Mwanamke wa Mwislamu wa Kisasa na C...

Egypt's Dar Al-Ifta

Mwanamke wa Mwislamu wa Kisasa na Changamoto za Zama za Mali

Question

Ni changamoto zipi zinazomkabili mwanamke wa mwislamau hivi sasa katika zama hizi za udhalimu wa mali?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
1) Hakika Uislamu ulikuwa na mtazamo wake kuhusu alama za ukombozi wa mwanamke wa kisasa ambapo ulipambana na vitendo anavyovitenda mwanamke wa kimagharibi siku hizi kwani vitendo vyake wanavyoviita uhuru wa kibinafsi vinaweza kutoa dalili juu ya kuvurugika maadili ya kibinadamu katika maisha yake, maisha ya familia na maisha ya jamii yote ya kimagharibi, kwani masuala ya kujizuilia na machafu, haya, heshima ya kibinadamu, uaminifu, kutimiza ahadi na mfano wake hayapatikani katika tabia na mahusiano baina ya watu, hasa baina ya mwanamume na mwanamke katika jamii ya kimagharibi.
2) Kuvurugika kwa maadili ya kibinadamu kunamaanisha dhuluma ya uchumi dhidi ya madhumuni ya maisha au dhuluma ya mwelekeo wa mali katika maisha ya watu na mahusiano yao licha ya kuchagua upande wa kimwili na manufaa ya mali katika maisha yao dhidi ya maana za kibinadamu zinazowahifadhia kiwango cha kibinadamu; maana mwanamke wa kimagharibi k.m. matamanio ya kimwili yanamuathiri zaidi kuliko kujizuia na machafu,basi anaifanya zina bila kuwa na shaka, rafiki anapendelea kukutana kwa matamanio na mpenzi wa rafiki yake kuliko kulinda uhusiano wake wa kiurafiki na mwenzake, mfanyakazi anapendela kula rushwa kumsaidia mwenye kutoa rushwa bila ya haki kuliko kutekeleza amana na uadilifu na kuelekea kumpa haki kila mwenye haki, kaka anapendelea kula mali ya mirathi ya dada yake kuliko kumsaidia aweze kuolewa anamkandamiza ili aache mirathi yake, na mfanyabiashara anapendelea kutojaza kipimo sawa sawa apate manufaa zaidi.
3) Maana hizo za kibinadamu k.v. kujizuilia na machafu, kutekeleza amana na uadilifu, kusaidiana, rehema, kutekeleza haki n.k. zinavurugika katika maisha ya watu wa mali au wale wanaopendelea zaidi mali wakaiabudu bila ya Mwenyezi Mungu.
4) Uislamu haufanyi lengo la ndoa ni kusaidiana kiuchumi na matumizi ya familia kama mwelekeo wa mali unavyoelekeza watu katika maisha yao, bali Uislamu ulifanya lengo la ndoa lipatikane katika maana ya kibinadamu; utulivu, mapenzi na huruma. Mwenyezi Mungu Amesema: {Na katika Ishara Zake (za kuonyesha ihsani zake juu yenu) ni kuwa Amekuumbieni wake zenu katika jinsi yenu ili mupate utulivu kwao, naye Amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Bila shaka katika haya zimo Ishara kwa watu wanaofikiri} [AR-RUM, 21].
5) Na zama za kabla ya ujumbe wa Muhammad S.A.W. zilikuwa zinaitwa enzi za Ujinga (ujahili), ile enzi ambayo inasifika kwa dhuluma ya mali dhidi ya nafsi, dhuluma na masilahi ya kibinafsi dhidi ya maadili ya kibinadamu, na Uislamu ulipambana na jamii ya kibinadamu iliyokuwa na sifa ya mali na ustaarabu wa mali uliokuwa unaenea katika jamii kama ni dhuluma dhidi ya maadili ya kibinadamu.
6) Wakati anaoishi mwanamke wa leo ni zama za mali zinazopewa umuhimu zaidi kuliko maadili ya kibinadamu, nguvu za mali zimeunganishwa mpaka binadamu akawa anathaminiwa kwa mujibu wa nguvu yake ya mali siyo kwa kiwango chake cha kibinadamu.
7) Enzi ya mali inamweka mwanamke uso kwa uso mbele ya manufaa ya mali mpaka anachagua baina ya mienendo inayomletea manufaa zaidi licha ya kumfanya aweke maadili ya kibinadamu yaliyo juu katika cheo cha mambo ambayo hayana manufaa ya mali (hayana thamani kubwa).
