Usamehevu – ni katika Maadili ya Kiislamu.
Question
Ni ipi nafasi ya Usamehevu katika mfumo wa maadili mema ya Kiislamu?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
Quraani tukufu inaonesha upweke wa chimbuko la binadamu kwa sura mbali mbali, na aina tofauti za uelezaji wake. Na sura ya kwanza kabisa iliyotajwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kitabu chake kitukufu cha Quraani, ni kisa cha kuumbwa kwa Adamu baba wa wanadamu na asili ya utu, nacho ni kisa kimoja pekee kilichozungumziwa na madhehebu pamoja na sheria zingine juu ya asili ya mwanadamu na upweke wa chimbuko lake. Na kuhusu kisa hichi, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na pale Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa, wakasema: Utaweka humo atakayefanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutakasa kwa sifa zako na tunakutaja kwa utakatifu wako? Akasema: Hakika Mimi nayajua msiyo yajua. Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote, kisha akaviweka mbele ya Malaika, na akasema: Niambieni majina ya hivi ikiwa mnasema kweli. Wakasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hatuna ujuzi isipokuwa kwa uliyo tufunza Wewe. Hakika Wewe ndiye Mjuzi Mwenye hikima. Akasema: Ewe Adam! Waambie majina yake. Basi alipowaambia majina yake alisema: Sikukwambieni kwamba Mimi ninajua siri za mbinguni na za duniani, na ninayajua mnayo yadhihirisha na mliyo kuwa mnayaficha?} [AL BAQARAH: 30-33].
Kwa hivyo basi, watu wote wanatokana na ukoo mmoja wa baba mmoja, na wote ni warithi wa ukhalifa wa kuijenga Dunia hii na kueneza Usalama na Amani.
Na kwamba umwagaji damu na ufisadi Duniani ni njia mbaya asiyoipenda Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa watu wote wenye dini tofauti tofauti.
Na kwa ajili hiyo, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote. Na hakika waliwajia Mitume wetu na hoja zilizo wazi. Kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika nchi}. [AL MAIDAH: 32]
Na anasema Mwenyezi Mungu: {Walio kufuru miongoni mwa watu wa Kitabu na washirikina hawapendi mteremshiwe kheri yoyote kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Na Mwenyezi Mungu humkusudia kumpa rehema yake ampendaye. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kubwa}. [AL BAQARAH: 105]
Na Quraani tukufu imeweka misingi ya wazi kwa familia ya binadamu, na Uislamu umetangaza kuwa watu wote wameumbwa kutokana na nafsi moja, jambo ambalo linamaanisha kuwapo asili moja ya tu binadamu.
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaomba, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni}. [AN NISAA: 1]
Na kwa mtazamo wa Uislamu, watu wote ni watoto wa hiyo famailia moja ya binadamu, na kwamba wote wana haki ya kuishi na kuheshimika bila ya kutengwa au kubaguliwa.
Kwa hivyo mwanadamu anahishimika kwa mtazamo wa Quraani tukufu, bila ya kuangalia dini yake, rangi yake au hata umbile lake. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba}. (Alisraa: 70)
Na haikuwa tofauti ya watu kwa rangi, maumbile, lugha na dini zao, isipokuwa ni ishara miongoni mwa ishara za Mwenyezi Mungu zinazoonesha Uwezo mkubwa wa muumba aliyetukuka: anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na kutafautiana ndimi zenu na rangi zenu. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa wajuzi}. (Aruum: 22)
Na tofauti hii kati ya wanadamu haiwezi kuwa sababu ya kuchukiana na kufanyiana uadui, bali inapaswa iwe ni sababu ya kujuana na kukutana kwa mambo ya kheri na masilahi ya pamoja, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliyemchamungu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari}. (Alhujuraat: 13)
Na kipimo cha ubora kati ya mtu na mwingine mbele ya Mwenyezi Mungu, kimewekwa na Quraani tukufu ambacho ni yale ayafanyayo mwanadamu huyu miongoni mwa mambo mazuri kwa kuwafanyia watu wote pamoja na kumuamini Mwenyezi Mungu ukweli wa kuamini. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliyemchamungu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari}. (Alhujuraat: 13)
Na wala Quraani haijawaangalia wasio kuwa waislamu kwa mtazamo wa kuwadunisha bali imewaangalia kwa mtazamo wa kuwapa cheo cha juu hata kama watatofautiana na sisi. Mwenyezi Mungu wetu hakutuamrisha tuwauwe wale wasiofuata dini yetu, bali anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliyemchamungu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari}. (Alhujuraat: 13)
Amesema Ibnu Kathiir katika tafsiri ya Aya hii: kwamba ina maana msimlazimishe mtu yeyote kuingia katika Dini ya Uislamu. Hakika Mwenyezi Mungu amebaini wazi wazi na kuonesha dalili zinazoonekana juu ya jambo hili kwamba halazimishwi mtu kuingia katika Dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Na sababu ya kuteremshwa kwa Aya hii ni kama wanachuoni wa Tafsiri walivyoweka wazi upande wa utukufu wa Dini hii, ambapo Dini ya Kiislamu haikuwaruhusu waislamu wawachukue watoto wao waliowaingiza katika Uyahudi wakiwa wadogo. Imepokelewa kutoka kwa Ibnu Abas kuwa amesema: Mwanamke aliyekuwa na kizazi kidogo alikuwa anajiwekea yeye mwenyewe kuwa mtoto wake akiwa mkubwa basi atamyahudisha, na pale Banuu Nudhwair walikuwa ndani yao wana watoto wa wakristo, baba zao wakasema: hatuwaachi watoto wetu, ndipo Mwenyezi Mungu alipoteremsha Aya hii: {Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anayemkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisicho vunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua}. (Albaqarah: 256)
Ama kwa upande wa msingi uliowekwa na Quraani tukufu katika kutendeana na wasio waislamu, unapatikana katika tamko lake Mwenyezi Mungu: {Mwenyezi Mungu hakukatazeni kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu}. (Almumtahina: 8)
Kwa hivyo Aya hii iko wazi kwamba sisi Waislamu pale tunapoona kuwa mtu asie mwislamu hataki kuingia katika Uislamu basi tunapaswa kuwa nae karibu, kumfanyia uadilifu, na kutangamana nae vizuri kwa msingi wa kuheshimiana na uhusiano mzuri pamoja na kuyalinda masilahi yetu ya pamoja.
