Uislamu ni mfumo wa maisha
Question
Tunasikia sana wanavyuoni na wasomi wanapozungumzia Uislamu wanausifu kuwa ni mfumo wa maisha. Nini maana yake?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
• Uislamu ni ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa wanadamu wote, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Yeye ndiye aliyeleta Mtume katika watu wasiojua kusoma, anayetokana na wao, awasomee Aya zake na kuwatakasa na kuwafunza Kitabu na Hekima, (elimu nyinginezo). Na kabla ya haya walikuwa katika upotofu uliodhahiri}. [AL-JUMUA, 2]. {Amekwisha kufikieni Mtume wetu, anayekudhihirishieni mengi mliyokuwa mkiyaficha katika Kitabu, na husamehe mengi. Bila shaka imekwishakufikieni nuru kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Kitabu kinachobainisha (kila jambo)} [AL MAIDAH, 15]. Uislamu ni ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa wote waarabu na wasio waarabu, sawa waliokuwepo wakati wa utume wa Mtume Muhammad S.A.W au waliokuja baada yake hadi siku ya Malipo, Allah S.W. Amesema: {Na kwa wengine ambao bado hawajaungana nao. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.} [AL-JUMUA, 3].
• Uislamu -kama alivyobainisha marehemu Prof. Muhammad Al Bahiy mhadhiri wa falsafa ya kiislamu na mkuu mstaafu wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar- ni ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa kumwongoza binadamu ambaye ni kiumbe kinachokuwa na tabia ya kipekee ambayo Mwenyezi Mungu Ameiumba hasa kwake, Mwenyezi Mungu Amesema: {Na hakika tumewatukuza wanadamu na tumewapa vya kupanda barani na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewatukuza kuliko wengi katika wale tuliowaumba, kwa utukufu ulio mkubwa kabisa}. [BANI ISRAIL, 70].
• Uislamu katika kumwongoza binadamu unaangalia sifa zake za kimaumbile na kukiri kuwa ni maumbile yake, na unajaribu kumwongoza kwa mujibu wa tabia yake ya kibinadamu bila ya kujaribu kumhamisha kutoka tabia ya binadamu kwenda tabia ya Malaika. Aidha unajaribu kumwongoza asibadilike kitabia kutoka hali ya binadamu kuwa mnyama, kwani binadamu katika Uislamu ni mtu, na kwa Uislamu mtu anafikia daraja ya juu ya ubinadamu.
• Kwa hiyo, Uislamu ulikuwa mfumo wa maisha kwa yule asiyeweza kufika nafasi ya Uungu hata akiwa Mtume aliyeteuliwa na Mola wake, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Wambie: “Bila shaka mimi ni binadamu kama nyinyi (isipokuwa nimeletewa Wahyi tu, ndio tafauti yangu). Ninaletewa Wahyi ya kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Anayetarajia kukutana na Mola wake naafanye vitendo vizuri wala asimshirikishe yoyote katika ibada ya Mola wake} [AL-KAHF, 110]. Aidha ni mfumo wa maisha ya mtu asiyeweza kuachana na tabia yake ya kibinadamu ambayo inamtofautisha na viumbe vyengine.
• Kutokana na hayo, Uislamu unamwongoza binadamu katika nyanja zote za maisha ya kibinadamu; Uislamu unamwongoza kuosha sehemu za mwili wake mara kadhaa kila siku na kuosha mwili wake mzima katika wakati maulumu. Aidha binadamu kwa mujibu wa mfumo wa Uislamu anatakiwa awe msafi katika mavazi, mwili na mdomo wake katika mkutano wowote kama vile kukutana na watu katika Sala ya Ijumaa.
