Mfano wa Kuigwa kwa Mujibu wa Mtaza...

Egypt's Dar Al-Ifta

Mfano wa Kuigwa kwa Mujibu wa Mtazamo wa Maadili ya Kiislamu

Question

Ni upi umuhimu wa mfano wa kuigwa katika mfumo wa maadili ya Kiislamu ?

Answer

1- Hapana shaka kuwa matatizo ya maisha ya vijana wetu walioelimika hayajawa tukio la kijamii tu bali yanaongezeka na kuwa tatizo la kijamii lisilokosekana katika nyumba yeyote ya mwislamu, kwa namna ambayo haiwezekani kulidharau au kulinyamazia. Na katika uzio wake wa kulitatua tatizo hili, ni lazima pawepo na njia ya nadharia ya maadili ya Kiislamu katika makuzi ya kitabia, kimwenendo na kijamii, na ambayo huanzia kwa msingi wa kuwepo mfano wa kuigwa, msingi huo wa kimaadili ni muhimu na lazima. Na kuukana uwepo wa mfano wa kuigwa kama wafanyavyo baadhi ya watu wenye mielekeo mbali mbali, kwanza kabisa ni ukanushaji wa Uzazi, pili ni usambaratishaji wa familia, na baada ya hapo, tatu ni wito wa kwenda kinyume na maadili na thamani ya maadili mema na kiwango cha juu cha adabu.

2- Hakika kuukana uwepo wa mfano wa kuigwa ni kuukana ujumbe wa Mwalimu na Mlezi, na hatari zaidi ya hiyo ni wito wa kuukana ujumbe wa mitume na manabii wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kisha unakuwa ni ukiukaji wa risala ya Mtume wa Mwisho ambaye alikuja nayo, Muhammad S.A.W, naye ni mfano mzuri wa kuigwa ambao unamfaa kila mwislamu. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu, ametuamrisha kumuiga Mtume S.A.W aliposema: {hakika nyinyi mnacho kiigo chema kwa Mtume S.A.W kwa anaemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana} [AL-AHZAAB: 21].

3- Kwa hivyo kumuiga Mtume S.A.W ni wajibu wa kila Mwislamu na yeyote atakayekanusha jambo hili atakuwa ametoka katika ufahamu sahihi wa Dini ya Uislamu {na anachokupeni Mtume kichukueni na anachokukataneni jiepusheni nacho. Namcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu} [AL HASHR: 7]

4- Na kwa uwazi huu katika mweleweko wa Mfano wa kuigwa kwa mujibu wa mtazamo wa Kiislamu baadhi yao wanakuja na kudai kuwa Mfano wa kuigwa ni simulizi za kale na ni wito unaopotosha, na kusahau kuwa Moyo wa Mwislamu na akili yake pamoja na ulimi wake unatokana na mfano huo ambao haujawahi kutokea na wala hautatokea katika wakati wowote ule kuwepo mfano kama huo. Nao ni Bwana wetu Mtume Muhammad S.A.W.

5- Masahaba wa Bwana wetu Mtume S.A.W., waliuiga yeye kwa maadili, vitendo, kazi na mwenendo wake, na wakawa kwa fadhila zake Mola ni shule zaa kimaadili kijamii na kidini. Taabiyna (Wafuasi wa Masahaba) walijifunza kutoka kwao, na Taabiu Taabiyn (wafuasi wa wafuasi wa Masahaba) nao wakajifunza kutoka kwa waliowatangulia, na itaendelea kuwa hivyo hadi siku ya Malipo.

6- Hakika misingi ambayo mwislamu anapaswa kuifuata iko wazi kabisa, haina mkanganyo ndani yake ugumu, lakini kujiepusha na mfano mzuri wa kuigwa kwa madai ya kutokuwepo kwake ni tamko linalokataliwa na ni wito wa uwongo. Kwa hivyo basi, mfano mwema wa kuigwa ambao mtoto anaweza kuupata unapatikana katika familia yake, shuleni, chuoni na katika taasisi mbali mbali za kidini kama vile misikiti, Madhehebu mbali mbali ya Sufi, wanachuoni wakubwa na Mashekhe, walinganiaji miongoni mwa wanachuoni wa Azhar na sehemu nyingine nyingi miongoni mwa majukwaa ya kielimu katika nchi za Kiislamu. Lakini wagonjwa wa moyo hawaoni isipokuwa mfano mbaya tu. Hakika mgonjwa wa nyongo anaona ladha ya asali kuwa ni chungu.

7- Hakika mafanikio ya mchakato wa malezi ya kijamii na kutofanikiwa kwake hutwama katika mfano wa kuigwa, iwapo mfano huo utakuwa mwema basi utu wa mtu hukamilika kimaadili, kimwenendo na kijamii. Na iwapo mfano huo utakuwa mwovu basi huzalisha mharibiko wa kitabia, ufisadi na ukengeukaji wa kimaadili.