8) Urafiki wa kijinsia bila ya ndoa kama ilivyojulikana katika jamii ya kimagharibi unaweza kufananishwa na ilivyokuwa inajulikana katika enzi ya Utume “ndoa ya Mut’a (ndoa ya muda maalumu)”; kwani aina hizo mbili zinalenga jambo moja tu nayo ni kuridhisha matamanio ya jinsia, wala hazilengi kusimamisha maisha ya kibinadamu ambayo msingi wake ni familia, na Uislamu uliharamisha ndoa ya Mut’a kwani ni jambo la dhuluma ya mali inayosifika kwa ubinafsi na kuvurugika kwa maadili ya kibinadamu.
9) Uislamu kama ulivyoharamisha aina mojawapo wa ndoa iliyopatikana katika enzi ya kijahilia nayo ni ndoa ya Mut’a au ndoa yenye muda maalumu, hali kadhalika unaharamisha kwa uwazi kila aina ya ndoa inayofanana nayo siku hizi k.v. ndoa ya kirafiki au ndoa ya kipindi maalumu, ama mahusiano yaliharamishwa yanayoenea siku hizi katika jamii za kisasa za kimagharibi sababu yake inarejea kuzuia talaka katika ndoa ya kikatholiki na ugumu wake katika ndoa ya kiprotestanti, ilhali Uislamu ulimpa mume haki ya kutaliki mkewe hali kadhalika ulimpa mke haki ya kujitoa katika ndoa (kujikomboa) ili kuondosha madhara kwa mwanamume na mwanamke kwa sababu ya mkataba wa ndoa.
10) Mwanamke wa kisasa wa kimagharibi anakubali kubadilishana wake ikiwa katika hafla ya pamoja ya kijinsia au ile inayojulikana kwa ndoa ya pamoja kama inavyotokea katika baadhi ya nchi za kimagharibi, hivyo inatokea kwa kuja baadhi ya wanaume na wake zao na kila mwanamume anakuwa na uhuru wa kuingiliana na mke yeyote, ilhali watoto watakaokuja kama matokeo ya hafla hiyo wananasibika na mume wa kila mke wakiwa ni watoto wake au wa mwengine. Na katika aina hiyo ya ndoa ya pamoja inawezekana kwa kila mwanamume aingiliane na wake zaidi ya wanne, kadhalika mke mmoja anaweza kuingiliwa na wanaume zaidi ya mmoja, hivyo harakati za utetezi wa mwanamke hazikatai aina hiyo ya ndoa kama zinavyokataa ndoa ya mitaala katika Uislamu.
11) Ingawa wataalamu wa mambo ya nchi za Mashariki na baadhi ya wandishi wa kimagharibi na waandishi wenye asili ya kimashariki wanaowafuata wanashangaa wakati wa kutaja ruhusa ya mitaala katika Uislamu kwa dharura, ilhali hawazungumzii ndoa ya pamoja wala kubadilishana wake na marafiki (hawara) kiujumla. Mbali ya hayo, hawapambani na wazo la maisha ya Kibuutz ya kiisraeli ambayo mtoto analelewa bila ya kujua mama wala baba yake, yale maisha ambayo yanaweza kufananishwa na ndoa ya pamoja (Kibuutz ni ushirika wa wakulima walowezi wa Israel na wanachama wake ndio wamiliki wa Kibuutz, hapo panalelewa watoto kwa sura ya pamoja, ushirika huo ulianzishwa na walowezi wa Kiyahudi katika ardhi ya Palestina mwaka wa 1910).
12) Kadhalika zinaa katika nchi za kimagharibi linakuwa ni suala la kibinafsi, na jamii haihusishwi nalo, lakini Uislamu unalizingatia kama ni kosa la kijamii na kwa mujibu wa mtazamo huu Uislamu ulitoa wito wake kwa Waumini washuhudie wakati wa kutekeleza adhabu ya zinaa wawe mashahidi, Mwenyezi Mungu Amesema: {Na lishuhudie adhabu yao (hii) kundi la Waislamu] [AN-NUR, 2].
13) Hakika jambo la kubadilishana wake au marafiki (hawara) linatoa dalili ya wazi juu ya dhuluma ya mali (maada) na kupendelea mwelekeo wa mali katika kupata hamu ya kijinsia zaidi kuliko maadili ya kibinadamu, basi katika hali hii heshima ya mwanamke, kujizuilia kwake na machafu licha ya haya yake yote maadili yanakuwa katika hali ya chini zaidi kuliko hamu ya kijinsia inayopatikana katika mahusiano haramu.
