Kwenda Kinyume Kitabia na Sababu Za...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kwenda Kinyume Kitabia na Sababu Zake Katika Mtazamo wa Kitabia wa Uislamu

Question

Ni zipi sababu za kwenda kinyume kitabia katika mtazamo wa Kiislamu?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
1. Kuna sababu kadhaa ambazo zinapelekea kwenda kinyume kitabia kutokana na mtazamo wa Kiislamu. Miongoni mwa sababu hizo ni:
a. kuendekeza matamanio.
b. kumzulia uongo Mwenyezi Mungu.
c. kuwa mbali na Mwenye Mungu.
d. kuchanganya kati ya utashi wa Mola na utashi wa mwanaadamu.
e. fikra potofu – na sababu nyinginezo.

Tutazungumzia sababu hizi tulizozitaja kwa kina zaidi.
Kwanza: miongoni mwa sababu za kwenda kinyume kitabia:
Kuendekeza matamanio:
Kwa hakika, tatizo kubwa linalomkabili mwanaadamu maishani mwake ni kuabudu matamanio yake. Matamanio hayo yakiishinda nafsi, basi akili huenda kombo na moyo kupata giza. Na hupelekea kwa binaadamu huyo kutosikia neno la haki. Wala haoni lolote isipokuwa mambo ya batili. Na humfanya awe na simanzi na huzuni maishani mwake. Na wale ambao wanaabudu matamanio hayo, huwa hawajui kuzungumza. Kwa sababu wanayoyadiriki wao kwa usikivu wao na uoni wao katika mambo ya elimu hayatekelezeki katika mioyo yao.
{“Na bila ya shaka tumewaumbia moto wa Jahannamu wengi katika majini na wanadamu (kwa sababu hii): Nyoyo wanazo, lakini hawafahamu kwazo (Hawataki kufahamu kwazo), na macho wanayo, lakini hawaoni kwayo, na masikio wanayo, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama; bali wao ni wapotofu (wapotevu) zaidi. Hao ndio walioghafilika.”} [Al-ARAAF: 179].
Ama wale wanaoifuata haki, wao sio watiifu wa matamanio baada ya kuwajia elimu na utambuzi. Na hii ndio tofauti kati ya aswi na muumini; hawako sawa.
{“Je! Watu wenye kuwa na dalili zitokazo kwa Mola wao watakuwa sawa na watu waliopambiwa ubaya wa vitendo vyao (vibaya) na wakafuata matamanio ya nafsi zao?”} [MUHAMMAD: 14].
Na matamanio ni adui wa elimu ya haki. Kiasi kwamba inamwongoza mwenye matamanio hayo kufanya maovu na machafu na kukengeuka njia ya Mwenyezi Mungu mtukufu. Huwa anaidhulumu nafsi yake na ameiharamisha kupata neema ya imani na ameizinga kutokana na nuru ya maarifa, akaishi maisha ya woga, khofu na fazaa; na akajaza husuda na chuki katika nafsi ya mtu mwengine. Akapotezwa na shetani na akapotea na kutoka njia iliyosawa.
{“Na kama hawakukujibu, basi jua ya kuwa wanajifuatia tu matamanio yao. Na nani aliyepotea zaidi kuliko yule anayefuata matamanio yake pasi na uwongofu utokao kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaogopi watu madhalimu (wa nafsi zao).”} [AL-QASAS: 50].
Na amesema Mwenyezi Mungu mtukufu: {“Lakini waliodhulumu (nafsi zao) wamefuata matamanio yao pasipo kujua; basi ni nani awezaye kumuongoza ambaye Mwenyezi Mungu Amemuacha kupotea (kwa kuwa mwenyewe hataki kuongoka)? Nao hawatakuwa na wenye kuwanusuru.”} [AR-RUUM: 29].
Basi kuabudu matamanio ni ujinga na ni kwenda kinyume na kutoka katika uongofu wa Mwenyezi Mungu. Matamanio ni dhana ya uongo na mjumuisho wa shetani na kumpitikia wasiwasi unaomwongoza katika upotevu, ufisadi na uharibifu.
