Kumpa Mzaliwa Jina

Egypt's Dar Al-Ifta

Kumpa Mzaliwa Jina

Question

Je, Haki ya kumpa mzaliwa jina ni ya baba au ya mama?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehema na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:

Kusudio la jina la mzaliwa ni kumtambulishia kwalo na ni kama kumpa alama inalomtofautisha na wengine, tena kwa njia nzuri na kwa heshima yake kama mwanadamu, na hili linadhihiria kutokana na asili ya mnyambuliko wa jina; ambapo imesemwa: kwamba jina linatoholewa kutokana na neno la "Al Wasamah" yaani: alama.

Na Ibn Hazm amenukulu ijimaai kwa kuwajibika kumpa mtoto jina, basi akasema katika kitabu chake [Maratib Al Ijimaai, uk. 154, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah]: "Na waliafikiana kuwa kumpa mtoto jina, awe wa kiume au wa kike ni faradhi."

Ama kuhusu haki ya kumpa mzaliwa jina, basi asili kuwa ni thabiti kwa baba yake, siyo kwa mama yake; ambapo iwapo wazazi tabishana katika kutoa jina basi baba atatangulizwa; kwani mzaliwa ananasibishwa na baba yake duniani, basi inasemwa kwa mzaliwa katika kumwita kwake: "Ewe mwana wa mwanamume fulani!", na katika kumtambulisha: "Fulani bin fulani" na wala haisemwi: "Mtoto wa bibi fulani". Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Waiteni kwa (ubini wa) baba zao, maana huo ndio uadilifu mbele ya Mwenyezi Mungu} [Al AHZAB 5], yaani muwanasibishe kwa baba zao na mwahusishe nao.

Na siku ya Kiyama watu wataitwa kwa ubini wa baba zao basi wataitwa: (Fulani bin mwanamume fulani): na Al Bukhariy amepokea katika sahihi yake kutoka kwa Ibn Omar Radhi za Allah ziwafikie wote wawili, kwamba Mtume S.A.W. amesema: "Kuwa msaliti atanyanyuliwa kwa ajili yake bendera siku ya Kiyama na pakasemwa: huo ni usaliti wa fulani bin fulani". Na imepokelewa na Abu Dawud katika Sunna zake kutoka kwa Abi Al Dardaa R.A. kwamba Mtume S.A.W. alisema: "Nyinyi mtaitwa siku ya Kiyama kwa majina yenu na majina ya baba zenu basi boresheni majina yenu!".

Na kwa kuwa mzaliwa anafuata nasaba ya baba yake, na kumpa jina ni utambulisho wa nasaba na anayenasibishwa kwayo, basi yeye baba ndio mwenye haki zaidi ya kumpa mtoto wake jina, kama ambavyo baba ndiye anaebeba jukumu la usimamizi wa mke wake na kuitunza familia yake basi hayo yanauthibitisha ukweli huo.

Na Al Bihaiqiy amepokea katika kitabu cha [Shuab Al Imaan] kutoka kwa mama wa waumini Aisha R.A. kwamba Mtume S.A.W. amesema: "Haki ya mtoto juu ya baba yake kuwa ampe jina zuri, na amchagulie mnyonyeshaji mzuri, na amfunze katika maadili mema", na hadithi hiyo ingawa ina udhaifu ndani yake, lakini ni ushahidi tosha wa maana inayokusudiwa katika sentensi hiyo.

Na Imamu Muslim alipokelea kutoka kwa Anas Bin Malik R.A. kwamba Mtume S.A.W alisema: "Usiku huu amezaliwa mtoto wangu wa kiume, basi mimi nikapa jina la baba yangu Ibarahim".

Na hayo ndiyo waliyoyataja wanavyuoni wa madhehebu yanayofuatwa, na baadhi yao waliyasimulia kama ni hukumu iliyopatikana kwa maafikiano ya wanavyuoni.

Shekh Eleesh Al Malikiy alisema katika kitabu cha [Manhu Al Jaleel, 2/2, Ch. Dar Al Fikr]: "Kumpa mzaliwa jina ni haki ya baba yake".

Na Al Sharawaniy Al Shafiy alisema katika kitabu chake cha Hashiyah juu ya [Tuhfat Al Muhtaaj 372/9, Ch. Dar Ihiyaa Al Turaath Al Arabiy]: "Na ni lazima iwe kwamba kumpa jina ni haki ya mwenye uwalii kama vile baba yake mtoto, hata kama hakulazimishwa kutoa gharama za matumizi ya mzaliwa kwa sababu ya ufuata wake, kisha (baada yake anafuatia) babu yake mtoto".

Na Al Mardawiy Al Hanbaliy alisema katika kitabu cha [Al Insafu 111/4, Ch. Dar Ihiyaa Al Turaath Al Arabiy]: "Inapendeza kumpa mzaliwa jina siku ya saba ... , na kumpa jina ni haki ya baba na siyo ya mama".

Na Ibn Al Qaiym alisema katika kitabu cha [Tuhfat Al Maudud, Uk. 96, Ch. Maktabat Al Quraan]: "Kumpa jina mzaliwa ni haki ya baba siyo ya mama, hili ni katika mambo yasiyokuwa na ubishi ndani yake baina ya watu; na kwamba wazazi wawili kama wakibishana katika kumpa mtoto jina, basi baba ndiye atakayetoa jina."

Lakini inalazimu kujua kwamba huu ni mlango wa haki. Ama mlango wa kuridhiana baina ya mke na mume ni mpana zaidi na unafaa mno kwa kuwa ndio ubora wa maadili, basi kama mwanamume hakutumia ubabe kwa kumpa jina mtoto na akaamua kumshirikisha mke wake katika kuchagua jina la mtoto wao basi hiyo itakuwa ndio njia ya kuimarisha ukaribu wao na kutaleta mapenzi, kuhurumiana na kutendeana wema kati yao. Al Tiramiziy amepokea kutoka kwa Aisha R.A. kuwa Mtume S.A.W, alisema: "Aliye bora kwenu nyinyi ni Yule aliye bora kwa watu wake." na huruma ya mume kwa mke wake na kuchunga kwake maoni ya mke wake, na kuungana naye kinafsi, hapana shaka kuwa haya ni miongoni mwa mambo mazuri yasifiwayo katika Hadithi hii tukufu.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi zaidi ya wote.

Share this:

Related Fatwas