Ukhalifa (Uongozi) wa Kiislamu

Egypt's Dar Al-Ifta

Ukhalifa (Uongozi) wa Kiislamu

Question

Je, kuna Dola linalozingatiwa ni la Kiislamu baada ya Ukhalifa (Uongozi) wa Kiuthmani ? Je, nini hukumu ya kuwatii watawala katika hali hiyo?

Answer

 Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:

          Ukhalifa (Uongozi) ni kufanya kazi kwa niaba ya mwenye sheria ili kuhakikisha masilahi ya kidini na kidunia; Ibn Khalduun alisema katika kitabu cha [Muqadimat Al-Taarekh, 1/239, Ch. Dar Al Fikr, Bairuut]: "Ukhalifa ni kuwachukulia watu wote kwa mtazamo wa kisheria katika masilahi yao ya kidunia na ya akhera yarejeayo katika ukhalifa huo ; kwani hali zote za dunia zinarejea kwa mwenye sheria kwa kuzizingatia ni masilahi ya akhera, basi kwa hakika ukhalifa ni huo unaofanya kazi kwa niaba ya mwenye sheria katika ulinzi wa dini na siasa ya dunia kwa dini hiyo"

          Wanachuoni wametaja kwamba kuunda ukhalifa ni faradhi KIFAYA juu ya Umma, kwa sababu ni lazima kuwepo chombo kinachoendesha mambo ya kidini na kidunia, na kwa kupitia chombo hiki Mwenyezi Mungu Mtukufu anawaondoshea watu dhuluma na anawaletea masilahi yao na anawaondoshea ufisadi.

          Na Al Saad Al Taftazani alisema katika kitabu cha [Sharh Al Aaqaid Al Nasafiyah, Uk. 96, Ch. Maktabat Al Kuliyaat Al Azhariya]: "Makubaliano ya wanachuoni yanaeleza kwamba kumtii Imamu ni wajibu".

          Na Ibn Abdeen alisema katika [Hashiyatahu, 1/548, Ch. Dar. Al Fikr]: "(Kauli yake na kumtii) yaani: Imamu, (kauli yake: ni kati ya mambo wajibu sana) yaani ni muhimu sana kumtii Imamu kwa kuwa mambo mengi ya kisheria yanaegemezwa juu yake."

          Na Al Sheikh Zakariya Al Ansariy alisema katika kitabu cha [Asny Al Mataalib, 4/108, Ch. Dar Al Kitaab Al Islamiy]: "(Mlango wa Uimamu) mkuu (ni faradhi KIFAYA) kama Ukadhi; yaani ni lazima katika Umma kuwepo Imamu anayesimamia dini, ananusuru Sunna, anawatendea haki wanaodhulumiwa na anachukua haki zote na anaziweka mahali pake (na kama hakufaa) kushika Uimamu (ila mtu mmoja), na hakuuomba (lazima aombe uimamu huo) kwani yeye ni mtu anayefaa, (na analazimishwa) kushika uimamu (kama alikataa) kuukubali".

          Na Al Ramliy Al Kabeer alisema katika [Hashiatahu alaa Asny Al Mataalib,4/108]: "Kaumu fulani walisema: Uimamu ni mtu maalumu kuongoza mambo ya dini na dunia. Na ni bora zaidi kusemwa ni Ukhalifa wa Mtume S.A.W katika kusimamisha dini na kuhifadhi Mila, na ni wajibu juu ya watu wote wa Umma kumfuata. (Na kauli yake: Uimamu ni faradhi KIFAYA) ni makubaliano ya wanachuoni. Na masahaba waliharakia katika kusimamisha Ukhalifa, na waliacha mambo ya kutayarisha mazishi ya Mtume S.A.W. kwa sababu ya khofu yao kwa kutokea jambo fulani; na kama watu wangeliachwa katika fujo wasingekusanywa tena juu ya haki, na watu wabaya wangeliwatawaliwa waja. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na kama Mwenyezi Mungu asingalizuia watu baadhi yao kwa wengine kwa yakini ardhi ingaliharibika} [AL BAQARAH: 251].

