ameamuru kufupisha jibu liwe (waalaikum) kutokana na sababu iliyotajwa, ambayo walikuwa wanaitumia katika salamu yao, na ameiashiria Mtume S.A.W. katika hadithi ya Bibi Aisha R.A., akisema: "Ati, hunioni nikisema: (waalaikum), hapo waliposema (assamu alaikum), kisha akasema: watu wa Kitabu wakikusalimieni, semeni: (waalaikum)".
Na tuyazingatie haya kwamba jibu la salamu linakuwa kwa mujibu wa salamu yenyewe ilivyotolewa. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na wafikapo kwako wanakuamkia kwa (maamkizi) ambayo siyo maamkizi aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu uwamkie kwa maamkizi hayo, na husema katika nyoyo zao: "Mbona Mwenyezi Mungu hatuadhibu kwa haya tunayoyasema?" kama sababu ikiondoka, na mtu wa Kitabu akisema: (salaamun alaikum warahmatul Lahi), hapo uadilifu katika kujibu unalazimika kumjibu sawa sawa na salamu yake. [Ahkaamu Ahl Al-Dhimah, 1/199-200, Ch. ya Dar Alilm Lilmalaayiin].
Al-Nafrawiy anasema: "kama mwislamu ana yakini kuwa mtu wa Dhima ameshatamka salamu, hapo analazimika kumjibu, huenda kusudio lake ni dua, na hivi ndivyo alivyosema Al-Ajhuuriy. [Alfawakeh Aldawany, 2/425-6, Ch. ya Mustafa Al-Halabiy].
Al-Mawardiy anataja rai moja ya wanazuoni wa Fiqhi wa Madhehebu ya Al-Shafiiy, nayo ni: anajibu salamu yao kwa kauli yake: (waalaikum ssalaam), lakini hasemi (warahmatul Lahi), kama itakavyokuja katika maneno ya Al-Nawawiy katika (Al-Adhkaar).
Ama kuanza kwao kutoa salamu- na hili ni suala la pili-: huenda maamkizi ya kawaida, au maamkizi ya kiislamu, nayo ni (assalaamu alaikum). Ikiwa maamkizi kwa salamu, inawezekana kutoa dalili ya kujuzu kwa hadithi inayopokelewa na Al-Bukhary, kutoka kwa Abdillahi Ibn Amr kuwa mtu mmoja alimuuliza Mtume S.A.W. "Uislamu gani ni bora? Akasema: Kuwalisha masikini chakula, kutoa salamu kwa unayemjua na usiyemjua".
Ibn Rajab Al-Hanbaliy anasema katika maelezo ya Hadithi hii: kauli yake: "kutoa salamu kwa unayemjua na usiyemjua" inazingatiwa ni aina bora zaidi ya namna ya kutoa salamu. Na imepokelewa katika Almusnad (Kitabu cha Imam Ahmad), kutoka kwa Ibn Masu'ud, kutoka kwa Mtume S.A.W. "Hakika miongoni mwa alama za Kiyama ni kutoa salamu kwa unayemjua tu". Na hapo wanaepushwa wale ambao haijuzu kwetu kuanza kuwasalimia kama watu wa Kitabu, kwa mtazamo wa wengi wa wanachuoni. Lakini rai hii si ya pamoja, kwa kuwa idadi kubwa ya wanachuoni walieleza kuwa inajuzu kwetu kuanza kuwasalimia watu wa Kitabu, na miongoni mwao wamesema kuwa ni Makruhu (Jambo lenye Kuchukiza) lakini si haramu, na miongoni mwao wameruhusu hayo wakati wa masilahi au haja. [Fath Al-Bariy, na Ibn Rajab, 1/44, Ch. ya Maktabat Al-Ghurabaa' Al-Athariyah, Al-Madinah Al-Munawarah].
Ibn Hajar alisema- na Al-Ainiy alimfuata- kuwa: huenda hadithi hii ilikuwa katika mwanzo wa Uislamu, kwa ajili ya kufanya urafiki, kisha likaja katazo. [Rejea: Fath Al-Bariy, na Ibn Hajar, 1/56, Ch. ya Dar Al-Maarifah; Umdatul Qary, 1/138, Ch. ya Dar Ihyaa' Al-Turaath Al-Arabiy].