14) Uislamu kwa mujibu wa ujumbe wake wa kibinadamu ulipandisha cheo maadili ya hali ya juu katika maisha ya binadamu dhidi ya dhuluma ya mali katika ujahilia kwa kupambana na ndoa ya Shighaar (ndoa ya kubadilishana “mwanamke aolewa badala ya mwanamke mwengine bila ya wote wawili kupata mahari”), basi Uislamu uliiharamisha aina hiyo ya ndoa na ukaibatilisha kiujumla, hivyo mwanamke akapata heshima yake baada ya kuiharamisha; kwani akawa hapuuzwi tena, maana mwanamume katika aina hiyo ya ndoa alikuwa anaozesha binti au dada yake bila ya mahari sharti aoe dada au binti ya mwengine, hivyo tukiangalia vizuri aina hiyo ya ndoa, tutagundua kwamba inafanana na hali ya kubadilishana wake kwa ajili ya kuonja ladha tu. Kwa hali hiyo, mwanamke anakuwa ananyimwa haki yake ya kimaumbile na cheo chake katika kumsaidia mumewe na badala ya hayo anakuwa bidhaa mikononi mwa mwanamume.
15) Mwanamke siku hizi na kwa sababu ya mtazamo huu wa mali wa kimagharibi usio wa kimaadili anakuwa kama mfereji tu kwa machafu ya mwanamume, licha ya mtazamo huu wa mali mwanamke kwa kuingiliana na mtu baki siye mume wake anakuwa anaingia katika uhusiano haramu (zinaa) hata akikubali mume wake na akiwa na ridhaa na uhusiano huo; maana radhi yake haiwezi kuondosha haki ya jamii katika mtazamo wa Uislamu, ile hali inayoambatana na nasaba, kuwepo kwa heshima na nafsi ya kibinadamu kwa kila mtu katika jamii, kwa hiyo zinaa haitakuwa ni haki ya mume tu, bali aidha haki inarejea kwa jamii husika. Kwa hiyo, hali ya zinaa inapatikana hata baada ya kuacha mume haki yake kama inavyotokea katika hali ya kubadilishana wake; kwani uharimishaji wa zinaa hauhusiani naye tu, bali unahusiana na jamii kiujumla.
16) Uislamu siku hizi unapambana na yanayoitwa mapinduzi makuu ya kijinsia yanayoingia ndani ya jina la enzi ya ukombozi wa mwanamke, ambapo unapambana na dhuluma ya isiyothamini maadili yoyote ya kibinadamu, kwa hiyo Uislamu unaionya jamii kama hiyo maangamizi makubwa, Mwenyezi Mungu Amesema: {Na tunapotaka kuuangamiza mji (kwa kuwa watu wake wanafanya mabaya) tunawaamrisha (hao) mafisadi wake (waache ubaya); lakini wanaendelea na maasiya yao humo. Hapo kauli (ya kuadhibiwa) inathubutu juu yake (mji huo) na tunauangamiza maangamizo makubwa} [BANI ISRAIL, 16].
17) Kuenea kwa zinaa ambayo inakuwa kazi ya rasilimali ambapo mwanamke anauza mwili wake kutafuta mali, inakuwa ni jambo la dhuluma ya kimwili ile dhuluma ambayo haithamini maadili ya kibinadamu katika uhusiano unaokuwa baina ya mtu na mtu mwengine na badala ya hayo inaweka mbele maada peke yake kwa kutafuta starehe ya kimwili na yale manufaa ya kimaada, hali kadhalika inakuwa inahusika zaidi na mwili kuliko nafsi na roho.
18) Malaya alikuwa katika enzi ya kijahilia anaweka bendera juu ya mlango wake kama dalili au alama ya kuwepo uasherati ili wanaume waliokuwa wanataka kuingia wasione haya, na mwanamke wa kisasa wa kimagharibi - katika harakati yake kujikomboa - anafanya kama alivyokuwa anafanya mwanamke wa aina hiyo katika enzi ya kijahilia, na hapo lazima tubainishe kwamba mwanamke Mwislamu hana uhusiano kabisa na hali hiyo ya kuporomoka kwa tabia na maadili ambayo watu wa jamii ya kimagharibi wanaiita “ukombozi”, ambayo ni ghushi ya wazi, uongo na udanganyifu tu.