• Uislamu unashughulikia kumwongoza binadamu katika vyakula na vinywaji vyake, ukamharamishia baadhi ya aina za vyakula na baadhi ya vinywaji. Mwenyezi Mungu Amesema: “Mmeharimishiwa nyamafu na damu na nyama ya nguruwe, na kinyama kilichochinjwa si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na kilichokufa kwa kusongeka koo, na kilichokufa kwa kupigwa, na kilichokufa kwa kuanguka, na kilichokufa kwa kupigwa pembe (na mwengine), na alichokila mnyama (kikafa), ila mkiwahi kukichinja (kabla hakijafa). Na (pia mmeharamishiwa) kilichochinjwa panapofanyiwa ibada isiyokuwa ya Mungu - kama mizimuni}. [AL MAIDAH, 3]. {Bila shaka ulevi na kamari na kuabudiwa (na kuombwa) asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na kutazamia kwa mishare ya kupigia ramli (na kwa vinginevyo); (yote haya) ni uchafu (ni) katika kazi ya Shetani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufaulu} [AL MAIDAH, 90]. Adabu za chakula zilizotajwa katika Quraani Tukufu na Sunna kutoka kwa Mtume S.A.W. zinampa nasaha binadamu asije kunywa au kula ila akiwa na haja ya kunywa au kula kwa kiasi anachokihitajia, Allah S.W. Amesema: {Na kuleni na kunyweni (vizuri) wala msifanye israfu, Hakika Yeye, Hawapendi wafanyao israfu} [AL AARAF, 31].
• Kuhusu mavasi ya binadamu: ni haramu kwa mwanamume kuvaa mapambo ya dhahabu na hariri, pia mwanamke katika Uislamu ni haramu kuonyesha mapambo yanayoweza kuchochea fitna. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na wambie Waislamu wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasidhihirishe viungo vyao isipokuwa vinavyodhihirika (uso na vinganja vya mkono –na wengine wanasema na nyayo). Na waangushe shungi zao mpaka vifuani mwao, na wasionyeshe mapambo yao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenziwao, au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, (watumwa wao), au wafuasi wanaume wasio na matamanio (kwa wanawake) au watoto ambao hawajajua mambo yanayohusu uke. Wala wasipige miguu yao ili yajulikane wanayoyaficha katika mapambo yao. Na tubieni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waislamu ili mpate kufaulu}. [AN-NUR, 31].
• Kuhusu kujiliwaza na mchezo: Ni haramu kutenda kinachofitinisha akili yake au kuiharibu kama kucheza kamari kwa aina zake mbalimbali. {Enyi mlioamini! Bila shaka ulevi na kamari na kuabudiwa (na kuombwa) asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na kutazamia kwa mishare ya kupigia ramli (na kwa vinginevyo); (yote haya) ni uchafu (ni) katika kazi ya Shetani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufaulu}. [AL MAIDAH, 90].
• Kuhusu kutendeana baina ya watu: Uislamu unapanga ushirikiano kwa hali ya juu. Uislamu unamnasihi baba au mama kutofitinishwa kwa sababu ya mtoto. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na jueni ya kwamba mali zenu na watoto wenu ni mtihani (huo Aliokupeni Mwenyezi Mungu kutazama mtaendesha vipi) na jueni ya kwamba kwa Mwenyezi Mungu yako malipo makubwa kabisa} [AL ANFAL, 28]. Na Uislamu unamnasihi mtoto kuchunga uhusiano wake na baba yake na mama yake, kujali sana hisia zao na kuepukana na kila kinachowaudhi. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Basi usiwaambie hata Ah! Wala usiwakemee. Na useme nao kwa msemo wa heshima}. [BANI ISRAIL, 23]. Na Uislamu umemwamuru mume kuishi na mkewe kwa wema au kuachana kwa vizuri kama Alivyoeleza Mwenyezi Mungu: {Kisha ni kukaa kwa wema au kuachana kwa ihsani}. [AL BAQARAH, 229]. Na Uislamu unamnasihi mtu kushirikiana na kuwasaidia jamaa zake. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na anawapa mali kwa kupenda kwake, jamaa}. [AL BAQARAH, 177], pia Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema: {Na wenye nasaba wana haki zaidi wao kwa wao katika kitabu cha Allah}. [AL-AHZAB, 6]. Na Uislamu umemwamrisha mtu kuwafanyia wema watu wote kiujumla, na ukaambatanisha hilo na kumwabudu na kumpwekesha Allah S.W. {Mwabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni ihsani wazazi wawili, na jamaa na mayatima na masikini na jirani walio karibu na jirani walio mbali, na rafiki walio ubavuni na msafiri aliyeharibikiwa, na wale iliyowamiliki mikono yenu ya kulia. Bila shaka Mwenyezi Mungu Hawapendi wenye kiburi wajivunao}. {{AN NISAA, 36}. Naye Mtume S.A.W. alisema: “Jibrili hakuacha kuniusia kumtendea wema jirani mpaka nikadhani atamfanya awe mrithi”. [Kutoka kwa Ibn Omar, hadithi ya 5669 kwa Bukhari, na 2625 kwa Muslim].