Na kwa ajili ya kuuelewa uhusiano kati ya mwislamu na asiye mwislamu, wanachuoni wa Kiislamu wamesema: si vibaya kwa mwislamu kuunga undugu wake na mtu awe mshirikina – kwa maana kati yake na mtu huyu kuna undugu – au asiye na undugu, awe ni adui au dhimii (mwenye mkataba wa ulinzi na waislamu), kwa Hadithi ya Salamatu Bin Alakwaa amesema: niliswali swala ya asubuhi nikiwa na Mtume S.A.W, nikakuta akiligusa bega langu kwa kiganja chake cha mkono, na mimi nikageuka nyuma, na Mtume akasema: ((je wewe unataka kunipa mtoto wa kike au mama Qirfa?)) nikasema: ndio. Basi nikampa, nae akamtuma kwa mjomba wake ambaye ni Haznu bin Abii Wahab, ambae ni mshirikina na yeye pia ni mshirikina. Kwa hivyo basi, Uislamu ni dini inayokwenda na uhalisia na huongoza kuyaelekea yaliyo bora katika maadili, na kwa kupitia mtazamo tulivu wa uhalisia, tunagundua kuwa wanafikra wa kimataifa na waleta marekebisho, hivi sasa wanawatolea wito watu wote Duniani waishi pamoja na kuleta amani kamili yenye uadilifu na mazingira mazuri wanayoishi ndani yake watu wote.
Hakika kila mtu anaeuchunguza urithi wa ustaarabu wa kiislamu kwa kuangalia historia yake iliyoangaza na yenye heshima, na akawa mtu huyo na sifa ya uuwiano na ukweli, itaonekana wazi kuwa Dini ya Kiislamu ni Dini ya Huruma na Usamehevu kwa maana na viwango vyake vya juu. Kwani Usamehevu wa Kiislamu ni matunda ya Imani, na dalili yake yenye nguvu juu ya kuyapa nyongo mabaki ya Dunia inayoteketea, na utashi wa kujisogeza kwa Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote.
Aya za Quraani tukufu ni katiba ya Usamehevu unaotakiwa:
Hapana shaka kwamba Uislamu uko wazi zaidi miongoni mwa Dini, katika kulingania Usamehevu, tena kwa juhudi ndogo tu maana yake huwa wazi, na sisi tunataka kutoa ushahidi wa Aya za Quraani ambazo zinalingania Usamehevu, na zinatangaza kwa upeo wa uwazi kuwa Dini ya Uislamu ni Dini ya Usamehevu.
Kwanza: Aya za Usamehevu zinazomuhusu Mtume S.A.W, aliye mbora wa viumbe:
Mtume Muhammad ni alama ya Umma huu wa Kiislamu, naye ni mfano wa pekee wa kuigwa ambae kila mwislamu anajitahidi kufanana nae, iwe wazi au hata kwa undani wake; na kwa ajili hii, tutaonesha Aya hizo ambazo zimetendeana na mbora wa waislamu, na kiongozi wao, Mtume mteule, na ya kwanza miongoni mwa aya hizi ni tamko lake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote}. [AL ANBIYAA: 107]
Na kutoka kwa Ibnu Abas akichambua kauli hii ya Mwenyezi Mungu, alisema kuwa: atakaemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho ataandikiwa huruma Duniani na Akhera, na asiyemwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ataepushwa na yale yaliyowapa umma zilizopita miongoni mwa majanga kama kuondoshewa nuru na kutupwa tupwa.
Na ikiwa watu wasio waislamu ambao hawaiamini Quraani lakini wanaamini kuwa sisi tunasema kweli kwa Quraani tukufu, wanaamini pia sisi sote tunakubaliana kuwa Aya hii iko kwenye kitabu chetu kitukufu, kwa hivyo wanalazimika kuamini vile vile kuwa sisi tunatangamana na Dunia hii kwa msingi wa Aya hii na kwa Urithi wa Huruma ya Mtume Muhammad, na sisi tunakuwa ndio warithi wa Mtume wetu Mtukufu katika maadili yake yote na ambayo yanaongozwa na Huruma.
