Maadili ya Kiislamu – Chanzo chake

Egypt's Dar Al-Ifta

Maadili ya Kiislamu – Chanzo chake

Question

Nini chanzo cha maadili katika Uislamu?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:

Kwa mujibu wa kauli ya profesa Hamed Taher, mhadhiri wa falsafa ya Kiislamu, Chuo Kikuu cha Kairo, na makamo wa zamani wa mkuu wa Chuo hicho … katika uwanja wa maadili ya Kiislamu, tafiti zinapaswa kuelekea kwa kutoa vipengele vya fikra za kimaadili na mifano yake ya kivitendo kutoka Quraani Tukufu, Sunna ya Mtume S.A.W, mwenendo wa watu wema waliotangulia na majaribio ya baadhi ya watu mashuhuri katika historia ya Kiislamu kama Omar Ibn Abdulaziz, Al Hasan Al Bassriy, Al Harith Al Muhasabiy, Ahmed Ibn Hanbal, Al Ghazaliy na Ibn Hazm. Na pia vitabu vya wasomi wanaojali sana marekebisho ya kijamii kama Al Jahedh, Ibn Al Juwziy, Al Subkiy na Al Raghib Al Asfahaniy.

Kwa hakika maadili ya Kiislamu yana asili ya umbo la dini ya Kiislamu. Na ni uwanja wa mafanikio, mtafiti anaweza kutoa sifa za utambulisho wa Kiislamu kama zilivyowekwa kinadharia na kutokea kivitendo. Na upande huu wa mwisho una umuhimu sana kutokana na nafasi yake ya kuendelea kueneza Uislamu nje ya mipaka yake baada ya utawala wa dola la Kiislamu kupungua. Kwa hivyo hatuafikiani na nadharia za maadili ya Kimagharibi katika kuunda elimu ya kimaadili ya Kiislamu ili elimu hii iwe nakala asili inayotokana na upande wa Kimagharibi, kwani mihimili ya elimu ya kimaadili ya Kiislamu inategemea misingi ya kivitendo, yaani yanatokea kweli katika maisha ya watu. Aidha jaribio binafsi linacheza nafasi kubwa katika jambo hilo. Na baada ya hayo inawezekana kulinganisha madhehebu ya kimaadili ya Kimagharibi ili kusaidia katika utafiti wa kisayansi na upanuzi wa peo za utafiti. Ama kitabu cha TAHDHIBUL AKH-LAK cha Mskoweh ambacho watafiti wengi wanakizingatia ni mwakilishi wa elimu ya kimaadili ya Kiislamu- kwa kweli kitabu hiki si msemaji kwa niaba ya maadili ya Kiislamu, bali kilichomo ndani yake kinakaribia sana maadili ya Kigiriki hasa ya Arosto. Na kwa hivyo, lazima masomo katika elimu ya maadili ya Kiislamu yategemee matini asilia za Uislamu, na wahusika wa kweli katika uwanja wake.

Na misingi muhimu iliyojengwa na ulinganio wa Muhammad S.A.W. iliyotajwa na marehemu profesa Muhammad Dhiyaa Al Din Al Kurdiy mhadhiri na mkuu wa kitengo cha akida ya Kiislamu na falsafa katika Chuo Kikuu cha Al-Azhar ni kukuza na kusaidia upande wa kimaadili ili mwanadamu asimili katika matamanio yake mabaya. Kwa hivyo Mtume S.A.W. amesema: "Hakika nimetumwa ili kutimiza tabia nzuri".

Maadili ya Kiislamu ni kigezo kizuri ambacho mtu analazimika kukiiga, na ajaribu kukitekeleza ili afanikishe amani katika maisha yake na furaha kwa jamii yake.

Maadili ya kiislamu chanzo chake ni vyanzo asilia vya Uislamu, vyanzo vya uhakika na madhubuti, na hayo ni kinyume cha maelezo ya baadhi ya wanafalsafa kama Muntaniy na Beskal kwamba hakuna uhalisia wa kimaadili, na maadili daima yana mabadiliko na kutafautiana katika nchi moja kutoka enzi hadi enzi, na kutoka nchi hadi nyingine.

Wanachuoni wengi wa zamani na wa sasa kama profesa Abdul-Hamid Madkour wanasema kwamba elimu ya maadili ni elimu ya kupimo na kigezo hata yawezekana kusema aghalabu ya wanachuoni wamesema hivyo. Na maana ya kipimo ni kwamba inaeleza mfano mzuri kwa tabia ya kibinadamu, na inaweka ufahamu kamili wa kuwa nao tabia.

Elimu ya maadili ikiwa ni ya kipimo au ya sifa, kwa kweli inafanya kazi muhimu katika kufundisha maadili kwa ajili ya kutusaidia ili kufikia ufahamu mzuri zaidi wa hulka ya kibinadamu na kutujuza malengo yanayotupeka katika hulka kwa njia maalumu, pia elimu ya maadili iliyowasilishwa na wataalamu wa maadili inatuzidishia kiwango kikubwa cha ujuzi na majaribio ya fikra na rai zinazohusiana na uhalisia wa kitendo cha hulka, vipengele vyake, vyanzo vyake na malengo yake. Vile vile tunaweza kufaidika na mafunzo ya baadhi ya wanachuoni wa maadili hususan mifumo ya kimaadili ili kusahihisha hulka, kuinyoosha na kupambana na baadhi ya maradhi ya kimaadili yanayoikumba nafsi, na jambo hili linadhihiri kwa wanachuoni wa maadili wa Kisufi kama Al Harith Ibn Saad Al Muhasabiy katika kitabu chake ARRIAYAA LIHUQUWQILLAHI, na kitabu cha Al Ghazaaliy AL-IHYAAU kinachozungumzia baadhi ya maradhi ya kisaikolojia na kimaadili.

