Haki za Binadamu – Mtazamo wa Kiuju...

Egypt's Dar Al-Ifta

Haki za Binadamu – Mtazamo wa Kiujumla

Question

 Je, kuna nadharia inayohusiana na haki za binadamu katika Uislamu?

Answer

 Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., jamaa zake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:

1) Sisi katika juhudi zetu za kujibu swali hilo, lazima tuanze jaribio ka kufahamu haki za binadamu kwa mujibu wa mtazamo wa Kiislamu bila ya kutosheleza na kuweka anwani tu za Kiislamu kwa masuala yenye mitazamo na mielekeo tofauti. bali lazima jaribio hilo liangalie upande wa Kiislamu katika viwango vyote pamoja na kushikamana na mifumo ya Kiislamu, na katika wakati huo huo tunapaswa kutodharau juhudi za kifikra za wengine zinazoleta hali yenye upeo wa juu kwa binadamu.

2) Kwa hiyo, utafiti unatafuta maana ya neno la “haki” katika ustaarabu wa Kiislamu kwa mujibu wa maana ya neno la “haki” katika lugha ya Kiarabu, pamoja na kuangalia maana ya neno hilo na matumizi yake katika Qurani Tukufu na Sunna ya Mtume S.A.W. iliyotakasika. Kwa hiyo, utafiti huu unajaribu kubainisha sifa za haki katika Uislamu kuwa ni: thabiti, wazi, wajibu, sahihi, zenye ukweli licha ya kuafikiana na uhalisia.

3) Halikadhalika, tunaona matumizi mbalimbali ya neno la “haki” katika Sunna yenye iliyotakasika; neno la “haki” limetumika kwa maana ya wahyi, dini sahihi, aidha mawajibiko ya kiraia yanayomlazimisha mtu kwa jamii na serikali yake.

4) Maulamaa wa sheria ya Kiislamu baada ya kusoma matini za sheria kwa undani walifikia nadharia ya Uislamu kuhusu haki jumuishi wakabainisha kwamba haki ziko katika aina nne: haki ya Mwenyezi Mungu Mtukufu juu ya waja wake, haki ya mja juu ya nafsi yake, haki ya waja wenyewe kwa wenyewe na haki ya wanyama kwa watu. Kuanzia hapo, utafiti ulianzisha mtazamo wa haki za binadamu katika Uislamu kwa mujibu wa mtazamo huo jumuishi wa haki za wote.

5) Uislamu kama ulivyompa mtu haki zake halikadhalika ulimfaridhishia wajibu wake na ukamwekea uwiano baina ya haki na wajibu kwa hali ya uadilifu, na kuanzia hapo lazima tuangalie maana ya haki kwa mkabala wa wajibu kama pande mbili za mizani ya uadilifu ziliyo sawa.

6) Kama tulivyozungumzia haki za binadamu tukabainisha mtazamo wa Uislamu unaohusika na haki, inatubidi tuzungumzie mtazamo wa Uislamu juu ya binadamu ilhali kwa mitazamo miwili, unatokea mtazamo jumuia unaohusika na haki za binadamu katika Uislamu.

7) Binadamu katika Uislamu ni kiumbe mwenye jukumu, aliebaleghe. Naye kwa mujibu wa mtazamo wa Uislamu, unakuwa na roho na mwili, halikadhalika Uislamu ulimpa binadamu uhuru ukamfaridhishia kutekeleza amana na kuwajibika na kulazimika kisheria.

8) Utafiti baada ya hayo, unatoa mwangaza juu ya Azimio la haki za binadamu katika ustaarabu wa kimagharibi kwa kutoa muhtasari wa kihistoria unaobainisha haki za kimsingi katika ustaarabu huo, kama vile, haki za Kiingereza, za Kimarekani na za Kifaransa, na haki za binadamu za kimataifa. Halikadhalika utafiti unabainishia uzito wa kihistoria wa mikataba ya haki za binadamu kwa kutoa rai za kisheria katika suala hilo.

9) Utafiti baada ya hayo, unaanza kwa kuzungumzia tangazo la haki za binadamu katika ustaarabu wa kimagharibi ukabainisha mapambano ya madhehebu ya kimagharibi na haki za binadamu, mapambano ya mamlaka ya nchi na haki za binadamu na mapambano ya kimataifa na haki za binadamu.

10) Kuhusu mapambano ya madhehebu ya kimagharibi na haki za binadamu, utafiti ulibainisha uhusiano uliokuwapo baina ya haki za binadamu katika Umagharibi na falsafa za kimagharibi zinazohusiana na suala hilo, na hasa madhehebu binafsi.

