Haki za Binadamu Zinazoambatana na ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Haki za Binadamu Zinazoambatana na Kusudio la Nafsi

Question

 Ni nini haki za binadamu zinazoambatana na makusudio ya kisheria (kusudio la nafsi)?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Haki za binadamu zinazoambatana na kusudio la nafsi ni pamoja na: 1. Haki ya kuishi. 2. Haki ya uhuru. 3. Haki ya usawa. 4. Haki ya uadilifu. 5. Haki ya kujilinda kutokana na matumizi ya nguvu. 6. Haki ya binadamu ya kulinda sifa maalumu. 7. Haki ya kupata makazi na uhuru wa kutembea na kukaa. 8. Haki ya binadamu ya kupata kinachomtosheleza kuhifadhi nafsi na afya yake.
Hapa tutazungumzia katika maudhui hizi mbili:

1. Haki ya kuishi.
2. Haki ya uhuru.
Na baadaye, tutajadili haki za binadamu zilizobaki katika maudhui zinazofuatia.
1. Haki ya kuishi:
Haki ya kuishi ni ya mwanzo katika haki za binadamu, bali ni haki ya asili inayokuja mwanzoni kabisa; maana maisha yakitoweka, haki nyengine hazitakuwa na maana wala faida. Kwa hivyo, haki ya kuishi inakuwa na umuhimu mkubwa zaidi katika Uislamu.

Ikiwa suala la haki ya kuishi lilitajwa kwa muhtasari katika Azimio la haki za binadamu (kila binadamu ana haki ya kuishi, uhuru pamoja na kuilinda heshima yake), basi Uislamu ulitanguliza haki hiyo, ukaifanya kuwa haki yenye utukufu; maana katika Uislamu haijuzu kwa mtu yeyote kuvuka mipaka ya maisha ya mtu mwengine akiwa Mwislamu au asiye Mwislamu, muungwana au mtumwa, mwanamume au mwanamke, mkubwa au mdogo; wote katika Uislamu wana haki sawa ya kuishi. Mwenyezi Mungu Amesema: {Atakayemwua mtu bila ya yeye kuua mtu, au bila ya kufanya ufisadi katika nchi, basi ni kama amewaua watu wote; na mwenye kumwacha mtu hai (kumsaidia kuishi) ni kama amewaacha hai watu wote} [AL MAIDA, 32].

Kuheshimu maisha ya watu katika Uislamu ni haki isiyo na mipaka, ni ya wote, awe mtu huyo ni Mwislamu au si Mwislamu. Naye Mwislamu akivuka mipaka ya maisha ya mwenye ahadi (aliyewekeana mkataba wa usalama wake na Waislamu) hataingia peponi kama alivyosema Mtume S.A.W.: “Yeyote atakaemuua mwenye ahadi na waislamu, hatanusa harufu ya Pepo”.

Hakika haki ya binadamu ya kuishi ni haki inayokuwa na utukufu katika Uislamu, na mtu hanyimwi haki hiyo ila kwa sharti ambazo sheria ya Kiislamu iliziweka pamoja na kanuni zinazopanga utekelezaji wake. Licha ya hayo, Uislamu ulipofaridhisha kisasi, ulimwachia ndugu wa waliouawa kutolipiza kisasi kwa kusamehe, na hiyo ni kwa kuheshimu haki ya binadamu katika maisha.

Ubinadamu una thamani na heshima yake katika Uislamu, na hiyo haihusiani na hali ya binadamu wakati wa uhai wake tu. Bali, haki hiyo ni njia ya kuulinda ubinadamu na hudumu hata wakati wa kifo na baada ya kifo cha mtu; kwani binadamu anapokufa, ni haki ya mwili wake kuheshimiwa na kuhurumiwa, kwa kauli ya Mtume S.A.W.: “Yeyote miongoni mwenu atakaemvika mwenzake sanda, basi anapaswa afanye hivyo vizuri”.

