Mwenendo wa Kibinadamu kwa Mtazamo ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Mwenendo wa Kibinadamu kwa Mtazamo wa Maadili ya Kiislamu

Question

Wanazuoni wa maadili ya Kiislamu wanauzungumzia sana Mwenendo wa Kiislamu. Je nini mwenendo wa Kiislamu kwa mtazamo wa maadili wa Kiislamu?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

1) Kwa ujumla, elimu ya maadili huwa inashughulika katika kuusoma mwenendo wa binadamu, machimbuko yake, misukumo yake na lengo lake. Nayo ni kama asemavyo Marehemu Prof. Abdulmaqsuud Abdulghaniy, aliyekuwa Mwalimu na Mkuu wa Kitengo cha Falsafa ya Kiislamu hapo zamani kuwa ni moja kati ya maeneo ya tafiti zenye thamani kubwa na ambayo ililetwa na Elimu ya Kisasa ya Maadili na ambayo sisi twaweza kujinufaisha kwayo.

2) Na mwenendo ni alama ya maadili na ni mwonekano wake wa nje, kwa namna ambayo maadili kama ijulikanavyo huwa ni pambo ndani ya nafsi. Na kinachokusudiwa kutafitiwa ni mwenendo mzinduko utokanao na watu wenye akili timamu na kwa utashi wao. Na kwa utashi wao usio na kizuizi chochote na huwa unaweza kusifiwa vyema au vibaya. Kwa hivyo basi, kila mwenendo usio kuwa na matokeo haya hauingii katika katika maadili.

Kwa hivyo basi, mwenendo ni: Uchangamfu tashi ambao husababisha athari nzuri au mbaya iwe ni kwa msababishaji au kwa mtu mwingine au kwa wote wawili.

3) Na kwa hivyo, inawezekana kuutambulisha mwenendo kuwa ni Uchangamfu wa kiutashi ambao athari nzuri au mbaya hutokana na uchangamfu huo iwe ni kwa mwenye nayo au kwa wengine au kwa pande zote mbili kwa pamoja.

4) Na mwenendo wa kibinadamu wenye utashi wa kiakili ni kitendo anachokifanya mtu na kinakuwa kwake na uhusiano wa kinafsi au kiakili. Na sifa zake muhimu ni kufanya kazi ya kufikia lengo maalumu, na ni tofauti na mwenendo unaojiendesha kinyume na utashi wa mtu kama vile kitendo cha jicho kujifunga na mtu akashindwa kulifungua pale mwanga unapokuwa mwingi. Na mwenendo wa binadamu una misukumo, machimbuko, peo, na malengo yake. Na maadili yanaweza kubadilishwa na kuboreshwa kwa kufanya marekebisho ya misukumo na kuzielekeza peo zake na malengo.

5) Na kuna misingi maalumu ya kinafsi ambayo ni: Misukumo, Mazoea na Utashi.
6) Kwanza kabisa tuanze na Misukumo: ni Visababishaji vya ndani ya nafsi ya mtu ambavyo huwa ni nguvu ya ndani elekevu au ni hali ya ndani inayomsukuma mwanadamu kuwa na mwenendo maalumu, wazi wazi au kwa kificho, kwa ajili ya kuyafikia malengo maalumu.

