Mwanamke na Familia Katika Uislamu ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Mwanamke na Familia Katika Uislamu Misingi yake kwa Ujumla na Mtazamo wa Kiislamu.

Question

Je, tunaweza kupata baadhi ya misingi kwa ujumla ya mtazamo wa Kiislamu kuhusu mwanamke na familia?

Answer

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehema na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:
Bila shaka kuna misingi ya mtazamo wa Kiislamu kuhusu mwanamke na familia, inayobainisha ni namna gani Uislamu unatilia maanani familia na mwanamke, na kuliweka jambo hili katika daraja ya juu ambayo haijafikiwa na mifumo na nadharia zingine zozote.
Ifuatayo ni baadhi ya misingi ya mtazamo wa Kiislamu kuhusu mwanamke na familia:
Kwanza: Kuhusu mwanamke.
1 - Haki za kisheria za mwanamke hulindwa kwa maneno ya Mwenyezi Mungu, hata zile zisizopitishwa na sheria zingine za kidunia, Mwenyezi Mungu mtukufu anasema: {Nao (wanawake) wanayo haki ya kisheria (kutendewa na waume zao) kama ambavyo kuna haki ya kisheria ya kuwatendea waume zao. Na wanaume wana daraja zaidi kuliko wao. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu na mwenye hekima} [AL-BAQARAH: 228].
2 - Wajibu wote wa kisheria unawahusu wanaume na wanawake, Mwenyezi Mungu amesema: {Na waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki walinzi wao kwa wao, wanaamrisha mema na wanakataza mabaya na wanasimamisha Sala na wanatoa Zaka na wanamtii Allah na Mtume wake. Hao Allah atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu na mwenye hekima.} [AT TAWBA: 71] .
Na Quraani tukufu inaeleza ahadi waliyoitoa wanawake mbele ya Mtume S.A.W., Mwenyezi Mungu anasema: {Ewe Nabii! Watakapokujia wanawake walioamini wanakuahidi ya kwamba hawatamshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote, wala hawataiba, wala hawatazini, wala hawatawaua watoto wao, wala hawataleta uzushi wanaouzusha tu wenyewe baina ya mikono yao na miguu yao, wala hawatakuasi katika jambo jema, basi peana ahadi nao na uwatakie msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe, mwingi wa rehma.} [AL MUMTAHINAH: 12] .
3- Ndani ya Quraani tukufu kuna visa vya wanawake vyenye mafunzo na mazingatio kama kisa cha mwanamke wa Firauni, mwanamke wa Nuhu, mwanamke wa Luut, mwanamke wa Imrani, kisa cha Issa Ibn Mariam A.S., kisa cha mfalme wa Sabaa, na visa vya mama wa waumini (wake wa Mtume S.A.W.).
4- Na katika Quraani tukufu kuna sura zilizochukua majina ya wanawake. Mfano Suratu AN-NISAA (wanawake), MARIAM , AL-MUMTAHINAH, na AL-MUJADILAH naye ni mwanamke aliyemwendea Mtume S.A.W kutokana na mume wake kumfananisha na mama yake na si mkewe(kwa kumwabia wewe ni sawa na mgongo wa mama yangu) jambo ambalo lilizingatiwa kuwa ni sawa na kumpa talaka, mpaka Mwenyezi Mungu akateremsha aya za Quraani ziafikianazo na rai yake, bali Quraani tukufu imekusanya baina ya mwanamke huyo na Mtume S.A.W katika aya moja, Allah S.W. amesema: {Mwenyezi Mungu amekwishasikia kauli ya yule (mwanamke) anayejadiliana nawe (ee Muhammad) kuhusu mumewe, na anamshitakia Allah, na Allah anayasikia majibizano yenu. Hakika Allah ni mwenye kusikia yote daima na Mwenye kuona yote daima}. [AL MUJADILAH:1]
5- Na historia inatufahamisha kwamba miongoni mwa waumini wa kwanza katika Uislamau ni Bi Khadija Bint Khuweylid R.A mama wa waumini, na shahidi (aliyekufa kishujaa) wa kwanza ni Bi Sumaiyyah mama wa Ammar bin Yasir, na mwaminifu wa kwanza juu ya kitabu cha Mwenyezi Mungu Quraani baada ya kukusanywa wakati wa enzi ya khalifa wa kwanza Abu Bakar Swiddiyq R.A. ni Bi Hafsa Bint Omar aliyekihifadhi kitabu cha Mwenyezi Mungu mpaka Othman bin Affan alipochukua uongozi na akatoa nakala za misahafu na kuzipeleka katika miji mbalimbali duniani.
