Uharibifu wa Miundo Mbinu katika Vi...

Egypt's Dar Al-Ifta

Uharibifu wa Miundo Mbinu katika Vita

Question

Je, Waislamu wakipigana vita na maadui, wanaruhusika kuharibu miundo mbinu ya barabara na madaraja ya maadui?

Answer

Sifa zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata, ama baada ya hayo:
Miundo Mbinu ni istilahi inayotumika kuashiria viwanda, huduma na mambo ya kimsingi yanayoihatajia jamii. Kwa mfano njia za usafiri kama barabara, viwanja vya ndege na garimoshi, na njia za mawasiliano kama mtandao wa simu, simu ya mkononi, tovuti, nukushi, barua pamoja na mfumo wa maji taka na maji safi.
Jihadi katika Uislamu ina lengo tukufu, nalo ni kuondoa batili, kuondosha dhulma na madhalimu wenyewe, na kuwaondoshea wanyonge uadui. Lengo la Jihadi si kulipiza kisasi, wala kuua, wala si uharibifu wa mali za maadui, au kuitumia vibaya miundo mbinu yao wala kuiba.
Jihadi inatakikana iwe kwa ajili ya njia ya Mwenyezi Mungu kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Basi wapigane katika njia ya Allah wale ambao wanaouza (wanaochagua) uhai wa dunia kwa Akhera. Na atakayepigana katika njia ya Allah akauliwa au akashinda basi tutampa ujira mkubwa.} [AN NISAA, 74].
Aidha Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na mna nini (mpaka mkawa) hampigani katika njia ya Allah, na walio wanyonge kati ya wanaume na wanawake na watoto ambao husema: “Mola wetu tutoe kutoka katika mji huu ambao watu wake ni madhalimu, na tujaalie kutoka kwako mlinzi na tujaalie kutoka kwako mwenye kunusuru.} [AN NISAA, 75].
Na njia ya Mwenyezi Mungu ni ile ambayo Mtume S.A.W. amebainisha katika yale yaliyopokelewa na Imamu Bukhari kutoka kwa Abu Musa R.A ambapo alisema: “Mtu alikuja kwa Mtume s.a.w. akasema: yupo anayepigania ngawira, yupo anayepigania apate kutajwa, na yupo anayepigania apate cheo. Basi, ni nani kati ya hawa anayepigania katika njia ya Mwenyezi Mungu? Mtume s.a.w. alisema: “Yule anayepigania ili neno la Mwenyezi Mungu (dini ya Mwenyezi Mungu) liwe juu, basi anapigania katika njia ya Mwenyezi Mungu”. Na neno la Mwenyezi Mungu ni Uislamu na kuulingania, kueneza haki na uadilifu, kuondosha dhulma na kujibu uadui.
Sheria ya Kiislamu imeharamisha kuwaua wanawake, watoto, wazee na raia wasiokuwa na hatia, pia imeharamisha dhulma, ujeuri, kuharibu majengo na kukata miti. Sheria ya Kiislamu imeharamisha hata kuua wanyama. Na linaingia katia uharamu huo kila jambo linalouchafua Uislamu na kuufanya uonekane vibaya na kusababisha watu wauchukie na kujiepuka nao na pia kuepukana na maadili ya watu wake. Ndani ya hali hii itakuwa ni sawa na kuwazuia watu kuingia katika njia ya Mwenyezi Mungu; kinyume cha lengo linalotakiwa katika Jihadi. Imepokelewa na Abu Daudi kutoka kwa Rabah Bin Rabii’ alisema: “Tulikuwa na Mtume S.A.W. katika vita, basi akawaona watu wamekusanyika kwa ajili ya jambo, akamtuma mtu na kumwambia: kaangalie wamekusanyika kwa lipi, aliporudi alisema: mwanamke ameuawa. Akasema Mtume S.A.W.: hakustahiki mwanamke huyu kuuliwa. Mbele alikuwepo Khalid bin Walid, basi Mtume S.A.W. alimtuma mtu kwa Khalid amwambie “haifai kuua mwanamke wala mzee mkongwe”. Pia imepokelewa na Abu Daudi kutoka kwa Anas bin Malik kwamba, Mtume S.A.W. alisema: “Nendeni kwa jina la Mwenyezi Mungu na kwa msaada wake Mwenyezi Mungu, na juu ya mila ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, na msiue mzee mkongwe, mtoto mdogo, mtoto mchanga na mwanamke, msipindukie mipaka, kusanyeni ngawira zenu, suluhisheni na mfanye wema kwani Mwenyezi Mungu anapenda watendao wema”. Imam Malik alitaja katika Muwatwaa, hadithi iliyopokelewa na Yahya bin Said: “Abu Bakar R.A alipeleka majeshi mjini Sham, basi akatoka pamoja na Yazid bin Abu Sufiyan hali ya kuwa wanazungumza, akasema: nakuusia mambo kumi: usimuue mwanamke, mtoto, mzee mkongwe, na usikate miti iliyokuwa na matunda, wala usiharibu miji, wala usikame maziwa ya mbuzi au myama, wala usiteketeze mitende na wala usiizamishe, usipindukie mipaka na uwe na ushujaa”.