7) Na kwa kawaida namna binadamu alivyo, hawezi kamwe kuepukana na mjumuiko wa misukumo na mielekeo ya kitabia ambayo huelezea mahitaji ya nafsi yake ya hali na mali, kama vile kuhitajia chakula, na maji. Na misukumo ina umuhimu mkubwa sana katika maisha ya mwanadamu kwa sababu hufasiri mwenendo wa binadamu na utendaji wake kwa upande mmoja, na huyatuma mawazo kufanya kazi kwa upande mwingine, kwa sababu mwanadamu huyo hafanyi kazi bila ya kisababisho cha msukumo au mwelekeo. Na kama Mwenyezi Mungu angeliiumba akili inayoyajua matokeo ya mambo bila ya kuumba chimbuko lake linalokwenda na hali ya akili basi hali ya akili ingepotea. Na kwa upande wa tatu, Utashi hautoi maamuzi magumu bila ya misukumo au mwelekeo. Na mwelekeo unapokunwa na nguvu zaidi ndipo unapowajibisha maamuzi ya Utashi na maendeleo ya nguvu. Na kwa upande wa nne, misukumo ndiyo inayomsukuma mwanadamu na kumpelekea katika mwenendo wake. Kama mwanadamu angeliona chakula na baadae akakifikia chakula hicho basi asingelikuwa na haja ya kukielekea au kuwa na shauku nacho. Hapatatokea utashi wa aina yoyote kwa ajili ya chakula hiki na kujisukumia kwa kuelekea upande wake ingawa mtu huyu amekiona kwa macho yake.

8) Wanachuoni wa maadili wanaona kuwa kuna misukumo ya kimaumbile na mingine ya kujifunza, ingawa kuna ugumu wa kutofautisha kati ya aina hizi mbili za misukumo, kama anavyosema Imamu Ghazaliy, na hiyo inatokana na athari za visababisho vya akili na malezi pamoja na Sheria. Na kwa ajili hii wanavyuoni wa Kiislamu wa Maadili wanapinga uainishaji wa mwenendo wa binadamu kwa kutumia idadi maalumu ya misukumo ya kimaumbile, kwani mtu kujifunza na kufanya marekebisho kutokana na misukumo yake, na uzoefu wake huwa na athari kubwa katika uundaji wa misukumo hiyo, ingawa baadhi yake huwepo kwa misingi ya kimaumbile, kisha huwa na umbo maalumu katika kivuli cha aina mbali mbali za uzoefu huo wa mwanadamu.

9) Tunaweza kusema kuwa kumili katika chakula ndio msingi wa kwanza wa misukumo yote na mielekeo inayoungana na maisha ya mwanadamu, kwani matamanio ya tumbo yanazingatiwa kuwa ndio maangamizi makubwa ya mwanadamu, na kwa sababu yake, Nabii Adam A.S, na Bi Hawa walitoka Peponi katika kisa maarufu tulichosimuliwa na Quraani Tukufu zaidi ya mara moja, na miongoni mwake ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu {Na tulisema: Ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani, na kuleni humo maridhawa popote mpendapo, lakini msiukaribie mti huu tu; mkawa katika wale waliodhulumu. Lakini shetani aliwatelezesha hao wawili na akawatoa katika waliyokuwamo, na tukasema: Shukeni, nanyi ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Katika ardhi yatakuwa makaazi yenu na starehe kwa muda} [AL BAQARAH: 35-36]

10) Na katika mtazamo wa Kiislamu tunaweza kusema kuwa misukumo au mielekeo inagawanyika sehemu mbili: Misukumo ya Dini na Misukumo ya Matamanio.

11) Misukumo ya dini: ni ile ya kibinadamu iliyopevu ambayo hupelekea Utiifu, Kazi na Wema, nayo ni mielekeo tiifu inayofanya kazi kwa ishara ya akili inayotambua kukumu za kisheria ambapo ndani yake kuna msukumo wa kumuogopa Mwenyezi Mungu na kuwa na matumaini ndani yake, na hungana na misukumo au visababisho na michemko ya hisia, na hisia zenyewe mbalimbali kama vile za mapenzi, kumtegemea Mwenyezi Mungu, kushukuru, kuridhika na zingine mfano wa hizo ambazo wanazuoni wa Kiislamu wa Sufi wamezizungumzia sana. Na pia ndani ya misukumo hii kuna visababisho vya misukumo hiyo ya kimaumbile ambayo hutekeleza kazi yake katika maisha ya mtu na humlindia mwanadamu maisha na nguvu za mwili wake miongoni mwa yale yanayoingina katika eneo la kuyalinda mambo makuu matano ya kisheria ambayo ni: dini, nafsi, akili, heshima na mali. hutekeleza kazi pelekea.