• Binadamu ni mhusika akibeba dhamana na uongozi. Mtume saw anasema “Nyote ni wachungaji, na kila mmoja ataulizwa juu ya alichokichunga, kiongozi ni mchungaji, na ataulizwa kuhusu raia wake. Na mwanamke katika nyamba ya mumewe ni mchungaji, na ataulizwa juu ya alichokichunga. Na mtumishi katika mali ya bwana wake ni mchungaji, na ataulizwa juu ya alichokichunga. Aidha Uislamu unamwamrisha kila mwenye kutoa ahadi aitimize. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na timizeni ahadi mnazozitoa kwa jina la Mwenyezi Mungu mnapoahidi wala msivunje hizo ahadi baada ya kuzithibitisha, hali mumekwisha mfanya Mwenyezi Mungu kuwa shahidi wenu. Hakika Mwenyezi Mungu Anayajua mnayoyafanya}.[AN NAHL, 91]. Kuhusu wafanyabiashara, Uislamu unawaongoza wawe na mizani iliyo sawa na uadilifu katika biashara yao. {Basi kamilisheni sawa sawa vipimo (vya vibaba) na mizani (pia) wala msiwapunguzie watu vitu vyao}. [AL AARAF, 85]. Kuhusu mashahidi na majaji, Uislamu umewalazimisha waseme ukweli kwa haki. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na msemapo semeni kwa uadilifu ingawa ni jamaa. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu itekelezeni. Hayo amekuusieni ili mpate kukumbuka}.[AL-AN-AM, 152]. Pia Mwenyezi Mungu Mtukufu Alisema: {Enyi mlioamini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu, mtowao ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu; ijapokuwa ni juu ya nafsi zenu au wazazi wawili na jamaa zenu. Akiwa tajiri au masikini Mwenyezi Mungu Anawastahikia zaidi (kuliko wewe). Basi msifuate matamanio mkaacha kufanya uadilifu. Na kama mkipotoa ushahidi au mkajitenga nao basi Mwenyezi Mungu anajua vyema mnayoyatenda}[AN NISAA, 135].
• Kuhusu binadamu kumwabudu Mola wake: Mwenyezi Mungu anamwelekeza binadamu aamini kuwa Mungu Anayeabudiwa ni mmoja tu ambaye hana mshirika. “Sema: {Namuabudu Mwenyezi Mungu kwa kuitakidi kuwa yeye tu ndiye Mwenyezi Mungu} [AZ-ZUMAR, 14].
• Uislamu umemweka binadamu katika cheo cha juu zaidi nacho ni sura ya binadamu asiyetawaliwa na matamanio, kama matamanio ya mali au utupu. Mwenyezi Mungu Amesema: {Na ambao wanaiogopa adhabu itakayo kwa Mola wao. Hakika adhabu ya Mola wao si ya kusalimika nayo. Na ambao wanahifadhi tupu zao. Isipokuwa kwa wake zao au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, basi hao hawalaumiwi. Lakini wanaotaka kinyume cha haya, basi hao ndio wanaoruka mipaka. Na ambao wanaangalia amana zao na ahadi zao. Na ambao ni imara katika ushahidi wao. Na ambao wanazihifadhi Sala zao. Hao ndio watakaokuwa katika Mabustani wakiheshimiwa} [AL-MA’ARIJ, 27- 35].
