Zaka na Ndoa

Egypt's Dar Al-Ifta

Zaka na Ndoa

Question

Je, inajuzu kumpa Zaka mvulana anayetaka kuoa lakini hana gharama za ndoa?

Answer

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:

Maana ya Zaka katika lugha ni tohara, kukua na baraka [Rejea: Al Nahayah Fiy Ghareeb Al Hadeeth, kwa Ibn Al Atheer, 2/307, Ch. Al Maktabah Al Elmiyah. Bairut]. Na maana ya Zaka katika sheria: Jina la kiwango maalumu kutoka mali maalumu ambacho ni lazima kupewa watu maalumu kwa masharti maalumu [Rejea: Mughniy Al Muhtaaj, 2/62, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah.

Na wanaostahiki kupewa Zaka ni aina nane za watu zilizotajwa katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema katika Quraani tukufu: {Sadaka hupewa (watu hawa) Mafakiri na Maskini na Wanaozitumikia na Wanaotiwa nguvu nyoyo zao (juu ya Uislamu) na katika Kuwapa Uungwana watumwa na katika kuwasaidia Wenye deni na katika (kutengeneza). Mambo aliyoamrisha Mwenyezi Mungu na katika (kupewa) Wasafiri (walioharibikiwa). Ni faradhi inayotoka kwa Mwenyezi Mungum na Mwenyezi Mungu ni mjuzi (na) Mwenye hekima} [ATTAWBA 60].

Na asili ni kuwa haja ya mwanadamu ya ndoa na maisha ya kifamilia inazingatiwa ni haja ya kiasili katika ngazi ya umma na jamaa, pia inazingatiwa ni kujitosheleza katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, na huwenda ikafikia katika haja ya kiasili kwa mtu endapo atahitajia ndoa, na kuchelea kuzini na kuanguka katika haramu kama vile zinaa, kutazama uchi na madhambi mengine. Kama mwislamu hana kinachomtosheleza kukidhi haja hizo, basi inajuzu kumpa sehemu ya Zaka ili kuziba haja yake kwa kumzingatia ni miongoni mwa maskini ambao hawapati mahitaji yao kamili.

Wanachuoni wa madhehebu ya Hanafiy wanasema kuwa fakiri ni mtu mwenye kitu kidogo, ambacho ni chini ya Nisabu (kiwango maalumu cha zaka ya Mali) au kiasi cha Nisabu kisichokua, na ambacho kinatumika kukidhi mahitaji yake ya kimsingi, [Rejea: Fath Al Qadeer, 2/261, Ch. Dar Alfikr], na wanazingatia kuwa ndoa ni miongoni mwa haja zake za kimsingi wakati moyo unapoitaka ndoa na kuogopa kwa kuangukia katika haramu kama vile kutazama kwa yaliyoharamishwa na kupiga punyeto; kwani ndoa katika hali hiyo ni wajibu, [Rejea: Hashiyat Ibn Abdeen Ala Al Dur Al Mukhtaar, 2/462, Ch. Dar .[ Al Kutub Al Elmiyah.

Na wanachuoni wa Malikiy wanasema fakiri ni mtu anayemiliki kitu kisichotosheleza chakula cha mwaka mzima. [Rejea: Hashiyat AlDesuqiy juu ya Al Sharh Al Kabeer, 1/492, Ch. Dar Ihiyaa Al Turaath Al Arabiy] na walizingatia kujiepusha zinaa kwa ndoa ni miongoni mwa jumla ya vyakula, Al Nafrawiy alisema katika kitabu cha [AlFawakeh Al Dawaniy, 2/69,Ch. Dar Al Fikr]: "Mtoto analazimika kumuepusha baba yake na Uzinzi kwa kumuozesha mke, kwani jambo hili ni miongoni mwa jumla ya yaliyo wajibu wa motto kwa mzazi wake”.

Na wanachuoni wa Shafiy wanasema maskini ni mtu anayemiliki au anayechuma kitu kisichomtosheleza kama vile mtu anayehitaji kumi na hana ila nane ambazo hazimtoshelezi katika nyumba, mavazi na matumizi [Rejea: Asny Al Mataaleb Sharh Raudh Al Taaleb, 1/394, Ch. Dar Al Kitaab Al-Islamiy], na wamezingatia kumpa mali anayehitaji kuoa na hana kitu ni katika mahitaji, [Rejea: Mughniy Al[Muhtaaj, 4/175].

Na wanachuoni wa Hanbaliy wanasema maskini ni mtu asiyepata mahitaji kamili ya kutosheleza [Rejea: Kashaf Al Qinai kwa Al Bahotiy, 3/85-86, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah, na Al Insaf kwa Al Maradawiy, 3/217, Ch. Dar Ihiyaa Al Turaath Al Arabiy], na walitaja kuwa haja ya kuoa ni miongoni mwa mahitaji ya kujitosheleza kama vile haja ya kuwa na mtumishi. Al Bahotiy alisema katika kitabu cha [Daqaiq Auliy Al Noha, 3/242, Ch. Alam Al Kutub]: “Ni wajibu kumpa mtumishi matumizi, tena matumizi yake yote kwa kuwa ana shida nayo kama vile mke kwani hayo ni miongoni mwa matumizi ya kujitosheleza”.