Kwa upande mwingine uhalisia wa kihulka uko wazi sana katika nyasia kuu za Uislamu - kama anavyosema profesa Madkor, kwa hivyo, watu walipoona nyasia hizi walikiri utukufu wa daawa ya Uislamu, kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu {Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha uadilifu….}.

Na Quraani inaunganisha moja kwa moja baina ya desturi za kimaadili, akida ya Kiislamu na sheria, na baina ya tabia ya kivitendo katika maisha, na inasisitiza kwamba hayo ni ukweli wa wema, na siyo matambiko ya kidhahiri. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema {Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. ..… na hao ndio wanaochamungu}. Tunaweza kusema maana ya kimaadili inapatikana ndani ya akida ya Kiislamu na sheria zake, kwani yote haya yanalenga kuifunza adabu nafsi na kutengeneza jamii na kuiinua kwa maadili.
Maana ya kimaadili katika akida na sheria ya Kiislamu:

Uhusiano baina ya kumuamini Mwenyezi Mungu Mlezi, Muumbaji, Mungu na Muabudiwa na baina ya maadili ni imara, kwani kumuamini Mwenyezi Mungu ni kumchunga, kumuogopa, kuona haya na kuwa na imani naye, kumtegemea na kuridhia uamuzi wake, kuvumilia mitihani yake na kushukuru neema zake. Kwa hivyo akida ya Kiislamu kwa kumuamini Mwenyezi Mungu ndio chanzo kikuu cha moja kwa moja kwa maadili ya Kiislamu.

Ama kuamini siku ya mwisho humsukuma mwanadamu kutekeleza amri za Mwenyezi Mungu na kuyafuata maadili ya Uislamu kwani Mwenyezi Mungu atakusanya viumbe vyote mbele yake ili kuwahukumu kutokana na waliyoyatenda. Na ndio maana tutakuta maadili mazuri chanzo chake ni kuamini Siku ya mwisho kama akida, na pia tukizingatia kwa kina tunaona tabia njema zote zinatokana na akida ya Kiislamu.

Na maana ya maadili haiko mbali na ibada, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Hakika Sala inakataza machafu na maovu}.

Na Zaka humtakasa anayeitoa kutokana na maovu na ubahili. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema {Chukua sadaka kutoka mali zao ili uwasafishe na uwatakase}.

Ama Saumu, Mtume S.A.W amehusisha kukubaliwa kwake kwa kuacha tabia mbaya. Amesema S.A.W. "Asiyeacha kauli ya uongo na kuifanyia kazi, Mwenyezi Mungu hana haja ya kuacha chakula chake na kinywaji chake.". [Imetolewa na Bukhary.]

Ama Hija, Mwenyezi Mungu ameusia kuwa lengo lake ni mtu kuuzuia ulimi wake kutokana na machafu: {Hija ni miezi maalumu. Na anayekusudia kufanya Hija katika miezi hiyo, basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika Hija}.

Na miamala katika Uislamu haikuwa mbali katika kutupia jicho upande wa kimaadili, kwani Mtume S.A.W. alitoa wito wa usamehevu katika kuuza na kununua, uaminifu na kutoghushi, na alikataza kupunguza mizani. Na aidha mipaka ya Mwenyezi Mungu imekuja ili iwe ni kizuio kwa wanaokwenda kinyume na akida za dini, desturi zake na sheria zake, na ili iwe ni ukuta unaowalinda watu wa haki kutokana na watu wa batili, na pia iwahifadhie watu dini yao, maadili yao, utu wao na mali zao.

Tabia zimetumika sana katika ujenzi wa Uislamu, ndio maana ni kawaida kwa tabia kushikamana kiasi kikubwa na Imani. Na kila Imani ikinyooka na kuwa imara moyoni, basi na maadili nayo yanakuwa imara na kunyooka. Mtume S.A.W anasema: "Aliyekamiliki Imani kati yenu ni mwenye tabia njema".

Kwa hakika, anayeangalia kwa makini katika Quraani na Sunna ya Mtume S.A.W anaona kwamba maadili yanajikita sana katika pande zote za sheria ya Kiislamu, na tunaweza kuyakuta katika kila uwanja miongoni mwa nyanja zake, kwa mfano yanaonekana katika ndoa, maisha ya watu, familia urafiki, ujirani, biashara, na kuchunga haki za wanyonge na masikini. Vile vile yanaonekana wakati wa talaka baina ya mume na mke, na yanahitajika wakati wa kuwashughulikia wahalifu, katika jihadi dhidi ya adui, na wakati wa kuwashughulikia wanyama. Mambo haya yote ushahidi wake unapatikana katika Aya za Quraani na hadithi za Mtume S.A.W.

Mambo yote hayo yanaonesha kwamba chanzo kikuu cha tabia na maadili katika Uislamu ni Quraani Tukufu na Sunna ya Mtume S.A.W. Na kwa kweli Uislamu ni akida na sheria zake zinakuwa pamoja na upande wa kimaadili na kitabia. Tena ni mfumo mmoja.
Marejeo:
1- Profesa Hamed Taher, MADKHAL ILAA ILMU ALMANGAJ, Kairo , DN, DT,uku ( 133-134).
2- Profesa Muhammad Dhiyaa Aldin Alkurdy, Al-Akhlak Al-islamiyah wa Alsufiyah, Kairo, cha. Al-saadah, mwaka 1409 H -1989, uku(3-15-16).
3-Profesa Abdulhamid Madhkour, Dirasat Fi Ilm Al-Akhlak, Kairo, Dar Al-Hanii, mwaka 1426 H- 2005, uku ( 29-30,107-112 ).
 

Share this:

Related Fatwas