• Mbali ya hayo, kuna mifano mingi inayodhihirisha utunzaji wa Uislamu kwa mambo yote ya binadamu yakiwa katika maisha yake binafsi au ya kiujumla pahala popote anapokwenda.
• Na tujiulize: Ni ulazima gani umeupelekea Uislamu kuingilia katika upangaji wa maisha kwa namna hiyo? na tuna wajibu gani kama Uislamu utampuuza binadamu na kumwacha aishi maisha yake binafsi kama atakavyo bila ya maelekezo?
• Hayo yote yanahusiana na maumbile ya binadamu mwenyewe na tabia yake ya kuwa ni kiumbe cha kijamii ambaye kwa mujibu wa tabia yake anakuwa na matamanio na ubinafsi. Licha ya hayo, binadamu ana haja ya kukutana na wenzake, kwa hiyo akiachwa tu kwa hisia zake za ndani za kimaumbile bila ya kuongozwa, binadamu atakosa haiba ya kibinadamu, ujasiri, kuchagua na kupambanua, badala yake ataelekea katika ugomvi, msuguano na uadui unaoendelea.
• Kwa kuwa binadamu ameumbwa na tabia na maumbile maalum ili awe na haiba kwa upande, na mwelekeo wa kijamii kwa upande mwengine, basi ujumbe wa Uislamu unasaidia tabia hiyo na unakuza mwelekeo wa kujamii; maana ujumbe wa Uislamu ulikuja kupanga njia inayomfikisha mtu kuwa na nguvu, uwezo wa kupambana na kushinda na ushirikiano wa kijamii. Ujumbe wa Uislamu unaamsha mwamko wa dhati ya kibinadamu na ufahamu wa jamii. Madhara ya kibinadamu ni katika ukosefu wa matakwa ya watu na ukosefu wa ushirikiano wa jamii kati yao.
• Lakini, vipi Uislamu unampelekea Mwislamu kuwa ni mtu mwenye matakwa na ushirikiano imara katika jamii?
• Tukiangalia aina za ibada katika Uislamu; Sala, Saumu, Zaka na Hija, tutakuta kwamba zote zinamtia nguvu mtu na kuendeleza ushirikiano wake katika jamii. Sala na Saumu ni ibada mbili zinasaidia kukuza haiba ya mtu na nguvu, kwani Sala ni kunong’ona na Mwenyezi Mungu pekee mara tano kwa siku, jambo ambalo linaepusha moyo na mapambo ya dunia na starehe zake kwani mkutano wa mwenye kusali na Mola haufanani na manufaa ya maisha ya dunia kwa hali yoyote. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na usimamishe Sala. Bila shaka Sala (ikisaliwa vilivyo) humzuiliya (huyo mwenye kusali na) mambo machafu na maovu, na kwa yakini kumbuko la Mwenyezi Mungu (lililomo ndani ya Sala) ni jambo kubwa kabisa (la kumzuilia mtu na mabaya). Na Mwenyezi Mungu Anajua mnayoyatenda} [AL-ANKABUUT, 45]. Mwislamu akiwa hajali starehe za maisha ya dunia na matamanio yake, na akaelekea katika kikao cha Mwenyezi Mungu na kumnomg’oneza katika Sala, bila shaka matakwa na matamanio yake yatazuilika, na hapo mtu ataweza kidogo kidogo kuyatawala matamanio yake na kuweza kuchagua chakula halali akisikia njaa na kuchagua starehe halali wakati wa matamanio, na hapo mtu anakuwa na uwezo wa kuchagua yaliyo na manufaa na kuacha yaliyo na madhara, na hayo ni matokeo ya Sala ambayo inamzuilia mtu na machafu na maovu.