11) Kuhusu mapambano yaliyokuwa baina ya mamlaka ya nchi na haki za binadamu, basi kimsingi kila nchi ina mamlaka ya uhuru wa kuchagua falsafa ya kijamii na kisiasa, ila Azimio la haki za binadamu lilikuwa na athari za wazi, ambapo umagharibi kutokana na Umoja wa nchi za kimataifa, ulijaribu kutowajibika na mifumo ya utawala inayoambatana na haki za binadamu, jambo ambalo liliingiza suala la haki za binadamu katika mapambano ya kimataifa baina ya nchi za Magharibi na nchi za Mashariki na ulimwengu wote kiujumla; nchi za Magharibi zinafanya bidii kuzitawala mpaka haki za binadamu, zinakuwa sehemu mojawapo ya mapambano yaliyokuwa baina ya nchi za Magharibi na mifumo ya kisiasa iliyokuwa inapinzana na nchi hizo, na kutumia Azimio la haki za binadamu kama chombo cha kisiasa dhidi ya mifumo hiyo, katika hali ya kutochunga mifumo inayofuatilia nchi za kimagharibi licha ya kuwepo vitendo vingi vya uvunjaji wa haki za binadamu katika nchi hizo, jambo ambalo linaashiria mgogoro wa kutokuwepo dhamira ya Magharibi.

12) Halafu utafiti ulishughulikia zaidi kuweka Azimio la haki za binadamu kwa mujibu wa mizani ya Uislamu, ambapo utafiti ulitoa mtazamo mpya kuhusu haki za binadamu kwa uhusiano na makusudio matano ya kisheria: (dini - nafsi - akili - heshima ya mtu - mali), basi haki za binadamu zinakusanya haki ya kuamini (itikadi), haki ya ulinganiaji, haki ya kufikiri, haki ya kutoa mawazo (maoni), haki ya ukimbizi, haki ya wachache na haki ya kushiriki katika maisha kwa ujumla.

13) Kusudio la nafsi linahusiana na haki zifuatazo: haki ya maisha yenye amani, haki ya uhuru, haki ya usawa, haki ya uadilifu, haki ya kulindwa, haki ya kulinda kila kilicho binafsi, haki ya kutembelea na kukaa, na haki ya kutosheka. Kusudio la akili linahusiana na kazi zifuatazo: haki ya malezi na kupata elimu. Kusudio la heshima ya mtu linahusiana na haki zifuatazo: haki ya kulinda heshima ya mtu na umaarufu wake. Kusudio la mali linahusiana na haki za kiuchumi na haki za wafanyakazi.

14) Utafiti unazitaja haki za binadamu kwa mujibu wa mtazamo wa Uislamu kwa upambanuzi zaidi kwa kuthibitisha ukweli wake kwa dalili za kisheria zinazotokana na Qurani Tukufu na Sunna tukufu, pamoja na kutaja maneno ya wanavyuoni na watafiti katika suala hilo.

15) Kiini cha utafiti wa haki za binadamu katika Uislamu ni kuzungumzia Azimio la haki za binadamu kwa mujibu wa mizani ya fikra za kiislamu ambapo tunaunganisha baina ya haki za binadamu na nadharia ya makusudio matano ya kisheria na tunabainisha maana ya haki za binadamu zinazohusiana na kusudio la dini, haki za binadamu zinazohusiana na kusudio la nafsi, na zile haki zinahusiana na kusudio la akili n.k. … mpaka tunamalizia makusudio matano ya kisheria yanayojenga nadharia ya makusudio ambapo katika suala hilo tuna dalili za kisheria zinazotokana na matini za Qurani Tukufu na Sunna iliyotakasika.

16) Haki za binadamu katika Uislamu zinaambatana na maumbile ya Uislamu: Maana ya neno "Uislamu" kilugha: ni unyenyekevu, kunyenyekea. Na neno "Uislamu" lina maana nyingi, na miongoni mwazo ni: amani, suluhu, usamehevu na dini ya haki.