19) Mwanamke wa kimagharibi wa kisasa anakimbilia unaoitwa -uongo na udanganyifu- ukombozi wa mwanamke mpaka aliingia katika hali ya dhuluma ya kimwili na akabadilisha ubinadamu wake kwa alama anazoziita alama za uhuru ambazo kwa hakika alama za kuporomoka kwa maadili ya kibinadamu katika maisha yake. Hakika harakati za ukombozi wa mwanamke katika jamii ya kimagharibi zinamfanya mwanamke aache nafsi yake chini ya matamanio ya mwanamume afanye anavyotaka kufanya katika wakati wo wote na kwa njia na hali yo yote anayoitaka, basi wapi ukombozi wake?
20) Ikiwa mwelekeo wa Uislamu kuhusu hali ya mwanamke wa kimagharibi inayokuwepo siku hizi kwamba hauruhusu utoaji mimba, kuingiliana kabla ya kufunga ndoa, kubadilishana wake na wanaume, uzinzi wala kuonyesha mapambo ya mwanamke, basi mwanamke Mwislamu katika jamii za kisasa hatakiwi kulalamika juu ya sheria ya Mwenyezi Mungu kuhusu suala la kuharamisha alama au mionekano ya mwili; kwani sheria ya Mwenyezi Mungu inamtakia kiwango cha kibinadamu kizuri kwa mwanamke.
21) Hakika hali ya mwanamke katika Uislamu kama dhati yenye kujitawala anakuwa na haki na wajibu, hali hiyo haihitaji kujikomboa; basi mwanamke ashikamane na dini yake akiwa ni miongoni mwa waliopewa Kitabu akija kuolewa na Mwislamu, mwanamke ana haki ya kuweka mali yake mbali na mali ya mumewe, mwanamke anakuwa na haki sawa na mumewe katika kisasi hali kadhalika ana haki sawa na mwanamume katika msamaha wa muuaji, mwanamke ana haki kamili kutekeleza ibada, mwanamke anakuwa na majukumu wazi kwa familia yake, suala la kuwa mwanamke si mwenye kulazimishwa kutoa matumizi katika familia yake wakati ambao mwanamume analazimika kutoa matumizi ni kwa ajili ya kuhifadhi kuwa huru na mali yake na kutokandamizwa na mwanamume. Licha ya kuwa haki na wajibu zinazogawanyika baina ya nguzo za familia “mume na mke”, basi Mtoaji wa Sheria Alizianzisha na kusimamisha kwa uwiano uliothabiti unaompa mwanamke uhuru na hadhi na kumhifadhia heshima yake.
22) Miongoni mwa Hadithi za Mtume zilizo nzuri zaidi ni: (Kila mtu ni mchunga, na kila mchunga ataulizwa juu ya kile anachokichunga, kiongozi ni mchunga na ataulizwa kuhusu raia wake, mwanamume ni mchunga juu ya familia yake na ataulizwa juu yao, mwanamke ni mchunga juu ya nyumba ya mumewe na watoto wake na ataulizwa, mtumwa ni mchunga juu ya mali ya bwana wake na ataulizwa. Kila mtu ni mchunga, na kila mchunga ataulizwa juu ya kile anachokichunga) “ilipokelewa na Imamu Bukhari “853” na Imamu Muslim “1829” kutoka kwa Ibn Umar R.A.”. Uongozi wa mwanamume kwa familia yake na uchungaji wao hauathiri uhuru wao; mwanamke akiwa anachungwa na mumewe lakini pia yeye ni mchunga na ana majukumu kiukamilifu, mfano wake ni kama imamu na kila mwenye utawala na uongozi, kusimamia bila kuzembea.
23) Mwanamke Mwislamu wa kisasa analalamika kwamba Sheria ilimpa mwanamume tu haki ya kufunga mkataba wa ndoa malalamiko yake hayana msingi; kwani Uislamu ulimpa mwanamke haki sawa na mwanamume katika suala la kutoa maoni kuhusu uhusiano ulio baina yao “ndoa” ikiwa katika wakati wa posa “posa ya ndoa” au wakati wa kufunga mkataba. Pengine mwanamke akiwa bikra, basi Uislamu hausisitizi awe na maoni wazi na hivyo kwa kuhifadhi na kulinda haya yake na heshima yake; kwani bikra aghalabu anakuwa hapendi kuonyesha nia na utashi wake mbele ya watu hasa katika jambo la ndoa, ingawa Uislamu haumlazimishi bikra akae kimya tu bila ya kutoa maoni yake, hali kadhalika mwanamke akiendelea katika uchumba wa ndoa, basi atakuwa anakubali hiyo ndoa na yule mume wa baadaye, aidha mwanamke Mwislamu akiwa bikra anatakiwa awe na hayo asije kuomba ndoa na mwanamume , kutokana na hayo yanakuja madaraka ya ndoa kwa mwanamke bikra kwa ajili ya kulinda heshima yake siyo kwa kumwondoshea haki. Tena suala la kumkandamiza mwanamke kwa kumwozesha bila ya matakwa yake, basi litakwenda kinyume na kusudio la Mtoaji wa Sheria ambapo Mtume S.A.W Alisema: "Mwanamke mjane (si mwenye bikira) au aliyetalakiwa ni mwenye haki kwa nafsi yake zaidi kuliko walii wake na mwanamke mwenye bikira anamwamirishwa na kimya yake ni alama ya kukubali kwake" (ilitolewa na Imamu Muslam (1037) kutoka kwa Ibn Abass R.A.).