Aidha inajuzu kutoa mali ya Zaka kumsaidia mwislamu anayehitaji kuoa, kwa mujibu wa kauli ya wanachuoni waliozama katika kufasiri kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na katika njia ya Mwenyezi Mungu} ambapo kauli hii inajumuisha mambo yote ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa hiyo huingia kila mtu anayemtii Allah s.w na anayefanya njia za kheri, na bila shaka ndoa ni mfano wake. [Rejea: Hashiyat Ibn Abdeen, 2/343, na Badaa'i Al sanaa'i, 2/45, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah na Al Tafseer Al Kabeer lil Imamu Al Raziy, 16/115, Ch.[Dar Al Fikr].

Na Tirmidhiy, Al Nasaiy na Ibn Majah wamepokea katika Sunna zao kutoka kwa Abu Hurairah R.A. amesema: Mtume S.A.W. amesema: “Watu watatu wana haki ya kusaidiwa na Mwenyezi Mungu; mwenye kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, mwenye ahadi ya kuachwa huru na anataka kulipa haki yake, na anayetaka ndoa ii kujiepusha na zinaa”. Basi kauli ya Mtume S.A.W.; "Watu watatu wana haki ya kusaidiwa na Mwenyezi Mungu" inamaanisha watatu hawa wanastahiki msaada kutoka Mwenyezi Mungu Mtukufu. Alhafidh Abdulrau'uf Al Menawiy anasema katika kitabu cha [Faidhu AlQadeer,3/317, Ch. Al Maktabah AlTojaariyah Al Kubra]: "Maana ya kauli hiyo ni kuwa mambo hayo matatu ni miongoni mwa mambo yenye ugumu ambayo yanamchokesha mwanadamu na yanamvunja mgongo wake, kwa hiyo yanahitaji misaada ili mwanadamu aweze kuyashugulikia, Altibbiy amesema: jambo gumu zaidi kuliko yote ni kujiepusha na zinaa na kuzuia matamanio yaliyotawala katika nafsi. Mtu anapoangukia katika zinaa anakuwa katika daraja ya mnyama na huwa chini kuliko walio chini. Ama anayejiepusha na zinaa na kuwahi msaada wa Mwenyezi Mungu, basi huyu hupanda katika daraja ya ya Malaika juu kuliko walio juu.

Tanbihi: Al Aarif Bin Arabiy amesema: Ukimwona mmoja kati ya watatu hawa, basi msaidie kwa sehemu ya mali au kwa kauli njema au kwa hali, kwani ukimsaidia basi wewe ni naibu wa haki katika kuwasaidia, kwa sababu ikiwa kusaidiwa ni haki juu ya Mwenyezi Mungu basi mtu anayewasaidia anatekeleza kwa niaba ya Allah s.w aliyejilamizisha mwenyewe, kwa hiyo anamkirimu mwenyewe”.

Na msaada wa Mwenyezi Mungu kwa watu watatu hawa ni kihali kwa kurahisisha mambo na kuwaondoshea vizuizi au unakuwa ni msaada wa kimali kwa fedha ambazo wanazitegemea katika kukidhi mahitaji yao(Jihadi - Uhuru - kujiepusha na zinaa). Msaada wa Allah s.w kwao unajumuisha mambo mawili; mali na hali kutoka kwa Allah S.W. Wanachuoni wamekubaliana kwamba anayepigana jihadi na mwenye ahadi ya kuachwa huru wanaostahiki msaada wa Mwenyezi Mungu kwa mali ya Zaka. [Rejea: Almajmuui Sharh Almuhadhab, 6/200, Ch. Dar Alfikr].
Kwa mujibu wa hadithi hiyo tukufu, anayetaka kuoa ili kujiepusha na zinaa anashirikia nao katika kustahiki msaada kwa mali ya Zaka, na kumtenga katika wanaostahiki kupewa Zaka ni kwenda kinyume na maana ya hadithi na udhahiri wake, kwani haja ya anayetaka ndoa ni kama haja ya mwenye kupigana jihadi au mwenye ahadi ya kuachwa huru, basi anapewa kutoka mali ya Zaka kiwango kinachomsaidia kujiepusha na zinaa kwa ndoa, kwani katika hayo ni kumsaidia anayestahiki msaada wa Mwenyezi Mungu.

Maelezo ya juu yanaungwa mkono na dalili mbali mbali, kama:
Jambo la kwanza: Allah S.A. anasema kuhusu mwenye ahadi ya kuachwa huru-: {Na wapeni katika mali ya Mweyezi Mungu aliyokupeni} [AN NUR 33]. Hapa alibainisha kuwa mwenye ahadi ya kuachwa huru anapewa kwa sababu ni haki yake juu ya Allah s.w kuokat mali ya Mwenyezi Mungu, na muradi katika aya ni mali ya Zaka kama walivyosema Ibn Abaas R.A, Al Hassan Bin Zaid Bin Aslam na Muqatil Bin Hayaan, na aliichagua Imamu Mfasiri Ibn Jareer Al Ttabariy, [Rejea: Tafseer Al Quraan Aladheem li Ibn Katheer, 6/53-54, Ch. Dar Ttibah, na Rejea: Zad Al Maseer fiy ilmu Tafseer li Ibn Al Jauziy, 3/293, Ch. Dar Al Kitaab Alarabiy]. Pia mwenye kupigana jihadi anapewa kutoka mali ya Zaka kwa itifaki ya wanachuoni, na anayetaka kujiepusha na zinaa kwa ndoa anapewa kutoka mali ya Zaka, kwani watu watatu hawa ni sawa katika kutegemea msaada wa Mwenyezi Mungu kwa mali na wanastahiki msaada wake kwa kuwa wamefikia malengo yao.