          Uislamu ulipokuja uliwaondosha waarabu kutoka uchungaji wa kondoo na kuwa viongozi wa watu, na uliwaingiza katika utamaduni katika nyanja mbalimbali za maisha, ndogo na kubwa. Na miongoni mwa dalili za utamaduni huo ni kuwatoa katika ukabila na kuwaingiza katika dola lenye mfumo wa ukhalifa. Na waislamu wanahifadhi utawala katika dola, na wanalinda umoja wake kwa kiasi ya uwezo wao, hata katika zama za udhaifu wa Ukhalifa na kudhihiri vidola vidogo na masulutani, waislamu wengi waliendelea kufuata ukhalifa kwa kumuombea dua kiongozi juu ya mimbari. Ukhalifa uliangushwa mwaka 1342 H (1925 M), halafu Dola la Kiislamu likagwanywa katika mfumo wa nchi ndogo ndogo, mipaka yake ilichorwa kwa mujibu wa mkataba wa Sakis Biko.

          Baada ya kugawanywa, kila nchi ikawa na katiba yake, rais, sheria inayohukumu, na utawala juu ya ardhi yake huru. Kwa hiyo tunaweza kuzingatia hali hiyo inafanana na hali ya nchi ndogo ndogo zilizojitokeza wakati wa zama ya udhaifu wa ukhalifa, kinje nje utaziona zinafuata ukhalifa, lakini kiukweli baadhi yake zimejitenga na kila nchi ikawa ina Ukhalifa wake. Kwa mfano dola la Andalusia lilipoanza lilifuata ukhalifa mmoja kisha Abdulrahman Al Dakhil aliposhindwa, hakuwa mtawala wa Al-abbasiy isipokuwa kwa kuombewa dua tu, halafu ikawa marufuku kumuombeao na dola likaitwa (ufalme) kisha lilitangaza (Ukhalifa).

          Licha ya hayo ufalme ulikuwa unaendesha kikamilifu mambo ya kiuchumi, vita, mahakama n.k kwa amri ya ukhalifa. Na askari hakukataa jihadi katika dola, na pia maimamu waliendelea kufanya kazi misikitini, makadhi na wanachuoni waliendelea kufanya kazi ya ukadhi, kutoa fatwa, kufundisha na kutunga.

          Ibn Khalduun alisema katika kitabu cha [Muqadimat Al Tareekh . 1/260]: "Amri imekuwa ni ya mfalme, na maana za ukhalifa zilibaki kama kuhifadhi dini, madhehebu yake na kuendelea juu ya utaratibu wa haki. Hivi ndivyo amri ilivyokuwa wakati wa enzi ya Muawia, Marawaan na mtoto wake Abdulmalik, na mwanzo wa enzi ya makhalifa wa Bani Al Abaas hadi Alrashid na baadhi ya watoto wake, halafu maana za ukhalifa zikatoweka na hazikubaki isipokuwa jina lake, na amri ikawa ya kifalme tu. Watoto wa Abdulmalik na waliokuja baada ya Alrashid miongoni mwa wana wa Al-abaas walikuwa wanamiliki amri, ama jina la ukhalifa likabakia kwao kwa kubakia ulokole wa waarabu.

Ukhalifa na ufalme ni mambo mawili yenye kuingiliana, kisha ukhalifa na athari yake ukatoweka baada ya kutoweka ulokole wa waarabu, kumalizika vizazi vyao na kuharibika hali zao, kwa hivyo amri ikabakia ni ya kifalme tu.

          Wafalme wa Uajemi huko mashariki waliongoza kwa kumtii Khalifa (kiongozi) kwa ajili kutabaruku, na mfalme licha ya majina yake na vyeo vyake si lolote si chochote mbele ya Khalifa, aidha wafalme wa Zinata nchini Morroco walifanya hivyo, kama Sinhaja, Al Ubaidieen, Magharwa na wana wa Yefrin mbele ya makhalifa wa Bani Umaiya katika Andalusia na Al Ubaidieen katika Qairawaan.

          Hapo awali, Ukhalifa umekutwa kabla ya ufalme, kisha maana zake zikaingiliana na zikachanganyika, halafu ufalme ukawa peke yake baada ya kutengana na ulokole wa ukhalifa. “Na Mwenyezi Mungu anakadiria usiku na mchana, na yeye ni Mmoja na Kahari".