24) Mbali ya hayo, tunakuta hukumu za kisheria zinazohusiana na mwanamke tu, ambapo Mwenyezi Mungu Alimpa baadhi ya haki mbali ya mwanamume, basi kwa nini mwanamke Mwislamu wa leo analisahau kimakusudi jambo hilo, Mwenyezi Mungu Alimruhusu mwanamke avae hariri na mapambo ya dhahabu wakati mwanamume haruhusiwi. Aidha Mwenyezi Mungu Alimpa mwanamke haki ya kupata mahari na matumizi yakiwa ni haki yake ingawa manufaa ya ndoa na starehe yanakuwa ni ya kushirikiana baina ya wanandoa, hayaambatani na mume peke yake lakini Uislamu ulimpa haki hizo mwanamke ukamnyima mwanamume, na kwa mantiki hiyo ya mwanamke wa leo anayeomba usawa, basi mwanamume anaweza kutoa wito wa kubadilisha baadhi ya hukumu za kisheria pamoja na kuomba usawa na mwanamke hasa katika suala la kutoa matumizi na baadhi ya hukumu nyingine. Licha ya hayo, panapokuwa na baadhi ya hukumu nyingine za kisheria ambazo Uislamu uliangalia hali ya mwanamke na maumbile yake; maana ulimruhusu kuacha kutekeleza sala na saumu kwa siku maalumu katika siku zake kwa kuangalia hali yake ya kimwili na kinafsia akawa na hukumu zake hasa zinazomtofautisha na mwanamume. Kwa hiyo, haiwezekani kusema kwamba Sheria inamili kwa upande wa mwanamume; maana kutofautiana katika hukumu hasa kunakuwa kwa kulinda heshima na cheo cha mwanamke.
25) Tofauti na yanayoenea katika jambo la mirathi, kuna hali zinazofikia thelathini na zaidi ambazo mwanamke anachukua fungu sawa na mwanamume na pengine zaidi kuliko yake na baadhi ya hali anaweza kurithi yeye mwanamume ananyimwa. Hali hizo zinazomhusu mwanamke hulinganishwa na hali nne tu, ambapo mwanamke anarithi nusu ya fungu la mwanamume. Jambo hilo lilitajwa katika mlango wa kutetea Uislamu chini ya anwani: (kwa nini Uislamu ulimpa mwanamke nusu ya fungu la mwanamume?), hivyo uangalizi wa utungaji wa Sheria ya Kiislamu kwa mwamko unatuwezesha kuona mawazo mengi yaeneayo zaidi yanakuwa ni mambo ya shaka tu (tuhuma).
26) Suala la ukombozi wa mwanamke katika maisha ya Ulaya na suala la kutoa kwake maoni ukifikia uhuru wa kuingiliana kijinsia na mwanamume kuangalia kama atafika naye katika hali ya kutosheleza kwenye tendo hilo kabla ya kufunga ndoa, basi uhuru huu wa uongo hauaibishi mtazamo wa Uislamu kwa haya ya mwanamke ambayo ni msingi wa ubinadamu na uke wake kwa pamoja, ambapo mwanamke akiyaacha, basi ataelekea uasherati.
27) Hiyo ndiyo sababu iliyoelekeza Sheria ya Kiislamu kuweka sharti ya kuwepo mahari kwa mwanamke ambapo mwanamume kwa kuitoa anaonyesha utashi na ombi lake la kumwoa, hakumaanishi kupata manufaa yenye thamani, tofauti na maneno ya wataalamu wa mambo ya nchi za Mashariki wanaodai kuwa mahari ya ndoa inatolewa ili mwanamume aweze kuingiliana na kujitosheleza kwenye tendo la ndoa na mkewe.