Hata kama Quraani isingekuwa na Aya nyingine yeyote inayozungumzia Usamehevu ispokuwa Aya hii moja tu, basi ingelitosha, lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu amethibitisha maana hii tukufu kwa zaidi ya Aya moja, kama vile tamko lake aliposema: {Au waliweza kupitisha amri yao? Bali ni Sisi ndio tunao pitisha}. [AZ ZUKHRUF: 89]
Na Mwanachuoni mkubwa wa kiislamu, Imamu Twabriy ametaja ufafanuzi wa aya hii akiyasema yale aliyoyasema Mwenyezi Mungu kwa Mtume Muhammad kama ni jibu lake kutokana na dua aliyoiomba. Na usemi wake (Mtume) ni: {Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hawa ni watu wasio amini.} [AZ ZUKHRUF: 88]
{Na uwasamehe ewe Muhammad na uachane na maudhi yao na kisha uwaambie: Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yenu}. Na kuondosha neno Salamu kwa kutumia neno "alaikum au lakum"
Na aya hii ni Maneno yanatoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu akimwambia Mtume wake na wafuasi wote wa Mtume katika zama zote. Mwenyezi Mungu amemuamrisha Mtume asamehe na kupuuza, na jambo hili linakusanya kutazwa kulipiza kisasi au kulichukulia kila jambo, na Mwenyezi Mungu Mtukufu amelinganisha Usamehevu na Amani kwa tamko lake: Salaamu (Amani). Na amani ni matumaini yanayolinganiwa ambayo waislamu wanayohangaikia katika historia yao yote na pia katika historia yao mpya kuna juhudi za kweli ambazo haziwakilishwi na madai ya baadhi ya watu wadanganyifu. Na Mwenyezi Mungu anayajua yote yaliyomo ndani ya nyoyo za watu wote.
Ingawa Mwenyezi Mungu Mtukufu amemwamrisha Mtume kuwa msamehevu kwa amri ya wazi katika Aya iliyopita, isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ametaka kulisisitizia jambo hili na kuongeza uzuri wake, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ila kwa ajili ya Haki. Na hakika Kiyama kitafika.Basi samehe msamaha mzuri}. [ALHIJR: 85]
Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu amebainisha kuwa Usamehevu unaokusudiwa hapa sio ule usio na mipaka bali ni maalumu ambao ni wa jambo jema, usamehevu ambao ndani yake una uzuri na ukarimu. Anasema Twabriy katika tafsiri yake: ya maneno Usamehevu Mzuri: anasema: epukana nao vizuri na uwasamehe usamehevu mwema. Na vile vile, Mtume alikuwa akifuata maamrisho ya Mola wake katika jambo lake lote na wala hakuwa akizusha kamwe.
Na mtu ambae hakumfuata Mtume wetu Mtukufu katika Dini yake baada ya kupewa Utume basi atanasibika na Umma wa Mtume kwa kuzingatiwa kuwa ni Umma wa Ulinganio wa Mtume. Umma ambao ameulinda Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ujumla – wafuasi na wasio kuwa wafuasi – kwa kuwapo miongoni mwa wafuasi. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na Mwenyezi Mungu hakuwa wa kuwaadhibu nawe umo pamoja nao, wala Mwenyezi Mungu si wa kuwaadhibu na hali ya kuwa wanaomba msamaha}. [AL ANFAAL: 33]
Na katika Aya za Usamehevu wa Kiislamu unaohusika na Mtume Mtukufu, ni kauli yake Mwenyezi Mungu aliyetukuka, anasema: {Shikamana na kusamehe, na amrisha mema, na jitenge na majaahili}. [ALARAAF: 199]
Kwa hivyo Mwenyezi Mungu amemuamrisha Mtume wake kusamehe, na kukubali kilichochepesi kutoka kwa watu, na wala asiwafanyie ugumu juu yao. Na Mwenyezi Mungu akamuamrisha kuwapuuza wajinga na kutowachukulia wayafanyayo, kama ni hakikisho juu ya maana ya Usamehevu na Upole, na Huu ni mwelekeo wa Umma wa Kiislamu kwa ujumla na katika zama zao zote.
Na Maadili yanayolinganiwa hayawezi kuwa mwenendo kwa kuamrisha na kukataza tu, bali kwa vitendo na kazi, na kwa ajili hii, wamesema wahenga: Kati ya Mtu mmoja kwa watu elfu moja ni bora zaidi kuliko kauli ya watu elfu moja kwa mtu mmoja. Na Mwenyezi Mungu aliyetukuka kwa utukufu wake na uwezo wake wa hali ya juu ametuchukulia sisi kwa upole, usamehevu na kutufutia makosa yetu.
Na katika mwelekeo huu wa uungu wake, Mwenyezi Mungu aliyetukuka anamuamrisha kipenzi cha viumbe wake awafanyie hivyo maswahaba wake, basi akasema Mola: {Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungelikuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangelikukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. Na ukisha kata shauri basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaomtegemea}. [AALI IMRAAN: 159]
Baada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kumwambia Mtume wake sala na salamu zimwendee, kuwa awabainishie wafuasi wake, akamwamrisha yeye awe laini kwao na awasamehe. Basi Mtume akawa mpole na mpole zaidi, na mwenye upole juu ya upole. Na haya yote yamefanyika ili awafundishe maswahaba zake huruma, ulaini na upole. Maana aliyoitaka Mwenyezi Mungu ikawa inatembea ardhini, na akawafundisha walimwengu wote huruma na usamehevu.