Lakini tukikubali kauli hii, basi suala la kufanya urafiki halimaliziki; na Mwislamu anaamrishwa kufikisha Dini ya Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Sema: "Hii ndiyo njia yangu; ninaita (ninalingania) kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa ujuzi wa kweli; mimi (nafanya hivi) na (kila) wanaonifuata. Na Mwenyezi Mungu ametakasika na kila upungufu; wala mimi simo miongoni mwa wanaomshirikisha (Mwenyezi Mungu)".
Al-Nawawiy anasema: " Ama juu ya watu wa Dhima, wenzetu walihitilafiana katika hukumu yao, wengi wanasema kuwa: haijuzu kuanza kuwasalimia, na wengine wanasema: hayo si haramu, lakini ni Makruhu (inachukiza), wakimsalimia mwislamu, basi atawajibu: (waalaikum) na bila kuongeza. Na Kadhi mkuu AlMawardiy alitaja rai kwa baadhi ya wenzetu kuwa: Inajuzu kuanza salamu, lakini mwislamu anapotoa salamu aseme: (assalaamu alaika), kwa kutumia tamko la umoja, na si la wingi. Kuna rai nyingine ya Almawardiy kuwa: mwislamu anawajibu wa kujibu salamu, wakianza wao kumsalimia aseme: (waalaikum assalaam), wala hasemi: (warahmatul Llahi). Lakini rai hizi mbili zilizotangulia si za kawaida na hazikubaliki.
Abu Saad Almutawaliy anasema: Mwislamu akitaka kumsalimia mtu wa Dhima amsalimie bila ya kutumia tamko la salamu, kama vile, (Mungu akuongoze) au (Aipendezeshe asubuhi yako). Kwa vyovyote, rai hii ya Abu Saad haidhuru, ikiwa na haja. Kwa hiyo mwislamu anaweza kusema: (Sabalkheri), (asubuhi ya furaha), (asubuhi ya afya), (asubuhi ya neema) n.k. [Aladhkaar, na Imam Al-Nawawiy. Uk. 263, Ch. ya Dar Al-Ghad Al-Arabiy].
Al-Haskafiy wa Madhehebu ya Hanafiy anasema: "Mwislamu anawasalimia watu wa Dhima akiwa na haja, lakini asipokuwa na haja, basi inachukiza. Na hii ni rai sahihi. Kama ambavyo inachukiza pia kwa mwislamu kupeana mkono na mtu wa Dhima. Hapo, Yahudi, Mkristo, au Majusi akimsalimia mwislamu, si kosa kumjibu, lakini haongezi isipokuwa aseme (waalaika), kama ilivyokuja katika Al-Fatawa Al-Khaniyah. [Al-dur Al-Mukhtaar, 5/733].
Ibn Abidiin anasema katika kitabu chake (Alhashiyah), katika sura ya (Mwislamu anawasalimia watu wa Dhima): "Je, inajuzu kutumia tamko la wingi, ikiwa anayesalimiwa ni mmoja? Ni wazi kuwa anatumia tamko la umoja, kwa kipimo cha kujibu. Katika Sheria: Mwislamu akiwasalimia watu wa Dhima, atasema: (Salamu juu ya anayefuata uongofu), na hivyo hivyo, anapowaandikia.
Katika Fatawa Al-Ttatarkhaniyah, Imamu Muhammad anasema: ukimwaandikia myahudi au mkristo kwa ajili ya haja, uandike: salamu juu ya anayefuata uongofu.