Bali, mtu analazimika kusitiri aibu binafsi za mwenzake, licha ya kusitiri uchi wake usionekane kwa yeyote, vilevile Mtume S.A.W. alikataza kumlaani na kumtukana mfu kwa kusema: “Msiwatukane wafu; kwani wao wameyamaliza waliyoyajia”.

Basi ni haki ya binadamu aliyekufa na kuzikwa aheshimiwe, wala asiaibishwe kwa kutaja aibu na mabaya yake; kwani shani yake sasa iko mikononi mwa Mola wake, licha ya hayo, Uislamu ulikataza tabia ya kuyakojolea na kuyanajisi makaburi.

Uislamu ulitilia umuhimu mkubwa sana na utukufu katika haki ya kuishi, ambapo ulilifanya suala la kuokota mtoto aliyetupwa ni faradhi ya kutoshelezana; yeyote miongoni mwa waislamu, atakaelitekeleza jambo hili, basi wengine wanasamehewa, na wote wakiliacha wanapata dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hatua hii ni kwa ajili ya kulinda haki na heshima ya binadamu.
2. Haki ya uhuru

Haki ya binadamu katika uhuru ni haki yenye utukufu, pindipo haipunguzi haki yake ya kuishi; uhuru katika sheria ya Kiislamu ni sifa asili kwa kila binadamu, anazaliwa nayo na inafungamana naye mpaka kufa kwake; kwani kila mtoto anazaliwa juu ya maumbile ambayo Mwenyezi Mungu Amemwumba nayo.

Hakika uhuru maana yake ni ubinadamu, na ubinadamu unamaanisha uhuru, kwa hiyo yeyote akikosea hali ya uhuru, basi anakosea ubinadamu; kwani maana ya uhuru ni uwezo wa kuchagua kitendo na kuamua kitendo bora katika vitendo vingi licha ya kuwepo hali ya uwiano wa kutoa hukumu. Ubinadamu ambao ni sifa asili ya binadamu kuliko mnyama ni uwezo wa mtu kufikiria na kufanya uwiano katika anayoyafikiria, kisha achague linalostahiki kutekelezwa.

Binadamu asingalikuwa na uwezo huo wa kimaumbile angalikuwa - kwa mujibu wa maumbile asili - katika cheo sawa na mnyama; hawezi kupambanua baina ya madhara na faida au mema na mabaya. Hivyo basi, binadamu anakuwa mfuasi bila ya kufikiri.

Hivyo binadamu peke yake ni mwenye ubinadamu na mwenye uhuru miongoni mwa viumbe hai vyote, ana uhuru wa kufikiria, uhuru wa kutoa rai, uhuru wa kuitikadi, uhuru wa kumiliki na uhuru wa kutendana na wengine. Uhuru huo hauna sharti isipokuwa kujipepusha madhara yeye mwenyewe na wengine wanaoishi naye katika jamii ya kiubinadamu.

Ikiwa uhuru ni sifa asili ya kimaumbile ambayo binadamu aliumbwa nayo, na ikiwa uhuru ni maana ya ubinadamu wa binadamu, na ikiwa uhuru una utukufu huo, basi haijuzu kwa mtu yeyote avuke mipaka ya uhuru wa mtu mwengine. Kwa hiyo, Umr R.A. alisema: “Tangu lini mliwafanyia watu watumwa, ilhali mama zao waliwazalia waungwana”

Ikiwa hivyo, basi inalazimika kuangalia ulinzi kwa uhuru wa binadamu; uhuru hauwezi kunyimwa ila kwa sharti zilizowekwa na sheria ya Kiislamu, ile sheria ambayo kimsingi iliwekwa kwa ajili ya kumletea binadamu manufaa na kumwepushia madhara.

Hakika Uislamu ulitangulia tangazo la kimataifa la haki za binadamu kwa kutunga haki ya uhuru lile tangazo ambalo lilitajwa ndani yake:

“Watu wote walizaliwa waungwana wakati wana usawa wa heshima na haki”, na katika paragrafu ya tatu: “kila binadamu ana haki katika maisha na uhuru”.