Jambo la pili: Zaidi ya mwanachuoni mmoja waliutumia ushahidi wa hadithi hiyo katika kuwajibisha kumsaidia mwenye ahadi ya kuachwa huru kwa mali, basi hawakuhusisha msaada kwa upande wa hali tu, bali wamesema hadithi hiyo inaashiria msaada wa mali pia. Kwa hiyo kumvua anayetaka ndoa miongoni mwa wanaostahiki msaada wa kimali ni kuhusisha watu maalumu wa kupewa msaada.

Imamu Al Zailaiy amesema katika kitabu cha [Tabeien Al Haqaiq, 1/297-298, na katika Hamishahu Hashiat Al Shalabiy Ala Al Sharh, Ch. Dar Al Kitaab Al Islamiy]: "{Na katika kuwapa uungwana watumwa} [AT TAWBA, 60], wenye ahadi ya kuachwa huru yaani wanasumbuka katika kukombolewa, hii ni kauli ya Jamhuri ya wanachuoni.

Na Albaraai Bin Aazeb amepokea kutoka kwa Abu Huraira kuwa Mtume S.A.W. amesema: "Watu watatu wana haki ya msaada juu ya Mwenyezi Mungu, mwenye kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, na mwenye ahadi ya kuachwa huru anayetaka kulipa haki ya bwana wake, na anayetaka kuoa anayetaka kujiepusha na zinaa". Imepokelewa na Tirmidhiy, Nassaiy na wengineo.

Na mwanachuoni Alzailaiy anatoa ushahidi kwa hadithi tukufu hiyo kutafsiri kutoa Zaka katika kuwapa uungwana watumwa kuwa ni kumsaidia mwenye ahadi ya kuachwa huru kwa mali za Zaka. Ibn Qudama alisema katika kitabu cha [Almughniy, 10/342, Ch. Dar Ihyaa Al Turaath Alarabiy]: "Bwana inampasa kumpa mwenye ahadi ya kuachwa huru sehemu ya mali, amfanyie wepesi katika kipindi cha mwisho cha mkataba wake, kumliwaza na kushukuru neema ya Allah S.W. pia Zaka hutolewa kwa kuliwaza kutokana na neema aliyomneemesha Mwenyezi Mungu mja wake, kwa sababu mtumwa alitumika katika kukusanya mali hiyo na alichoka katika kazi hiyo, basi ni wajibu kumliwaza kwayo, kwa kuwa Mtume S.A.W. aliamrisha kumlisha mtumwa kutoka chakula ambacho alikifanya kazi katika joto lake na moshi wake. Kauli hii inapelekea wajibu, kwa sababu ndani yake ni kumsaidia katika kuachiwa huru na kumsaidia anayestahiki msaada wa Allah s.w. Kisha akataja hadithi.

Na dalili hapa ni Ibn Qudama kuleta sababu ya wajibu wa kumsaidia mwenye ahadi ya kuachwa huru kwa mali kwa sababu ni kumsaidia anayestahiki kusaidiwa na Allah s.w. Kuitumia hadithi hii kwamba ni ushahidi inabainisha kuwa ni wajibu kutoa msaada wa kifedha kwa wale ambao Allah s.w amejilazimisha kuwasaidia. Kwa hiyo kuhitajia kwao fedha ni kufanikisha lengo lao, ambalo ni jihadi katika njia ya Allah s.w, kujikomboa kwa ahadi ya kuachwa huru na kujiepusha na zinaa kwa ndoa.

Alhafidh Ibn Kathiyr alisema katika Tafsiri yake [6/54] alipofasiri kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na wapeni katika mali ya Allah s.w aliyokupeni} [AN NUR 33]. Ibn Abaas R.A. alisema: "Mwenyezi Mungu amewaamirisha waumini kusaidia wakati wa kumkomboa mtu. Mtume S.A.W. amesema watu wa aina tatu ni haki yao kusaidiwa na Mwenyezi Mungu, akamtaja mwenye ahadi ya kuachwa huru na anataka kulipa haki ya bwana wake.

Jambo la Tatu: Kuna dalili zinazoelekeza kuwa aina zilizotajwa katika hadithi tukufu hiyo ni miongoni mwa wanaosatahiki kupewa Zaka wanapohitaji msaada wa mali ili wafanikishe lengo lao.

Alhafidh Ibn Kathiyr amesema katika kitabu cha [Jam'i Al Usul, 9/7314, Ch. Maktabat Alhalawaniy, Matabait Al Malaah, na Maktabat Dar Albayaan]: "Na katika riwaya nyingine badala ya mwenye ahadi ya kuachwa huru basi ametajwa mwenye deni ambaye anataka kulipa deni.

Na Alhafidh Suyuwti alisema katika kitabucha [Sharhuhu Ala Sunnan Al Nassaiy, 6/61, Ch. Maktabat Al Matbu'aat Al Islamiyah - Halab]: "(Watu watatu wana haki ya kusaidiwa na Allah S.W.) hadithi hii inataja mtu wa nne ambaye ni mwenye kuhiji", na nimewaandika katika beti mbili. Maana zake ni: Haki juu ya Allah ni kusaidida na yeye kesho atawalipa, mwenye ahadi ya kuachwa huru, mwoaji ili kujiepusha na zinaa, na anayekuja Makka kuhiji na mwenye kupigana jihadi.

