Utashi wa Kiutu kwa Mtazamo wa Kim...

Egypt's Dar Al-Ifta

Utashi wa Kiutu kwa Mtazamo wa Kimaadili ya Kiisilamu

Question

Ni nini ufahamu wa utashi kwa upande wa maadili, na Je, Waisilamu wameweza kuonyesha ufahamu wenye kuthihirisha hilo?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Hakika ya utashi kwa upande wa maadili ni mojawapo ya nguzo tatu muhimu za kinafsi za mwenendo wa kibinaadamu, nazo; nia, desturi na utashi. Na tumezungumzia nguzo ya kwanza tulipoelezea kuhusu tabia za kibinaadamu kwenye anuani (Tabia za mwanaadamu kwa mtazamo wa kiisilamu). Ama kuhusu desturi imezungumziwa kwenye anuani ya (tabia kati ya desturi na mazoea). Ama sasaa tutazungumzia maudhui ya utashi kwa upande wa maadili ya kiisilamu.

Maana ya utashi kilugha ni, kumili nafsi katika kitendo ambacho itakifanya. Husemwa pia utashi una nguvu ambazo ni chanzo cha kumili, ni nguvu zenye kusababisha kitendo. Na iwapo wanyama wana aina ya utashi basi itakuwa ni ile ya matamanio, kwa maana kuwa mnyama atafanya kitu kwa msukumo wa hisia na si kwa utashi uliokamilika.

Kwa maana hiyo haitahesabiwa kuwa ni utashi kamili, aina hii huwa inaitwautashi uliopindukia. Lakini utashi ulio kamili ni ule anaoumiliki mwanadamu, pamoja na kuwa mwanadamu anashirikiana na wanyama kwa kile kinachoitwa utashi wa matamanio, isipokuwa yeye anahusika na aina ya utashi wenye kuwa na matokeo ya kufahamu upeo wa jambo na njia sahihi zenye masilahi ndani yake. Na kuwepo na shauku ya kupambanua masilahi na kuelewa sababu za utashi huo.

Imam Ghazali yeye anaona kuwa utashi ni: kumili kwa moyo kwa kile ukionacho kuwa ni muwafaka kwa malengo, ima kwa muda huo au kwa baadae, au ni kile kinachopelekea viungo kufanya tendo kwa mujibu wa akili.

Kwa maana hii ya mwisho ya utashi, hupatikana msaada wa nguvu mbili:
A) Nguvu yenye kusababisha kitendo ambayo inakuja kwa sababu ya utashi wa matamanio na ambayo inakuwa ni sababu ya kumili kwa mujibu wa kukifuata au kukikimbia kwa kutegemea jambo lililopo liwe linafaa au halifai.

B) Nguvu ya utendaji, nayo hupambanuka kwa kuwa nayo mwanadamu, ambayo ni nguvu, nafsi na chanzo cha kitendo cha mwili wa mwanadamu, na wala hakitatokea (kitendo) isipokuwa kwa nguvu na utashi pamoja na ujuzi. Kwani elimu huhamasisha utashi, na utashi huhamasishwa na uwezo nao uwezo hutenda kwa ajili ya utashi.

Inaonekana kwa namna hii, utashi ni ule umfanyao mwanadamu kuelekea upande wa upeo na malengo yake, kwa ajili hiyo inapasa utashi uwe wa mfano wa kipekee na kufahamu hekima katika kila jambo, nayo kama alivyoelezea imamu Ghazali aliposema: (… utashi kwa namna hii, unahusisha moyo wa mwanadamu, kwani akielewa kupitia akili, atafahamu mwisho wa jambo, na njia sahihi itakayomili kwa umakini mwelekeo wenye masilahi, na kufuatilia sababu za utashi. Nayo hii inatafautiana na utashi wa kimatamanio na utashi wa kinyama. Lakini huwa kinyume na matamanio kwani matamanio hupelekea mgonjwa kutamani chakula kizuri, wakati ambapo akili inakataa hata kama matamanio ya nafsi yanataka).

Kwa ajili hiyo, tunawezasema kuwa utashi ni msukumo wa nafsi ambao unamsukuma mtu kutenda kitu, sawa kiwe kizuri au kibaya. Lakini kinachoelezwa hapa ni msukumo wa utashi wenye mtazamo wa kufahamu na kumili na hisia. Kuwepo kwa hatua hizi ndio kunakopelekea kufanyika kwa kitendo cheye utashi.

Kiufupi, tunaweza kukusanya hatua hizi kama ifuatavyo: Lengo au shauku na hisia –hekima – nia au kusudio – na utendaji. Ama kuwepo kwa lengo au shauku na hisia haya ni lazima yawepo, kwani hayo ni msukumo wa mwanzo wa utashi, nao hauwezi kuonekana bila ya kuwepo ishara ya shauku, na shauku inapokuwa kubwa na hisia za malengo zikawa wazi namna hii huathiri sana nguvu za utashi kiasi ambacho mtu huwa hawezi kujiepusha na kutenda jambo husika. Na inahitajika kuwa shauku au lengo liwe limeshikamana na kumili na hapana budi vilevile pamoja na kuwepo hisia,pawepo pia na kumili kwa utashi, kwani nafsi inamili sana kwenye kitendo kwa kuitikia wito unaokwenda sambamba na malengo.

