Kutumia dawa ya kuzuia damu ya hedh...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kutumia dawa ya kuzuia damu ya hedhi kwa ajili ya kufunga saumu.

Question

Nini hukumu ya kisheria ya kutumia mwanamke dawa ambazo zinaweza kuzuia damu ya hedhi kwa muda ili aweze kutimiza saumu ya mwezi wa Ramadhani?

Answer

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:

Hedhi: ni damu inayotoka katika sehemu iliyo mbali kutoka tumbo la uzazi katika wakati maalumu [Asniy Al Mataleb, 1/99, Ch. Dar Al Ketab Al Islamiy], na inaendelea kutoka kila mwezi takriban baada ya umri wa kubaleghe mpaka umri wa kukatika kwa hedhi. Kawaida wanawake katika kipindi cha hedhi wanaona alama maalumu zinazohisiwa, huanza kwa kutoka damu katika tumbo la uzazi na hushuka taratibu na kuhisi maumivu na udhaifu wa nguvu na kutojisikia vizuri. Na humalizika kwa kukatika hedhi na hali kutulia. Muda wa hedhi unatofautiana kutoka mwanamke mmoja hadi mwingine, na kila mwanamke ana mfumo wake wa hedhi na idadi ya siku zake za kupata hedhi.

Ibn Majah amepokea kutoka kwa mama wa Waumini Bi Aisha R.A. alisema: "Tulitoka na Mtume S.A.W. kwenda Kuhiji, na tulipokaribia Sarifa, nikapata hedhi, Mtume S.A.W. aliponiona hali ya kuwa nalia alisema: Je umepata hedhi? Nikamjibu: Ndiyo, akasema: “hilo ni jambo ambalo Mwenyezi Mungu ameliandika juu ya mabinti wa Adam, basi timiza ibada zote za hija isipokuwa kutufu Al Kaaba” [Imepokelewa na Ibn Majah na Imamu Ahmad].

Ibn Bital alisema katika kitabu cha: [Sharh Sahihi ya Bukhariy 1/411, Ch. Mak-tabat Ibn Rushd, Al Riyadh]: “Hadithi hiyo inabainisha kwamba hedhi ilifaradhishwa juu ya mabinti wa Adam ikaendelea baada yao juu ya mabinti wote kama alivyosema Mtume S.A.W., na ni maumbile yao asili yanayoleta manufaa kwao. Mwenyezi Mungu amesema kuhusu Zakariya A.S.: {Basi tukampokelea (dua yake) na tukampa Yahya} [AL-ANBIYAA, 90]. Watu wa tafsiri walisema: yaani Mwenyezi Mungu Mtukufu alimrejeshea (mke wa Zakariya) uwezo wa kupata hedhi ili apate mimba na hiyo ndiyo hekima ya Muumbaji ambayo ameifanya sababu ya kupata uzazi; kwani mwanamke akiwa hapati hedhi hapati mimba, nayo ni kawaida isiyobadilika”.

Mtume S.A.W. alibainisha kwamba wanawake wanasifika kuwa wenye upungufu katika dini, na upungufu huo unatokana na hukumu za kisheria zinazoambatana nao, na sifa hiyo ya kimaumbile siyo ya kuchukiza lakini inakuwa kwa njia ya tanbihi kwao na kuwahimiza wajitahidi na wazidi kufanya mambo mema na kuacha kufanya mambo mabaya ili wazibe upungufu huo. Naye Mtume S.A.W. alibainisha upungufu huo kuwa ni: mwanamke analazimika kisheria kuacha ibada ya sala na saumu katika siku zake za hedhi, kinyume na mwanamume ambaye hana upungufu huo wa kimaumbile unaomzuia kutimiza ibada ya sala na saumu. Ilitajwa katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Said Al Khudariy R.A. alisema: “Mtume S.A.W. alipotoka katika Eid el Adh-haa au Eid el Fitri kwenda pahala pa kusali akapita kwa wanawake, akasema: Enyi makundi ya wanawake toeni sadaka kwani niliwaona nyinyi mko wengi sana motoni. Walisema: kwanini ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema: mnakithirisha laana na mnakanusha wema aidha sijaona wenye upungufu wa akili unaoondosha akili ya mwanamume kama nyinyi. Wakamwuliza Mtume S.A.W.: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu kwanini tuna upungufu wa dini na akili? Akawajibu Mtume S.A.W.: je, shahada ya mwanamke mmoja ni sawa na nusu ya shahada ya mwanamume? Wakasema: ndiyo. Mtume S.A.W. akasema: basi hiyo ndiyo dalili ya upungufu wa akili yake. Je, mwanamke akipata hedhi hasali wala hafungi saumu? Wakamjibu: ndiyo. Mtume S.A.W. akasema: basi hiyo ndiyo dalili ya upungufu wa dini yake” [Imepokelewa na Bukhari na Muslim].