28) Mwanamke Mwislamu wa kisasa anashtaki kwamba Sheria haiweki sawa mwanamke na mwanamume katika haki ya kutoa talaka, basi akaanza kutoa ombi lake la kufuta haki ya kutoa talaka mkononi mwa mwanamume na kumwachia kadhi anayehusika na masuala ya kutatua matatizo ya wanandoa, lakini haki ya kutoa talaka ikiwa mkononi mwa mwanamume, basi mwanake pia alipata haki ya kujikomboa, Mwenyezi Mungu Amesema: {Wala si halali kwenu kuchukua cho chote mlichowapa (wake zenu) isipokuwa (wote wawili) wakiogopa ya kwamba hawataweza kusimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu. Basi mkiogopa kwamba hawataweza kusimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu, hapo itakuwa hapana dhambi kwao (mwanamume wala mwanamke katika) kupokea (au kutoa) ajikomboleacho mwanamke. Hii ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu; basi msiiruke. Na watakaoiruka mipaka ya Mwenyezi Mungu, hao ndio madhalimu wa nafsi zao} [AL BAQARAH, 229]. Kadhalika kuondoka kwa haki ya kutoa talaka kutoka mkononi mwa mwanamume kwa kadhi hakuafikiani na Sheria ya Mwenyezi Mungu iliyomfanya mume awe na uongozi wa familia yake, hali kadhalika hakuafikiani na majukumu yake kiujumla wala hakuafikiani na kutunza siri za uhusiano wa kindoa unaotakiwa usitoke nje ya nyumba ya ndoa.
29) Kuondoka kwa madaraka ya kutoa talaka kikamilifu kwa kadhi kunakuwa jambo la kuathirika na tamaduni na staarabu na mifumo inayotofautiana na jamii zetu, Sheria yetu na maadili yetu. Hali kadhalika madaraka ya kutoa talaka yaliwekwa mkononi mwa kadhi katika nchi za kimagharibi kwani ilikuwa hakuna talaka katu katika ndoa ya Kikristo, basi wakaelekea ndoa ya kiserikali inayotolewa na kadhi kwa mujibu wa hukumu ya mahakama kinyume na mfumo wa ndoa na hukumu zake katika Ukristo. Kuanzia hapo, tatizo hilo silo la Kiislamu kimsingi ambalo linahitaji kulitatua kutokana na njia ya mahakama isipokuwa baadhi ya hali ambapo Sheria ilimpa kadhi haki ya kutoa talaka k.v. kutotolea matumizi au madhara kwa ulemavu.
30) Ili watulie wanaoiga wengine, basi mwelekeo wa kumkomboa mwanamke katika nchi za Magharibi siku hizi unakwenda sambamba na kuondoa madaraka ya kutoa talaka kutoka mkononi mwa kadhi kwa wanandoa; maana wakiafikiana juu ya talaka basi itakuwa hakuna haja kwenda mahakamani kupata hukuma ya kadhi na hapo inatosha kuandikisha katika ofisi za uzazi na vifo, na kweli yamefanyika mabadiliko ya sheria za familia nchini Sweden kwa mfano huu. Wanaozungumzia ustaarabu wa kimagharibi wanaona marekebisho hayo ni hatua ya kwanza kwenda mbele katika njia ya ukombozi wa mwanamke wa Ulaya, lakini hali za mwanamke wa Ulaya ni za chini kabisa kuliko mwanamke wa Kiislamu hasa katika kiwango cha utungaji wa Sheria na kinadharia.
31) Sheria ya Kiislamu ilimtunza mwanamke Mwislamu dhidi ya upungufu huo wa kiutungaji uliokuwepo Magharibi ambapo watu wake walijaribu kuurekebisha kwenye karne kadhaa kwa kuangalia harakati za jamii kidogo kidogo bila ya kulazimisha watu, basi kwa nini wanataka kulazimisha watu wa jamii yetu, nao hawalazimishi watu wa jamii zao.
32) Hukumu za kisheria zinazomhusu mwanamke Mwislamu zinamweka mwanamke mbele zaidi kuliko kanuni za kimagharibi na zinampa uhuru wake wa kimaana kama tulivyobainisha katika suala la talaka.
