Mkataba wa Geneva wa mateka wa vita...

Egypt's Dar Al-Ifta

Mkataba wa Geneva wa mateka wa vita na Sheria ya Kiislamu

Question

Vipi mkataba wa Geneva wa mateka wa vita unakubaliana na Sheria ya Kiislamu. Na Inajuzu kwa waislamu kuutekeleza?

Answer

Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimshukie Mtume wa Mwenyezi Mungu, watu wake, masahaba wake na waliomfuata, na baada ya hayo:

          Neno Mateka katika lugha ya Kiarabu ni “Asiir”, lililochukuliwa kutoka neno (Isaar) yaani (Pingu), sababu walikuwa wakiwafunga mateka pingu. Kwa hiyo, kila mtu anayekamatwa katika vita, au kufungwa pingu au kufungwa jela, anaitwa mateka. [Lisaan Alarab, 4l19, Kidahizo: ASARA, Ch. ya Dar Saader].

Kuhusu kauli ya Mwenyezi Mungu: {Na huwalisha chakula maskini na mayatima na mateka, na hali ya kuwa wenyewe wanakipenda (chakula hicho)}. [AD- Dahr: 8]. Mujahid anasema: Mateka ni mfungwa. [Tafsiir Al-Tabariy, 23/545, Ch. Dar Hajar].

          Ama katika istilahi ya wanafiqhi: Mateka ni wapiganaji na mfano wao miongoni mwa makafiri, wakichukuliwa wakiwa hai wakati wa vita au mwishoni mwake, au bila kutokea vita , kwa kuwa uadui bado upo na vita vinaweza kutokea. Pia mwislamu aliyetekwa na makafiri huitwa mateka. [Almausuuat Alfiqhiyah, 4/195, Istilahi ya ASRAA, Ch. ya Wizara ya Awqaaf ya Kuwait].

          Kuhusu ufafanuzi wa mateka katika mkataba wa Geneva, hautofautiana na ule uliotangulia, lakini mkataba huu unamzingatia mateka ni mateka, bila ya kujali dini au uraia wake.

          Kukamata mateka ni halali ili kumdhalilisha adui na kuvunja nguvu yake, kwa kauli ya Mwenyezi Mungu: {Basi mnapokutana (vitani) na wale waliokufuru wapigeni katika shingo zao (wafe mara moja) mpaka mkiwashinda sana, hapo wafungeni (muwachukue makwenu, hali ya kuwa ni mateka)}. [MUHAMMAD: 4]. Ili iwezekane kubadilishana nao kwa mateka waislamu.

          Mkataba wa Geneva uliandikwa tarehe 2 Agosti 1949, unahusu kutendeana na mateka wa vita, , uliwasilishwa ili kutiwa saini, kuidhinishwa na nchi kujiunga nao katika mkutano wa kidiplomasia wa kuweka mkataba wa kimataifa kwa ajili ya kulinda wahanga wa vita, mkutano huo ulifanyika Geneva, Uswisi.

          Mkataba unalazimisha nchi wanachama zilizotia saini mkataba huo kuwatendea vizuri mateka. Pia unalazimisha kutowaua majeruhi na wagonjwa, kutowaadhibu, kulinda mali zao binafsi, kutibu wagonjwa miongoni mwao, kutohatarisha maisha yao, kutowafanya kuwa ngao za kibinadamu, kuhifadhi nguo zao na malazi yao na chakula chao, kuwaacha wafanye kazi zao za kiakili, kimwili, na kidini kwa uhuru kamili na kuwaacha wafanye kazi katika nyanja zisizokuwa za kijeshi. Na mwishoni mwa vita na baada ya kumalizika ugomvi, mateka hawa wapelekwe nchini mwao.

          Mkataba huo unakubaliana na Sheria ya Kiislamu, na hakuna kosa kwa kiongozi mwislamu kuutekeleza. Kwa sababu, kutendeana na mateka kwa upole, na kuwawekea vyakula vya kutosha, vinywaji na nguo, hayo yote yapo katika Sheria, na Mwenyezi Mungu anasema: {Na huwalisha chakula maskini na mayatima na mateka, na hali ya kuwa wenyewe wanakipenda (chakula hicho)}. [AD  DAHR: 8].