6- Na Usawa huu wa kisheria katika haki na wajibu sio usawa katika utendaji na ugawanaji wa nyadhifa za kazi, kwani jambo hilo halina dalili yoyote ya uasilia wa binadamu au kutoka katika majaribio ya mataifa mbali mbali, wala hukumu ya utazamaji, bali dalili imekuja kinyume cha mazingatio haya yote.
Pili : Kuhusu familia katika Uislamu.
1 - Familia ni jambo la kidini, mwanadamu anafanya kazi kwa bidii ili kutimiza wajibu wake, na kuwa na familia ni Sunna ya manabii na watu wema. Mwenyezi Mungu amesema: {Na tuliwapeleka mitume kabla yako, na tukawajaalia kuwa na wake na kizazi; (si kiroja ukiwa Mtume wewe una wake na watoto). Na haiyumkiniki kwa Mtume kuleta miujiza isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kila muda una hukumu aliyoiandika Mwenyezi Mungu, (ukitimu muda wake huo hukumu hiyo itafika)} [AR RAAD: 38].
2 - Familia ni umoja wa kijamii, kauli mbiu yake ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na katika ishara zake (za kuonesha ihsani zake juu yenu) ni kuwa amekuumbieni wake zenu katika jinsi yenu ili mupate utulivu kwao, naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Bila shaka katika haya zimo ishara kwa watu wanaofikiri.} [AR RUM: 21].
3 - Na katika kudhamini kuendelea maisha ya ndoa, Uislamu unathibitisha kwamba familia na ndoa ni katika dini, Mtume S.A.W amesema: "Mwanamke huolewa kwa mambo manne: kwa mali yake, nasaba yake, uzuri wake na dini yake. Basi muowe alieshika dini (usipofanya hivyo) mikono yako itafukarika." Imepokelewa na Bukhary (H.4802). na Muslim (H. 1466) kutoka kwa Abu Huraira R.A.
4 - Na katika mazingira ya kiroho ya juu na utohara (usafi) wa kiutu zinaanza hatua za kutengeneza mustakabali wa familia, Mwenyezi Mungu akiweka upendo wa mwanamke katika moyo wa mwanamume fulani, basi mwanamume anaruhusiwa kumtazama mwanamke bila ya kuchupa mipaka wakati wa kuposa. Mtume S.A.W. anasema "Nenda ukamtazame, kwani jambo hilo linasaidia kutimiza na kuafikana baina ya mioyo yenu", hadithi hii kutoka kwa Al-Mughira Ibn Shuubah imetolewa na Annas (H. 3235) na Al-Termidhiy (H. 1087) aliyesema ni hadithi Hasan.
5 - Na mwanamume ni lazima ampe mwanamke zawadi (mahari) kama ni dalili ya upendo na utekelezaji. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na wapeni wanawake mahari yao kwa maridhawa. Lakini wakitoa chochote wenyewe katika mahari yao kwa hiari zao, basi kuleni kwa raha na muruwa.}. [AN-NISA: 4]. Zawadi (Mahari) ni mfano wa hiba na tuzo, mahari si thamani ya kustarehe na mke wala si kwa ajili ya kuandaa vifaa na samani ya nyumba, kwa sababu kuitaarisha nyumba ni jukumu la mume lakini mwanamke anaweza kushirikiana na mumewe. Mtume S.A.W. alikuwa anataarisha nyumba ya watoto wake wa kike wanapotaka kuolewa, kama ilivyopokelewa katika hadithi ya ndoa ya Bi Fatma, hadithi ambayo ameitoa Ahmad (H 643) na wengine kutoka kwa Ali bin Abi Talib.
6 - Na Uislamu unaweka utaratibu wa familia katika mfumo kamili utokanao na hukumu za kisheria zinazolinda na kuipa familia kila aina ya heshima pamoja na kujali maendeleo na amani yake tangu kufunga ndoa na kuitangaza. Mtume S.A.W. anasema, “Itangazeni ndoa yenu, na muifungie misikitini, na pigeni dufu” Imetolewa na Al-Termeziy (1089) kutoka kwa Bi Aisha, na amesema kuwa Hadithi hii ni Gharib Hasan (ngeni na nzuri).
