Haki za binadamu zinazohusu akili

Egypt's Dar Al-Ifta

Haki za binadamu zinazohusu akili

Question

Haki za binadamu zinazohusu akili.

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Sheria ya Kiislamu inasisitiza suala la kutunza akili, kwani akili katika sheria ya Kiislamu ni msingi wa kuwajibika kisheria ambapo nadharia ya kuwajibika kisheria ilijengwa juu ya msingi wa akili, hivyo sheria ya Kiislamu imeharamisha kila kileweshacho au dawa za kulevya (kileo) ili kuhifadhi akili ya binadamu, licha ya kuwa sheria ilipunguza adhabu au kuondosha hukumu juu ya mwenye kupoteza akili, sharti asiipoteze kwa makusudi au kwa kuvuka mipaka kama mwenye kupotea akili yake kwa sababu ya maradhi kama mwendawazimu n.k.

Aya za Quraani Tukufu zilihimiza watu watumie akili na wazingatie Aya kiakili, miongoni mwa Aya hizo ni maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na Anakuonyesheni Dalili zake ili mpate kufahamu} [AL BAQARAH, 73], {Je! Hawatembei katika ardhi ili wapate nyoyo (akili) za kufahamia} [AL-HAJJ, 46], aidha Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Au je, unafikiri ya kwamba wengi katika wao wanasikia au wanafahamu? Hawakuwa hao ila ni kama wanyama, bali wao wamepotea zaidi njia} [AL-FURQAN, 44].

Mwenyezi Mungu Amesisitiza kwamba hazingatii Aya na mifano iliyotajwa katika Quraani Tukufu ila mwanachuoni. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na hiyo mifano tunawapigia watu; na hawaifahamu ila wajuao} [AL-ANKABUUT, 43].

Wanachuoni wa Kiislamu walichukua akili kama moja ya dalili zinazofaa kwa elimu, na walifikia kutafuta dalili za kiakili katika elimu ya Tauhidi, pamoja na masharti yake, nyanja zake na namna ya kuzipanga dalili hizo ili elimu ifaidishe kwa yakini.

Ikiwa akili katika Uislamu ina cheo hicho, basi lazima cheo kiwe na athari na haki, na haya yote tunayaweka katika anwani: HAKI ZA BINADAMU ZINAZOAMBATANA NA KUSUDIO LA AKILI. Miongoni mwa haki hizo ni zile zilizotajwa katika ilani ya kimataifa ya haki za binadamu: 1. Haki ya kutoa rai 2. Haki ya malezi na elimu.

Haki ya kutoa rai.
Uislamu kama ulivyolinda uhuru wa itikadi, kutafakari na kutoa mawazo -kama ilivyotajwa katika haki za binadamu zinazoambatana na kusudio la dini– aidha uislamu umedhamini uhuru wa kutoa rai katika mambo yote ya kidunia yasiyo na tabia za kidini, pia Uislamu umeiheshimu akili na umehimiza kutafakari na ubunifu wa kweli.

Naye Mtume S.A.W. alikuwa anashauriana sana na Masahaba zake, akiifanyia kazi kivitendo kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na ushauriane nao katika mambo} [AALI IMRANI, 159].

Haukuwa msingi wa kushauriana katika uhalisia wake isipokuwa ni kuheshimu haki ya kutoa rai, kwa hiyo suala la kutoa rai katika Uislamu ni haki iliyokwisha thibiti hawezi mtu kuiondosha.

Uislamu umeupa uhuru wa kutoa rai uangalifu mkubwa kwa kuwa ni njia ya kutangaza ulinganiaji na kuwabainishia kwa watu, kwani Mtume S.A.W. alikuwa anasambaza daawa yake kwa watu wa makabila akiwa katika mlima wa Safa ili atangaze neno la Tauhidi.

Mtindo wa ulinganiaji ulikuwa unaambatana na majadiliano na hoja kama ni alama ya uhuru wa kutoa rai.

Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Kusudi yule aangamiaye aangamie kwa dalili zilizo dhahiri, na asalimike wakusalimika kwa dalili zilizo dhahiri} [AL ANFAL, 42], {Nyinyi hamna dalili kwa hayo} [YUNUS, 68], aidha Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na hizi ndizo (baadhi ya) hoja zetu tulizompa Ibrahimu juu ya watu wake} [AL-AN-AM, 83].

Naye Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema katika kisa cha Firauni:
{Firauni akasema: Na nani huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote?” Hadi kauli yake “Akasema: Je! Ijapokuwa nitakuletea kitu cha kubainisha wazi?} [AS SHURAH 23 – 30] .

Uhuru wa kutoa rai ni njia ya kumshinda hasimu, kukiri kwake, kudhihirisha haki na kuondosha shaka. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora}. [AN NAHL, 125]. Quraani Tukufu huanzia mwanzo wake mpaka mwisho inajadiliana na makafiri.

Hayo yanabainisha thamani ya kutoa rai na vipi Uislamu unavyoitegemea rai kubainisha hoja na kupata dalili.

Anayetazama yaliyotokea huko Thaqifa Bani Saada wakati wa kuchagua khalifa wa Mtume s.a.w anakuta utekelezaji ulio bora zaidi wa uhuru wa kutoa rai, uhuru wa mawazo na uhuru wa majadiliano yaliyotokea baina ya Muhajirina na Answaari, na hoja zilizotolewa na pande mbili kuhusu uchaguzi wa khalifa. Jambo hilo lililokuwa sura ya kwanza ya bunge katika Uislamu ambapo khalifa alichaguliwa.

Uhuru wa rai katika Uislamu ni haki iliyokwisha thibiti hata zikiwa zinapigongana na rai za kundi la Waumini madamu hawalazimishi watu kufuata rai kwa nguvu.

Kutokana na umuhimu wa suala la uhuru wa kutoa rai kwa wanachuoni wa Kiislamu, ilianzishwa shule ya rai katika elimu ya fiqhi ya Kiislamu, na wasomi wake wakaitwa Wanafiqhi wa rai, na kiongozi wao ni Ibrahim bin Yazid Al Nakhi’y na Hammad bin Abi Sulaiman na wengineo. Hawa ni wahitimu wa shule ya Abdallah bin Masoud R.A. Pia Imamu mkuu Abu Hanifa na wafuasi wake huko Iraq waliifuata shule hiyo.

Wanafiqhi hawa katika suala la kutoa fatwa wanategemea rai zao zinazotokana na dalili za Quraani Tukufu na Hadithi za Mtume S.A.W. sharti ziwe sahihi; kwani hawategemei Hadithi dhaifu. Wanafiqhi hawa walikuwa wanaogopa kukosea wakati wa kuzungunzia Hadithi za Mtume S.A.W. zaidi kuliko kufanya jitihada zao ili wasimsingizie uongo Mtume S.A.W.

Kutumia akili kufikia maoni katika mambo ya kifiqhi ambayo sheria haijaainisha kwa matini za wazi kutoka Quraani na Sunna iliyotakaswa ni wajibu wa kisheria juu ya Wanafiqhi wa Kiislamu katika zama zote kila ikipatikana dharura ya kutafutia jambo lolote ili jamii ya Kiislamu ishikamane na sababu za maendeleo na mafanikio, na hiyo haiwezi kutokea ila kwa kuwepo uhuru wa kutoa rai na mawazo kwani hayo ni miongoni mwa haki za asili za Mwislamu zilizokwisha thibiti ambazo wananchi wananufaika nazo katika dola la Kiislamu.

Uislamu unaonya mtazamo mbaya, kujitenga na kutochangia katika mambo ya jamii kwa rai na kauli, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na wawepo katika nyinyi watu wanaolingania kheri (Uislamu) na wanaoamrisha mema na wakakataza maovu. Na hao ndio watakaotengenekewa}[AALI IMRAN, 104].