Alhafidh Suyuwti anasema:- Kuna hali zinastahiki kupewa Zaka wakati wa haja, nazo ni: Jihadi husaidiwa kwa mali ya Zaka, kukomboa mtumwa mwenye ahadi ya kuachwa huru husaidiwa kwa Zaka, Hijja husaidiwa kwa Zaka na kulipa deni la mwenye deni husaidiwa kwa Zaka. Kwa hiyo dalili zinaashiria kuwa riwaya mbali mbali zilizokuja katika hadithi zinaruhusu kumsaidia anayetaja kuoa kwa mali ya Zaka ikiwa anahitaji mali ili kufanikisha lengo lake. Kwa hiyo kutaka kujiepusha na zinaa kwa ndoa ni kunazingatiwa ni miongoni mwa makusudio yanayopelekea mwislamu kusaidiwa kutoka mali ya Zaka.

Na Abu Dawud amepokea katika Sunna zake kutoka kwa Almastawrad Bin Shadad na alisema: nimemsikia Mtume S.A.W. anasema: "Mwenye mfanyakazi kwa ajili yetu basi apate mke, na kama hana mtumishi basi apate mtumishi, na kama hana nyumba basi apate nyumba", alisema: Abu Bakar alisema: niliambiwa kuwa Mtume S.A.W. alisema: “Mtu yoyote asiyechukua hivyo basi yeye ni mnyonyaji na mwizi”.

Na Imamu Ahmad aliipokelea kwa lafdhi mbili Kwanza: “Mtu yoyote alitawala kazi yetu na hana nyumba basi achukue nyumba, au hana basi achukue mke, au hana mtumishi basi achukue mtumishi, au hana mnyama basi achukue mnyama, na asiyechukua vitu hivyo basi ni mnyonyaji”
Pili: "Mtu yoyote alitawala kazi yetu na hakuwa na mke basi aoe, au hakuwa na mtumishi basi achukue mtumishi, au hakuwa na nyumba basi achukue nyumba, au hakuwa na mnyama basi achukue mnyama, asiyepata vitu hivyo basi ni mnyonyaji au mwizi”.

Na ushahidi ni kwamba Mtume S.A.W aliruhusu kumpa mfanyakazi mahitaji yaliyotajwa, ikiwemo ndoa, na kauli yake S.A.W.: "Mtu yoyote alitawala kazi yetu" kauli hii inajumuisha kila mfanyakazi, wakiwemo wafanyakazi wakusanyaji wa Zaka, kwa hiyo inajuzu kuwapa Zaka wenye shida zilizotajwa na Mtume S.A.W., kwa hiyo inajuzu kuwapa wafanyakazi wa Zaka na wengineo. Kutokana na hayo inajuzu kumpa Zaka mfanyakazi kwa ajili ya kuoa. Hadithi hii imejulisha kuwa kuhitajia ndoa katika sheria kunazingatiwa ni miongoni mwa mahitajio ya kimaumbile kama vile; nyumba, huduma kwa asiyeweza kujihudimia mwenyewe na chombo cha usafiri kwa masafa ya mbali ili kufanya kazi yake.

Mambo hayo yanamuondoshea mtu taabu na maangamizi. Na kama kukidhi haja ya ndoa hakuzingatiwi ni miongoni mwa mambo yenye umuhimu kwa mwanadamu, basi anachochukua mfanyakazi ili aoe ni unyonyaji, wizi na dhulumu kwa waislamu, kwani ni kuweka kitu sehemu isiyokuwa yake. Hadithi inajulisha kujuzu kutoa fedha za waislamu – ikiwemo Zaka- ili kukidhi haja ya ndoa.

Mala Aliy Al Qaar'i anasema katika sherehe yake ya hadithi katika kitabu chake [Marqaat Al Mafateeh Sharh Meshkaat Al Masabeeh, 7/294, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah]: "(Mtu yeyote katika sisi waislamu, (akiwa ni Kibarua basi apate) yaani kwa mali ya zaka (mke, na kama hana mtumishi basi apate matumishi, na kama hana nyumba basi apate nyumba), Al Mdhahar amesema: yaani inajuzi achukue mali kutoka katika Baitullmali kiasi cha mahari ya mke, matumizi na mavazi yake, na kwa kitu chochote ambacho ni lazima katika maisha yake bila ya kufanya ubadhirifu wa mali hiyo au kujineemesha, na kama atachukua zaidi ya mahitaji yake ya dharura basi hiyo itakuwa ni haramu juu yake ... na kilichowazi zaidi ni kuwa ana haki ya kutumia kiasi cha dharura na kutodhuru mali ya waislamu, na katika mapokezi mengine (anayechukua kinyume cha hayo) yaani Kinyume cha yaliyotajwa au yaliyomo katika maana yake, basi yeye ni mnyonyaji, imepokelewa." na Abu Dawud.

Na kauli yake: "achukue kutoka katika mali aliyonayo mikononi mwake kutoka katika mali ya Baitullmali", inaashiria kuwa mfanya kazi wa Zaka achukue kwa namna ilivyotajwa; yaani mahari ya mke, matumizi na mavazi yake. Na kauli yake: "Na iwapo atachukua zaidi ya haja na matumizi yake ya dharura basi hivyo ni haramu", inaashiria kuwa ndoa haikuwa zaidi ya haja yake ya dharura, bali ndoa ni miongoni mwa mambo ya dharura, basi kutokana na hayo ndoa ni miongoni mwa mahitaji ya dharura ya kibinadamu ambayo Fikihi ya Zaka inatilia mkazo wa kuliondosha tatizo hilo. Ni Kama hali ambayo itajikita yenyewe kwa watu, na wakajikuta wamo ndani yake, na inapelekea kuyaangalia na kuyatimiza masilahi yao na kuwaondoshea mambo yanayowadhuru.