Na amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu haikuishia kwa kipenzi na chaguo lake kuwahurumia na kuwasamehe maswahaba tu, bali Mwenyezi Mungu alimwamrisha aufuate mwenendo huo huo katika kuwahurumia mayahudi. Mtu anaeiangalia Aya hii, anaweza kushangazwa, kwani amri ya kuwa na huruma na usamehevu ilifuatiwa na utajo wa baadhi ya makosa ya uhalifu wa mayahudi hao, na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Basi kwa sababu ya kuvunja agano lao tuliwalaani, na tukazifanya nyoyo zao kuwa ngumu. Wanayabadilisha maneno kutoka pahala pake, na wamesahau sehemu ya yale waliyo kumbushwa. Na huachi kuvumbua khiana kutokana nao, isipokuwa wachache miongoni mwao. Basi wasamehe na waache. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema}. [AL MAIDAH: 13]
Ni kama vile Mwenyezi Mungu Mtukufu anataka kumwambia Mtume wake: hata kama na wao wanatengua ahadi yao na Mola wao, na wanavuruga maneno ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya masilahi yao ya kidunia, usiwatendee kwa matendo yao, bali wasamehe makosa yao na usiwachukulie, ili uwafundishe walimwengu usafi wa maadili mema na mazuri ya tabia njema, na si vinginevyo, Mtume alikuwa na tabia njema za hali ya juu.
Bali Mwenyezi Mungu alimuamrisha Mtume wake wazi wazi afanye jema anapofanyiwa ovu, akasema: {Mema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa liliojema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye panauadui atakuwa kama rafiki jamaa wa kukuonea uchungu}. [FUSWILAT: 34]
Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu akamfundisha Mtume wake namna ya faida za usamehevu zinavyokuwa. Na usamehevu na Msukumo wa lile lililo bora zaidi ni miongoni mwa amani ya kijamii, mpaka adui atakapogeuka na kuwa kama mzazi/liwali mpole, na ni uzuri ulioje wa picha ambayo Uislamu umeihangaikia, kuitolea wito katika mfumo wake wa kinadharia,waislamu wakautekeleza kupitia historia yao ng'avu.
Na zifuatazo ni Aya za Quraani Tukufu zinazouzungumzia Usamehevu wa Kiislamu na ambao haujahusika na Mtume tu bali Umma wote wa Kiislamu.
Pili: Aya za Quraani ambazo zinawatolea wito Waislamu wawe wasamehevu:
Maelekezo ya Quraani Tukufu kwa Umma wa Kiislamu juu ya Usamehevu yako wazi. Si tu baina ya wanajamii ya Kiislamu peke yao, bali hata kwa wale wanaowafanyia maudhi miongoni mwa Makafiri; ambapo Mwenyezi Mungu amewaamrisha Waumini wawasamehe wale wasiokuwa waislamu, kama ni jibu la maudhi wanayokumbana nayo. Na kiwango hichi cha juu cha maadili hakina mfano wake katika mataifa yote ya mwanadamu.
Na mtu anaweza kusema: wao walikuwa wakisameheana na wale waliokuwa wakiwaudhi kwa sababu hawakuwa na uwezo au nguvu. Jibu lake ni kuwa: kama jambo hili lingekuwa ni kwa sababu ya unyonge basi Mwenyezi Mungu angeliwaambia: vumilieni hadi mtakapokuwa na uwezo na kisha mlipize kisasi, lakini aliwaambia: wawasamehe na waachilie mbali, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Waambie walio amini wawasamehe wale wasio zitaraji siku za Mwenyezi Mungu, ili awalipe kwa waliyo kuwa wakiyachuma}. [ALJAATHIAH: 14]
Na Quraani tukufu inasisitizia juu ya msukumo wa kutenda jambo zuri zaidi na faida zake, na kuwa kwake pamoja na wale wanaotaka kuwafitinisha waumini na Dini yao, akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {wengi miongoni mwa watu wa kitabu wanatamani lau wangekurudisheni nyinyi muwe makafiri baada ya kuamini kwenu kwa ajili ya uhasidi uliomo ndani ya nafsi zao, baada ya kwisha wapambanukia Haki. Basi wasamehe na uwaachilie mbali mpaka Mwenyezi Mungu atakapoleta amri yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu}. [AL BAQARAH: 109]
Kwa hivyo mweleweko huu unazitahadharisha akili, baada ya Mwenyezi Mungu aliyetukuka kuzungumza yale wanayoyakusudia watu wa Kitabu, miongoni mwa hisia za chuki na husuda, anawaamrisha waislamu wasamehe na watupilie mbali, na anawataka wangojee amri ya Mwenyezi Mungu na wala wasilipize kisasi kwa ajili yao.