Ikiwa Uislamu unamkataza mtu kuvuka mipaka ya uhuru wa mtu mwengine, basi Uislamu katika wakati huo huo haukubali kwa sababu yoyote umati wa watu wavamie uhuru wa wengine au taifa livamie taifa lengine au nchi ivamie nchi nyengine, na ikitokea uvamizi basi mwenye kuvamiwa uhuru ana haki ya kujitetea kujipatia uhuru wake kwa njia na nyenzo zozote, Mwenyezi Mungu Amesema: {Na wale wanaolipiza kisasi baada ya kudhulumiwa, hao hakuna njia ya kulaumiwa} [ASH-SHUURA, 41]. Kadhalika jamii ya kibinadamu inawajibika kumsaidia mwenye kupigana katika njia ya uhuru wake mpaka ajipatie, halikadhalika Waislamu wote wanalazimika kumsaidia mwenye kupigana katika njia ya Uhuru; kwani Waislamu ni umma bora kuliko umma zote wanaamrisha mema na wanakataza maovu, wanaeneza amani, usalama na uhuru duniani zote na hiyo ni lengo kuu na jukumu la juu linalopaswa kuhifadhiwa.

Misingi ya Uhuru katika Uislamu:
Dini ya Uislamu ilitilia umuhimu mkubwa heshima ya binadamu kwa kuwa ni binadamu (asli yake) ikapandisha cheo maadili ya kibinadamu, kumrudishia mtu heshima yake iliyotekwa, kumdhaminia riziki na mambo mema pamoja na kumfadhilisha (kumtukuza) kuliko viumbe wote; Mwenyezi Mungu Ametangaza mafunzo yake katika Quraani Tukufu Akasema: {Na hakika tumewatukuza wanadamu na tumewapa vya kupanda barani na baharini, na tumeruzuku vitu vizuri, na tumewatukuza kuliko wengi katika wale tuliowaumba, kwa utukufu ulio mkubwa kabisa}[BANI ISRAIL, 70]. Mwenyezi Mungu Aliweka misingi inayodhamini hali ya kuondosha mfumo wa utumwa, halikadhalika Alikataa mtu amchukue mwenzake mtumwa kwani hakuna mwabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mmoja Anayestahiki kukusudiwa.

Kadhalika Mwenyezi Mungu Alibatilisha mfumo wa kitabaka kabisa kwa kutangaza kwamba: watu wote ni sawa, haijuzu kumfadhilisha mtu juu ya mtu ila kwa msingi wa ucha-Mungu. Mwenyezi Mungu Amesema: {Enyi watu! Kwa hakika tumekuumbeni (nyote) kwa (yule) mwanamume (mmoja; Adamu) na (yule yule) mwanamke (mmoja; Hawwa)} [AL-HUJURAT, 13], aidha Mwenyezi Mungu Mtukufu Alisema: {Enyi watu! Mcheni Mola wenu ambaye Amekuumbeni katika nafsi (asli) moja. Na Akamuumba mkewe katika nafsi ile ile. Na Akaeneza wanaume wengi na wanawake kutoka katika wawili hao. Na mcheni Mwenyezi Mungu Ambaye kwaye mnaombana. Na (mwatazame) jamaa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mlinzi juu yenu Anayeona kila mnayoyafanya} {AN NISAA, 1}. Hapo, Mwenyezi Mungu Amesisitiza kwamba asli ya wanadamu wote ni moja kwa hiyo hakuna kubaguana kwa misingi ya tabaka wala kubaguana kwa misingi ya kabila.

Uislamu uliondosha ushirikina (shirki) ili kuanzisha upweke wa Mwenyezi Mungu, na uliweka misingi ya uhuru wa kisiasa kwa msimamo wa wastani baina ya ulazimishaji (utenzaji nguvu) na kujuzu kisheria. Basi, nini inayoanzisha misingi hiyo nyoyoni mwa wenye kushika dini mpya?