Faradhi ya saumu ni ibada ya mwezi mmoja iliyofaridhishwa kwa mwaka mara moja, kwa hiyo mwenye hedhi analazimishwa kulipa funga ya siku ambazo hakuweza kufunga kutokana na hedhi, ama sala ilifaradhishwa mara tano kila siku, kwa hiyo mwenye hedhi anasamehewa kwa kutolazimishwa kulipa sala za siku zake za hedhi.

Na hukumu ya mwanamke kutumia dawa ambazo zinaweza kuzuia damu ya hedhi kwa muda ili aweze kutimiza ibada hiyo ya msimu, basi inajuzu kisheria. Na wanachuoni walijuzisha jambo hilo; kati ya hao ni maimamu wa Hanbali” Mtunzi wa [Al-Mughniy 1/221, Ch. Dar Ihiyaa’ Al Turath Al Arabiy] alisema: “ilipokelewa kutoka kwa Ahmad Mwenyezi Mungu amrehemu ya kwamba: inajuzu kwa mwanamke kutumia dawa ya kuzuia damu ya hedhi ikiwa dawa hiyo inafahamika uhalali wake.

Na mwanachuoni Al Bahutiy alisema katika kitabu cha: [Al Rawdh Al Muraba’, uk. 604, Ch. Mua’sasat Al Risala]: “ni mubaha kwa mwanamke kutoa mbegu ya uhai iliyochanganyika kwa kutumia dawa iliyo halali sharti isifike siku arobaini, aidha kutumia dawa apate hedhi kabla ya kuja mwezi wa Ramadhani au kuchelewesha hedhi mpaka baada yake”.

Lakini kutumia dawa ya kuzuia damu ya hedhi siyo ruhusa ya moja kwa moja, bali inashurutishwa kuepukana na madhara yanayodhuru. Ibn Mufleh alisema katika kitabu cha: [Al Mub-di” 1/258, Ch. Dar Al Kotub Al Elmiya]: “si kosa kutumia dawa iliyo halali kuzuia damu ya hedhi, sharti isiwe na madhara”.

Kwa Imamu Malik ni Makruhu kufanya hivyo (kutumia dawa ya kuchelewesha hedhi); ambapo aliulizwa: nini hukumu ya mwanamke anayeogopa kupata hedhi, akashauriwa kutumia dawa ya kuchelewesha hedhi, akajibu: jambo hilo si sahihi tena alilichukia (Makruhu). Ibn Rushd alisema: Imamu Malik alihukumu kuwa ni makruhu kwa kuogopa mwanamke kupata madhara ya kimwili [Al-Hateb, Mawarid Al-Jalil, 1/366, Ch. Dar Al Fikr].

Ibn Rushd Al Malikiy alisema katika [Al Bayan wa Al Tahseel 18/616, Ch. Al Gharb Al Islamiy]: “Ibn Kenana alisema: Yaliyonifikia ni kwamba ni Makruhu kwa mwanamke kuharakisha kujitoharisha kutokana na hedhi kwa kunywa dawa za miti shamba kama tiba au kwa njia yoyote nyingine. Na Ibn Rushd alizidisha kusema: sababu ya kuchukiza ni uondoshaji wa madhara ili mwanamke asipate madhara ya kimwili kwa kutumia dawa inayoweza kusababisha madhara ya kiafya”.

Na mwanamke akitumia kinachozuia (kwa muda) damu ya hedhi, basi anakuwa katika hali ya kutahirika, madamu hajapata damu ya hedhi, tena halazimiki kisheria na hukumu za hedhi katika muda huo; kwani hukumu za hedhi zinaambatana na kutoka damu ya hedhi kutoka pahala pale (haziambatani na mzunguko wa hedhi au kipindi chake).

Sheikh Taqiy Al Dini bin Taimiya Al Hanbali alisema katika kitabu cha: [Al Fatawa Al Kubra 3/349, Ch. Dar Al Kutob Al Elmiya]: “mwanamke akitumia dawa ya kuzuia damu ya hedhi (kwa muda) au kuchelewesha, lazima awe katika hali ya kutahirika”.

Kutokana na yaliyopita: mwanamke kutumia dawa ya kuzuia (kwa muda) damu ya hedhi ili awahi faradhi ya msimu (saumu ya mwezi wa Ramadhani) ni jambo linalojuzu kisheria sharti ajiepushe na madhara, aidha mwanamke katika hali hiyo lazima awe katika hali ya kutahirika.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.
 

Share this:

Related Fatwas