Wanachuoni wameweka makusudio maalumu ya sheria kwa kutunga kwamba ndoa inazingatiwa kuwa ni miongoni mwa mambo ya dharura ambayo hayaachwi hata kidogo, basi Al Ezz Ibn Abdulsalaam anasema katika kitabu chake [Kawaid Al Ahkaam, 2/93, Ch. Kampuni ya Umm Al Quraa ya uchapishaji na usambazaji - Kairo]: "Basi masilahi ya duniani na ya akhera yamegawanyika sehemu tatu na kila sehemu miongoni mwazo ipo katika vyeo mbalimbali. Ama masilahi ya dunia yanagawanyika na kuwa mambo ya dharura, mahitaji na mambo ya vikamilishavyo. Na mambo ya dharura: Ni kama vile chakula, vinywaji, mavazi, nyumba, ndoa, vipando vya uchukuzi wa vyakula na vitu vingine vinavyohitajiwa maishani. mambo hayo yote ni ya dharura na kidogo chake kinachoweza kukidhi haja ya mtu kinazingatiwa kuwa ni dharura".

Imamu Al Shattbiy anatilia mkazo kuwa kuhitaji ndoa kunazingatiwa kuwa ni miongoni mwa mambo ya dharura hata kama itatuka shaka ndani yake. Anasema katika kitabu cha [Al Mwafaqaat, 3/134, Ch. Dar Al Mairefah - Bairut]: "Labda limetokea agizo na katazo katika mambo ya dharura juu ya Sunna au uhalali na utukufu katika yanayofahamika kwa mwelekeo wake na ikatuka shaka katika kuwa kwake ni miongoni mwa mambo ya dharura kama ilivyotangulia kuelezwa kwake katika vyakula, vinywaji, mavazi, ndoa, na kadhalika, aina za kujilinda na madhara na viangamizavyo na kila kinachofanana navyo, basi yeye anaona kwamba hayo hayaendi sambamba na mambo ya dharura, lakini mambo hayo ni miongoni mwayo kisheria", na Al Shattbiy anakubali mahali pengine katika kitabu chake kwa kuizingatia ndoa kuwa ni miongoni mwa mambo ya dharura kwa upande mmoja, na kuizingatia kuwa ni miongoni mwa mahitaji kwa upande mwingini, na anasema [2/101]: "Ndoa kwa kusudio la kumaliza haja, ikiwa inaingia na kuwa chini ya makusudio yanayoungana na mambo ya dharura basi inaingia pia upande mwingine na kuwa chini ya mahitaji; kwani inarejea katika kusudio la kuwapanulia waja wapate wanayoyakusudia na watimize haja zao na kuwandoshea uzito wa aina yeyote kwao".

Na hakuna hitilafu baina ya wanachuoni katika uwajibu wa mwislamu kujiepusha na zinaa na kuangukia katika haramu, kwa hivyo kuacha mambo ya haramu kunazingatiwa ni miongoni mwa mambo ya dharura na kwa masilahi ya kiakhera. Al Ezz Bin Abdulsalaam anasema katika kitabu cha [Kawaid Al Ahkaam, 2/93]: "Na ama masilahi ya akhera ya kwamba kutenda yaliyo ya wajibu na kuacha mambo yaliyo ya haramu ni miongoni mwa mambo ya dharura". Na kutokana na hayo basi anayeogopa kuangukia katika mambo ya haramu na hawezi kujieweka mbali nayo ila kwa kupatikana jambo maalum, matakwa yake yatakuwa ni haja ya msingi ya dharura kwa njia yake, ambayo kwayo huilinda na kuihifadhi dini yake na utiifu wake kwa Mwenyezi Mungu; basi kama hakupata nija ya kujipatia haja yake hiyo ya kimsingi atakuwa na haki ya kupata Zaka kwa kumzingatia kuwa ni fakiri au maskini.

Na kutokana na hayo kwamba haja ya vijana wanaotaka kuoa na hawana uwezo wa kifedha wa ndoa wana haja ya dharura yenye pande mbili: wa kwanza: kwa kuizingatia ndoa ni miongoni mwa masilahi ya kidunia ya kidharura, na wa pili: kuizingatia ndoa kuwa ni katika mambo yanayotimiza masilahi ya kiakhera ya kidharura, na hakuna shaka kuwa mwenye mambo hayo mawili ya dharura anastahiki kupewa fungu la mali za Zaka".

Wanachuoni wa madhehebu ya Shafiy walitaja kuwa anayehitajia kuoa na hana kitu cho chote basi anapewa fungu la zaka kwa ajili ya dharura [Rejea: Nihayat Al Muhtaaj, 7/153, Ch. Dar Al Fikr, na Tuhfat Al Muhtaaj, 7/152, Ch. Dar Al Kitaab Al Islamiy] na wanachuoni wa madhehebu ya Malikiy wamesema kuwa mtoto wa kiume analazimika kumuepusha baba yake na zinaa kwa kumuozesha mke; kwani ndoa hiyo ni ni miongoni mwa mambo ya wajibu kwa mtoto [Rejea: Al Fawakeh Al Dawaniy, 2/69], na wanachuoni wa madhehebu ya Hanafiy wanasema kuwa ndoa huwa wajibu pale mtu inapoogopa kutumbukia katika mambo ya haramu, na inatosha kuwa wajibu kwa kuogopa tu kuangukia katika Uzinzi hata kama haijatokea. Ama inapotokea basi ndoa inakuwa Faradhi na si wajibu – kwa mujibu wa Istilaahi ya Madhehebu ya Hanafiy katika kutofautisha baina ya Faradhi na Wajibu – na wala si sharti kuchelea kuangukia hasa hasa kwenye Zinaa bali huwa wajibu pia kuchelea kuangukia katika makatazo mengine kama vile jicho la matamanio au kupiga punyeto na mengineyo mengi.