33) Mwanamke Mwislamu wa kisasa anashtaki ruhusa iliyotolewa na Sheria ya Mwenyezi Mungu kwa mwanamume aoe zaidi ya mke mmoja, bali amekwenda mbali zaidi kuomba ruhusa hiyo ifutwe, ingawa mitaala katika Sheria ya Allah siyo msingi wa kumlazimisha mwanamume, bali ni ruhusa inayotumiwa kwa kuwepo dharura; maana mwanamume anayehisi anahitaji mke mwengine akiwa hana ruhusa ya kisheria kuchukua mke mwengine, basi atatoka nje kutafuta uzinzi badala ya mitaala na hilo ndilo linalotokea katika maisha ya kimagharibi.
34) Ni jambo la ajabu tuone mwanamke wa kisasa anakataa suala la mitaala ingawa mwanamume anakuwa na jukumu sawa kwa wake zake, ilhali anaweza kukubali hali ya uzinzi wake na hali ya kutokuwa na jukumu, licha ya kutoshughulika na athari zinazohusiana na uhusiano haramu. Zaidi ya hayo anaona haya ni miongoni mwa njia za uhuru na maendelea.
35) Hakika mitaala kwa masharti yake ya kisheria yanayowajibika ni dharura ya kibinadamu na kijamii katika baadhi ya hali, aidha ni njia inayoweka watu mbali na kosa la zinaa, lakini hali ya kutumia ruhusa hiyo vibaya haimaanishi kwamba maisha ya kibinadamu hayaihitaji kama ni njia iliyohalalishwa k.v. misingi ya kijamii ya kiujumla ikitumika vibaya, basi inaweza kusababisha kuzuka maradhi na matatizo ya kijamii.
36) Mwanamke Mwislamu wa kisasa anashtaki kwamba Sheria ya Allah haiweki shahada ya mwanamke katika hali ya usawa na shahada ya mwanamume, na anaomba usawa, hapa tunamtaka mwanamke kabla ya kuomba usawa na mwanamume katika suala la kutoa shahada, na yeye awe na usawa katika sifa zake za kinafsi, kimwili na kiakili licha ya kufuta tofauti hizo ambazo maulamaa wa kisaikolojia na wa kijamii walijikuta hawana budi kuzikiri; maana kuzikanusha tofauti na sifa hizo za kiutu baina ya mwanamke na mwanamume kunaweza kuingia katika mlango wa kiburi na hila, tena Aliyewaumba na Akawatofautisha kwa sifa na tofauti hizo ni yule Aliyetofautisha baina yao katika suala la kutoa shahada.
37) Sisi hatudhani kwamba fikra ya Kiislamu ya kisasa ina wajibu wa kumfahamisha mwanamume sifa za kimaumbile ambazo Mwenyezi Mungu Alimpa wala kumfahamisha mwanamke sifa zake za kimaumbile ambazo Mwenyezi Mungu Alimpa; kwani mwanamke akipoteza sifa zake za maumbile, basi hatakuwa tena mwanamke, na hali hiyo hiyo kwa mwanamume.
38) Hakika tofauti katika baadhi ya hukumu za kisheria zinarejea uangalifu wa tofauti zinazokuwa baina ya wote wawili; mwanamke na mwanamume. Licha ya kugawanya wajibu baina yao ili washirikiane katika kutekeleza mambo wanayotakiwa kuyafanya katika kiwango cha kijamii, kistaarabu na kibinadamu.
39) Hakika tunayoyaona na tunayoyasikia kuhusu wito ambao umevuka mipaka ya mapambano baina ya mwanamume na mwanamke, kufikia mapambano baina ya mwanamke na nafsi yake, kisha itafikia wapi? Na vipi inaachwa fikra huru inamuangamiza mwenyewe na kutuangamiza pamoja naye.
40) Je, sisi tunataka katika jamii zetu za Kiislamu tufikie tatizo hilo la kibinadamu, kistaarabu, kiutungaji wa kisheria na kimaadili? Je, tunataka tuingie katika mapambano ya uongo yasiyokwisha ambayo yanatuweka mbali na mapambano ya kweli na ufukara, maradhi, hali ya kutoendelea … n.k.
41) Hakika mwanamke Mwislamu na mwanamume Mwislamu na hata jamii ya Kiislamu kiujumla wote wanakuwa hawana haja ya mfumo kama ule; sisi tunaohitaji ni ufahamu na ukikamilifu sahihi pamoja na utekelezaji sahihi kwa Sheria yetu na maadili na mifumo yetu ya kifikra, kimaadili na ya kiutungaji.