Vidhibiti vya uhuru wa kutoa rai.
Vidhibiti vya uhuru wa kiujumla vinaainishwa kwa mujibu wa dhana ya fikra za mfumo wa kiujumla zinazotawala mifumo tofauti ya kisiasa.

Mfumo wa kiujumla ni mkusanyiko wa masilahi ya kimsingi kwa kundi la watu; mikusanyiko ya misingi ya awali ambayo uundaji wa jamii unaihitaji ili uwe na amani na utulivu.

Vidhibiti vya uhuru wa kiujumla vinaainishwa na msingi wa kisheria, kwa hiyo matumizi ya vidhibiti hivyo yanaweza kupanuka au kufinyika kwa mujibu wa dhana ya fikra za mfumo wa kiujumla inayokwenda pamoja na mwelekeo wa dola la kisiasa.

Uislamu haujaacha hivyo swala la uhuru wa kutoa rai, bali uliviweka vidhibiti vinavyoutawala ili kuepukana na fitina, utengano, kuleta madhara kwa wengine, kuwavunjia heshima wengine n.k.

Maana, uhuru wa kutoa rai ukivuka mipaka ya mambo ya maadili, adabu, mfumo wa umma au ukivuka mipaka ya fadhila, basi inawajibika kuusimamisha. Kwa hiyo, mtu akikatazwa kugusa vibaya mambo hayo, kwa hakika anakatazwa asivuke mipaka, na katika hali hiyo anakuwa hakunyimwa haki yake.

Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Kawaambieni maneno laini huwenda atashika mawaidha au ataogopa} [TAHA, 44], {Shikamana na kusamehe na amrisha mema na wapuze wajinga}[AL AARAF, 199], {Na wajinga wakisema nao (maneno mabaya) huwajibu. (maneno ya) salama} [AL-FURQAN, 63], {Wala msiwatukane wale ambao wanaabudu kinyume cha Mwenyezi Mungu, wasije wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri zao bila kujua} [AL AN-AM,108], pia Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Mwenyezi Mungu hapendi kutoa maneno ya kutangaza ubaya (wa watu) ila kwa yule mwenye kudhulumiwa} [AN NISAA, 148].

Hayo yote ni matokeo ya kimantiki kwa yanayotakiwa kuwepo katika mtindo wa mazungumzo, majadiliano kwa namna ya adabu, utulivu na heshima.

Aidha, uhuru wa kutoa rai haujuzu kufikia kiwango cha kueneza matamanio, upotevu au uzushi. Imamu Shaafiy alisema katika jambo hilo: “watu wakijua yanayotokana na maneno ni matamanio, basi watakimbia kama wanavyowakimbia simba”.

Imamu Aly bin Abu Taled R.A. alipigana na zandiki, akawachoma kwa kueneza kwao upotevu na uzandiki.

Uislamu ulikataza watu wasivunje heshima ya wengine au kutangaza siri zao; kwani hilo haliwezi kuhusiana na maana ya uhuru wa kutoa rai. Kwa hiyo, Uislamu uliweka adhabu endapo mtu atakashifu wengine hata likiwa jambo hilo halijafikia kiwango kinachoweza kuainishwa kuwa ni kukashifu. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Mwenyezi Mungu hapendi kutoa maneno ya kutangaza ubaya (wa watu) ila kwa yule mwenye kudhulumiwa} [AN NISAA, 148].

Quraani Tukufu iliweka vidhibiti katika majadiliano na wenye akida tofauti, ili yasifikie hali ya kutukanana au ugomvi, bali lazima yawe na mtindo mzuri wa kujizuilia na machafu. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Waite (waite watu) katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora}[AN NAHL, 125], pia Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Wala msibishane na watu waliopewa Kitabu (kabla yenu) ila kwa yale (majadiliano) yaliyo mazuri} [AL-ANKABUUT, 46].

