Mwislamu kumpa mkono wa pole (kuhani) kafiri.
Question
Jirani yangu si Mwislamu, baba yake alikuwa anajulikana kwa ulokole wa dini yake, kuisambaza na kuutilia shaka Uislamu kwa kupitia taasisi za kijamii ambazo alikuwa anazisimamia, na amefariki mtu huyu hivi karibuni, je naruhusika kumpa pole jirani yangu?, na nimwambie nini wakati wa kumpa pole?
Answer
Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:
Uislamu umeeleza hukumu nyingi zinazojuulisha ujumbe wake wa kuishi pamoja na kukomesha utengano, Ofisi ya fatwa ya Misri imetoa Fatwa Namba 189 Mwaka 2011 Tarehe: 18/05/2011 ambapo imeelezea mfumo wa Kiislamu katika kuishi pamoja, na sura za sheria zinazoimarisha msingi wa kuishi pamoja na mwengine (asiye mwislamu), dini ya Kiislamu si dini ya upweke na kukawia kimaendeleo, bali ni mfumo wa kiungu uliokamilika kwa ajili ya ubinadamu kwa ujumla licha ya tofauti ya maeneo, rangi na aina.
Miongoni mwa sura za kisheria ambazo zinathibitisha kanuni ya kuishi pamoja na wengine katika Uislamu ni rambirambi kwa wasio waislamu, kufariji familia zao na kuwahimiza wawe na subira, na wanavyuoni wana maelezo mengi kuhusu hukumu ya rambirambi kwa upande wa anayetoa rambirambi na anayetolewa rambirambi, kuhusu kutoa asiye Mwislamu rambirambi kwa asiye Mwislamu wanavyuoni wanasena inajuzu, hii ni rai ya Imamu Abu Hanifa, Shafiy, Malik, nayo ni moja ya kauli ya madhehebu ya Imamu Ahmad Ibn Hanbal. Kwa mujibu wa rai hii, rambirambi kwa wasio Waislamu inaingia katika mlango wa wema kama ilivyokuja katika aya: {Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu.} [AL MUMTAHINA 8]. Aidha mkono wa pole inajuzu kwa kufananisha na kuwatembelea wagonjwa. (Mtume S.A.W alikuwa akitembelea wagonjwa wasio Waislamu.
Katika hadithi ya Anas R.A, alisema: Mvulana myahudi mtumishi wa Mtume aliumwa, Mtume S.A.W akamtembelea, akaketi karibu na kichwa chake na kumwambia: silimu, mvulana huyo akamtazama baba yake, basi baba yake akamwambia mtii Abal-Qaasim (yaani Mtume S.A.W) basi akasilimu). [Imepokelewa na Bukhari]. Kutoa rambirambi na kumtembelea mgonjwa ni kufariji na kupunguza makali katika msiba. Lakini pamoja na kuruhusiwa, wanavyuoni wameweka sharti kwa anayetoa rambirambi achague maneno ya rambirambi kwa familia ya marehemu yanayolingana hali yao, kama kuwahimiza uvumilivu na kuwakumbusha kuwa hiyo ni ada ya Mwenyezi Mungu katika uumbaji wake, kwa mfano aseme: Mwenyezi Mungu awalipeni kheri, n.k. Wanavyuoni wa madhehebu ya Shaafii wameshurutisha kafiri mwenye heshima, ama kafiri mpiganaji na aliyeritadi, basi hakuna kuwapa pole katika misiba yao, isipokuwa wakitarajiwa kusilimu, na anaingia katika hukumu hii kila anayejulikana kwa uadui wake dhidi ya Uislamu na kuutilia shaka Uislamu kwa kusambaza shaka na kulingania dini nyingine isiyokuwa Uislamu, basi mtu kama huyu hapewi mkono wa pole ila kama anatarajiwa kusilimu.
Wanavyuoni wa madhehebu wa Hanbali hawakukubaliana na wanavyuoni wa madhehebu ya Shafiy, wanasema ni haramu kabisa kumpa mkono wa pole kafiri, kauli hii pia ni mtazamo wa Al-Mardaawi, baadhi ya wanavyuoni wa madhehebu ya Hanafiy, na baadhi ya wanavyuoni wa madhehebu ya Maalik. Hoja yao ni kauli ya Allah sw: {Huwakuti watu wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kuwa wanawapenda wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa ni baba zao,...} [AL MUJAADALAH 22], kutoa rambirambi kwa kafiri ni aina ya upendo, basi ni haramu. Na kutoa rambirambi kunafananishwa na kutoa salamu, sasa kwa kuwa tumekatazwa kuanza kuwasalimia basi pia tumekatazwa kuwapa mkono wa pole.
Zifuatazo ni matini za wanavyuoni zinazoonesha tuliyoyaeleza kwa ujumla:
Ibn al-Nujaim katika kitabu cha: [Al-Bahri Al-Raaiq 8/232, Dar Al-Kitab Al-Islamiy.]: “(na kumtembelea) inakusudiwa inaruhusiwa kumtembelea mtu wa dhimmi mgonjwa. Imepokelewa kwamba Myahudi aliumwa karibu na Mtume S.A.W. akasema: "Simameni tukamtembelee jirani yetu Myahudi" wakasimama, Mtume akaingia na akaketi karibu na kichwa chake, na akamwambia: (Sema: Nashuhudia kwamba hakuna Mungu ila Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu), mgonjwa akamtazama baba yake, akasema: mjibu, akatamka neno la kuingia Uislamu, Mtume S.A.W akasema: "shukrani kwa Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kumwokoa mtu kutokana na moto". Na kwa kuwa kumtembelea mgonjwa ni aina ni wema, nayo ni moja ya fadhila za Uislamu, basi hakuna ubaya ... na kafiri akifariki basi baba yake au jamaa yake huambiwa katika kumpa pole: Mwenyezi Mungu akulipe bora kuliko hayo, akuongoze na akuruzuku mtoto Mwislamu”.
