Kutoa damu na upeo wa usafi wake.

Egypt's Dar Al-Ifta

Kutoa damu na upeo wa usafi wake.

Question

Je, damu ni safi au hapana? Kama ikiwa ni najisi, je, inajuzu kuitoa kutoka kwa mtu mmoja na kumpa mwingine anayeihitajia? Na je, inajuzu kuchukua malipo kwa kuitoa?

Answer

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehema na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfua, na baada ya hayo:
Hapana hitilafu kati ya wanachuoni katika unajisi wa damu iliyomwagika, wala katika uharamu wa kuila kwake. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Sema: “Sioni katika yale niliyofunuliwa mimi (niliyoletwa wahyi; sioni) kitu kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni mzoga au damu inayomwagika au nyama ya nguruwe, kwani hivyo ni uchafu; au kile ambacho kwa kukhalifiwa amri ya Mwenyezi Mungu kimechinjwa kwa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Lakini aliyelazimika (kula kwa ajili ya njaa au mengine) pasipo kupenda wala kuruka mipaka, basi (huyo atasamehewa, kwani) Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu}. [Al An—am: 145].
Na damu iliyomwagika ni ile iliyotiririka na kumwagika, ama isiyomwagika hukumu yake ima haidhuru kama vile damu chache iliyobaki katika mifupa ya mnyama baada ya kuchinjwa, au kuruhusiwa kama vile, ini na wengu. Na Aya tukufu iliyotangulia inaonesha unajisi wa damu iliyomwagika, kwa sababu kuieleza kama uchafu, na maana ya uchafu katika Sheria ni najisi. [Mughny Al Muhtaaj, na Al Khatiib Al Shirbiiniy, 1/225, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah].
Wanachuoni wengi walitaja kauli ya pamoja juu ya unajisi wa damu. Imamu Al Qurtubiy anasema katika kitabu chake [Al Jamii Li Ahkaam Al Quraan 2/221, Ch. Dar Al Shaab]: “wanachuoni wamekubaliana kuwa damu ni haramu na najisi, hailiwi wala haitumiwi”. Al Hafidh Ibn Abdilbar katika kitabu chake [Altamhiid 22/230, Ch. Wizara ya Awqaaf na Mambo ya Kiislamu, Moroko] anasema: “Kauli ya pamoja ya waislamu kuwa damu iliyomwagika ni uchafu na najisi”. Imamu Al-Nawawiy katika kitabu chake [Almajmuu 2/567, Ch. Al Muniiriyah] anasema: “Dalili za kuwa damu ni najisi ni wazi, na mimi sijui hitilafu kati ya waislamu kuhusu suala hili, isipokuwa ilivyopokelewa na mtungaji wa kitabu cha Alhawiy, kutoka kwa baadhi ya wanachuoni wa elimu ya Kalaam kuwa amesema: damu ni safi. Lakini kauli ya wanachuoni wa elimu ya Kalaam haikubali katika masuala ya pamoja na hitilafu kutokana na madhehebu sahihi ya wanachuoni wengi wa misingi, hasa katika masuala ya kifiqhi”.
Asili ilivyo, haifai kutoa damu na kuiingiza ndani ya mwili wa binadamu, kutokana na unajisi wa damu iliyomwagika kiujumla, sawa iwe damu ya binadamu imemwangwa na binadamu au na asiye binadamu.
Lakini kuna msingi wa Sheria ya Kiislamu unasema: “Dharura hujuzisha marufuku, na madhara huondoshwa, na mashaka huleta urahisi”. Kwahiyo, mgonjwa anayehitaji kupewa damu ni mtu mwenye dharura au yupo katika hali ya mwenye dharura, kwa sababu kama hajaingiziwa damu, tunachelea kupata madhara yanayosababisha kifo au kuharibika kiungo kati ya viungo vyake au kusita kazi ya kiungo au kuzidi maradhi, au kuchelewa kupona, mambo ambayo yanapelekea dhiki na mashaka, kwa hivyo mtu huyu yupo kati ya hali ya udhuru na haja. Kutokana na haya, inajuzu kumtibu kwa kumtia damu hata ikiwa najisi, maana dharura inajuzisha marufuku, na kwa sababu haja ya umma au binafsi inachukua hukumu ya dharura. Yamekuja haya katika kitabu cha [Al Ashbaah wa Al Nadhair, na Al Sayutiy, Uk. 88, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah].
Imepokelewa kutoka kwa baadhi ya wanachuoni waliotangulia na wafuasi wao kauli yao: “Inaruhusiwa kutibu kwa kutumia damu kwenye haja na zinapokosekana njia mbadala zilizo halali”. Imepokelewa na Abdul-Razaq katika kitabu chake [9/256, Ch. Al Maktab Al Islaamiy] kutoka kwa Ibn Juraij anasema: Nilimsikia Ataa’ anaulizwa na mtu mmoja aliyeagizwa atoe damu kutoka katika ini lake, kisha ainywe damu hiyo kutokana na ugonjwa aliyokuwa nao, Ataa’ alimuruhusu kufanya hivyo, lakini Ibn Juraij alisema: Mwenyezi Mungu ameharimisha, Ataa’ alisema: ni dharura, Ibn Juraij akamwambia kama angelijua kuwa ni dawa angefanya, lakini hajui. Kisha yakatajwa mbele yake maziwa ya punda na yeye akaruhusu kunywewa kama dawa.