{“…wala msifuate matamanio ya watu waliokwishapotea toka zamani; (nao ndio hao wanavyuoni wenu) na wakawapoteza wengi, na (sasa) wanapotea njia iliyo sawa, (hawataki kumfuata Nabii Muhammad).”} [Al-Maida: 77]
Na ili mwanadamu asiyafate matamanio hayo wala asijisahau kwenye njia iliyonyooka, inampasa amtaje Mwenyezi Mungu muda wote ili asisahau. Kwa sababu kumtaja Mwenyezi Mungu kunaziweka karibu nyoyo na kuziambatanisha na Mwenyezi Mungu kwa mwambatano madhubuti. Na atakapomsahau Mwenyezi Mungu na ukapita muda mrefu, moyo wake hufunikwa na kughafilika na kutumbukia katika makucha ya matamanio na kupotea njia ya Mwenyezi Mungu. Hivyo kuendelea kumtaja Mwenyezi Mungu daima kunamhakikishia mwanadamu neema kubwa katika maisha yake ya duniani. Neema hiyo ni utulivu wa nafsi na moyo.
{“…Sikilizeni! Kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu nyoyo hutulia.”} [AR-RA’AD: 28].
Na kinyume cha hayo, basi watu wanaoendekeza matamanio wanaishi maisha yao yote katika masikitiko makubwa na khofu ya kudumu hata kama wataonekana kuwa na furaha. Kwa sababu ukweli ni kwamba ndani mwao umetanda ukungu wa simanzi na huzuni.
Wala watu wanaoendekeza matamanio hawaachi kujidhihirisha kwa waumini, kuwafanyia vitimbi na kujaribu kuwaharibu. Hivyo, Mwenyezi Mungu mtukufu anawahimiza waja wake wasiwaangalie wala kuwafuata au kuwatii kwa ajili ya matamanio yao ya kihisia (kimwili) au kiroho.
{“Wala usiwatii wale ambao tumezighafilisha nyoyo zao wakafuata matamanio yao, na mambo yao yakawa yamepita mipaka (yaani makafiri).”} [AL-KAHF: 28].
Kuyafuata matamanio ya utupu na tumbo na kukithirisha kupindukia ndio tabia za wenye kuyaendekeza matamanio. Kufanya kwao ubadhirifu katika kutimiza matamanio ya uongo pamoja na kufanya israfu katika kutaka kupata ladha ya haraka haraka kunawafanya wawe waja wa wazi wazi wenye kuabudu matamanio hayo, na linakuwa ndilo lengo lao kuu hata kama likipingana na tabia njema, dini na desturi sahihi. Pia, ndio hivyo hivyo kwa matamanio ya kiroho kama vile matamanio ya kufanya uadui, kiburi na majigambo, sawa sawa iwe kwa kutumia ulimi na kusababisha maudhi kwa kila silaha au zana.
Wanaoendekeza matamanio wanamalizikia kuwa na maradhi makali ya kinafsi. Wala hayatibiwi maradhi hayo isipokuwa kwa kurejea kwenye ngome ya imani. Maradhi hayo ya kinafsi yanadhihiri katika sura ya wasiwasi, shaka, dhana mbaya, khofu iliyotawala, kutetemeka, fazaa na huzuni nzito. Na wenye maradhi haya nyoyo zoa zimepigwa na giza na kupasuliwa na chuki ya ndani ya nafsi, kughururika, wahka, kiburi, ubakhili, tamaa na ulafi. Basi pindi yakirundikana maradhi haya ya kinafsi inakuwa ni vigumu kutibiwa isipokuwa kwa rehema ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa yamekusanyika baadhi yake, mtu mwenye hali hii huitwa mjinga. Maradhi yakizidi, mtu huitwa mwenye kuendekeza matamanio (mwenye ashiki). Na yataporundikana magonjwa haya, mtu mwenye hali hii huitwa mkengeukaji, mpaka afikie mwisho wa jambo lake na kuwa mtu wa shari. Na watu wa shari ni wale wanaoifanya kheri kuwa shari na shari kuwa ni kheri. Sifa ya kiutu imetoweka kabisa. Na miongoni mwa neema za Mwenyezi Mungu mtukufu kwetu ni kwamba watu wa aina hii ni adimu mno kupatikana. Lakini mjinga, mwenye kuendekeza matamanio na mkengeukaji ni miongoni mwa watu wa matamanio; wao huishi katika kila jamii na idadi yao inaongezeka na kupungua kwa mujibu wa tabia za jamii hiyo, utaratibu na nyenendo zake.