17) Uislamu maana yake ni: kumnyenyekea Mwenyezi Mungu na kuelekeza uso kwa Mwenyezi Mungu. Kadhalika Uislamu ni: kujisalimisha kikamilifu kwa ukamilifu kwa utukufu wa Allah, na uhakika wa Uislamu ni: kumtakasia Mwenyezi Mungu katika dini, hakuna mwabudiwa isipokuwa Allah, jambo linalomaanisha kusafisha moyo kutoka maovu ya shirki iliyojificha na iliyo wazi, Mwenyezi Mungu Amesema: {Wawe wananiabudu, hawanishirikishi na chochote} [AN-NUR, 55]. Na kuitakasa nafsi kutoka riyaa na unafiki, Mwenyezi Mungu Amesema: {Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu. Anahadithia yaliyo kweli; naye ni mbora kuliko wote wanaohukumu} [AL AN-AM, 57]. Kwa hayo, nafsi inakuwa safi zaidi na inajiepushia hofu na shirki mpaka watu wawe wenye usawa katika uhuru kwani Uislamu umeleta mapinduzi dhidi ya shirki na ukafiri, halikadhalika ni mapinduzi dhidi ya utumwa na dhulma.

18) Uhuru na usawa ni matokeo ya hali ya kuingia katika Uislamu. Uislamu unasisitizia uhusiano bayana uliopo baina ya mja na Mola wake; hakuna uwakilishi kati ya mja na Mola wake wala ukuhani. kwa hiyo, binadamu katika Uislamu ana matakwa yake yenye uhuru usiozuiliwa bila ya kuwepo waombezi au wapatanishi.

19) Mfumo wa Kiislamu ni mkusanyiko wa misingi ya awali na misingi jumuishi ambayo Qurani Tukufu inaifaradhisha pamoja na Sunna iliyotakasika, iliikubali kuwa ni mfumo unaoendesha mambo ya utawala. Misingi ya awali ilitekelezwa mwanzoni mwa Uislamu kwa njia sahihi iliyonyooka, na miongoni mwa misingi jumuishi ambayo ililetwa na Uislamu ni:

20) Msingi wa uadilifu: huu ni msingi uliofaradhishwa kama msingi jumuishi dhahania, nao ni miongoni mwa misingi ya awali ambayo inatakikana kutekelezwa na serikali ya Kiislamu katika jamii yake; maana haihusiki na taifa au nchi maalumu, bali inatakikana kutekelezwa katika nchi zote misingi ambayo haitofautishi baina ya Mwislamu na asiyekuwa Mwislamu, mwanamume na mwanamke, mweupe na mweusi wala rafiki na adui. Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: {Na mnapohukumu baina ya watu mhukumu kwa haki. Bila shaka mawaidha anayokutoleeni Mwenyezi Mungu ni mazuri sana. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Asikiaye (na) Aonyaye} [AN NISAA, 58], Aidha Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutowafanyia uadilifu. Sema, Fanyeni uadilifu; huko ndiko kunakomkurubisha mtu na uchamungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo habari za (yote) mnyayoyatenda} [AL MAIDAH, 8].

21) Msingi wa usawa: Uislamu unauweka kama msingi jumuishi dhahania unaotakikana kutekelezwa katika sekta zote za kibinadamu bila ya kuwepo hali yoyote ya ubaguzi wa kijinsia, ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa kidini wala ubaguzi wa kiitikadi. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Enyi watu! Kwa hakika tumekuumbeni (nyote) kwa (yule) mwanamume (mmoja; Adamu) na (yule yule) mwanamke (mmoja; Hawa). Na tumekufanyeni mataifa na makabila (mbalimbali) ili mjuane (tu basi; siyo mkejeleane). Hakika ahishimiwaye sana miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule amchaye Mungu zaidi katika nyingi. Kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye habari (za mambo yote)} [AL-HUJURAT, 13]. Kadhalika Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Enyi watu! Mcheni Mola wenu ambaye Amekuumbeni katika asli moja. Na Amemuumba mke katika nafsi ile ile. Na Akaeneza wanaume wengi na wanawake kutoka katika wawili hao. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana. Na (muwatazame) jamaa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mlinzi juu yenu (anayaona kila mnayoyafanya)} [AN NISAA, 1].