12) Ama ile misukumo ya matamanio: ni ile ambayo huwa ya nafsi inayoamrisha maovu, ambapo hujumuisha matamanio na hasira, na huwa na mawasiliano na vivutio vya dunia {Mmeandikiwa kupigana vita, navyo vinachusha kwenu. Lakini huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui} [AALI IMRAAN: 14]

13) Kwa hivyo basi, misukumo ni kitu cha msingi kwa mwanadamu na huwa hakitoweki katika maisha ya mwanadamu hali ya kuwa yuhai. misukumo ya kimaumbile kamwe haiwezekani kuzuiwa kiukamilifu, na wala Uislamu haumwambii mwanadamu aizuie au kuiua kabisa kwani misukumo hii ina kazi muhimu kwa ajili ya kuyalinda maisha ya mwanadamu huyu. Na bila ya kutamani chakula, au tendo la ndoa, mwanadamu huyu hawezi kuyalinda maisha yake na uendelezaji wa kizazi katika dunia hii. Kinachotakiwa ni kuweza kuidhibiti misukumo hiyo na kuifunza ipasavyo kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu. Na ndio maana Uislamu hauna mfumo wa watawa na wala haupambani na misukumo ya kimaumbile ya mwanadamu isipokuwa unaielekeza tu na kufanya kazi ya kuipa mafunzo ya kuinyoosha.

14) Kwa hivyo basi, misukumo ina athari katika kuuelekeza mwenendo wa mwanadamu, na kwa hiyo hapana budi kuidhibiti na kuifundisha ili isije ikatoka nje ya mipaka ya uaminifu. Na wala isiwe mbali na hukumu za sheria, na wala isije ikaushikilia mwenendo wa mwanadamu na kumweka mbali na ufanyaji wa mambo mazuri na kumpelekea katika kujihusisha zaidi na matamanio ya hisia na kumtumbukiza katika uadui, chuki, kinyongo na husuda pamoja na mengine mengi miongoni mwa mambo mabaya.

15) Na urekebishaji wa misukumo na kuiongezea cheo, Mwislamu anapaswa kufanya kazi ya kuifanya akili iyashinde matamanio kwa namna ambayo matamanio hayo yatakuwa chini ya akili yake daima na kufuata atakavyo. Na jambo hili linahitaji juhudi pevu katika nafsi na kuipeleka kwa mujibu wa hali ya sheria na hukumu. Na kwa ajili hii Mtume S.A.W. amesema: "Uingiaji wa Peponi ni kwa kuyachukia maovu, na Uingiaji wa Motoni ni kwa Matamanio" [imetolewa na Imamu Muslimu: kutoka kwa Anasi. 2822]. Na akili kwa jinsi ilivyo, huona mazuri na mabaya ya mwenye nayo, lakini matamanio huishia katika kuyaona ya upande wake tu, huwa hayaoni yajayo katika yachukizayo, wakati ambapo kheri nyingi zipo katika hayo yanayochukiza. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Mmeandikiwa kupigana vita, navyo vinachusha kwenu. Lakini huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.} [AL BAQARAH: 216]

16) Na mwanadamu hatengemai na wala hawi mwanadamu wa kweli isipokuwa kwa akili yake kushinda na kuwa kiongozi ambapo matamanio yanakuwa chini ya udhibiti wake. Na njia yake ya kuelekea huko ni kujilinda kwa kutaka msaada kutoka kwa Mola wake Mtukufu na kumtegemea yeye pamoja na kujikinga kwake na shetani na vitimbi vyake. Na mwono mpevu wa moyoni mwake umfichulie ubilisi wa shetani na umfunulie pia nuru aliyonayo yenye kuangaza na iliyo wazi. Na kwa njia hii uwiano utapatikana.