Kwa hiyo, vita katika Uislamu havitakiwi kuwa na lengo la kifedha au kudunia, bali vinatakiwa kuwa kwa ajili ya kuliweka mbele neno (dini) la Mwenyezi Mungu ili lishinde, kuwasaidia wanyonge na kubainisha ukweli wa Uislamu kwa yule asiyeujua. Vita katika Uislamu vinatafautiana na vita vyingine ambavyo lengo lake huwa ni kutawala nchi, uadui,kuua nafsi,na kuharibu nchi na kuipora. Tukiangalia kwa makini vita vya Mtume s.a.w. tunakuta kwamba idadi ya waliouawa katika miaka kumi na moja ni chini ya watu (waislamu na washirikina) elfu moja, ama idadi ya waliouawa katika vita vya pili vya dunia katika kipindi cha miaka minane ni kiasi watu milioni sita, pamoja na kuharibiwa zaidi ya asilimia sabini ya miundo mbinu. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na katika watu yupo mwenye kukuvutia kauli yake katika uhai wa dunia (lakini akhera utabainika uovu wake) na humshuhudisha Allah kwa yale yaliyomo katika moyo wake na hali yeye ndiye khasimu mbaya zaidi. Na anapotawala hujitahidi (kufanya akitakacho) katika ardhi ili afisidi humo na aangamize mimea na vizazi. Na Allah hapendi ufisadi.} [AL BAQARAH, 204: 205].
Na Imamu Qurtubi amesema katika tafsiri yake juu ya aya hiyo: “Aya hii inajumuisha kila aina ya ufisadi ukiwa katika ardhi, mali au dini” [Al Jami’ Li Ahkam Al Quran, 3/18, ch. Dar Al Kutoob Al Masriya].
Ibn Qudama alisema: “Ikiwa miti, mimea na majumba ni miongoni mwa vitu ambavyo waislamu wanapata madhara vikiharibiwa; kwani wananufaika kwa kuwepo vitu hivyo; maana wanavitumia katika chakula au kama vivuli au kula matunda yake, basi tukiwafanyia maadui hivyo na wao watatufanyia, kwahivyo ni haramu kuharibu milki za maadui, kwani waislamu wenyewe watanufaika navyo” [Al Mughniy, Ibn Qudama, 9/233, Dar Ihiya’ Al Turath Al Arabiy].
Kuharibu Miundo Mbinu ni haramu katika vita vya Waislamu na wengine; kwani ni kuangamiza nchi na watu, tena hilo si lengo linalotakiwa na vita katika Uislamu kama tulivyobainisha katika wasia wa Abu Bakar R.A kwa Yazid bin Sufyian, na kwa kauli ya Mtume S.A.W.: “suluhisheni na mfanye wema kwani Mwenyezi Mungu anapenda watendao wema”.
Na katika hukumu hii tunavua majengo ambayo maadui wanayatumia katika kupigana na sisi waislamu, pia vinatoka vitu ambavyo katika kuviharibu ni masilahi ya kivita au katika hali ambayo maadui walikuwa wakiingia nchi za Kiislamu walikuwa wanavitumia kufanyia uharibifu, kwahiyo wakivitegemea vitu hivi katika kutupiga au tukiviharibu kuna manufaa ya kivita kwetu basi ni halali kwetu kuviangamiza na kuviharibu ili maadui wasije kuvitumia tena dhidi ya jeshi la waislamu.
Ibn Qudama alisema: “Haikatwi miti yao wala haichomwi mimea yao pasipo na haja ya kuiangamiza. Ni ruhusa kuikata miti yao na kuichoma ikiwa karibu na ngome zao na inazuia kupigana nao ila baada ya kuiharibu au maadui wanaitumia ili kujificha waislamu wasiwaone, au ikiwa kuna haja ya kutanua barabara au kurekebesha barabara, au katika hali ambayo wale maadui walikuwa wanatufanyia hivyo. Inajuzu kuharibu miundo mbinu katika hali hizo ili kuwakomesha na wasitufanyie uadui tena”. [Al Mughniy, Ibn Qudama, 9/233, Dar Ihiya’ Al Turath Al Arabiy].
Kutokana na yaliyopita: Kuharibu miundo mbinu ya maadui ni haramu kisheria ila katika hali ambayo maadui wanaitumia kutupiga vita au ikiwa kuna faida ya kivita au wakiwa walitangulia kutufanyia hivyo; kwani malipo yanatokana na utendaji wa kazi. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi zaidi wa yote .
 

Share this:

Related Fatwas