Haki ya malezi na Elimu.
Ikiwa wema na kuwafanyia wema wazazi ni haki ya wazazi juu ya watoto, basi malezi mema ni haki ya watoto juu ya wazazi.

Kila binadamu – awe mwanamume au mwanamke - ana haki ya kupata elimu, na kutafuta elimu ni wajibu kwa wote. Imepokewa kutoka kwa Mtume S.A.W. kwamba: “Kutafuta elimu ni faradhi juu ya kila Mwislamu mwanamume na mwanamke”.

Vile vile elimu ni haki ya asiyesoma juu ya mtu aliyesoma kama alivyosema Mtume S.A.W.: “mwenye kushuhudia amfikishie asiyekuwepo”.

Jamii lazima itoe nafasi ya kupata elimu na maarifa kwa kila binadamu, kwa upande mwengine kila mmoja anachagua tawi la elimu linaloafikiana na kipaji na uwezo wake wa dhati kama alivyosema Mtume S.A.W.: “kila mmoja ana uwezo wa kufanya aliloumbiwa”.

Uislamu ulihimiza watu watafute elimu na ukapandisha cheo elimu na wenye elimu mpaka ukawafanyia wenye elimu ni warithi wa Manabii, kwa hivyo Uislamu unafungua uwanja wazi mbele ya kutafuta na kupata elimu.

Aidha, Uislamu umetoa mwelekeo sahihi wa kupata elimu kutokana na kuwepo misingi inayotoa heshima ambayo Uislamu uliidhamini kwa watafutaji elimu.

Kwa upande mwingine, Uislamu ulimpa binadamu haki ya kuwa elimu anazozipata ni sahihi ambapo umeharamisha jambo la kusema bila ya elimu, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Wala msiseme uwongo, kwa kuropokwa na ndimi zenu: Hichi halali, na hichi haramu -mkimzulia uwongo Mwenyezi Mungu. Hakika wanaomzulia uwongo Mwenyezi Mungu hawatafanikiwa} [AN NAHL, 116]; Maana Uislamu ulisisitiza kwamba chanzo cha elimu lazima kiwe sahihi bila ya kuwepo shaka. Ama malezi, basi Uislamu ulikuja na maadili mema ukawaamrisha watu washikamane nayo kama alivyosema Mtume S.A.W.: “Jipambeni kwa tabia za Allah.”

Basi kila binadamu ana haki ya kupata malezi mema ambayo Uislamu uliyadhamini kwake, na ukawahimiza wenye madaraka watekeleze haki hiyo kwa ajili ya kuwatunza.

Jambo linalodhihirisha umuhimu wa elimu katika Uislamu ni Aya ya kwanza iliyoteremshwa katika Quraani Tukufu, ni Aya ya elimu ambayo ndani yake ni wito wa kusoma na kupata elimu, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Soma kwa jina la Mola wako Aliyeumba. Amemuumba mwanadamu kwa pande la damu. Soma na Mola wako ni Karimu sana. Ambaye Amefundisha kwa kalamu. Amemfundisha mwanadamu aliyokuwa hayajui} [AL-ALAQ, 1-5].

Uislamu unawaheshimu wenye elimu na kuithamini elimu, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Mwenyezi Mungu Ameshuhudia ya kwamba hakuna aabudiwaye kwa haki ila Yeye tu. Na Malaika na wenye elimu, (wote wameshuhudia hayo); (Yeye) ndiye Mwenye kusimamisha uadilifu} [AALI IMRANI, 18], {Mwenyezi Mungu Atawainua wale walioamini miongoni mwenu; na waliopewa elimu watapata daraja zaidi} [AL-MUJADALAH, 11], {Sema: “Je, wanaweza kuwa sawa wale wanaojua na wale wasiojua?”}[AZ-ZUMAR, 9], {Sema: “Mwenyezi Mungu Anatosha kuwa shahidi baina yangu na baina yenu (kuwa mimi ni Mtume) na (pia) yule mwenye elimu ya Kitabu. (Kila aliyeisoma Taurati iliyo sahihi na Injili iliyo sahihi ameziona habari za Nabii Muhammad humo)”} [AR RAAD, 43], aidha Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na hiyo mifano tunawapigia watu; na hawaifahamu ila wajuao} [AL-ANKABUUT, 43].