17) Na ukamilishaji ni mchakato wa kurekebisha misukumo na kuipandisha cheo na hapana budi ufungamanishe mwenendo wa mwanadamu na malengo ya juu ya maisha ya mwanadamu huyu na kumkumbusha daima malengo haya kila anapoponyoka na kutoka nje yake. Na upeo huu ni kumfikia Mwenyezi Mungu Mtukufu na kufanya kazi ya kumridhisha na kumtii daima. Kwa hivyo basi mwanadamu anapaswa kulikumbuka daima lengo hili la juu na atambue kuwa lengo la kuumbwa kwa matamanio ya kula kwa mfano ni mwili kuendelea kuwa salama mpaka uwe na nguvu ya kumuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu.

18) Kila wakati mwanadamu anapaswa kufanya kazi ya kuvitia nguvu visababishaji vya dini na kudhoofisha visababishaji vya matamanio, kwani aina zote mbili za visababishaji husimama mbele ya nyingine. Na visababishaji vya matamanio huwa ni elementi ya uchochezi kwa mwanadamu, wakati ambapo visababishaji vya dini ni vipangiliaji, vielekezaji na vidhibiti vya mwenendo wa mwanadamu. Au ni kama asemavyo Imamu Ghazaliy: Tabia ni kisababishaji na Sheria ni kizuizi.

19) Na kuvitia nguvu visababishaji vya dini huwa kwa kumkumbusha mwanadamu matokeo mazuri ya duniani na akhera kwa kusimama kwake kidete mbele ya udhibiti wa matamanio yake. Na udhoofishaji wa visababishaji vya matamanio huwa ni kwa kudhoofisha uasili wa nguvu yake unaotokana na vitendo vya kimaumbile, mawazo ya moyoni na utashi wa kinafsi. Na kuondosha sababu chochezi kwa hayo, na kuiliwaza nafsi kutokana na visababishaji hivyo kwa aina zote za utiifu na vya halali, na kuyaelekeza mawazo katika kumuwaza Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuziwaza Aya zake pamoja na kudumu katika kumtaja na kumshukuru.

20) Ya Pili ni Mazoea: kama kazi ya misukumo ni kuuelekeza mwenendo wa binadamu, basi kazi ya mazoea ni kuurekebisha mwenendo huo na kujifunza maadili mema. Na tumezungumzia jambo hili kwa kirefu kwenye maudhui isemayo (Maadili kati ya Mazoea na Kuzoea) kwa upande wa Kimaadili.

21) Ya Tatu ni Utashi: Utashi ni msingi wa tatu wa kinafsi wa mwenendo wa mwanadamu na tumeuzungumzia pia kwa kirefu chini ya anuani isemayo (Utashi wa Mwanadamu kwa Mtazamo wa Maadili ya Kiislamu)

22) Kwa kuwa misukumo, mazoea na aina zote za utashi huwa na athari za wazi katika mwenendo wa mtu, sisi tunakuta kuwa pia mchemko wa hisia na hisia pole huwa na athari katika mwenendo huo vile vile. Na mchemko wa hisia ni hali ya ndani ya moyo inayoambatana na mwenendo wa mwanadamu kama vile kuhisi uchungu, chuki, hasira au hata woga. Na kwa maana hii mchemko huu wa hisia unakuwa ni miongoni mwa misukumo ya mwenendo na vichochezi vyake. Mchemko ili ufanye kazi yake unatakiwa kuwa na vichochezi vya nje kama vile kuona kitu kinachotisha ni kufadhaisha, au vichochezi hivyo vinaweza kuwa vya ndani kama vile kutazamia kutokea kwa jambo ambalo linachelewa kutokea kwake.