Na Mwenyezi Mungu amewasifu waumini ambao wanaulinda utiifu wao kwa Mwenyezi Mungu, na wanapoangukia katika Maasi wanarejea haraka. Na akawasifu pia kuwa wao wanasamehe wanapokasirika, akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na wanayoyaepuka madhambi makubwa na mambo machafu, na wanapokasirika wao husamehe} [ASHURAH: 37]
Na akawasifu Mwenyezi Mungu wavumilivu wa maudhi na waachao kulipiza kisasi kwa ajili yao, kwa tamko ambalo linahimiza kuuvutia usamehevu na kuachilia mbali, akasema Mwenyeizi Mungu Mtukufu: {Na anaye subiri, na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa}. [ASHURAH: 43]
Vile vile, Mwenyezi Mungu amewasifia waumini ambao wanasifa za kuwa na mambo mazuri, kama kutoa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kujizuia na hasira, na kuwasamehe watu wote, na akasema aliyetukuka: {Ambao hutoa wanapokuwa na wasaa na wanapokuwa na dhiki, na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema}; [AALI IMRAAN: 134]
Njia zinazolingania usamehevu ziko nyingi katika Quraani tukufu, wakati mwingine huwa zinakuja kwa njia ya amrisho, na wakati mwingine huja kwa tamko la kumsifu msamehevu, hadi mwenyezi Mungu awatendee hivyo hivyo. Anasema Mwenyezi Mungu: {Watadumu humo milele. Hakika kwa Mwenyezi Mungu yapo malipo makubwa}. [ATAUBAH: 22]
Kisha Mwenyezi Mungu aliyetukuka anasisitizia maana hiyo hiyo ya kwamba malipo ya usamehevu ni kusamehewa, na malipo ya wema ni wema, hata kama maana ya Aya hii itakuwa katika tamko shurutishi, anasema Mwenyezi Mungu: {Enyi mlio amini! Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto wenu wamo maadui zenu. Basi tahadharini nao. Namkisamehe, na mkapuuza, na mkaghufiria basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu}. [ATAGHABUN: 14]
Na Quraani inaendelea kubainisha kuwa maadili mema ni kuachia mbali na usamehevu. Mwenyezi Mungu Mtukufu amebainisha kuwa hakuna anaeyajua malipo ya usamehevu isipokuwa Mwenyezi Mungu Mwenyewe, jambo ambalo linamaanisha uwepo wa thawabu nyingi kama vile katika swaumu, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo. Lakini mwenye kusamehe, na akasuluhisha, basi huyo malipo yake yapo kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye hawapendi wenye kudhulumu}. [ASHURAH: 40]
Na tunamalizia kutoa ushahidi huu wa Quraani tukufu, kwa ulinganiaji wake juu ya Usamehevu hadi katika maeneo ya vita, ambapo, Mwenyezi Mungu anatoa kwa mwenye kufiwa na ndugu yake kwa kuuawa amsamehe muuaji: {Enyi mlioamini! Mmepewa ruhusa kulipa kisasi katika waliouwawa -muungwana kwa muungwana, na mtumwa kwa mtumwa, na mwanamke kwa mwanamke. Na anayesamehewa na ndugu yake chochote basi ashikwe kulipa kwa wema, na yeye alipe kwa ihsani. Huko ni kupunguziwa kuliko tokana na Mola wenu Mlezi, na ni rehema. Na atakayevuka mipaka baada ya haya, basi yeye atapata adhabu chungu}. [AL BAQARAH: 178]
Kwa hivyo Mlezi wa Walimwengu, amebainisha kuwa maadili haya ni kutuoshea uzito kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na ni rehma kutoka kwake pia. Na ni wajibu kwa waja wake Mwenyezi Mungu Mtukufu, walioamini, wajipambe kwa maadili haya mazuri yatokayo kwa Mola wao, na wawe na tabia njema zitokazo kwa Mola wao.
Na yafuatayo ni kuzizungumzia Hadithi za Mtume aliyezileta, yeye ni mbora wa viumbe, rehma na amani zilivyokamilika zimfikie.
Usamehevu katika Sunna ya Mtume S.A.W. inapelekea Maadili mema:
Mtume alisema kuwa Mola wake Mtukufu alimtuma aje kukamilisha maadili mema, na kuyatimiza mazuri yake, na maana hii haikuchimbuliwa kutoka katika Hadithi za Mtume kwa kiasi cha kuwa kwake wazi katika Maneno yake, Kutoka kwa Abuu Huraira amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema (Hakika mimi nimetumwa nije kukamilisha maadili mema)
Mwandishi mwenye kitabu cha Faidh-AlQadiir anasema: amesema Al-hakiim: kuwa Mtume ametuambia kuwa Mitume walipita na maadili haya yakiwa bado hayajakamilika, kwa hivyo Mwenyezi Mungu akamleta Mtume Muhammad ili akamilishe yaliyobakia juu ya walimwengu. Na baadhi yao wanasema: ameashiria kuwa Manabii –rehema na amani ziwafikie– waliokuja kabla ya Mtume, walitumwa waje na maadili mema na yakabakia yaliyobakia miongoni mwa yale waliyokuwa nayo na kwa ukamilifu wake.
