Kulisha Chakula ni Miongoni mwa Ma...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kulisha Chakula ni Miongoni mwa Maadili ya Uislamu

Question

Suala linaloenea zaidi katika miaka iliyopita ni meza iliyoandaliwa kwa ajili ya kulisha mafukara bure kwa ajili ya Allah na benki ya chakula, basi nini maoni ya Uislamu kuhusu suala hilo?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Mwenyezi Mungu Mtukufu Ametuamrisha tufanye juhudi zetu za kuondosha njaa. Akawasifu wafanyao hilo kwa sifa ya wacha- Mwenyezi Mungu Mtukufu akisema: {Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa} [AL INSAAN: 8], kadhalika Mwenyezi Mungu Aliwaaibisha kundi la watu wanaokataa kutoa mali katika njia ya Mwenyezi Mungu wala kuwalisha mafukara kama alivyosema Mwenyezi Mungu: {Na wanapo ambiwa: Toeni katika aliyo kupeniMwenyezi Mungu, walio kufuru huwaambia walio amini: Je! Tuwalishe ambao Mwenyezi Mungu angependa angeli walisha mwenyewe? Nyinyi hammo ila katika upotofu uliodhaahiri} [YAASIN: 47].

Mtume S.A.W. Alisema: “Enyi watu! Enezeni desturi ya kutoa salamu, lisheni chakula, watendeeni mazuri jamaa wa karibu na salini wakati watu wamelala, basi mtaingia Peponi kwa amani” (1), kadhalika Nabii wetu Muhammad S.A.W. Aliamrisha kumlisha mwenye njaa na akabainisha kwamba jambo hilo ni nguzo ya kheri akisema: “Mlisheni mwenye njaa na mtembeleeni mgonjwa” (2).

Chakula ni dharura ya kimaumbile ya kibinadamu ambayo wanazuoni wa Fiqihi ya kiislamu wamekifafanua kama ni: kitu cha msingi katika maisha ya binadamu na akikikosa basi ataangamia au atakaribia kuangamia. Baada ya hayo, inakuwa ni haja ya dharura ambayo binadamu akiikosa anapata dhiki maishani mwake. Halafu wanazuoni hao wametaja viwango vitatu navyo ni: manufaa, mapambo na ziada;

Manufaa: Daima yanakuwepo mikononi mwa watu lakini hayana athari juu ya uhai wa binadamu au kupata dhiki maishani mwake.

Mapambo: Kiwango chake ni cha juu zaidi kuliko manufaa.
Ziada: ni mlango wa israfu iliyokatazwa ingawa asili yake ni mubaha (Halali) lakini inaweza kukatazwa inapofikia hali ya israfu.

Wanazuoni wa Fiqhi waliutaja mgawanyiko huo unaotosheleza ambapo Maulamaa wa elimu za kijamii na za kibinadamu wameshindwa kufikia mgawanyo kama huo, ambapo wamesema kwamba dharura ni haja inayotakikana kutimizwa katika wakati kwa mfano. chakula, na haja kwao ni kila kinachohitajiwa na binadamu kama vile makazi na mavazi n.k. Pengine mgawanyiko wa wanazuoni wa Fiqhi unaweza kuwasaidia wahusika wa uchumi katika uchunguzi wa tatizo la kiuchumi ambapo wanabainisha tatizo hilo kuwa ni hali ya kuenea kwa haja wakati wa kuwepo hali ya kutoridhika. Hapo kutotenganisha baina ya dharura na haja katika suala hilo kumeanzisha hali mchanganyiko ya matamanio ambayo waliyaita kwa majina tofauti; mara wanayaita haja, mara nyingine wanayaita dharura na wakati mwingine wanayaita kwa jina tofauti mbali na dharura.

Maana ya chakula katika Urithi wa Waislamu ni kama: nafaka, matunda, dawa na viungo. Chakula: ni kile ambacho binadamu anakihitaji kwa ajili ya kuupa lishe na nguvu mwili wake kama vile; tende, zabibu na nafaka kama vile: ngano, shairi, fiwi na maharagwe na mhindi. Viungo: chumvi na pilipili na vinginevyo, ambavyo vinaweza kuongeza ladha ya chakula. Dawa: kila kinachosaidia kutibu. Aidha maji na vimiminika huweza kuingia katika maana ya chakula.

Chakula ni mojawapo ya vitu vitatu vya msingi kwa binadamu, na uanzishaji wa benki ya chakula unaweza kuwa hatua ya kwanza katika mradi ulio mkubwa zaidi unaojumuisha nyanja za kukusanya mavazi na makazi ambapo unaweza kuondosha tatizo la watoto walalao barabarani na ambalo limeenea sana siku hizi ulimwenguni na limeanza kuenea kwetu na kuzingatiwa kuwa ni laana katika uso wa ubinadamu hasa kwa wanaoshikamana na Uislamu; dini ya huruma, uuwiano na mshikamano wa kijamii.