23) Inajulikana kuwa watu wanatofautiana katika uitikiaji wa wito wa visisimuzi vya mchemko wa hisia. Baadhi yao huathirika kidogo kidogo au taratibu mno. Vile vile uitikiaji wa wito wake hutegemeana na mambo kama vile utamaduni na ujuzi wa mtu. Kwa hivyo, mtu ambaye anmjua zaidi Mwenyezi Mungu Mtukufu humuogopa zaidi kuliko yule asiyemjua. Na mchemko huo unaweza kufikia kiwango cha nguvu zake ambacho kinaathiri mwili wake, kama alivyotuambia Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu sifa ya waumini wachamungu wanapokuwa wanasoma Quraani Tukufu {Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, Kitabu chenye kufanana na kukaririwa; husisimua kwacho ngozi za wenye kumkhofu Mola wao Mlezi. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Huo ndio uwongofu wa Mwenyezi Mungu, na kwa huo humwongoa amtakaye. Na ambaye ameachwa na Mwenyezi Mungu kupotea, basi hapana wa kumwongoa} [AZ ZUMAR: 23]

24) Na mwanadamu anapaswa daima kufanya juhudi ya kudhibiti michemko ya hisia zake ambayo hupelekea kupotoka, kuharibu na kuyavuruga mawazo. Kama vile kwa mfano katika udhibiti wa mchemko wa hasira ya mwanadamu. Na kwa ajili hii, Mtume S.A.W anatuusia kutokuwa na hasira. Kutoka kwa Abu Huraira R.A. anasema "Mtu mmoja alimwambia Mtume S.A.W: Niusie, Mtume akamwambia: Usikasirike. Akakariri kwa kusema Usikasirike" [imetolewa na Imamu Bukhari 5765]
25) Lakini hapana budi kutanabahi kuwa mchemko wa hisia ulio wa kati na kati ni jambo la lazima kwani humsukuma mwanadamu katika kuyalinda maisha yake na kupambana na anayemzuia haki yake au anayeshambulia heshima yake. Kama hasira isingelikuwepo na ambayo Mwenyezi Mungu ametuumbia, basi haki za watu zingepotea kwa mfano. Na vile vile mchemko wa hisia humsukuma mwanadamu auelekee mwenendo mzuri na kufanya mema kwani woga hulingana na kuchapa kwa kiboko unaohimiza kazi au utendaji. Inaeleweka kuwa kwa mfano, kumuogopa Mwenyezi Mungu kuna athari kubwa katika kuunyoosha mwenendo wa mtu na kuwajibika na utiifu wa kila aina pamoja na yaliyo bora na kujiepusha na maasi pamoja na machafu, kwani woga huo huyakandamiza matamanio na huvizuia viungo kufanya maasi na kuvifungamanisha na utiifu wa kila aina kwa mwenyezi mungu. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Kwa hakika hao ambao kwa kumwogopa Mola wao Mlezi wananyenyekea. Na wale ambao Ishara za Mola wao Mlezi wanaziamini. Na wale ambao Mola wao Mlezi hawamshirikishi, Na wale ambao wanatoa walichopewa, na hali nyoyo zao zinagopa kwa kuwa watarejea kwa Mola wao Mlezi, Basi wote hao ndio wanaokimbilia katika mambo ya kheri, na ndio watakao tangulia kuyafikia} [ALMUMINUUN: 57-61]

26) Hisia ni maandalizi ya nafsi kutokana na zingatio la mkusanyiko wa michemko juu ya jambo fulani kutokana na kukariri mawasiliano ya mtu na jambo hilo, kisha mtu huyo akawa tayari kuitikia wito wa michemko hiyo ya jambo hilo. Kwa hivyo basi, hisia ni mwelekeo wa ndani ya nafsi kuelekea jambo fulani linalopatikana kwa uzoefu na kwa kujifunza. Na hisia kama ilivyo, katika hali zote za undani wa moyoni, hutegemea misukumo ya kimaumbile. Na hisia kuu za binadamu ni: upendo, chuki, na kila kinachotokana na hisia nyingine huwa ni kutokiana na hisia hizi mbili kuu.

27) Na miongoni mwa elementi za hisia: ni ujuzi. Kwani haifikiriki kuwa mwanadamu anaweza kukipenda kitu fulani isipokuwa baada ya kukijua, kwani mapenzi hayo hayaji isipokuwa baada ya kukijua kitu na kukifikia, na elementi hii ambayo ni ujuzi katika mtazamo wa Imamu Ghazali ni moja kati ya sababu muhimu ambazo watu wametofautiana katika maandalizi ya kujichumia hisia mbali mbali, kwani kila ujuzi wa mwanadamu unapoongezeka kuhusu jambo fulani ndipo hisia zake zinapoongezeka pia kulielekea jambo hilo.