Bila shaka, kuimarisha misingi hiyo dhamirini sababu yake ni mwenendo wa kimalezi ambao Mtume S.A.W. aliufuata kuokoa Umma kutoka upotovu wake; Mtume S.A.W. alianzia kitendo cha kuokoa akili za watu kutoka kumnyenyekea na kumtukuza asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Hivyo,mwanzo ulikuwa kwa kukomboa imani “akida” na hiyo ni msingi wa uhuru.

Ilimuradi, watu wakishikamana na imani, basi wataweza kutambua kheri na mabaya, mema na madhara, yenye uadilifu na yenye dhuluma wajiepushe na mabaya na dhuluma ambapo Mwenyezi Mungu Aliteremsha ujumbe wa Uislamu kukataza mabaya na kuamrisha mema. Ibn Al Qaiym alisema: “hakika Mwenyezi Mungu alituma Mitume wake na Akateremsha Vitabu vyake ili watu washikamane na uadilifu unaokuwa msingi wa kuumba mbingu na ardhi. Ilhali, zikionekane alama za haki na dalili za uadilifu zikifuatwa, basi sheria ya Mwenyezi Mungu, dini yake, ridhaa yake na amri zake zitatekelezwa”.

Tukirejea hukumu za kisheria, tutagundua lengo linalotakikana nalo ni kuimarisha masilahi ya watu na kueneza uadilifu baina yao; masilahi ya mtu na jamii inakuwa na mambo tatu;
1. Mambo ya dharura (ulazima) ambayo maisha ya mtu na jamii haiendi ila kwa kuyapatikana yale mambo
2. Mambo ya haja ambayo maisha ya watu yanayahitaji kuelekea vizuri
3. Mambo ya ziada ambayo yanasaidia kukamilisha mfumo wa maisha.
Sheria ya Kiislamu ilidhamini mambo hayo tatu kila aina kwa hukumu mbili; hukumu zinazoyaanzisha na hukumu zinazoyahifadhi na kwa hayo masilahi ya watu inaenda.
Dini: ni jambo la dharura maishani na sheria ya Kiislamu ilitunga hukumu za imani, itikadi na ibada kusimamia dini na hukumu za jihadi, ulinganio ziliwekwa kuihifadhi na kuilinda dini.
Kizazi: ni jambo la dharura maishani na hukumu za ndoa ziliundwa ili kizazi kipatikane. Kadhalika, adhabu za kuua nafsi na kuharamisha kuiangushia maangamizo, maudhi au madhara ziliwekwa ili kuilinda nafsi na kuitetea.

Mali: ni jambo la dharura maishani na sheria ya Kiislamu ilitunga hukumu za matendeano ya fedha na njia za kupata na kuchuma mali kama ilivyoweka adhabu ya kuiba na kuvamia mali au kuharibu mali za watu ili kulinda na kuhifadhi mali. Hivyo, tunaona kwamba kila linalikuwa dharura kwa mtu na umma, basi sheria ya Kiislamu ilitunga hukumu ili lipatikane pamoja na hukumu zinazoweza kulilinda na kulisaidia kudumu.

Uislamu kama ulivyodhamini mambo ya dharura, halikadhalika ulidhamini mambo ya haja nay a ziada kwa kutunga aina nyingi za hukumu za kutendeana pamoja na kuwasamehe wenye jukumu kisheria kutotekeleza wakiwa na shida licha ya kuhalalisha yaliyoharamishwa kisheria wakati wa dharura au haja na kuweka adabu za kutendeana na hukumu za twahara; hivyo Mwenyezi Mungu hakutunga hukumu ila kwa kudhamini mambo ya dharura kwa watu au kuwaepushia madhara au kuwakamilishia maisha yao na hiyo ndiyo elementi za masilahi yao.

Falsafa ya uhuru katika Uislamu
Inajulikana kwamba uhuru katika fiqhi ya kisheria unamaanisha uwezo wa binadamu wa kufanya kitendo cho chote kisichodhuru wengine.