Ibn Najm anasema akieleza hukumu ya kuoa katika kitabu chake cha [Al Bahr Al Raiq, 3/84, Ch. Dar Al Kitaab Al Islamiy]: "Na sifa yake kama vile Faradhi, Wajibu, Sunna, Haramu na Halali, ama ya kwanza: kuwa anaogopa kuangukia katika zinaa kama hakuoa ambapo hawezi kujiepusha ila kwa kufunga ndoa, kwani yasiyomfikisha mtu katika kuacha haramu ila kwayo basi huwa ni faradhi. Ama ya pili: ni kuwa anaogopa zinaa kidogo si kama ilivyozungumzwa, kwani woga wake huo si ule usio na udhibiti ambao unamlazimisha kufikia kutokuwa na uwezo".
Ibn Abdeen anasema katika kitabu chake cha [Hashiat Ala Al Dur Al Mukhtaar, 3/6]: "Na kadhalika katika yanayodhihiri kama mtu alikuwa haweza kujizua na kutazama haramu au kupiga punyeto, basi inalazimika kuoa hata kama hakuwa anachelea kuangukia katika zinaa.

Ibn Abdeen ametaja kuwa ndoa iko katika hali ya kutakiwa na inakuwa ni miongoni mwa mahitajio ya kiasili [2/462] anaseama; "Suala hili linanukuliwa kutoka kwa Abi Hanifa katika kutanguliza Hija kabla ya kuoa, na ufafanuzi huu uliotajwa aliusema mwenye kitabu cha Al Hedaya katika sehemu ya [Al Tajnees], na aliutaja katika Al Hedaya bila udhibiti, na akautuma kama ni ushahidi wa kwamba Hija ni ya kutekelezwa haraka kwa aonavyo yeye na maana yake ni kutanguliza Hija kabla ya ndoa, na hata kama itakuwa wajibu wakati inapotakiwa na hili liko wazi katika Al Hedaya ingawa wakati huo ni miongoni mwa haja za kiasili, kwa hiyo Ibn Kamal Basha alimpinga katika [Sharh yake ya Al Hedaya] kwamba katika hali hiyo kutakwa ndoa inatangulia kabla ya Hija kwa makubaliano (ya wanavyuoni) kwani katika kuiacha ndoa kuna mambo mawili; kuacha faradhi na kuangukia katika zinaa, na jawabu la Abi Hanifa ni katika hali isiyokuwa ya kutakiwa kwake, yaani katika hali isiyopelekea kutokea zinaa, kwani kama inaweza kupelekea zinaa, basi kuoa ni faradhi. Na iwapo mtu aliogopa zinaa basi ndoa ni wajibu na siyo faradhi, na kwa hali hiyo Hija inaitangulia ndoa, kwani Hija ni faradhi".

Na Ibn Qudama, Mhanbaliy, katika kitabu cha [Al Mughniy, 4/7] anasema kwamba wanavyuoni wote wa Fiqhi wanasema kuwa ndoa inakuwa wajibu pale mtu anapochelea kutumbukia katika yaliyoharamishwa, anasema: "Na watu katika ndoa ni aina tatu; miongoni mwao ni yule anayejiogopa kuangukia katika yaliyokatazwa kama ataacha kuoa, basi huyo anapaswa kuoa kutokana na kauli ya wote wa Fiqh; kwani analazimishwa kujiepusha na zinaa na kuhifadhi roho yake na haramu, na njia ya kuyafanya hayo ni ndoa".

Vijana wengi wa leo – isipokuwa waliopata rehma za Mwenyezi Mungu –wako hatarini kutumbukia katika madhambi ambapo dogo la madhambi hayo ni angalio la haramu kwa sababu ya kutaka kwa kuoa, na kutokuwa na uwezo ma kifedha wa kufanya hivyo.

Na wanavyuoni wa madhehebu ya Shafii wanasema kuwa anaehitaji kuoa, kama matamanio yake hayataondoka kwa saumu –na ni bora zaidi kwa yule ambaye hawezi kufunga kwa sababu ya hali ya kazi au kwa sababu ya hali yake kiafya– basi kama hna mali, analazimika kukopa na kuoa. Na hakuna shaka yeyote kwamba wakati huo mtu huyu anakuwa ni miongoni mwa wenyekustahiki kupewa Zaka, na hasa kama hakupata mtu wa kumkopesha mali ya kutosha kwa ajili ya lengo lake hilo, tena mkopo halali na wa kisheria, na kama si hivyo, inatosha kuwa kwa mkopo huo yeye anakuwa ni miongoni mwa wenye deni wanaostahiki kupewa Zaka.

Sheikh wa Uislamu, Zakariya Al Ansaariy wa madhehebu ya Shafiy anasema katika kitabu cha [Sharh Al Bahja Al Wardiya, 4/92 na katika kitabu hichi kuna Hashiyat Al Qaasem na Hashiyat Al Sherbeiniy, Ch Al Matba'ah Al Maimaniyah]: "Na kama anayehitaji ndoa hata kuwa na uwezo, basi ni bora kwake kuiacha kama ilivyotajwa katika kitabu cha [Al Menhaaji] na vinginevyo, na imetiliwa mkazo zaidi katika kitabu cha [Sharh Muslim] basi anasema mwandishi: Kwa hali ya mtu huyo, Ndoa inachukiza, na analazimika kuvunja matamanio yake kwa Saumu, kutokana na hadithi ya Mtume S.A.W. "Enyi vijana", anasema katika kitabu cha [Al Raudhah]: Nai iwapo matamanio hayatabasi hayataondoka kwa njia nyingine yoyote isipokuwa kwa ndoa.