Na huwenda mtu akajiuliza: inakuwaje watu wanaoendekeza matamanio wanakuwepo katika kila jamii?
Jawabu ni kwamba: bila ya kuifahamu shari hakutopelekea kuwepo kheri. Kama shari haikuvutia kheri na kheri haikuvutia shari, basi binaadamu angepoteza chaguo na asingeweza kutafakari na vilingo vyake na hukumu zake vingeharibika kwenye mambo yote. Na vipi binaadamu achague kazi njema na aiache mbaya ikiwa anashindwa kupambanua kati ya kheri na shari, au haki na batili?! Bila ya shaka kuwepo kheri na shari katika maisha ni lazima ili utimie uadilifu kati ya watu, na wapambanue kati ya waumini na wanaoendekeza matamanio.
Pili: miongoni mwa sababu zinazopelekea kwenda kinyume kitabia:
Kumzulia Mwenyezi Mungu uongo:
Ni wepesi kwa wanaoendekeza matamanio kumzulia Mwenyezi Mungu uongo. Na ni vigumu kwa sehemu fulani kufuata adabu ya kuabudu na kumtii Mwenyezi Mungu wakiomba msamaha na toba. Kwa hakika adabu na heshima ya mja na Mola wake inamlazimu mja kujua mipaka yake, basi asiivuke mipaka hiyo kamwe. Ajijue kwamba yeye ni mja dhaifu na Mwenyezi Mungu ndio mwenye nguvu. Na yeye Mwenyezi Mungu mtukufu ndie mkwasi na mja ndio mwenye kuhitaji daima, na ataendelea kuwa fukara.
{“Enyi watu! Nyinyi ndio wenye haja kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu Mkwasi (na nyinyi – hakuhitajieni), Asifiwaye (kwa neema zake juu ya viumbe vyake vyote).”} [FAATER: 15].
Hakika ya mja mwema hazembei katika wajibu wa kuabudu wala habishani na uungu. Wala hajipi nguvu, wala kuiruhusu nafsi yake kumwabudu Mwenyezi Mungu nusu nusu, na kuchezea hukumu za Mwenyezi Mungu na hoja zake katika ulimwengu, uumbaji, maisha na kifo. Kwani mja kujitanguliza kushiriki katika maswala ya uungu katika hukumu na amri ni kuidhulumu nafsi na kuizulia uongo haki na ni shirki iliyojificha ambayo itamwangamiza mwanaadamu.
{“Fahamuni. Kuumba (ni Kwake tu Mwenyewe Mwenyezi Mungu) na amri zote ni zake (Mwenyezi Mungu). Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote.”} [AL-ARAAF: 54].
{“…Mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu…”} [AR-RAD: 31].
Hakika mwenye akili timamu ni yule ambae hajadili kitu kwa Mwenyezi Mungu bila ya ujuzi na elimu na wala bila ya kitabu kilichowazi, kinyume chake ataiweka nafsi yake ikituhumu na kuhukumu bila ya haki.
{“Na katika watu wako wanaobishana juu ya Mwenyezi Mungu pasipo elimu, na wanamfuata kila shetani asi.”} [HAJJ: 3].
{“Na katika watu wako wanaojadiliana juu ya Mwenyezi Mungu bila ilimu wala uwongozi wala Kitabu chenye nuru.”} [HAJJ: 8].
Mwenyezi Mungu mtukufu ametufafanulia katika kitabu chake kitukufu kila anachokihitaji mtu kukijua katika maisha yake duniani. Akambainishia mtu huyo njia ya haki na usalama. Kama alivyombainishia njia batili na upotevu. Akamwacha mwanadamu achague bila ya kumlazimisha wala kumtenza nguvu kuchagua baada ya kuwa keshamjuza na kumwelimisha juu ya njia hiyo. Basi kwa namna yoyote ile nafsi ya mja itakavyojizungumzia kwa kumzulia uongo Mwenyezi Mungu, na kuyakubali mambo batili ya shetani; basi…
{“Ni neno kubwa hilo litokalo katika vinywa vyao. Hawasemi ila uwongo tu.”} [AL-KAHF: 5].