22) Msingi wa mashauriano: Uislamu unaufaradhisha msingi huu, na unawasifu Waumini katika Qurani Tukufu kwa maneno yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na wanashauriana katika mambo yao} [ASH-SHUURA, 38]. Halikadhalika Mwenyezi Mungu anamwamrisha Nabii wake kushikamana na msingi huu ambapo anasema: {Basi kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu umekuwa laini kwao (Ewe Muhammad). Na kama ungekuwa mkali na mwenye moyo mgumu bila shaka wangalikukimbia. Basi wewe wasamehe na uwaombee msamaha (kwa Mwenyezi Mungu) na ushauriane nao katika mambo. Na ufungapo nia mtegemee Mwenyezi Mungu (tu ufanye hili uliloazimia). Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda wamtegemeyao} [AALI IMRAN, 159]. Qurani Tukufu inaziacha njia za kutekeleza msingi wa mashauriano kwa kila nchi na kila Umma; wahusika wake wawe na uhuru wa kuchagua njia inayofaa na inayolinda masilahi ya wote ili kuutekeleza msingi huo. Mashauriano hayo yanaweza kutekelezwa kwa njia ya kidemokrasia moja kwa moja; kuchagua wabunge kwa namna inayoleta masilahi ya nchi kama vile; kupiga kura au kuwachagua wabunge miongoni mwa wagombea wenye sifa maalumu za kielimu au kimaadili. Mambo hayo yote yanaachwa mikonomi mwa wenye madaraka watumie njia zinazofaa kwa ajili ya kuleta masilahi ya umma.

23) Qurani Tukufu inaashiria wakuu -wenye madaraka- nao ni wenye mamlaka ya kutoa maoni na wanafikra ambao Umma unawaelekea wao katika mambo yake yanayohusu utungaji wa sheria au ya mpango katika hali ya kuzuka jambo linalohitaji utafiti na jitihada ya kisheria, na Qurani Tukufu inawalazimisha watu wayatii maneno yao, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka juu yenu, walio katika nyie (Waislamu wenzenu). Na kama mkikhitalifiana juu ya jambo lo lote basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ikiwa mnamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Hiyo ndiyo kheri, nayo ina matokeo bora kabisa} [AN NISAA, 59]. Aidha Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na linapowafikia jambo lo lote la amani au la khofu hulitangaza. Na kama wangalilipeleka kwa Mtume na kwa wenye mamlaka kwao, wale wanaopeleleza (wanaojua kupima mambo) miongoni mwao wangalijua (kuwa hilo ni jambo la kutangazwa au si la kutangazwa)} [AN NISAA, 83]. Halikadhalika Qurani Tukufu inauachia Umma husika na wasomi wake suala la kuainisha Jopo la viongozi na wataalamu na masharti yake na mikutano yake na uhusiano wake na mamlaka ya nchi.

24) Uislamu kama ulivyoshughulikia kuweka uhusiano baina ya mamlaka tofauto za nchi, halikadhalika unaainisha uhusiano wa mamlaka za nchi na wananchi. Aidha uhusiano uliopo baina ya watu wenyewe ili kuyalinda makusudio matano ya kisheria ambayo sheria za mbinguni zililetwa kwa ajili ya kuyalinda kwa hiyo Mwenyezi Mungu Amewahadithia wanajamii kwa kusema: {Na wawepo katika nyinyi watu wanaolingania kheri (Uislamu) na wanaoamrisha mema na wakakataza maovu. Na hao ndio watakaotengenekewa} [AALI IMRAN, 104].

25) Kwa hiyo, Uislamu unaelekeza namna ya kuanzisha Jopo au taasisi katika jamii ya Kislamu ili iwe na jukumu la kutekeleza malengo matatu nayo ni nyadhifa zinazotakiwa kushikiliwa kwa jina la jamii ya Kiislamu, na nyadhifa hizo ni mkusanyiko wa mambo ya kiutawala katika nchi.

26) Ulinganiaji wa kheri huleta hali ya raha, wasaa, furaha ya watu na hulinda hali ya usalama pamoja na kutosheleza mahitaji ya maisha. Masuala ya kuamrisha mema na kuyakataza maovu yanajumuisha kila shughuli za nchi kama vile; kueneza uadilifu, kuheshimu mikataba na kutekeleza ahadi. Na hayo yote kwa pamoja yanakuwa ni nyadhifa zinazohakikisha kuwa masilahi ya watu wote yanapatikana; Imamu, makamu wake na wasaidizi wake pamoja na watu wanaoaminika kwa vitendo vyao, huwa pamoja na hushirikiana zaidi na kuhakikisha masilahi ya wote yanafikiwa, ambapo wasomi wa kiislamu wameainisha maana ya masilahi wakisema: ni kitendo cha kuhifadhi makusudio matano ya kisheria ambayo ni: dini, nafsi, akili, kizazi na mali.

27) Kwa ajili ya kuyatekeleza makusudio hayo matano, Uislamu unawapa watu haki zao, na unawalindia aina zote za uhuru wanaoutumia, pamoja na kuwalindia utendaji wa uhuru huo. Kadhalika Uislamu unakemea na kutoa adhabu kwa yoyote atakaeushambulia utendaji huo wa uhuru. Na Uislamu umeweka usawa baina ya watu katika uadilifu, ukadhi, na hata katika utungaji wa sheria na katika suala la kutoa maamuzi.