Mwanachuoni mkubwa Al Sherbeiniy anasema: "Tamko lake: (bali anaoa) na anakalifishwa kukopa mahari iwapo hatakuwa na uwezo wa kufanya hivyo.

Imamu Al Qaraafiy wa madhehebu ya Malkiy anasema katika kitabu cha [Al Zakheerah, 3/148. Ch. Dar Al Gharb Al Islamiy - Bairut]: "Kuchukua Zaka ima kwa kuihitajia kama vile mtu fakiri, au sisi kuwa na haja ya mtumishi maalum kama vile mkusanyaji Zaka, na mtu anaehiji hahitajii kupewa Zaka kwa kutopasa Hija juu yake iwapo yeye ni fakiri wakati huo, na pia kama yeye ana mali inayomtosha kama ni tajiri, na sisi hatumuhitaji.

Na inachukuliwa kauli ya Imamu Al Qaraafiy kwa kutostahiki kupewa Zaka mtu anayetaka kwenda Hija kwa sababu Hija si wajibu kwake, kwa hiyo yeye hastahiki Zaka. Kwani kama Hija ingelikuwa wajibu juu yake basi angekuwa anastahiki kupewa Zaka. Na kutokana na hayo anayewajibika kuoa na hana uwezo wa kutosha ni haki yake asaidiwe kwa kupewa mali ya Zaka.

Wanachuoni wa Madhehebu ya Hanbaliy wanasema kuwa kuhitajia tendo la ndoa na ndoa yenyewe ni hitajio la kimaumbile kama chakula na mfano wake. Al Bahutiy anasema katika kitabu cha [Daqaiq Auliy Al Nuha, 2/615-616]: "(Na mama wa motto wa kiume huahiwa huru kwa kifo cha motto wake yaani bwana wake hata kama hakummiliki mtu mwengine kwa hadithi Ibn Abaas ambayo ni Marfuu: "Mtu yeyote atakaemwingilia mtumwa wake na akajifungua basi mtumwa huyo atakuwa huru kupitia utupu wake (kutumiwa na bwana wake kuzalishia motto)" imepokelewa na Ahmad na Ibn Majah.. Na kutoka kwake pia amesema: "mama Ibrahim alitajwa mbele ya Mtume S.A.W, basi akasema mtoto wake amemkomboa", imepokelewa na Ibnu Majah na Al Darqatniy, kwani kumzalisha kijakazi ni uharibu uliotokea kwa sababu ya haja ya kimaumbile, nayo ni kuingilia. basi ikawa ni miongoni mwa rasilimali kama vile chakula na vinginevyo".

Al Mardawiy anasema katika kitabu cha [Al Insaaf, 9/410]: "Faida: Lau mtu alimpotea mama wa mtoto wake na mama huyo akawa anahitaji fedha za matumizi: basi mama huyo ataozeshwa kwa usahihi wa madhehebu. Amesema katika kitabu cha [Al Furuu'i]: "Usahihi zaidi ni kuwa mama huyo ataozeshwa, na inasemekana: haozeshwi. Hata kama atakuwa na haja ya tendo la ndoa: hataozeshwa. Lakini ametoa maelezo katika kitabu cha [Al Fruu'i] na akasema: inaelekea katika kujuzu kwa yule anayeizingatia kuwa ni kama matumizi, nikasema: Na huu ndio usahihi wenyewe. Na madhara yanayokuja baadae yake ni makubwa zaidi kuliko madhara yanayotokana na (kukosekana) matumizi".

Ibn Qudama anasema katika kitabu cha [Al Mughniy, 8/172]: "Na inamlazimu mtoto wa kiume kumuepusha baba yake na Uzinzi, iwapo atahitaji kuoa... Nasi tunaona: kwamba hayo ni miongoni mwa anayoyahitaji na hudhurika kwa kuyakosa kwake, kwa hivyo yanamlazimu mtoto wake kama anavyolazimika kwa matumizi mengine. Na wala hayafanani na peremende; kwani hiyo haimsababishii madhara yoyote kwa kuikosa kwake, isipokuwa ianafanana na chakula na unga".

Na kwa kuongeza kwa yaliyotangulia, ni kuwa wengi wa wanazuoni wa Fiqh wanasemea kuwa inajuzu kutoa Zaka kwa ajili ya kuondosha tatizo la kutokuwa na uwezo wa ndoa na wameyasema hayo katika vitabu vya madhehebu yanayotegemewa, na wakaelezea sababu kwamba ni katika utimizaji wa kutoshelezeana au ni kama kutoa kwa ajili ya dharura. Miongoni mwa wanachuoni wa Madhehebu ya Shafiy; Al Khateeb Al Sherbeiniy anasema katika kitabu cha [Mughniy Al Muhataaj, 4/175]: "Na katika fatwa za Ibn Al Bazriy: ... na kama mtu alikuwa anauwezo wa chumo la kumtosha kwa chakula na mavazi lakini anahitaji kuoa basi apewe fedha kutoka katika Zaka ili aoe; kwani kufanya hivyo ni kukamilisha utoshelezaji", na huu ndio uwazi wake".