Na maneno ya kweli kutoka kwa Mwenyezi Mungu au kutokana na Mwenyezi Mungu na maneno yake Mwenyezi Mungu na aya zake zilizo wazi…
{“Na nani mkweli zaidi katika maneno kuliko Mwenyezi Mungu?”} [AN-NISAA: 87].
Na kwa ajili ya jambo hili, hakika miongoni mwa sababu kubwa za kumzulia Mwenyezi Mungu uongo ni: kupuuza aya za Mwenyezi Mungu.
{“Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayekumbushwa Aya za Mola wake akawa anazipuuza, na akayasahau (mabaya) yaliyotangulizwa (yaliyofanywa) na mikono yake? (Kama kwamba) sisi tumetia nyoyoni mwao vifuniko ili wasiifahamu, na kama kwamba katika masikio yao (tumetia) uzito (uziwi). Na ukiwaita katika uwongofu hawakubali abadan kuongoka.”} [AL-KAHF: 57].
Tatu: miongoni mwa sababu za kwenda kinyume kitabia:
Kuwa mbali na Mwenyezi Mungu:
Ni wema ulioje kwa mwanaadamu akiyapigia mfano maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyokamilika na akachukua kigezo kwa aya zake na ubainifu wake. Mwenyezi Mungu Mtukufu amejiwajibishia rehma kwa nafsi akasema: {“… Mola wenu amejilazimisha rehema…”} [AL-ANAAM: 54].
Na huku ni kufadhilisha kiungu ambako Mwenyezi Mungu amekuwa mtukufu kwa hilo, na akawaahidia watu na akawaahidia haki, na maneno yake ya kweli yanafanya kuwepo mfungamano kati ya mja na Mola wake. Mfungamano huo ni wa upendo na matarajio mema kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu. Na jambo hili ndilo linalofanya kuwepo uhusiano madhubuti kati ya uja na Uungu. Basi pindi mwanaadamu anapomuomba Mola wake kwa nia safi na toba ya kweli kweli, Mwenyezi Mungu mtukufu humjibu dua yake na kumteremshia rehma kutoka kwake.
{“Na waja wangu watakapokuuliza hakika yangu, (waambie kuwa) Mimi niko karibu nao. Naitika maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie na waniamini, ili wapate kuongoka.”} [AL-BAQARAH: 186].
Na kwa upande mwingine, hakika Mwenyezi Mungu mtukufu amekwishajiandikia kwa nafsi yake rehma. Basi akimkuta mja wake amekwenda kinyume na njia iliyonyooka au amedhulumu basi kutokana na upana wa rehma zake humsamehe.
Na Mwenyezi Mungu mtukufu anapendelea kumwona mja wake anatimiza ahadi zake. Kama ambavyo amelazimisha hivyo kwa nafsi yake.
{“… na tekelezeni ahadi yangu (ya kuwa akija Mtume mtamfuata), nitatekeleza ahadi yenu (ya kukupeni Pepo); na niogopeni mimi tu.”} [Al-Baqara: 40].
Na mja kumuahidi Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa atamtii yeye, kuzitekeleza amri zake na kuyaepuka makatazo yake, pamoja na kuzifanyia kazi sharia zake zote kwa uwazi na usiri.
Kuna mafungamano kati ya mja na Mola wake ambayo yanajengeka kwa ukweli, haki, matarajio ya ahadi ya Mwenyezi mungu na kuogopa vitisho vyake; mafungamano haya yanafupishika katika kuzifanyia kazi amri za Mwenyezi Mungu kwa upande mmoja na katika dua kwa upande mwengine wa mja. Mafungamano haya yanafanyika kwa adabu maalumu pamoja na Mwenyezi Mungu mtukufu pamoja na kumtii yeye.