28) Kwa kuwa hisia ziko nyingi na za aina mbali mbali, hakika za juu kabisa ni kupenda ukweli, kupenda wema na kupenda uzuri. Na hisia kwa ujumla huwa na mchango muhimu katika mwenendo wa mwanadamu na humuelekeza na kumnyoosha. Na athari ya hisia yenye nguvu na kishindo huonekana pale hisia fulani inapoutawala utu wa mtu na ikawa hisia hiyo ndiyo uongozi, na kisha kutawala shime na moyo wake, na vile vile huvitawala vitendo na mwenendo wake. Na hapo ndipo tunapopaswa kutumia njia mbali mbali ili tuweze kuifanya hisia ya kumpenda Mwenyezi Mungu Mtukufu iutawale mwenendo wa mwanadamu, na hisia hiyo iwe na nguvu kwa namna ambayo mja atampenda Mola na Mwenyezi Mungu wake aliyetukuka, kwa moyo wake wote. Kwani kwa kufanya hivyo, huwenda kukamsukuma katika kupendelea zaidi kumtii Mwenyezi Mungu Mtukufu na kujitafutia radhi zake. Kwani mapenzi ya kweli ni kwa yule anayependa na kutii. Na kwa ajili hii, Mwenyezi Mungu anasema: {Sema: ikiwa mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi na Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakusameheni nyinyi madhambi yenu na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe na mwingi wa huruma, sema: mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na iwapo mtakengeuka hakika Mwenyezi Mungu hawapendi Makafiri} [AALI: IMARAAN 31-32].

29) Na kwa kumalizia tu, tumeona kwa yale yaliyotangulia, Misingi ya Kinafsi ya Mwenendo wa Mwanadamu, na athari yake kubwa katika kuunyoosha mwenendo wake na kuurekebisha, na kuweka wazi mtazamo wa fikra ya maadili ya Kiislamu, kutokana na haya, hapana budi kwa mwanadamu kutafuta msukumo wa nguvu unaomsukuma awe na utashi wa wema, na msukumo huo uwe na nguvu za wazi na pia uamuzi.

30) Na mpaka hapa, inatudhihirikia sisi umuhimu wa kumwamini Mwenyezi Mungu kwa imani sahihi yenye nguvu katika nafsi ya mtu, kwani Imani inapotulizana katika moyo wa mja na kuvihodhi viungo vyake, huwa ni kichocheo cha nguvu na chenye kuathiri mwenendo wa Mwislamu, kwa sababu Imani hufanya kazi ya kuunganisha utashi wa mtu na mwenendo wake katika kumtii Mwenyezi Mungu na kumridhia.

31) Na umetudhihirikia sisi umuhimu wa utambuzi na uelewa wa thamani ya maadili mema na mambo bora yenye kusifika vyema, na yaliyomo katika utambuzi huu miongoni mwa athari za wazi katika kumsukuma mwanadamu ili ajichumie mambo hayo na kupata msukumo wa utashi wa kweli katika nafsi ili mtu awe na sifa hizi.

32) Na umetudhihirikia wazi umuhimu wa kuwepo baadhi ya michemko yenye nguvu na hisia kali kuyaelekea mambo mazuri na mema na mifano bora ili mwanadamu aikute nafsi yake inajisukumia katika kuyaelekea hayo na kuambatana nayo.

Chanzo: - Prof/Dkt Abdulmaqsuud Abdulghinaa Khashabah, Nadharia ya Tabia katika Uislamu _ utafiti linganishi, Cairo: Daru Thaqaafa Al-arabiyah, 1412 h./ 1991, (ukurasa wa 39-63).
 

Share this:

Related Fatwas