• Saumu ni kunyima tumbo na tupu kwa muda maalumu, hiyo ni ibada yenye kukuza matakwa ya binadamu na uwezo wake. Binadamu akifunga saumu mwezi wa Ramadhani kila mwaka na kufunga sunna akiweza, basi atakuwa ni miongoni mwa washindi, ataweza kuyatawala matamanio ya tumbo na utupu, na kuishinda hali ya kusitasita, udhaifu na kufuata bendera. Hapo tutafahamu maana ya Hadithi Qudusiy aliyoipokea Mtume S.A.W. kutoka kwa Mola Mtukufu: “Amali zote za binadamu ni zake, isipokuwa Saumu. Saumu ni yangu, Nami ndiye nitakayeilipa. Harufu ya kinywa ya anayefunga ni bora zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko harufi ya miski”. [Kutoka kwa Abu Huraira r.a, Hadithi ya 1805 kwa Imamu Bukhari, na ya 1151 kwa Muslim].
• Baada ya hayo, tukiangalia ibada za zaka na hija, tutazikuta kama tulivyobainisha hapo juu, ni utekelezaji wa kivitendo wa roho ya pamoja inayozinduliwa na sala inayosaliwa kwa jamaa katika nyakati zake tano kila siku, sala ya jamaa, sala ya Ijumaa kila wiki na sala ya Idi mbili kila mwaka. Aina zote za ibada zinazidisha uwezo wa kiroho; kwa sababu aina za ibada zilizofaradhishwa juu ya Waislamu na Uislamu katika nyakati zake na pahala pake kama sala, saumu, zaka au hija ni mazoezi kwa nafsi ya kibinadamu ili ipate uwezo unaotakikana na njia ya uchaguzi kwa upande, na kupata sifa ya kijamii na roho ya ushirikiano wa kijamii kwa upande mwengine. Kwa hivyo, roho inaweza kuzuia kufuata njia ya matamanio ya nafsi.
• Ibada hizo kwa namna zilizofaradhishwa na Uislamu zinamwendeleza mtu ili awe na ubinadamu. Kwa hiyo, zilifaradhishwa ili ziwe ni kinga kwa mtu kutokana na shari ya nafsi yake, uadui wa wengine na uadui wake kwa wengine, nazo ni kwa ajili ya kumtakasa mtu pamoja na kujenga jamii na kuidumisha.
• Kama tulivyoona hapo juu, maelekezo ya Uislamu yanahimiza kujenga jamii ya kibinadamu, na kukataza kila aina ya uadui unaovunja mahusiano ya umma, na Uislamu unataka utulivu katika maisha. Kwa hiyo nadharia ya Uislamu inawaangalia wote kwa mtazamo mmoja. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Enyi watu! Kwa hakika Tumekuumbeni (nyote) kwa (yule) mwanamume (mmoja; Adamu) na (yule yule) mwanamke (mmoja; Hawwa). Na Tumekufanyeni mataifa na makabila ili mjuane (tu basi; siyo mkejeliane). Hakika aheshimiwaye sana miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule amchaye Mungu zaidi kati yenu. Kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye habari za mambo yote}. [AL-HUJURAT, 13].
• Uislamu baada ya kukuza roho ya pamoja baina ya watu kwa njia ya ibada na kujenga jamii yake ya Kiislamu, ukasisitiza kutokaribia uadui. Mwenyezi Mungu amesema: {Saidianeni katika wema na taqwa, wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu}. [AL-MAIDAH, 2]. Kwa hiyo jamii ya Kiislamu ni jamii yenye sifa zifuatazo: usalama, uadilifu, ihsani, jamii yenye kuchukia maovu, uchafu na uadui, nayo ni jamii inayokuwa na sifa ya maadili lakini haiwi kwa hali yoyote jamii ya kudhalilika. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na wanaokushambulieni, nanyi pia washambulieni, kwa kadiri waliyokushambulieni. Na mwogopeni Mwenyezi Mungu (msiongeze kuliko walivyokufanyieni). Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaomwogopa} [AL BAQARAH, 194]. Aidha haiwi jamii ya dhulma. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutowafanyia uadilifu. Fanyeni uadilifu; huko ndiko kunakomkurubisha mtu na uchamungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu Anazo habari za (yote) mnayoyatenda} [AL MAIDAH, 8].