Ibn Abidin Al-Hanafi alisema: "Katika vitabu vya madhehebu ya Shaafii: Mwislamu anampa mkono wa pole kafiri kwa kusema: Mwenyezi Mungu akuze ujira wako na subira yako, na kafiri anampa pole Mwislamu kwa kusema: Mwenyezi Mungu amsamehe maiti wako na akufariji vizuri”. ]Rad Al-Muhtar 2/242, Dar Al-fikr].
Alisema katika kitabu cha" [Al-Taji wa Al-Iklil Al-Muwaq 3/38, Ch. Al-Kutub Al-Elmiya.]: “Imepokelewa kutoka kwa Malik kwamba inaruhusiwa kwa mtu kumpa pole jirani yake kafiri kwa kufa kwa baba yake kafiri kutokana na ujirani wake”.
Al-Khatib Al-Sherbini alisema katika kitabu cha: [Mughni Al-Muhtaaj 2/42, Dar Al-Kutub Al-Elmiya.]: “(na) Mwislamu anampa mkono wa pole (kafiri) ambaye ni dhimmi kwa kumwambia: Mwenyezi Mungu akupe malipo makubwa na uvumilivu, (na kafiri) anampa mkono wa pole mwislamu kwa kusema: Mwenyezi Mungu amsamehe maiti wako na akufariji vyema). Na mtungaji hakutaja rambirambi ya kafiri, kwa sababu haipendezi, bali inajuzu ikiwa hatarajiwi kusilimu kama tulivyoashiria”.
Al-Mardaawi alisema katika kitabu cha [Al-Insaaf 4/234, Ch. Dar Ihyaa Al-Turath Al-Arabi]: “Kauli yake: (Kuna riwaya mbili kuhusu kuwapongeza, mkono wa pole na kuwazuru). Riwaya ya kwanza: ni haramu kufanya hivyo. Riwaya ya pili: si haramu lakini ni Makruhu. Na kauli ya wanavyuoni: kafiri anatembelewa na anaelezewa Uislamu. Nilisema: hii ni sahihi. Na Mtume S.A.W. alimzuru mvulana Myahudi aliyekuwa akimtumikia, na alimwelezea Uislamu basi akasilimu. Na tulisema: anaweza kumtolea salamu za rambirambi, yametangulia anayosema katika kutoa salamu za rambirambi mwishoni mwa kitabu cha jeneza, na anamwombea kuishi umri mrefu, mali nyingi na watoto wingi”.
Na tunaona kwamba maoni ya Jamhuri ya wanavyuoni ni sahihi zaidi kwa nguvu ya ushahidi wao, lakini ule ushahidi wa kuharamisha kutoa rambirambi kwa sababu ati ni kama mapenzi, basi mtazamo huo si sahihi, bali ni miongoni mwa kuwafanyia wema kama alivyoamuru Mwenyezi Mungu katika kauli yake: {Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu} [AL MUMTAHINA 8]. Al-Qarafiy ameeleza katika tofauti ya mia moja na ishirini na tisa tofauti kati ya msingi wa kufanya wema na mapenzi, na alisema maneno yenye thamani kuhusu tofauti kati yao, na miongoni mwa aliyoyasema: “Ama aliyoyaamuru kuhusu kuwafanyia wema na pasipo na upendo wa moyo, yaani ni kuwarehemu wanyonge, kukidhi mahitaji ya maskini miongoni mwao, kumlisha mwenye njaa, kumvalisha ambaye yuko uchi, kuwapa maneno laini kwa huruma na upole si kwa hofu na udhalilishaji, kuvumilia maudhi ya ujirani wao pamoja na kuondoa kwa upole, si kwa hofu wala kujikweza, na kuwaombea waongoke, na wawe miongoni mwa watu wa furaha, kuwanasihi katika mambo yao yote ya kidini na kidunia, kutunza mali zao, watoto wao, haki na maslahi yao yote, kuwasaidia kwa kuwakinga na dhuluma na kufikisha haki zao zote na kila kitu kizuri. Yote haya ni miongoni mwa tabia nzuri. Yote tunayofanya nao yanapaswa kuwa kama hivi, na si kwa kiburi wala kujikweza, na isiwe kwa njia ya kuwatukuza ilhali tunadharau nafsi zetu kwa kuwafanyia hivyo.”.[Al-Furuq 3/15, Ch. Alam Al-Kutub].
Ama kufananisha kutoa salamu za rambirambi kwa kuanza kuwasalimia ni kipimo tofauti; kwa sababu kuanza kusalimia kuna ukarimu kutoka kila upande, na inawezekana kuiondoa katika msingi wa upendo unaokatazwa, lakini kutoa salamu za rambirambi na kuzuru upo uwezekano, pia inaingia katika msinigi wa kufanya wema uliotangulia hapo juu.
Kwa mujibu wa yaliyotajwa hapo juu: inaruhusiwa kutoa salamu za rambirambi kwa jirani yako asiye Mwislamu katika kifo cha baba yake, na unapaswa kuchagua maneno ambayo unaweza kumwambia, kama “Mwenyezi Mungu akupe heri zaidi kuliko alichokichukua kutoka kwako”, au kumkumbusha awe na subira na uvumilivu, na unapaswa uwe na nia ya kufanya wema, ujirani mwema na kumlingania dini ya Kiislamu.
Na Mwenyezi Mungu anajua zaidi ya wote.