28) Kwa kuwa binadamu kimaumbile, anamili katika kutaka kujua sababu na kukidhi mahitaji yake ya kiakili na kuangalia kila yanayomzunguka na hisia, basi Qurani Tukufu anakidhi maumbile yake na kubainisha sababu ya kuhumu kwa kumtolea wito Mwislamu akidhi hisia na kumhamasisha afikiri. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi na vitu alivyoviumba Mwenyezi Mungu?} [AL AARAF, 185]. Aidha Mwenyezi Mungu anawakosoa watu ambao hawaiweki mbele akili, ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na wanapoambiwa, “Njooni katika hukumu Alizoziteremsha Mwenyezi Mungu na (anazozisema) Mtume”, husema: yanatutosha yale tuliyowakuta nayo baba zenu} [AL MAIDAH, 104]. Kadhalika Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Kwa yakini tuliwakuta baba zetu juu ya dasturi (zao makhsusi), na hakika sisi tutafuata nyayo zao} [AZ-ZUKHRUF, 23].

29) Jukumu la Qurani Tukufu ni kuwaongoza watu njia iliyo rahisi zaidi ya uongofu na kuwatenga na madhara pamoja na kuwahifadhi wasikurubie njia ya maangamizi na kuwaepusha wasiingie motoni. Hivyo, Qurani Tukufu inalishighulikia suala hilo kwa mtindo wa kimalezi na kielimu. Katika Qurani Tukufu, tunakuta dalili nyingi juu ya hayo kama vile, suala la kuharamisha ulevi na kamari na mtindo ambao Qurani Tukufu iliutumia katika kuharamisha kikamilifu na mitindo mingine iliyotumiwa na nchi za kimagharibi katika suala hilo.

30) Uhuru wa kutafakari, uhuru wa usambazaji, haki za wanandoa, uhuru wa mtu binafsi. Hizi zote ni haki ambazo Uislamu ulizitolea utatuzi kwa mtindo wake wenye uuwiano ambao unatofautiana na njia ambazo zilifaradhisha hizo haki na uhuru baada ya mapinduzi ya kidini na ya kisiasa, yale mapinduzi ambayo yalipelekea umwagaji wa damu nyingi za watu wasio na hatia.

31) Nadharia za uhuru zinatofautiana katika kubainisha mtazamo wa aina za uhuru jumla: je, uhuru wa jumla unapatikana kwa matini na kwamba kisichokuwa katika uhuru huo kinakatazwa? Au vitu vyote kimsingi ni halali na haijuzu kukitundikia kitu chochote au kitendo chochote au hata kukiharamisha isipokuwa kwa matini maalumu?

32) Tukirudi katika fiqhi ya Kiislamu, tutakuta maoni tofauti ya mafaqihi katika suala hilo. Lakini rai bora zaidi ya kifiqhi iliyochaguliwa na wataalamu wa Fiqhi kuwa ni kuwa asili katika vitu vyenye manufaa ni halali, na vyenye madhara ni haramu. Kwa hiyo uhuru wa binadamu na haki zake lazima ziwe kwa mujibu wa mtazamo wa msingi huu wa kisheria.

33) Kwa mujibu wa yaliyotangulia, tutajadili suala la haki za binadamu kutokana na anwani zifuatazo: haki za binadamu na mtazamo wa haki katika lugha na sheria -haki za binadamu na nadharia ya haki katika Uislamu- haki za binadamu katika Uislamu na uhusiano wake na mtazamo wa Uislamu kwa binadamu -haki za binadamu: muhtasari wa kihistoria, kimagharibi na kikanuni- haki za binadamu na nyanja zake katika ustaarabu wa kimagharibi wa kisasa -haki za binadamu na mgogoro wa dhamira ya kimagharibi- haki za binadamu katika Uislamu na misingi ya kisheria kwa ujumla - haki za binadamu katika Uislamu zinazolihusu kusudio la dini - haki binadamu zinazolihusu kusudio la nafsi- haki za binadamu zinazolihusu kusudio la akili -haki za binadamu zinazolihusu kusudio la heshima ya mtu na murua - haki za binadamu zinazolihusu kusudio la mali.
Rejea: Sehemu ya Tafiti katika Idara ya Fatwa ya Kimisri.

Share this:

Related Fatwas