Kuhusu maelezo ya Al-Haskafiy yaliyotangulia, kauli yake (akiwa na haja), yaani mwislamu anamuhitajia mtu wa Dhima, na haya hufahamika kutokana na hali ilivyo. Imekuja katika Al-Fatawa Al-Tataarkhaniyah: katazo la kutoa salamu kutokana na kuiheshimu salamu hiyo. Na hali hii ya kuiheshimu salamu hapatikani ikiwa salamu itatolewa kutokana na haja. Kauli yake (na hii ni rai sahihi), yaani haidhuru kwa ujumla, kama ilivyotajwa katika Alfatawa Alkhaniyah, kutoka kwa baadhi ya mashekhe. Kauli yake (kama inachukiza kwa mwislamu kupeana mkono na mtu wa dhima), yaani bila haja, kama ilivyokuja katika Fatawa Al-Qunyah: Haidhuru kwa mwislamu kupeana mkono na jirani yake mkristo kama akirejea safari yake, na akiacha kumpa mkono hatadhurika. [Rad Al-muhtaar Ala Al-dur Almukhtaar, 5/265, Ch.ya Dar Ihyaa' Al-Turaath Al-Arabiy].
Kuhusu maamkizi kwa tamko lisilo la Salamu, kama vile (Sabalkheri), bila shaka yanaruhusiwa; kwa kuwa kuna ruhusa ya kuanza kwa kuamkia kutokana na maneno yaliyopatikana, basi kuamkia bila ya kutumia tamko la Salamu ni bora.
Miongoni mwa wanaoruhusu suala hili la (kuamkia bila ya kutumia tamko la Salamu), ni Imam Ibn Taimiyah; mwanafunzi wake Ibn Muflih amepokea kutoka kwake kuwa: Inajuzu kuamkia mtu wa Dhima kwa tamko kama vile (habari ya asubuhi)?, (Habari ya jioni)? (Habari yako)? na (Hali gani)? Kisha Ibn Muflih amesema: na afanye hivi kwa nia ya kwamba Mwenyezi Mungu amwongoe; kwa kuwa Alharbiy alimuuliza Imam Ahmad: nikiamkia mtu wa Dhima, inajuzu kusema: (Mungu akukirimu), Imam akajibu: Ndiyo, kwa maana ya: kwenye Uislamu, inajuzu pia kusema; (Mungu akuongoze). Imam Abu Almaa'ly aliongeza: (Mungu akuzidishie umri) n.k.
Ibn Muflih anasema: kama mtu wa Dhima akisalimia, inalazimika kujibiwa kwa kusema: (alaikum) au (alaika). Ibn Taimiyah anasema: kwa kujibiwa maamkizi yake, pia inajuzu kusema: Ahalan wasahlan.
Ibn Muflih anasema: "Inaharamishwa kuanza kumsalimia mtu wa Dhima, ama kwa haja inawezekana. Abudawuud amepokea kuwa: kwa haja haipendezi kwa upande wangu, vile vile: habari yako, habari ya asubuhi, au hali gani? Lakini Ibn Taimiyah aliyajuzisha hayo yote. Na afanya hivi kwa nia, kama Alharbiy alivyomuuliza Imam Ahmad: inajuzu kusema: Mungu akukirimu. Na Imamu akajibu: Ndiyo, yaani katika Uislamu, kama ambavyo inajuzu pia kusema: Mungu akuongoze. Na Abu Almaa'ly aliongeza: Mungu akuzidishie umri, n.k. kama mtu wa Dhima akisalimia, inalazimika kujibiwa kwa kusema: (alaikum) au (alaika). Ibn Taimiyah anasema: kujibiwa maamkizi yake, pia inajuzu kusema: Ahalan wasahlan". [Alfuruu', 6/271, Ch. ya Alam Alkutub, na Alfatawa Alkubra, 5/544, Ch. ya Dar Alkutub Alilmiyah].
Kwa mujibu wa yaliyotangulia: si vibaya kuanza maamkizi ya kawaida au kwa tamko la Salamu, wakati wa haja. Ama kujibu maamkizi ni wajibu. Ikiwa maamkizi hayo ni kwa tamko la Salamu, lazima jibu liwe kamili, iwapo hatukujua kuwa mwenye kusalimia amepotosha maana sahihi ya salamu, na kuwa yale maamkizi tunayoyachukia. Na hii ni kauli ya baadhi ya wanachuoni, kama ilivyotangulia.
Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa yote.
 

Share this:

Related Fatwas