          Uamuzi unaohusu mateka ni madaraka ya kiongozi au naibu wake. Kwa hiyo, yeye ana hiari ya kufanya vitu hivi: ima kuwaua, kuwatumia watumwa, kuwaacha huru, au kuchukua fidia. Al-Khatib Al-Shirbiniy anasema: “Kiongozi ana hiari kuhusu mateka afanye lililo bora kwa Uislamu na Waislamu, hivyo, achague moja ya mambo manne; kifo, utumwa, kuacha huru bila ya malipo, au fidia kwa mali au watu”. [Al-Iqnaa’ na Al Khatib Al Sirbiniy, 2/213, Ch. ya Mustafa Alhalabiy].     

          Ibn Qudamah anasema: “Kiongozi akiteka mateka, atakuwa na hiari. Anaweza kuwaua, au kuwaacha huru bila malipo, au kuwaacha huru kwa malipo, au kuwatolea fidia kwa mateka waislamu, au kuwafanya watumwa”. [Al Mughny, 10/400, Ch. ya Al Kitaab Al Arabiy].

          Al Mawaaq anasema katika kitabu cha (Altaj wal Ikliil): “Ibn Rushd anasema: Imamu Malik na wanachuoni wengi wanasema: Kuhusu mateka, kiongozi ana hiari katika mambo matano: Ima awaue, au kuwateka kama watumwa, au kuwaacha huru, au kuchukua fidia, au kuwawekea dhima na kuwafunga kwa Jizyah (kodi). Na hiari hizi si mtazamo binafsi, lakini ni mtazamo wa jitihada ya waislamu”. [Altaj wal Ikleel Sharh Mukhtasar Khaleel, 3/358, Ch. ya Dar Al Fikr].

          Katika swala la mateka, kiongozi anaangalia masilahi ya waislamu. Na bila shaka, kuwajibika na mkataba kama huu ni miongoni mwa masilahi ya waislamu, kwa sababu kutotekeleza mkataba ni jambo linalowasababishia vikwazo vya kimataifa ambazo zinawadhuru waislamu. Na madamu mkataba huu umewajibisha kuwaacha huru mateka kutoka pande zote zinazopambana, baada ya kumalizika mapambano, basi mkataba huu ni lazima, kwa sababu ni kama agano na mapatano lazima yatekelezwe. Na Mwenyezi Mungu anasema: {Enyi mlioamini! Tekelezeni wajibu (wenu)}. [AL MAIDAH: 1].

          Mtunzi wa tafsiri ya Roho Al Maaniy anasema katika kueleza “utekelezaji” maana yake ni “kuangalia yanayokuwepo katika mkataba na kuyatekeleza”. [Tafsiir Roho Al Maaniy, 6/48, Ch. ya Dar Ihyaa Al Turaath Al Arabiy].

          Al Tirmidhiy amepokea kutoka kwa Amr Ibn Auf Al Muzaniy kuwa Mtume S.A.W. amesema: “Waislamu watekeleze masharti yao, isipokuwa sharti linaloharamisha halali au kuhalalisha haramu”.

          Sheria ya Kiislamu imekubali jambo la kupatana na kuungana kati ya watu. Ibn Almulaqin anasema katika kitabu cha Albadr Almuniir: Alhumaidy na Albaihaqy wamepokea kwa Isnaad Sahihi, kutoka kwa Abdulrahmaan Ibn Abubakar R.A. kuwa Mtume S.A.W. amesema: “Hakika nimeshuhudia katika nyumba ya Abdullahi Ibn Judaan mkataba, lau ningeitwa kuhudhuria wakati wa Uislamu ningelihudhuria, waliwafikiana kurejesha fadhila (haki) kwa wenyewe, na dhalimu asimtishe mdhulumiwa.

          Al Waqidiy anasema: waliahidiana kuwa asiwepo mdhulumiwa hata mmoja ndani ya Makka au nje yake isipokuwa atanusuriwa, na kuwapa maskini na fakiri kiasi cha mali zao zinazozidi na mahitaji yao. Kwa kuwa ziada ya mali katika lugha ya Kiarabu ni “Fudhuul”, mkataba huu ukaitwa “Hilf Al Fudhuul”, yaani (Muungano wa ziada ya mali). [Rejea: Al Badr Al Muniir, na Ibn Al Mulaqin, 7/326, Ch. ya Dar Alhijrah].

          Na kwa mujibu wa yaliyotangulia: Mkataba wa Geneva unapatana na Sheria ya Kiislamu, na Waislamu lazima wautekeleze, endapo kiongozi wao mwislamu ataona kuwa kuna masilahi kwa waislamu, na ameukubali. Kwa sababu mkataba kama huu ni miongoni mwa mikataba ya wajibu na ahadi ambazo ni lazima zitekelezwe.

Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi.

Share this:

Related Fatwas