8- Na kwa hivyo basi, kwa upande wa kielimu taasisi za malezi zinafanya kazi ya kuonesha mfano wa kuigwa, kwa mfano, mtu ambaye anataka kujifunza hati nzuri basi anapaswa kumuiga mtu mwenye hati nzuri, na iwapo atamuiga mtu mwenye hati mbaya basi hakuna atakachokipata isipokuwa hati mbaya. Na hivyo hivyo ndivyo ilivyo kwa upande wa Maadili Mema kwani nayo yanahitaji mtu ajifunze kwa kuchagua watu wenye tabia njema.

9- Isipokuwa mtu anahitaji kujikalifisha – mwanzoni – ili aweze kujichumia maadili mema. Na kujikalifisha ni kazi nzito inayohitaji juhudi pevu na ngumu, na iwapo hatutajilazimisha na kuendelea kuvumiilia basi hakika kuwa hatutavuna maadili mema.

10- Hakika malezi ya chipukizi kwa ajili ya kujichumia mieleweko na thamani kubwa za kimaadili hayatafanikiwa isipokuwa kwa kujikalifisha, na kwamba nafsi ya mtu hupendelea uvivu, raha, na uzembe, kwa hivyo iwapo haitazoeshwa uvumilivu na kuongeza juhudi kwa ajili ya kuiga mfano mwema basi huenda kombo na kukengeuka kimaadili.

11- Na iwapo mfano mwema utachaguliwa na ukawa ndio mfano unaoigwa na kufuatwa na mtu, na huyo akafuata tabia, mwenendo na kuwa ndio mfano wake mkuu mpaka ikawa hiyo ndio tabia yake iliyokita ndani ya mtu huyo mfuasi, basi kamwe hatakwenda kombo kimaadili na kuwa mbali na tabia hiyo.

12- Hakika njia ya kutatua matatizo ya waislamu kimaisha iko katika kuwepo mfano mwema wa kuigwa, na kukosekana kwa mfano huo si dalili ya kutokuwepo kwake. Anayeukana mfano huo wa kuigwa amesahau kuwa alipokuwa mdogo wazazi wake walimlea. Na kwamba atake asitake, amechukua tabia zao katika mzunguko miongoni mwa mizunguko ya maisha, kama ambavyo, atakuwa amechukua tabia za baadhi ya walimu wake, walezi wake shuleni au katika chuo kikuu au katika maisha ya uraiani.

13- Na hapa tunasisitizia juu ya umuhimu wa kuwa mfano wa kuigwa unatakiwa uwe mfano mwema. Kwa hivyo mtu anayewafuata na kuwaiga watu wenye maadili mema huchukua tabia zao na kwa hivyo huwa ni rahisi kwake kuwa na tabia njema, kinyume cha yule anayefuata mfano mbaya, huchukua tabia mbaya na huwa nayo hadi ikajitokeza wazi wazi pamoja na uovu wake wa maadili. Na iwapo mtu atakanusha uwepo wa mfano wa kuigwa atakuwa amekanusha thamani za maadili na mifano ya maadili mema pamoja na misingi na risala mbali mbali za Mwenyezi Mungu na pia ukweli wa Dini. Na lazima mtu huyo atakuwa anatuhumiwa kwa kuwa na matatizo ya akili na kifikra katika maisha yake na mwenendo wake wa kimaadili.

14- Na mwislamu hawezi kutoa udhuru wa aina yeyote wa kutofuata mfano wa kuigwa au akadai kuwa mfano huo haupo au hautakikani, kwani kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu ndani yake kinabeba katika kila aya miongoni mwa aya zake yanayoweza kumsaidia mwislamu katika fikra, kimwenendo na maisha yake. Na katika Sunna ya Bwana wetu Mtume S.A.W, kuna mfumo mkuu na vipengele mbali mbali fafanuzi vinavyoelezea sehemu ndogo ndogo na kuna majibu ya maswali ya kila aina, na ya kila siku ambayo yanaweza kufikiriwa na mwislamu. Na hakika wanachuoni mbali mbali wa Kiislamu wamejaribu kufanya juhudi zao katika kutekeleza misingi hiyo katika matawi yake na mapya mbali mbali yanayojitokeza katika zama hizi, katika nyanja mbali mbali za kiuchumi, kisheria na kimaadili.

Marejeo: Pro/Dkt Hassan Asharqawiy, “Al-akhlaaqu Islaamiyya”, Cairo: Taasisi ya Mukhtar ya uchapishaji na usambazaji, mwaka 1988, (ukurasa wa 9-13), pamoja na kutia nyongeza ndogo kutoka kwa mhariri.

Share this:

Related Fatwas