• Kwa hiyo, tunaona Uislamu ni mfumo wa maisha unaoweka wigo kwa mwanadamu ambaye yuko hai na jamii yenye nguvu, kwa mwanadamu mwenye uwezo na jamii yenye uhusiano wa kuhurumiana, kupendana na wa udugu.
• Mwislamu kwa mujibu wa mtazamo wa Uislamu ana ujumbe wake, nao ni ulazima wa kuwa ni mtu mwenye nguvu, uwezo na utambulisho wa wazi. Katika mtazamo huo, jambo la kuishi maisha ya anasa linakuwa mbali sana na ujumbe wa jamii ya Kiislamu ambayo inapigania maadili yaliyo sawa, uadilifu, kuondosha dhulma na uadui pamoja na kupigania uhusiano wa karibu na udugu. Kimsingi uhusiano wa Kiislamu ni uhusiano wa udugu na malengo ya pamoja.
• Ujumbe wa Uislamu si mkakati wa kijamii unaowekwa na mwanadamu, aidha si njia za malezi ambazo mwanadamu aliziweka, ingalikuwa hivyo isingalifaa kwa wote, na isingalifaa isipokuwa kwa kundi tu la watu, kama tunavyoona katika nadharia za kibinadamu na kijamii zilizoambatana na majaribio ya kibinadamu.
• Uislamu ni ufunuo wa Mwenyezi Mungu Ajuaye kila kitu, Mwenyezi Mungu Amesema katika Quraani Tukufu: {Naye ndiye Ajuaye kila kitu}. [AL BAQARAH, 29]. Na Uislamu ni kujua Mwenyezi Mungu, kumwamini na kumcha. Kwa hiyo, Uislamu ni chanzo cha kuelekeza mtu utulivu wa nafsi na jamii.
• Hiyo ndiyo dini ya Uislamu ambayo ni mfumo wa maisha ya kibinadamu yenye sifa njema na utulivu, ni mfumo wa maisha kwa mtu na jamii unaotegemea mtazamo uliyo sawa, unaomwongoza binadamu mwenye tabia yenye matamanio na hisia za ndani za kimaumbile zinazopingana ambapo binadamu analazimika kuzitawala, kama alivyoongozwa na Uislamu kwa mujibu wa uwezo na nguvu zake ili asifuate matamanio yake kama alivyofanya mnyama au kifaa chengine. Kwa hiyo, Uislamu unaelekeza ufahamu wa mtu kwa jamii pamoja na kuirekebisha isiwe jamii yenye kudhoofika na kuporomoka ili iwe jamii yenye nguvu.
• Mwishoni, Uislamu hauna uhusiano na udhaifu wa Mwislamu na ufuataji wa matamanio yake, hali kadhalika hauna uhusiano na udhaifu wa jamii za Kiislamu lakini jukumu linakuwa katika kutofahamu vizuri Uislamu na kuvuka mipaka katika kutekeleza ibada zake. Aidha Quraani haina uhusiano na misingi inayotokana na fikra na nadharia za kimashariki au kimagharibi ambazo haziafikiani na jamii zetu, fikra hizo zimeshindwa kutatua matatizo ya jamii zetu.
Marejeo: Profesa. Muhammad Albahiy, Al-islaamu Kanidhaami Lilhayaa, Cairo, cha. Maktabat Wahba, 1402 Hijiriya, 1982, uk. 3 - 23.