Na Mtume wetu chaguo la Mwenyezi Mungu, ametuambia kuwa Umma wetu wote umetumwa na Mola wake, na kwamba Mwenyezi Mungu ameutuma Umma huu ili kuwarahisishia waja wake, na wala si kwa lengo la kuwatilia ugumu. Kutoka kwa Abuu Huraira amesema: Mwarabu mmoja alikojoa msikitini, na watu wakataka kumuadhibu, Mtume S.A.W akaawaambie: "mwacheni na mmwagie ndoo ya maji pale alipokojolea, kwani mimi nimetumwa kuja kuwarahishieni na wala sikutumwa kuja kuwatilieni ugumu"
Na kuhusu suala la Usamehevu na kusamehe, vitabu vya Sunna vimejaa Hadithi za Mtume zinazolingania Usamehevu na kusamehe, kwa hivyo Mtume akauongoza Umma wake uwe na tabia ya Usamehevu katika mitangamano yao yote, iwe mitangamano hiyo na Waislamu au na wasiokuwa Waislamu.
Kutoka kwa Jaabir Bin Abdillah –Radhi za Mwenyezi Mungu ziwafikie wote wawili– kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Mwenyezi Mungu humrehemu mja msamehevu anapouza, anaponunua au anapouza au anapotoa hukumu". Na ushahidi mwingine wa Haidthi hii, ni Hadithi iliyopokelewa na Bwana wetu Othman Bin Afaan, R.A, aliposema; Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, amesema: "Mwenyezi Mungu amemuingiza mtu mmoja peponi alikuwa mtenda mepesi, akinunua na kuuza".
Na Nabii Muhammad anaweka wazi akisema: Dini ya Kiislamu ni ya Usamehevu, ni nyepesi na ni rahisi. Na kutoka kwa Ibnu Abass R.A: Mtume aliulizwa: ni dini gani aipendayo zaidi Mwenyezi Mungu kuliko zote? Akasema: "Ni Dini yenye Usafi na yenye Usamehevu"
Na Imamu Shafi alitohoa kutoka katika Hadithi ya Mtume, Msingi ufuatao: Tabu huleta wepesi, na kwamba jambo linapobanwa sana basi hupanuka.
Na Mtume wetu mkarimu alimwamrisha Mwislamu asamehe na asameheane na wengine ili Mwenyezi Mungu amsamehe yeye. Kutoka kwa Ibnu Abass amesema: Mtume S.A.W, amesema: "kuwa msamehevu nawe utasamehewa"
Vile vile Mtume amebainisha kwamba iwapo usamehevu utatoweka miongoni mwa waislamu basi umauti kwao ni bora kuliko maisha, na iwapo usamehevu utaenea kati yao, basi maisha kwao ni bora kuliko umauti, na tunaweza kusema kuwa Mtume S.A.W, ameweka mwongozo wa kufanya marekebisho ya ndani katika nchi ya kiislamu, kabla hawajatoa wito wasiojua usamehevu na kusameheana na wengine na wanahangaikia uenezaji wa ufisadi duniani, ukweli ni kwamba wito wao wanautoa kama ni kisingizio cha kuiangamiza nchi na wananchi wake na Mwenyezi Mungu haupendi ufisadi.
Kutoka kwa Abuu Huraira, amesema: Mtume S.A.W, amesema:
"watakapokuwa maamiri wenu ni chaguo lenu, na matajiri wenu ni wasamehevu wenu, na mambo yenu ni kwa kushauriana kati yenu, basi mgongo wa Dunia ni bora kwenu kuliko tumbo lake. Na iwapo viongozi wenu watakuwa ndio washari wenu, na matajiri wenu ndio mabakhili wenu, na mambo yenu mkawaachia wanawake wayasimamie, basi tumbo la ardhi ni bora kwenu kuliko mgongo wake"
Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakuishia tu katika kuulingania Umma wake juu ya Usamehevu, kwa kuwaongoza kwa maneno, bali aliwatolea mifano bora ya Usamehevu na Upole, ili awafundishe maswahaba wake na Waumini watakaokuja baadae pamoja na ulimwengu kwa ujumla, vipi Mtu anaweza kumsamehe Mwenzake. Kutoka wa Anasi Bin Malik amesema: nilikuwa natembea pamoja na Mtume S.A.W akiwa na nguo nzito ya baridi ya kutoka Najraaniy, mwarabu mmoja akamkaribia na kumvuta kwa nguvu, mpaka nikaona shingo ya Mtume kuna athari ya nguo ile nzito kutokana na kuvutwa kwa nguvu, kisha akasema Mtu yule: Nisaidie mali ulionayo. Nikamgeukia Mtume, akacheka kisha akaamrisha yule mtu apewe chochote.
Amesema Imamu Anawawiy baada ya kutajwa Hadithi hii: "Ndani yake kuna uwezekano wa wajinga, na kukwepa kukutana nao, na kuondosha baya kwa zuri, na kutoa kwa yule mwenye moyo mkunjufu, na kumsamehe mwenye kufanya dhambi kubwa isiyokuwa na adhabu maalumu kutokana na ujinga wake, na kuhalalisha kucheka, kisha mambo ambayo anayapenda katika mazoea, na ndani yake kuna ukamilifu wa maadili ya Mtume wa Mwenyezi Mungu na upole wake pamoja na usamehevu wake mzuri."