          Kutokana na hayo, mtu yoyote anayetawala nchi ya kisasa, basi ana mamlaka, na watu ni lazima wamtii, madamu hawaamrishi maovu. Kazi ya uimamu ni kama kazi anayoifanya rais wa nchi ya kisasa; kama vile siasa , kuendesha mambo yao, kutekeleza hukumu, kutayarisha majeshi, kuwachukulia sheria wahalifu, na kudhihirisha ibada za kidini. Haya yote yalifanywa na na viongozi wa nchi ndogo ndogo hapo zamani, na mifumo ya ukhalifa mbalimbali baada ya ukhalifa mama (wa asili).

          Imepokelewa na Al Bukhariy kutoka kwa Anas Bin Malik R.A alisema: "Mtume S.A.W. alihutubia, akasema: Zaid alichukua bendera akajeruhiwa, kisha Jaafar akaichukua akajeruhiwa, halafu Abdullahi Bin Rawaha akaichukua akajeruhiwa, kisha Khaled Bin Al Waleed akaichukua bila ya kukabidhiwa basi Mwenyezi Mungu alimnusuru". Na katika hadithi hiyo Khaled Bin Al Waleed R.A. alichukua madaraka bila ya kukabidhiwa, na waislamu waliridhia jambo hilo na walimtii hadi vita vilimaliza, na Mtume S.A.W. alikiri jambo hilo bila ya kukataa, bali alimsifu, na Mwenyezi Mungu alimuunga mkono Khaled kwa ukombozi, na haukuteremka Wahyi kubadilisha aliyofanya au kumlaumu kama inavyotokea katika mambo kama hayo.

          Ibn Almuneer alisema: "Inachukuliwa kutoka hadithi hiyo kwamba anayeteuliwa katika uongozi na hakuweza kumrejea kiongozi mkuu katika jambo basi huyo anayeteuliwa ana mamlaka na anatakikana kutiiwa katika hukumu, pia alisema: Hadhira ikifikiana naye basi hakuna tatizo" [Rejea: Fateh Al Bariy, 6/180, Ch. Dar Al Maarifa].

          Imamu wa Al Haramaien alinukuu katika kitabu cha [Ghaiyaath Al Umam, Uk. 387, Ch. Maktabat Imamu Al Haramaien] kutoka kwa baadhi ya wanachuoni kwamba: "Kama hakuna sultani katika zama fulani basi lazima watu wa kila nchi na wakazi wa kila kijiji wawatoe watu wenye busara, kukataza, wenye akili na hoja, wanaosikilizwa na kushauriwa na wanaacha mambo mabaya ili wawe viongozi, na kama hawajafanya hivyo watakuwa wamezembea katika kutekeleza majukumu yao".

          Na Ustaadh Abu Is-haq Al-isfraiyeniy amesema inajuzu kuwatii maimamu wawili katika majimbo miwili wakati wa dharura. Imamu Al Nawawiy alisema katika kitabu cha [Al Rawdhah, 10/47, Ch Al Maktab Al Islamiy]: "Na Ustaadh Abu Is-haq alisema: inajuzu kuwatii maimamu wawili katika majimbo miwili, kwani huwenda akahitajiwa, na huu ni uchaguzi wa imamu -yaani Al Juwziy".

          Kauli hiyo inaungwa mkono na kanuni ya kisheria isemayo: "chepesi hakianguki kwa kigumu", kama yanayotakiwa kisheria ni kuwa viongozi watawale nchi chini ya uongozi mmoja; yaani chini Khalifa mmoja , kisha ikawa ni vigumu kuwepo Khalifa, katika hali hiyo uwajibu wa hukumu ya viongozi wa nchi haukuanguka, na katika maana yake ni maraisi wa nchi za kisasa.

          Kinyume na hayo, watu wanakuwa bila ya kiongozi na bila ya udhibiti unaowaongoza, na hali hii inapelekea fujo na kutikisika utulivu wa mambo ya nchi na waja, na haya ni dhidi ya makusudio ya sheria, kwa sababu mabaya yanayotokana na kutokuwepo kiongozi yanashinda makusudio matano ya kisheria yaliyotajwa katika mila zote, na kila mila imeyalinda kutokana na upungufu au batili, na makusudio matano hayo ni: kuhifadhi roho, akili, dini, heshima na mali.