Kauli yake: Inashurutishwa juu ya ini lake, maana yake ni kutoa damu kutoka mwilini mwake juu ya ini kwa kutumia kisu cha kupasulia au kinginecho.
Mwanachuoni Ibn Abdeen wa madhehebu ya Hanafiy amenukulu kutoka kwa baadhi ya vitabu vya madhehebu haya kuwa: inajuzu kwa mgonjwa kunywa mkojo, damu na kula mzoga kwa ajili ya tiba, akiambiwa na daktari mwislamu kuwa ni dawa katika vitu hivi, na hakupata njia mbadala halali. Kisha akataja kuwa kujitibu kwa kitu haramu ni halali, akijua kuwa ndani yake kuna tiba na hana dawa nyingine. Pia anasema katika kitabu chake kiitwacho [Alhashiyah Ala Al Dur Al Mukhtaar 5/228, Ch. Dar Al kutub Al Elmiyah] na katika kitabu cha Alnihayah na kitabu cha Altahdhiib: “Inajuzu kwa mgonjwa kunywa mkojo, damu na kula mzoga kwa ajili ya kujitibu, akiambiwa hivyo na daktari mwislamu kuwa ni dawa, endapo hakupata kitu halali mbadala. Daktari akisema: tiba kwa vitu haramu inaharakisha kupona, basi kuna rai mbili za wanachuoni. Je, inajuzu kwa mgonjwa kunywa pombe kwa ajili ya tiba, pia kuna rai mbili, kama alivyotaja Imamu Al-Tamartashi pia katika kitabu cha Al-dhakhirah. Ikisemwa kutibu kwa kitu haramu ni haramu, kauli hii haiko wazi kabisa. Na haijuzu kujitibu kwa dawa ya haramu wakati akijua kufanya hivyo hakuna faida, lakini akijua kuwa ipo faida na hakuna dawa nyingine, basi inajuzu.
Maana ya kauli ya Ibn Masoud R.A.: Kupona kwenu hakukujaaliwa kwa mlivyoharamishiwa, huenda alisema hivyo kuhusu maradhi yanayoweza kutibika kwa dawa isiyo haramu, hapo basi halali inatosha kuliko haramu. Pia inaweza kusemwa: kwenye haja uharamu huondoshwa, kwa hiyo uponaji huwa kwa halali na si kwa haramu”.
Mwanachuoni Al-Khirshiy wa madhehebu ya Malikiy katika kitabu chake [Sharh Mukhtasar Khalil 3/28-29, Ch. Dar Al Fikr] anasema: “Inajuzu kwa mwenye dharura kunywa damu, maji yenye najisi na mengineyo miongoni mwa majimaji isipokuwa pombe ambayo si halali, kwa sababu haina faida, bali huenda kiu Kikaongezeka kwa kuinywa kwake, na isipokuwa inapotokea kukwama na kitu kooni kooni na ikawa hakuna tiba ila pombe”. Imamu Al-nawawiy katika kitabu cha [Al Majmuu’ 9/54-55, Ch. Al Muniiriyah] anasema: kama akilazimika kunywa damu, mkojo au mengineyo miongoni mwa najisi za majimaji zisizolewesha, hakuna hitilafu kuwa inajuzu kunywa. Na kujitibu kwa najisi zisizokuwa pombe, inajuzu. Yaani inajuzu mambo yote ya najisi isipokuwa ulevi. Na hii ni kauli sahihi na rai ya wanachuoni wengi. Kama inajuzu kwenye haja au dharura kupata tiba kwa njia ya kutoa damu, kadhalika kujuzu kujitolea damu kwa ajili ya kuokoa mgonjwa, sharti yasije madhara kwa mtoaji damu, maana katika Uislamu hakuna kudhuru wala kudhurika. Na Mwenyezi Mungu anasema: {na mwenye kumwacha mtu hai (kumsaidia kuishi) ni kama amewaacha hai watu wote}. [AL MAIDAH 32]. Yaani amehuisha nafsi ya binadamu, na sifa hii inakusanya aina zote za kuhuisha na kuepusha katika maangamizi, na bila shaka mtoaji damu kwa ndugu yake anafanya hivyo kwa ajili ya kumwokoa asiangamie.
Wanaachuoni wameweka sharti katika kitu kilichouzwa kuwa kiwe safi, basi kuuza damu ni haramu. Lakini tunaweza kuepusha uharamu huu kwa kutoa mali kama mchango, au kwa njia ya kuacha haki ya kumiliki; yaani utoaji mali hapa si malipo ya damu, bali kuruhusu kuitumia haki yake, na hii ni maana ya kuacha haki ya kumiliki. Na sura kama hii haichukui hukumu ya kuuziana na masharti yake. Hivyo, wanachuoni wa madhehebu ya Shafiy waliamua kuwa: inajuzu kuacha haki ya kumiliki kwa malipo, kama ilivyokuja katika kitabu cha [Hashiyat Al-Sharwaniy Ala Tuhfat Almuhtaj 4/238, Ch. Al Maktabah Altijariyah Al Kubraa].
Kwa mujibu wa yaliyotangulia: hakika kutoa damu kwa kujitolea kunazingatiwa ni katika mambo yaliyo bora kisheria; kufanya hivi ni kuokoa nafsi ya binadamu ili isiangamie. Wakati wa kutoa damu ni lazima kuchunga mambo yafuatayo: mgonjwa ahitaji kuchangiwa damu kwa uamuzi wa madaktari waaminifu, ikosekane njia mbadala ya kumtibu, kutokuwepo madhara anayopata mtoaji damu, na kiasi cha damu kikadiriwe kutokana na dharura, kwa sababu dharura hukadiriwa kwa kiwango chake. Na hakuna kosa kutoa mali au kuikubali kwa kutoa damu, lakini si kwa upande wa malipo, bali kwa upande wa kuacha haki ya kumiliki.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.
 

Share this:

Related Fatwas