Na kutoka kwa Aisha R.A.: amesema: je imewahi kukujia ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, imewahi kukujia siku nzito kuliko siku ya UHUD? Akasema: "Nimekutana na watu wako, na kizito nilichokabiliana nacho kutoka kwao ni siku ya AQABA ; pindi nilipojionesha mimi mwenyewe mbele ya Abdiylail Bin Kulaal na hakunipa jibu ya nilichokitaka, nikaondoka huku nikiwa na hali ngumu usoni mwangu, na sijazinduka ila nilipokuwa katika eneo la Qarnu Athaalibu, nikainua kichwa changu, nikajikuta nikiwa katika uwingu ulioniwekea kivuli, kisha nikaangalia na kumuona Jiburilu ndani ya uwingu huo, akaniita na kusema: hakika Mwenyezi Mungu amesikia kauli ya watu wako waliyoisema na wala hawakukujibu, na umetumiwa mfalme wa majabali ili umuamrishe kwayo kwa chochote ukitakacho kwa watu hao, Mfalme wa Majabali akaniita na akanisalimia na kusema: Ewe Muhammad, hakika Mwenyezi Mungu amesikia kauli ya watu wao walivyokwambia na mimi ni mfalme wa majabali, nimetumwa na Mwenyezi Mungu nije kwako ili uniamrishe utakavyo, ni ukitaka nitawaangushia majabali mawili juu yao, mimi nikasema: bali natarajia kuwa Mwenyezi Mungu atatoa katika kizazi chao wale watakaomwabudu Mwenyezi Mungu peke yake na wala hawamshirikishi kwaye na kitu chochote".
Mtume S.A.W., pia ametoa mwongozo wa kuwa na shime ya Usamehevu na Uzuri hata katika Sauti ya Adhana,. Kutoka kwa Ibnu Abas R.A. kwamba Mtume alisema kumwambia mmoja wa waadhini wake: "Hakika adhana ni nyepesi na yenye usamehevu, na ikiwa adhana yako ni samehevu na nyepesi basi adhini, na kama si hivyo basi usiadhini"
Mtume S.A.W, ameuhimiza Umma wake juu ya Usamehevu na Kusamehe katika zaidi ya Hadihti moja miongoni mwa Hadithi zake. Kutoka kwa Abuu Huraia, kutoka kwa Mtume S.A.W, amesema: "Mali haipungui kwa kutoa sadaka, na Mwenyezi Mungu hamzidishii mja wake kwa kusamehe isipokuwa cheo cha juu, na hakuna yeyote aliyemnyenyekea Mwenyezi Mungu isipokuwa yeye humnyanyua juu cheo chake"
Na Mtume S.A.W, amesema kwamba tabia njema na bora zaidi kwa walimwengu kuliko zote ni maadili ya njia za usamehevu, kama vile anatuonesha aina mbali mbali za kuhimiza na kuvutia maadili haya mema.
Kutoka kwa Abdillah Bin Alhusein amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema; "Je? Nikujulisheni maadili bora ya walimwengu duniani na pia siku ya mwisho? Ni yule atakayemsamehe aliyemdhulumu, na akampa aliyemnyima, na unganisha undugu wa yule aliyeukata. Na anayependa abarikiwe katika umri wake na azidishiwe mali yake basi na amche Mwenyezi Mungu Mola wake, na aunganishe undugu wake."
Bali Mtume alikuwa daima ni msamehevu, na alikuwa akimvutia mwenye haki asamehe katika kulipiza kisasi.
Kutoka kwa Anas R.A. amesema: "Sijawahi kumuona Mtume pale alipopelekewa kitu kinachohusu kisasi isipokuwa aliamrisha ndani yake Usamehevu."
Na akasema: "atakaeizuia hasira yake hali ya kuwa ana uwezo wa kuitumia basi Mwenyezi Mungu humjaza usalama na Imani, na atakaeacha kuvaa nguo nzuri hali ya kuwa ana uwezo wa kuinunua, kwa ajili tu ya unyenyekevu, basi Mwenyezi Mungu atamvalisha vazi la ukarimu, na atakaemuozesha mtu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu basi atamvika Taji la Kifalme."