Ama kuwepo kwa hekima hili ni jambo muhimu kwa ajili ya kuchunguza aina tofauti za shauku, na njia mbalimbali ambazo zinajitokeza mbele ya mtu, na namna gani ya kuweza kuzipita ili afikie malengo tarajiwa, kwa namna hiyo, elimu itakuwa ni sharti la lazima katika utashi. Na katika jambo lisilo na shaka ni kuwa utashi haupatikani kwa mwanadamu isipokuwa upitie katika ngazi ya akili. Kwa kuwa umuhimu wa utashi unapatikana kwa kuwepo akili, na hii ndio faida ya kuwepo kwa kimoja wapo kwani vinategemeana. Kwa ajili hiyo imamu Ghazali anasema (Lau kuwa Mwenyezi Mungu ameumba akili zenye kujua mwisho wa matukio na wala asingeliumba shauku kwenye viungo kwa mujibu wa akili basi hukumu ya kuumbwa kwa akili isingelikuwepo, na umuhimu wa akili katika kuwa na hekima au kujua kuwa kitu hiki kinafaa au hakifai.

Ama nia ni hatua muhimu katika utashi, kwani hupelekea kuwepo kwa utulivu wakati wa kuchukua maamuzi Fulani na kufunga nia juu ya kutenda jambo, bila ya kusita. Nayo huwa baada ya kuelewa mitazamo yote na kujiweka mbali na vikwazo na sababu zitakazokwamisha au zenye kwenda kinyume. Na baada ya haya itahitajika njia ya utendaji na ushauri wa moyo juu ya matazamo wa lile unalolielekea.

Ama kuhusu hatua ya mwisho ni utendaji au tabia, na hatua hii huzingatiwa kuwani dalili ya nia na uamuziwa utashi. Kufanya atakacho mtu anaweza kukumbana na vikwazo na ugumu, na akiendelea kutenda pamoja na ugumu na vikwazo vilivyopo hii ina maana kuwa nia yake ni madhubuti. Kwani vikwazo na ugumu humfanya aliye na nia dhaifu kuacha kuendelea na akifanyacho.

Baada ya kuona yaliyotangulia itafahamika kuwa utashi huwa hauna maana bila ya uwepo wa kumili na matamanio, utashi wa mtu kwa kitu ndio huwa matokea ya kule kumili kwake. Pia ifahamike kuwa tendo au tabia haiwezi kutokea isipokuwa baada ya jaribio la msukumo na kumili. Kwani kipelekeacho kuwa na tabia mara nyingi huonekana kwa kuwepo kwa kumili au kuwepo mielekeo mengine.

Na hakika ya utashi unacheza nafasi muhimu katika kuelekeza tabia na kuidhibiti, kwani humuwezesha mtu kuweza kujidhibiti katika hisia zake na matendo yake. Nao ni roho ya matendo na msingi wake na matendo huwa hayana thamani pindi yakikosekana kuwa na utashi. Kupitia utashi ndio vitendo hufanyika au tabia huonekana, na iwapo utashi ni mzuri basina tabia nayo huwa nzuri, na iwapo ni mbaya basi nayo tabia vilevile huwa mbaya na yenye kuchukiza. Kwa maana hiyo kuna ulazima wa kuchunga utashi.

Kuchunga utashi ni lazima kwani mwenendo wa mtu wa kiroho hushikamana na utashi wake, na juu yake huchagua maisha mabaya au mazuri kutokana na hekima na uoni na uchaguzi wa mwisho mwema. Hivyo, utashi unapaswa kulelewa kwa misingi ambayo utakuwa ni mzuri wenye kupenda mazuri na yenye manufaa na kujikinga na maovu.

Na katika misingi muhimu ambayo inatakikana katika kuulea utashi ni kumuamini Mwenyezi Mungu na kumtiipamoja na kufanya ibada kwa ajili yake, kuwa na pupa ya kumrirdhisha na tamaa ya kufanikiwa kwa kupata malipo yake, na pia kuwa na utambuzi wa misingi ya kidini iliyo sahihi, na kuufuata uisilamu kwa vigezo vyema. Pasi na kuelekea katika kitu kilichokatazwa na kuharamishwa. Kwani upeo ulio juu zaidi ndio utakaomvutia mtu kuweza kumiliki utashi, hivyo, bila shaka utashi utakuwa ni mwema.

Na ili mtu awe na tabia njema ni lazima awe anajilazimisha kuifanya mara kwa mara tabia njema hiyo, na kuiambatanisha na vigezo vyema vya kiisilamu kama vile kumuelekea Mwenyezi Mungu na kumtakasa, na kuizoesha nafsi yake hisia njema, na kutoacha kuikumbusha kila siku juu ya hisia za kuridhika, utulivu na furaha.

Na italazimu kila siku kuitibu nafsi pale inapokuwa na udhaifu, na kuzitibu sababu zinazopelekea udhaifu huo, kwa mfano, udhaifu wa hisia ambazo ndizo chanzo cha utashi. Kwani kuendelea kukua kwa hisia zenye udhaifu na ndizo humfanya mtu asiwe na msimamo au kuingia katika msongamano wa mchanganyiko wa matamanio. Au kama mfano wa nguvu ya matamanio ambayo ndio nguvu kubwa kabisa kwa mtu, hisia humuathiri katika utashi na kumfanya asiwe na msimamo katika kutenda mema. Kwa ajili hiyo, inapasa kutibu yale yote yapelekeayo udhaifu na sababu zake na kuzishinda pamoja na kuizowesha nafsi katika utiifu au katika yale yaliyo halali.

Chanzo:- Prof. Abdul Maksud Abdul Ghani Khashaba, mtazamo wa maadili katika uisilamu – somo la mlinganisho. Cairo. Dar Thaqafa Al arabiya. 1412H – 1991 AD. (uk. 52-63).

Share this:

Related Fatwas