7 - Na katika aya na hadithi nyingi Uislamu umepanga haki na wajibu ndani ya familia baina ya mume na mke, miongoni mwake ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wawekeni humo humo mnamokaa nyinyi, kama mpatavyo (ijapokuwa mumewawacha; madamu eda yao haijaisha). Wala msiwadhuru kwa kuwatia dhiki. Na kama wakiwa na mimba, wagharamieni mpaka wajifungue. Na kama wakikunyonyesheeni watoto wenu, basi wapeni ujira wao. Na shaurianeni, kwa wema. Na kama mkiona udhia baina yenu, basi mwanamke mwingine amnyonyeshee mwanawe. Mwenye uwezo agharamie kadiri ya uwezo wake; na yule ambaye amepungukiwa na riziki, atoe katika kile alichopewa na Mwenyezi Mungu; Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu yoyote ila kwa kadiri ya alichompa. Mwenyezi Mungu atajaalia baada ya dhiki faraji.} [AT TALAQ: 6-7].
8 - Na Uislamu umeilinda familia kutokana na ubaya wa wageni. Mwenyezi Mungu anasema: {Enyi mlioamini : Msiingie nyumba ambazo si nyumba zenu mpaka muombe ruhusa, (Mpige hodi) na muwatolee salamu waliomo humo. Hayo ni bora kwenu; huenda mtakumbuka (mkaona ni mazuri haya mnayoambiwa]. (AN NUR: 27).
9 - Na Uislamu unazihimiza haki za watoto, kama kauli ya Mwenyezi Mungu: {Wala msiwaue watoto wenu kwa kuogopa umasikini. Sisi ndio tunaowaruzuku wao na nyinyi (pia) kwa yakini kuwaua ni kosa kubwa}. [BANI ISRAIL: 31]. Na kauli yake Allah S.W.: {Na waamrishe watu wako kusali, na wewe uendelee kufanya hayo. Hatukuombi riziki bali sisi ndio tunakuruzuku. Na mwisho mwema utawafikia wamchao Mungu}.[TAHA, AYA : 132].
10 - Na Uislamu umesisitiza juu ya haki za wazazi katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na tumemwusia mwanadamu afanye wema kwa wazazi wake; na kama wakikulazimisha kunishirikisha na yale usiyo na elimu nayo, basi usiwatii, kwangu ndiyo marejeo yenu, basi nitakwambieni mliyokuwa mkiyatenda}. [AL ANKABUT: 8]. Na kauli yake S.W.: {Na tumemuusia mwanadamu (Kuwafanyia wema) wazazi wake – mama yake ameibeba mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na (kumnyonyesha na kuja) kumwachisha kunyonya katika miaka miwili -ya kwamba unishukuru mimi na wazazi wako; marejeo yenu ni kwangu}. [LUQMAN: 14].
11 - Na Uislamu unailinda familia kwa maana pana zaidi inayojulikana katika ukoo. Uislamu unauhimiza uhusiano wa wenye ndugu, katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombeana. Na (muwatazame) ndugu zenu wote. Hakika Mwenyezi Mungu ni mlinzi juu yenu (anayaona kila mnayoyafanya}. [AN NISA: 1]. Na kauli yake Allah S.W.: {Na ndugu wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe (katika kurithiana. Ndiyo ilivyo) katika kitabu cha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu}. [AL ANFAL:75].
12 - Na Quraani imeusistizia umuhimu wa mwanamke kwa kutenda wajibu wake wa kimaumbile katika kumnyonyesha mtoto. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na wanawake waliozaa wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili, kwa anayetaka kukamilisha kunyonyesha}. [AL BAQARAH: 233].
13 - Na Uislamu unahimiza kumtunza mtoto, kumlea na kumhurumia. Mbali na hayo, Uislamu ndio pekee umesisitiza malezi ya mtoto kabla ya kuzaliwa kwake. Uislamu unamtaka mwanamume kuwa mwangalifu wakati wa kuchagua mwanamke wa kumuoa, achague mwanamke mwenye tabia njema na mwenye dini ili awe kigezo kizuri kwa mtoto na mtoto aje kulelewa katika mazingira mema ya kidini. Mtume S.A.W. anasema: "Mwanamke huolewa kwa mambo manne: kwa mali yake, nasaba yake, uzuri wake na dini yake. Basi muowe alieshika dini (usipofanya hivyo) mikono yako itapata vumbi (itapata umasikini).". Yaani utapata hasara. (Bukhary).
Hii ni baadhi ya mitazamo ya nadharia ya Kiislamu kwa ujumla kuhusu mwanamke na familia, mitazamo ambayo inabainisha wazi nafasi,umuhimu na daraja ya mwanamke na familia katika Uislamu.
Marejeo : Profesa / Muhammad Sayyed Ahmad Al-Mesayar, Almujtamaa almithaaaliy fi alfikri Alfalsafiy wamawqifu Al-islamu minhu, Cairo : Dar Al-Maaref, cha 2, 1989, uku : 92-95, 297.
 

Share this:

Related Fatwas