Kutoa Zaka na Mali za Sadaka kwa Wa...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kutoa Zaka na Mali za Sadaka kwa Watoto Wasiojulikana Nasaba Zao

Question

Je, Inajuzu kutoa Zaka na sadaka kwa watoto wasiojulikana nasaba zao? Au haijuzu kufanya hivyo kwa sababu wao ni (wana haramu) kama walivyodai baadhi ya watu?

Answer

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:

Mwenyezi Mungu alitaja makundi yanayostahiki kupewa Zaka katika kitabu chake kitukufu (Quraani) basi akasema: {Wa kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanaozitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wasafiri. Huu ni wajibu uliofaridhiwa na Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.}[AT TAWABAH 60].

Asili katika Zaka ni kutotolewa isipokuwa kwa aina nane hizo zilizotajwa katika Quraani, Imamu Al Baidhawiy akasema katika tafsiri yake [336/4 pamoja na Hashiyat Al Khafajiy, Ch. Dar Ssader]: "Yaani: Zaka kwa hawa ambao idadi yao ni maalumu na wala si wengine."

Lakini kwa upande wa sadaka ya kujitolea basi mlango wake ni mpana zaidi kuliko wa zaka, ambapo inajuzu kuitoa sadaka kwa aina zile nane za watu pamoja na zingine, wawe matajiri wa kiislamu au mafukara, tofauti na zaka, ambapo katika zaka kuna masharti yasiyokuwepo katika sadaka, kama vile kumiliki mali maalumu, kupita mwaka mzima na kufikia kiwango maalumu.

Imamu An Nawawiy anasema: "Sadaka ya kujitolea inasihi kwa matajiri bila ya kizuizi chochote, kwa hivyo inajuzu kuwapa matajiri na aliyeitoa anapata thawabu kwayo, lakini ni bora zaidi kwa asiejiweza anayezihitajia." [Rejea, Al Majmou' 236/6 Ch. Maktabat Al Ershaad - Jeddah].

Na watoto wasiojulikana nasaba zao ndio wanaofaa zaidi kulelewa, kwani wao hawajijui katika nafsi zao ni nani anayewasimamia mambo yao isipokuwa yule anayewalea, basi inapendeza zaidi kuwapa sadaka, na kama wakiwa mafakiri basi wao ni miongoni mwa wanaostahiki kupewa Zaka: wanapewa kiasi kinachowatosheleza katika maisha yao, vyakula vyao, vinywaji vyao, makazi yao, mafunzo yao, ndoa yao na mengineyo.

Na ama kujizuia kuwapa Zaka au sadaka kwa hoja kuwa wao ni watoto wa haramu ni tuhuma za kutunga zisizokuwa na uthibitisho wala dalili, kwani si kila aliyeokotwa au aliyekutwa karibu na msikiti au sehemu nyingine yoyote ni mtoto wa zinaa, na hata kama tutakubali hivyo haipelekei kutompa Zaka, kwani haijuzu kwa mtoto kubeba dhambi ya wazazi wake. Na Uislamu umebatilisha hayo kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wala habebi mbebaji mzigo wa mwengine.}[AL ISRAAI 15].

Na ikiwa zina si katika vizuizi vya kutoa Zaka kisheria kwa yule mwenye kustahiki kama atakuwa mzinzi, kwa hivyo ni bora zaidi kuwa si kizuizi cha kumpa mwanaye.

Na kutokana na hayo: inajuzu kwake kuwapa matumizi watoto wasiojulikana nasaba zao, kutoka katika mali ya Zaka na sadaka, bila kutofautisha.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.

 

Share this:

Related Fatwas