Mtume pia alikuwa akiwasifu wale wenye kusamehe miongoni mwa maswahaba wake, mbele ya watu, na anawaongoza maswahaba wengine wafuate mwenendo huo na wajiliwaze kutokana nao. Kutoka kwa Alhasan kwamba Mtume S.A.W, amesema; kwamba mtume amesema: "Je hata mmoja miongoni mwenu anashindwa kuwa kama Abuu Dhwamdhwama, alikuwa pindi anapotoka nyumbani kwake anasema: Ewe Mola wangu nimetoa sadaka ya mali yangu kwa waja wako". Na Mtume anaweka wazi kuwa hizi ni Tabia njema, mwislamu anatakiwa kumsamehe kila anaemsengenya, anayemtusi au yote yanayofanana na haya miongoni mwa uvunjaji wa heshima, jambo ambalo ameliharamisha Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Ama kwa upande wa Huruma katika Sunna njema za Mtume, Mtume wetu Karimu – sala na salamu zimwendee – ni mjumbe wa Amani, Upendo na Huruma, kwa Ulimwengu Mzima, kwani yeye ndiye aliyeuasa Umma wake juu ya kuwahurumia watu wote waliopo Duniani, kwa kusema: "Watu wenye Huruma, Mwenyezi Mungu huwahurumia, wahurumieni waliomo ndani ya dunia watakuhurumieni waliomo mbinguni"
Huruma na Usamehevu wake, viliwaenea watu wote mpaka vikawafikia viumbe wote walio hai. Amesema: "Mtu mmoja akiwa njiani, alijiwa na kiu, akakuta kisima, na akateremka kisimani na kunywa maji, kisha akatoka na kumkuta mbwa anahema kutokana na kiu – na anakula mchanga kutokana na kiu – akasema Mtu huyu: Mbwa huyu amefikwa na kiwango cha kiu kama kile nilichokifikia mimi, basi Mtu huyu akateremka tena kisimani na kukijaza maji kiriba chake cha ngozi na kumnywesha maji yule Mbwa, kisha akamshukuru Mwenyezi Mungu na Mola wake akamsamehe". Wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi hivi sisi tunalipwa ujira kwa kuwasaidia wanyama? Mtume akasema: "Mnalipwa ujira kwa kila kiumbe chenye maini yenye unyevunyevu"
Na Mtume mtukufu amewasifu vizuri watu wapole na akabainisha Upole wao huu kuwa ni neema kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na akawaongoza pia wenye kuhitaji waelekee kwa watu wenye huruma (wasamaria wema). Kutoka kwa Ali anasema kuwa Mtume amesema: "Tafuteni msaada kutoka kwa watu wenye huruma katika Umati wangu mtaishi chini ya uangalizi wao, na wala msitafute msaada kwa wenye mioyo migumu, kwani laana ya Mwenyezi Mungu huwashukia juu yao, Ewe Ali, hakika Mwenyezi Mungu ameumba wema na ameuumbia watu wake na akaupendezesha kwao na akawapendezesha kwa wema huo kuutenda, na akawaelekezea wanaoutafuta kama vile alivyoyaelekeza maji yaelekee katika ardhi kavu isiyo na mimea ili watu wake waweze kuifufua, na kwamba watu wa wema Duniani ni watu wa wema pia Akhera."
Mtume ameonya wazi wazi kuhusu ugumu wa moyo na ukosefu wa huruma, na akabainisha kuwa njia hiyo ni mbaya na hupelekea mwanadamu kunyimwa huruma ya Mola wa viumbe wote siku ya akhera, akasema: "Mwenyezi Mungu hamuhurumii mtu asiyewahurumia watu". Na maneno haya yanaweka wazi kuwa huruma ni kitu kililoamrishwa na kwa watu wote kwa ujumla. Na wala haiishii kwa wale wanaokubaliana katika Dini moja au kwa umbile linalofanana, au hata kwa rangi, bali ni huruma kwa ujumla. Kwani ni huruma iliyo tulivu ndani ya moyo wa Mwislamu.
Kutoka kwa Abuu Huraira R.A. amesema: nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu, Msema kweli anaeaminika, Baba wa Qasim, mmiliki wa chumba hichi akisema: "Hanyang'anywi Mtu Huruma isipokuwa mwovu".
Mtume alitunza kwa matunzo ya hali ya juu kwa kuelekeza Huruma kwa makundi ya wanyonge katika jamii na wale walio wachache pia, pamoja na kwamba huu ni mweleweko wa kuwa mfano wa yaliyotangulia miongoni mwa maelekezo na miongozo ya kiutume, inakusanya makundi yote ya Jamii, na vile vile inakusanya watu wote, bali imethibitika kuwa inakusanya hata wanyama.
Isipokuwa Usamehevu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ni mpana zaidi, kwa hivyo alitaka kusisitizia kusamehe, Usamehevu na Huruma kwa makundi haya mbali mbali kwa Hadithi maalumu. Kutoka kwa Abdullah Bin Omar amesema: Mtu mmoja alimjia Mtume wa Mwenyezi Mungu na akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni kwa kiwango gani naweza mimi nikamsamehe Mtumishi wangu? Mtume wa Mwenyezi Mungu akanyamaza kimya kisha akasema yule Mtu tena: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni kwa kiwango gani ninaweza Mimi kumsamehe Mtumishi wangu? Mtume akasema: "Kila siku mara sabini". Na kwa kuwa Mtumishi ni katika kundi la watu walio wanyonge katika Jamii, kwa hivyo Mtume wa Mwenyezi Mungu anazidisha mno katika kumhurumia mtu kama huyu, na vile vile kumsamehe pale anapokosea.
Mtume pia, alikuwa na shime ya hali ya juu ya Huruma na Usamehevu kwa walio wachache kidini – kwa msemo wa kisasa – na akaonya vikali kwa yeyote atakaemdhulumu mmoja kati ya watu hawana kusema: "Mtu yeyote atakaemdhulumu yule tuliyewekeana nae mkataba wa ulinzi, au akampunguzia haki yake, au kumbebesha jukumu zito asiloliweza au akachukua kitu kutoka kwake bila ya mtu huyo kuwa na ridhaa yake basi mimi nitakuwa ndio hoja dhidi yake siku ya mwisho."
Hadithi zote hizi nyingi zilizotajwa zinaonesha wazi Usamehevu wa Uislamu katika Urithi wa Waislamu, fikra na mitazamo yao, pamoja na yale yasiyopingana na akili ya Mwislamu katika eneo lolote la Dunia hii.
Chanzo: Kitabu cha Simaatul-Al-asri, cha Mufti wa Misri, Dkt Ali Juma.