Elimu ambayo ni faradhi juu ya wafuasi wa dini ya Uislamu ni ile elimu ambayo ni halali kisheria; inayokuwa njia ya kumwabudu Mwenyezi Mungu, miongoni mwa aina ya elimu hiyo ni ile inayoambatana na jambo la kuyalinda makusudio ya sheria katika mambo ya dharura na mahitaji. Aidha, masilahi ya jamii ni njia ya kuabudia kwani matendo ya mja katika mambo yake ya kidunia na akhera kwa mujibu wa uangalizi wa masilahi kwa namna iliyofaradhishwa na Mwenyezi Mungu siyo kwa kufuata matamanio yake, pamoja na elimu za dini kama Tafsiri, Hadithi, Fiqhi, na elimu zinazosaidia kuyalinda makusudio ya kisheria zinazoingia ndani ya elimu za kulinda masilahi ya jamii kama uhandisi, utibabu, kemia, hisabati n.k. pamoja na elimu nyingine zifaazo zinazolinda masilahi ya watu.

Kwa hiyo, elimu inayozingatiwa kisheria ni ile inayoambatana na kazi; hakuna kheri katika elimu isiyoleta manufaa. Ilipokelewa na Anas bin Malik na Abdulrahman bin Ghanm ya kwamba: Masahaba kumi wa Mtume S.A.W. walisema: “tulikuwa tunatafuta elimu katika msikiti wa Qubaa, akaja Mtume S.A.W. akasema: jifunzeni mtakayojifunza lakini hamtapata thawabu mpaka myafanyie kazi mliyojifunza”, aidha Mtume S.A.W. alisema: “tunajikinga kwa Mwenyezi Mungu na elimu isiyo na faida”.

Imamu Al Ghazaliy alisema kwamba elimu za kidunia zinaambatana na Fiqhi kama vile wenye elimu za kidunia wanavyoambatana na wanafiqhi; kwani Mwenyezi Mungu Aliiumba dunia iwe manufaa kwa nyumba ya Akhera. Na mwanafiqhi ni mjuzi wa mambo ya siasa na njia inayowaongoza watu wakifuata matamanio yao. Mwanafiqhi ni mwalimu wa mtawala na mwongozaji wake kumwelekeza njia ya kuokoka kwa kuwaongoza raia katika mambo yao ya dunia.

Wanafiqhi walibainisha wajibu wa kutafuta elimu uliofaridhishwa juu ya wote katika matawi yote ya maarifa. Imamu ibn Hazm alisema: “kila Mwislamu mwenye akili mwanamume au mwanamke, muungwana au mtumwa analazimika kujitaharisha, kusali na kufunga kwa kuwa ni faradhi zisizokuwa na hitilafu. Aidha, twahara na sala ni wajibu juu ya kila mtu mzima au mgonjwa. Kila tuliyomtaja anapaswa kujua kilichohalali na kilichoharamu kwake katika vyakula, vinywaji, mavazi, jimai, damu, kauli, vitendo n.k. Basi masuala hayo yote lazima yajulikane na wote wanaume, wanawake, watumwa au waungwana”.

Uislamu umelazimisha kuyajua yote yaliyotajwa kuanzia umri wa kubaleghe Waislamu au kuanzia kusilimu kwao baada ya umri wa kubaleghe.

Kisha ukafaradhisha juu ya kila mwenye mali ajifunze yanayohusiana na Zaka wanaume au wanawake, watumwa au waungwana, na yeyote akiwa hana mali basi halazimiki kujifunza mambo yanayohusiana na Zaka, kisha anayelazimika kufanya hija na umra basi ni juu yake ajifunze adabu za hija na asiyekuwa mzima wa kimwili au hana mali halazimiki kuzijua adabu hizo.