Uhuru unafuata kanuni zitolewazo na utawala ambapo zinaweza kuupanga na kuuainisha.
Tukiangalia fiqhi ya Kiislamu, tutakuta kwamba wajibu za kisheria zilizokuwepo katika hukumu za kisheria zinarejea jambo la kuhifadhi makusudio yake katika viumbe, pia kusudio kuu la Mtoaji wa sheria katika suala la kutunga hukumu ni kuhakikisha masilahi ya watu.

Hivyo, hukumu za kisheria na hekima za utungaji wa sheria na sababu katika milango (sehemu) tofauti zinabainisha kwamba Mtoaji wa sheria ya Kiislamu Anakusudia kwa kutunga hukumu kuhifadhi mambo ya dharura na haja za watu pamoja na mambo ya ziada na hayo yote yanaambatana na suala la masilahi ya watu.

Hekima ya Mwenye kuumba inalazimisha kila binadamu awe na uhuru; kwani kukosea uhuru wake kunaathiri maana ya ibada ambayo Mwenyezi Mungu Ametuumba kwa ajili yake, kadhalika haiafikiani na maana ya wajibu za kisheria ambazo tuliamrishwa kuzitekeleza.

Kwa hiyo, binadamu alifanyiwa mitihani, Mwenyezi Mungu Amesema: {Na tunakufanyieni mitihani kwa (mambo ya) shari na ya kheri} [AL-ANBIYAA, 35], aidha Mwenyezi Mungu Amesema: {Kukufanyieni mtihani; ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri} [AL-MULK, 2].
Naye Mtume S.A.W. alisema: “Pepo inazungukwa zaidi kwa machukizo, na Moto inazungukwa zaidi kwa matamanio”.

Hekima ya kutoa sheria inalenga kudhamini makusudio ya kisheria pamoja na uwiano baina ya hukumu za matamanio na hukumu ya akili; uwiano baina ya uhuru wa mtu (ambao unalazimika kupatikana) na haki ya jamii (ambayo ni lazima kuitekeleza).

Uislamu uliweka msingi wazi unaosaidia kueneza hali ya saada, amani na raha kwa watu wote, nao msingi unaotokana na maneno ya Mtume S.A.W.: “Hakuna madhara na hakuna hasara”.

Maulamaa wa misingi ya dini walisema kwamba haki ya mtu binafsi inakwenda sambamba na haki ya Mwenyezi Mungu ambayo inalazimisha kulinda haki za mwengine akiwa mtu au jamaa na suala la kulinda haki za wengine hauhusiki tu na kujizuia kuvuka mipaka bali unahusika kutotumia haki hiyo ikiwa inaweza kuleta madhara.

Binadamu akilitenda jambo linalohakikisha makusudio ya kisheria na linafanikisha masilahi na kuepusha madhara, basi hilo linaingia katika haki zake, naye ana uhuru uliokamilika katika kulitenda.
Hivyo, nadharia ya uhuru katika Uislamu inategemea kumtolea mtu uhuru wa kufanya alitakalo, sharti lisigongane na haki ya mwengine, kheri au masilahi ya wote; maana hayo yanakuwa mipaka ambayo ikivukwa, basi uhuru unakuwa uvamizi ambao ni wajibu kunyimwa na kuondolewa.

Hiyo ndiyo falsafa ya uhuru katika Uislamu; kila linalokuwa na kheri na masilahi ya wote, basi ni mubaha, na kila linalovuka mipaka na kukaribia mambo ya shari na madhara linakuwa linakatazwa na kunyimwa na sharti.

Utungaji wa sheria wa kiujumla ulibainisha hivyo kama ilivyotajwa katika Hadithi ya Mtume S.A.W. “Hakuna madhara, hakuna hasara”, kisha fiqhi ya kiislamu ilibainisha chini ya maudhui ya makusudio ya kisheria na uhusiano wake na masilahi ya wote katika suala la kutekeleza wajibu.
Rejea: Sehemu ya Tafiti za Kisheria katika Idara ya Fatwa ya Kimisri

Share this:

Related Fatwas