          Kwa hiyo anayepekua Fiqhi ya Kiislamu anakuta kwamba wanachuoni wamekubali mambo ambayo mwanzo wake ni mbaya, lakini yanapotokea kwa kuwa yana masilahi ya waja na nchi na utulivu, basi hugeuka na kuwa ni mambo halali. Mambo hayo huingia katika mlango wa yanayosamehewa katika kudumu na hayasamehewi katika kuanza.

          Miongoni mwa hayo; kukiria utawala wa mshindi; Al Hafedh Ibn Hajar alisema katika [Fath Al Bariy, 1/13]: "Wanachuoni wamekubaliana kwamba ni wajibu kumtii sultani mshindi na kushirikiana naye katika jihadi, hakika kumtii ni bora zaidi kuliko kumpinga, kwa sababu kutii kunasitisha umwagikaji damu na kuwatuliza wahalifu ... lakini kama sultani atadhihirisha ukafiri wa waziwazi, haijuzu kumtii, bali inapasa kupigana naye kwa anayeweza.

          Na pia alisema katika kitabu cha [Mataalib Auliy Al Nuha; -miongoni mwa vitabu vya madhehebu ya Hanbaliy-, 6/263, Ch. Al Maktab Al Islamiy]: "(kama sultani alishinda eneo fulani) miongoni mwa maeneo ya ardhi, na akalitawala kama vile inavyotokea katika (wakati wetu basi hukumu yake) yaani: mshindi wa eneo; basi anantendewa kama imamu, yaani ni wajibu kumtii katika mambo yasiyokuwa maasia, na inajuzu kusali nyuma yake, ana haki kuchagua makadhi na viongozi, na lazima zitekelezwe hukumu zao na kutomuasi baada ya utulivu wa hali yake; kwani kuwa dhidi yake ni uasi, na ni jambo baya".

          Na miongoni mwake pia ni kutoweka sharti la uadilifu kwa Imamu (Kiongozi) ili kuondosha ufisadi mkubwa unaoweza kutokea kutokana na kutoteuliwa kwake, na kutohukumu usahihi wa anaemteua miongoni mwa makadhi na wengineo.

          Al Ezz Bin Abdulsalaam alisema katika kitabu cha [Kawaid Al Ahkaam -, 1/79, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah]: "Na ama katika uimamu mkuu; ipo hitilafu katika kushurutisha uadilifu, kwa sababu ni aghalabu uovu kuwaelemea watawala, na kama tulishurutisha uadilifu basi vitendo vinavyoafikiana na haki katika kumtii mtu fulani miongoni mwa makadhi, watawala, watumishi na viongozi wa vita vinazoroteka, na pia kuyachukua wanayoyachukua, na kuyatoa wanayoyatoa, na kutoa sadaka na mali za Umma na kibinfsi zinazowekwa chini ya uongozi wao; mambo hayo yote yatasimama, basi uadilifu haukushurutiwa katika shughuli zao zinazoafikiana na haki, kwani katika kuushurutisha kuna madhara kwa Umma, na kupotea masilahi ni mbaya zaidi kuliko kupotea uadilifu wa sultani".

          Na nchi hizi madamu wakazi wake au wengi wao ni waislamu, na wanaweza kutekeleza ibada zao za kidini na kudhihirisha hukumu za dini yao bila ya kizuizi chochote, basi ni nchi za Kiislamu; Sheikh Al-islamu Zakariya Al Ansaariy alisema katika kitabu cha [Asny Al Mataalib, 2/499, Ch. Al Maktabah Al Islamiyah]: "(Daaru Al-islamu: nchi ya Kiislamu) ni nchi inakaliwa na waislamu, hata kama ndani yake kuna watu wa Dhimma (au ilikuwa kwa Uislamu) yaani ilifunguliwa na waislamu na waliiweka mikononi mwa makafiri au walikuwa wakiikalia, kisha waliwaondosha makafiri ".

          Na kutokana na yaliyotangulia hapo juu: Kwa sasa nchi ambazo zina sifa hizo basi ni nchi za Kiislamu, na viongozi wake ni wa kisheria, na ni lazima kuwatii kwa kuwa hawajawaamrisha watu kufanya maasia.

          Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi zaidi.

Share this:

Related Fatwas