Kisha Uislamu ulifaradhisha juu ya viongozi wa jeshi wajifunze hukumu za jihadi na mgawanyo wa ngawira.

Kisha Uislamu ulifaradhisha juu ya watawala na makadhi wajifunze hukumu na adhabu zile ambazo wengine wanakuwa hawalazimiki kuzijua.

Kisha Uislamu ulifaridhisha juu ya wafanyibiashara wajifunze hukumu za mauzo, yanayohalalishwa na yanayoharamishwa katika suala hilo, jambo ambalo haliwajibiki kisheria juu ya asiyeuza wala asiyenunua.

Halafu, Uislamu ulifaradhisha juu ya kila kundi la watu wanaoishi katika kijiji, mji na mtaa wachague mmoja awe mwakilishi wao katika kutaka hukumu zote za dini.

Kwa hiyo, Uislamu haujaacha makundi yoyote ya jamii bila ya kuwaelimisha, wala haujaacha namna yoyote ya elimu iliyo halali kisheria bila ya kuifaradhisha.

Wajibu wa nchi katika kulinda elimu.
Uislamu ulirahisisha elimu kwa watu, ukalazimisha dola litunze elimu; Uislamu haujaishia kuwafaradhishia watu wa kawaida elimu bali pia umewalazimisha watawala, waajiriwa na wenye mali watafute elimu. Na tukihesabu makundi yanayolazimika kujifunza tutakuta wote wanalazimika bila ya kuachwa hata kundi moja.

Uislamu umewalazimisha watawala wawafundishe raia, kwa hiyo Uislamu umehakikisha haki ya kupata elimu kwa wote wanaume au wanawake na waungwana au watumwa.

Uislamu unamlazimisha mume amfundishe mke wake na mjakazi, afundishe mwenyewe au amruhusu akutane na anayeweza kumfundisha.

Aidha, Uislamu umemlazimisha Imamu awahesabu watu kwa mujibu wa matendo hayo, na kuwachagua walimu ili kuwafundisha wajinga.

Hivyo, Uislamu umelazimisha wenye kujua kuwafundisha wasiojua, kama ulivyomlazimisha Imamu awafundishe wasio kuwa na uwezo; maana suala la kupata elimu ni haki kwa kila mtu juu ya dola, hakuna tofauti baina ya mwanamume wala mwanamke au muungwana wala mtumwa au mtu mzima wala mtoto mdogo.

Jitihada ni miongoni mwa nyanja za uhuru wa tafiti za kielimu: Uislamu uliwaelekeza watu watafakari ili wafikie ukweli, na hiyo haipatikani ila kwa njia ya kutafiti katika mambo na amali zinazoendesha maisha ya watu na kupangisha masuala yao ya kimaisha.

Rai ambayo ni msingi wa jitihada inamaanisha kufikiria kwa njia ambazo sheria iliziongoza; kwani zinakurubia ukweli, nazo ni: kutohoa hukumu kutokana na dalili zake za kisheria zikiwa za kiakili au za kunukuliwa.

Lakini jitihada inayotegemea njia za kufikiria kwa njia ambazo sheria haijaweka, basi ni sawa na kufikiria matamanio wala haitakuwa miongoni mwa vyanzo vya utungaji tena, kwahiyo ni haramu kisheria, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na kama haki ingalifuata matamanio yao (kama wanavyotaka), zingaliharibika mbingu na ardhi} [AL-MUMINUN, 71].

Kwa hiyo, haijizu kwa kila mtu ashughulike na jitihada; kwani masharti ya jitihada lazima yatimizwe.
Marejeo: Sehemu ya Tafiti katika Idara ya Fatwa ya Misri.
 

Share this:

Related Fatwas