Na Ibn Hajar Al Haitamiy anasema katika kitabu cha [Sharh Al Muqadimah Al Hadhramiyah, 2/154, na ndani yake kuna, Hawashiy Al Madaniyah, Ch. Dar Al Ttibaa'ah Al Amiriyah]: "Na mtu yeyote mwenye kumiliki nyumba na kipato chake hakimtoshi basi apewe kitakachomtosha kwa upungufu alionao... na vivyo hivyo kwa yule anayechuma kinahomtosha yeye lakini anahitaji kuoa basi ana haki ya kuchukua kinachomtosheleza kwa ajili ya ndoa, kwani hilo ni katika ukamilishaji kilichopungua ili kimtoshe".

Na anasema katika kitabu cha [Tuhfat Al Muhtaaj, 7/152]: "Kama aliweka nadhiri ya funga mwaka mzima na nadhiri ikathibiti, na kisha Saumu yake hiyo ikamzuia kufanya kazi, basi atapewa Zaka kwa ajili ya dharura wakati huo kama vile lau angelihitaji kuoa na hana kitu chochote basi angepewa uwezo wa kumtosha".

Al Ramliy anasema katika kitabu cha [Nihayat Al Muhtaaj, 7/153]: "ndiyo, Ibn Al Bazariy alitoa fatwa kuwa Kama mtu aliweka nadhiri ya kufunga mwaka mzima na nadhiri hiyo ikathibiti na Saumu yake hiyo ikamzuia kufanya kazi basi atapewa zaka kwa ajili ya dharura wakati huo kama vile lau mtu huyo angelihitaji kuoa na hana kitu, basi anapewa kiasi cha fedha za kumtosha kwa ajili ya ndoa".

Na miongoni mwa wanachuoni wa madhehebu ya Malikiy Al Hattaab, anasema katika kitabu cha [Mawaheb Al Jaleel, 2/347, Ch. Dar Al Fikr]: "Imeelezwa kutoka kwa Al Barzaliy kuwa msichana yatima anapewa Zaka kwa ajili ya matumizi ya mambo ya msingi ya ndoa, na amri ambayo kadhi anaiona vizuri katika haki ya anayezuiwa, basi kutokana na hayo; basi msichana asiyemiliki vyombo na vito vinavyomtosha kukidhi mahitaji yake ya dharura ya ndoa anapewa mali ya Zaka na hili ni bora zaidi. Basi lizingatie".

Na katika kitabu cha [Hashiyat Al Desuqiy Ala Al Sharh Al Kabeer, 1/493, na Rejea: Hashiyat Al Sawiy Ala Al Sharh Al Sagheer, 1/658-659, Ch. Dar Al Maarif]: "Faida: Al Mawaaq amenukulu kutoka kwa Ibn Al Fakhaar kwamba hakitolewi kitu katika Zaka kwa ajili ya kutayarishia Bi harusi yatima. Na wakati mwingine, kutoka kwa Al Barzaliy na baadhi ya masheikh wake, wanasema kuwa inajuzu, na kama kauli hiyo imekuja pia katika kitabu cha [Al Meiyaar] kutoka kwa Ibn Arafa kwamba aliulizwa hayo na akajibu: "Kwamba msichana yatima anapewa mali ya Zaka kwa ajili ya kumfaa katika mahitaji yake ya dharura ya ndoa na jambo ambalo kadhi analiona kuwa ni vizuri, katika haki ya anayezuiwa".

Wanachuoni wa madhehebu ya Malikiy wameeleza kuwa mali ya Zaka iwapo itatosha kwa ajili ya misaada ili kununulia vitu vya mtumishi au mahari ya mke basi itatolewa kwa ajili ya lengo hili. Al Sheikh Eleesh al Malikiy anasema katika kitabu cha [Manhi Al Jaleel, 2/86, Ch. Dar Al Fikr na Rejea pia katika: Mawaheb Al Jaleel, 2/348, na Hashiyat Al Desuqiy Ala Al Sharh Al Kabeer, 1/494]: "(Na) inajuzu (kutoa zaidi ya hivyo), yaani kiwango cha Zaka kwa maskini au fakiri ambacho hakizidi matumizi yake ya mwaka mzima (na) kutoa (kiwango cha maatumizi ya mwaka mzima) kwa fakiri au maskini na wala si zaidi ya hivyo na hata kama itakuwa chini ya kiwango basi hicho ndicho kinachozingatiwa. Na katika kitabu cha [Al Dhakheerah] kama mali itapatikana zaidi basi thamani ya mtumishi itaongezwa na mahari ya mke itazidishwa".

Na miongoni mwa wanachuoni wa madhehebu ya Hanbaliy, Al Bahutiy anasema katika kitabu cha [Kashaaf Al Qinaa'i, 2/85-86]: "(Na sehemu kwa ajili ya masikini) inarejea katika aya, nae ni Yule asiekuwa na uwezo wa kutosha (wanaingia ndani yake, mafukara, wao ni wa aina mbili katika Zaka tu, na katika Hukumu zingine kuna aina moja)".

Ibn Qasem anasema katika kitabu chake cha [Hashiyat Ala Al Raudhi Al Muraba', 3/311, Ch. Al Mataabi' Al Ahliyah]: "Na miongoni mwa utimizaji wa kutosheleza ni kile anachokichukua fakiri kwa ajili ya ndoa, iwapo hana mke na anahitaji kuoa".

Na kutokana na yaliyotangulia kuyataja miongoni mwa dalili na maandiko ya wanachuoni wa madhehebu manne: Inajuzu kumpa Zaka mwislamu anayehitaji kuoa na hana uwezo wa kukidhi mahitaji yote ya ndoa kama vile mahari, samani, makazi na mengineyo.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi zaidi wa wote.

 

 

Share this:

Related Fatwas