Chakula ni katika mahitaji ya lazima ya binadamu; na ni dharura inayotambuliwa na wanazuoni wa Fiqhi ya Kiislamu kuwa iwapo mtu hatakula basi ataangamia au atakuwa hatarini kuangamia, na asilimia 40 ya kipato cha mtu, hutumika kwa ya chakula katika viwango vitatu vya kipato: kiwango cha kijungujiko, kiwango cha kujitosheleza na kiwango cha kipato cha juu. Viwango vitatu hivyo vinakuwa na uhusiano na uainishaji wa wanaostahiki zaka; kwani zaka hutolewa kwa yule anayekuwa katika kiwango duni kuliko kiwango cha kujitoshelezea mahitaji muhimu ili afikie kiwango cha kujitosheleza. Mtazamo huu unaweza kubadilika kwa mujibu wa tabia ya kila nchi pamoja na kubadilika kwa wakati na malengo yanayoenea baina ya watu.

Kiwango cha chini cha pato la mtu: ni kiwango ambacho binadamu anaweza kupata mahitaji yake ya kimsingi tu, nayo ni chakula; kwani ni kitu cha dharura, na kwa mujibu wa elimu ya lishe, binadamu anahitaji milo tofauti mitatu au minne kwa siku, yenye protini, vitamini, madini na virutubisho kadhaa ili binadamu ajikinge na maradhi.

Hapo chakula kinapokuwa rahisi, yaani bei ya kati na kati au ghali, kinaweza kuainisha thamani ya chakula cha mtu cha kila siku, hali kadhalika chakula cha famila ndogo (familia ya mume na mkewe na mtoto mmoja). Na pindi idadi ya watu wa familia moja inapozidi, basi thamani ya chakula cha kila siku huongezeka.

Katika baadhi ya nchi makazi yanakuwa na gharama zaidi, na katika hali hiyo hayaingii katika uhusiano huo na badala yake huhesabika kwa mwaka.

Ama kiwango cha kutoshelezeana, basi suala la elimu na ufundishaji linaingia pamoja na masuala mengine kama matibabu, usalama wa kijamii, michezo, fasihi na nyanja zake.

Kuhusu kiwango cha kipato cha juu, basi mambo mengine huzidi pia, kama vile kujifunza lugha, michezo ya burudani, mashirikiano ya kijamii na kisiasa. Kwa hiyo tunampa zaka kila anayekuwa katika kiwango cha chini cha pato lake ili tumfikishe kiwango cha kujikimu kimaisha. Ama mwenye hali ya kujitosheleza, basi tunampa sadaka tumfikishe kiwango cha juu zaidi; kwani zaka haiwezi kutolewa kwa mtu tajiri au mwenye mali, lakini sadaka inaweza kutolewa kwa tajiri.

Umoja wa Mataifa pamoja na taasisi za kimataifa zinazohusika na masuala ya chakula na madawa, zimeandaa chunguzi katika suala hilo. Natumaini kuwa mfumo wa zaka wa waislamu, utafundishwa na kusomeshwa ili kuufahamu urithi wa Kiislamu kwa undani wake, na hadi ionekane ni namna gani ustaarabu huu uliojengeka katika Uislamu ulikuwa na unaendelea kuwa ni ustaarabu uliopevuka, na tunatarajia kuwa hali hii itaendelea. Na kwa Mwenyezi Mungu jambo hili haliko mbali.
Rejeo: KITABU SIFA YA ENZI, Mufti wa Misri Sheikh Aly Juma
ـــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــ
(1) Hadithi hiyo ilitolewa na Ibn Majah katika sehemu ya Al At’ema “VYAKULA” mlango wa kulisha chakula, 3251 & Al Darmiy katika sehemu ya Sala mlango wa fadhila ya Sala ya usiku, 1460 na sehemu ya istizan “ombi la kupata ruhusa” mlango wa kueneza desturi ya kutoa salamu, 3/14, 4283 kutoka kwa Hadithi iliyopokelewa na Abdulaah bin Salam.
(2) Hadithi hiyo ilitolewa na Imamu Al Bukhariy katika sehemu ya Al At’ema, 5373, na katika sehemu ya Wagonjwa, mlango wa ulazimishaji wa kumtembelea mgonjwa, 5649 kutoka kwa Hadithi iliyopokelewa na Abu Mussa Al Ashaariy.
 

 

Share this:

Related Fatwas