42) Hukumu za kisheria ambazo zimewapa mwanamke na mwanamume haki sawa, zimetoka kutoka kwa Mwenyezi Mwungu kwa wote wawili; maana hukumu hizo haziweki chini haki za mwanamume wala kupandisha cheo haki za mwanamke, naye Mwenyezi Mungu Amesema: {Wote hao (wema na wabaya) tunawapa - hawa na hawa - katika atia (kipawa) za Mola wako; na atia za Mola wako hazizuiliki “kumfikia kiumbe chake”} [BANI ISRAIL, 20]. Kwa hiyo, hukumu ambazo zinawatofautisha baina yao hazimaanishi kumpa mwanamume heshima zaidi kuliko mwanamke, wala kumdhalilisha mwanamke; kwani katika Uislamu hakuna jamii ya kiume wala kibaba, hali kadhalika hakuna jamii ya kiuke wala kimama, na uainisho huu kiujumla unakuwa na mtazamo finyu ambao ni maradhi yanayoathiri vibaya ustaarabu wa kisasa wenye kudumu.
43) Hakika ustaarabu wa Kiislamu unaanzishwa juu ya maelewano, mwafaka, uwiano na mwelekeo chanya wa kisaikolojia, kifikra, kiustaarabu na kijamii; ustaarabu wa Kiislamu uko mbali sana na mapambano bali unajitahidi kufikia amani kwani Mwenyezi Mungu ni mwenye salama. Hali kadhalika ustaarabu wa Kiislamu unasimamishwa na amani; amani baina ya madola, amani baina ya jamii tofauti, amani baina ya mwanamume na mwanamke, na mwishoni amani baina ya mtu na nafsi yake. Kwa hiyo, sisi Waislamu hatuna hali yoyote ya mapambano katika ustaarabu wetu wa Kiislamu yakiwa ya kifikra, kinadharia au ya kiutungaji wa Sheria. Kwa hiyo, hakuna mapambano baina ya dume na jike katika utungaji wa Sheria ya Kiislamu, hali kadhalika jamii ya kibinadamu, maisha na ulimwengu wote unaelekezwa na fikra ya Kiislam inayotegemea hali ushirikiano mwema baina ya wanandoa, Mwenyezi Mungu Amesema: {Na katika kila kitu Tumeumba dume na jike ili mpate kufahamu} {ADH-DHAARIYAT, 49].
44) Kuhusu mwanamume na mwanamke, basi Mwenyezi Mungu Amewaumba katika nafsi (asili) moja, na mwanadamu aliye na tabia nzuri hatakiwi kuwa na mapambano na nafsi yake; kwani jambo hilo linatokea tu na mtu mwenye maradhi kwa hiyo uhusiano unaokuwa baina yao hauwezi kufikia mapambano kwani ikitokea hiyo, itatokana na fikra finyu. Ama sisi Waislamu fikra yetu ya Kiislamu kuhusu jambo hilo inatokana na kauli ya Mwenyezi Mungu: {Enyi watu! Mcheni Mola wenu ambaye Amekuumbeni katika nafsi (asili) moja. Na Akamuumba mkewe katika nafsi ile ile. Na akaeneza wanaume wengi na wanawake kutoka katika wawili hao. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana. Na (mwatazame) jamaa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mlinzi juu yenu (anayaona kila mnayoyafanya)} [AN NISAA, 1], kadhalika Mwenyezi Mungu Amesema: {Yeye ndiye Aliyekuumbeni katika nafsi moja; na katika (nafsi) hiyo Amewaumba wake wao, ili (kila mwanamume) apate utulivu kwake (mkewe)} [AL AARAF, 189].
45) Hakika suala la kuendesha uhusiano baina ya mwanamume na mwanamke kama ni mapambano limeharibu jamii ya kimagharibi, kadhalika litaharibu jamii ya kimashariki. Kwa hiyo, lazima tuangalie hivyo wala tusiendeshwe na wito ambao hauna faida kwa jitihada yetu katika njia ya maendeleo ya ukweli, jitihada ambayo lazima isimamishwe juu ya ulezi mwema na ufahamu sahihi kwa mahitaji ya kiustaarabu na kiutamaduni pamoja na utekelezaji sahihi kwake ili mambo ya maafikiano, mwema, uadilifu, rehema, utulivu yaenee baina ya watu wa jamii.
Rejeo: Prof. Muhammad Al Bahiy. Uislamu na Mwelekeo wa Mwanamke Mwislamu wa kisasa, Cairo, Mak-tabat Wah-ba, cha 2, 1981, uk. 3: 54.

Share this:

Related Fatwas