Nne: miongoni mwa sababu za kwenda kinyume kitabia:
Kuchanganya kati ya utashi wa Mola na utashi wa mwanaadamu:
Pamoja na yote yaliyofikiwa na akili ya binaadamu katika ubora na maendeleo, lakini bado binadamu huyu atabakia kuwa na mapungufu tokea mwanzo hadi mwisho. Miongoni mwa sababu za kwenda kinyume kitabia kudai mwanaadamu mambo au kufanya mambo ya makosa na ambayo sio ya kisharia. Kisha akayanasibisha na utashi wa Mwenyezi Mungu mtukufu. Na kutokana na hivyo vinamkanganya haki na batili. Basi asitoe dalili ya uwepo wa Mwenyezi Mungu juu ya kumuasi Mwenyezi Mungu na kutoka katika utiifu wake.
{“Je! Yule aliyepambiwa amali zake mbaya na akaziona njema, (utamwambia nini hata asikiye)? Bila ya shaka Mwenyezi Mungu Humuacha kupotea Amtakaye (kwa kuwa hataki mwenyewe kuongoka); na Humuongoza Amtakaye. Basi roho yako isitoke kwa majonzi juu yao; kwa yakini Mwenyezi Mungu Anajua (yote) wanayoyafanya.} [FATER: 8].
Na ikiwa Mwenyezi Mungu mtukufu ni mmoja hana mshirika katika hukumu yake na anafanya anayoyataka, basi matokeo yote ya viumbe na watu yapo katika manufaa na madhara; kheri yake na shari yake yote yanarejea kwa Mwenyezi Mungu mtukufu. {“… Muumba wa kila kitu…”} [AL-ANAAM: 102].
Kwa hakika Mwenyezi Mungu ameumba kheri na shari na manufaa na madhara. Kisha akampa nafasi mwanaadamu achague kufuata kheri na kuikataa shari. Ikiwa mwanaadamu atamwasi Mwenyezi Mungu basi kunatokana na kusahau au kughafilika, hivyo mlango wa kuomba msamaha na toba upo wazi. Lakini haifai mwanadamu kuchanganya katika maasi yake kati ya utashi wa Mwenyezi Mungu na utashi wake katika kufanya shari kwa sababu tu ya uchaguzi wake na uhuru wake.
Kwa hakika anayoyafanya binadamu muumini na kafiri, mwema na mwovu, mwenye kutubu na mwasi; huwa ni kwa mujibu wa ujuzi na elimu ya Mwenyezi Mungu na kusudio lake na hekima zake za hali ya juu, na inakuwa ni hoja nzito katika uumbaji na ulimwengu. Basi aliyoyataka Mwenyezi Mungu ndio yaliyokuwa na ambalo hakulitaka, halijakuwa.
{“Na kama Mwenyezi Mungu angependa bila shaka angewakusanya katika uwongozi (huu kwa miujiza hiyo; lakini hataki). Basi usiwe miongoni mwa wasiojua.”} [AL-ANAAM: 35].
Tano: miongoni mwa sababu za kwenda kinyume kitabia:
Fikra potofu:
Kiasi kwamba uhuru wa kiakili na mambo mengine kama hayo katika maadili mema ya kibinadamu na kifikra yamegeuka kutoka maadili yanayomsaidia mwanadamu kuwa mtu bora na mwenye maendeleo kuwa vigezo vipya vya upotoshaji vinavyojaribu kuifanya haki kuwa batili na batili kuwa haki, na vinajitengenezea mifano inayotokana na akili kuwa ndio kipando kinachoshambulia dini, maadili na sharia tukufu ya kiisilamu.
Kwa hakika akili pekee haiongoi kwenda kwenye uhakika wa dini, bali dini ndio inayoiongoa akili. Na kama akili haijafungamana na imani basi itaporomoka, na kupoteza vigezo vya upambanuzi kati ya sahihi na potofu kwa yale yaliyo nyuma ya hisia, hata kama ikiwa inaweza kupambanua kati ya sahihi na batili miongoni mwa mambo ya kiroho na yale yanayopatika kwa hisia.
Wanafalsafa na wasomi wamejaribu kuyazungumza mambo juu ya uwezo wa akili ambayo hata haina imani, wakakosea na kwenda kombo kwa kiasi kikubwa. Na kila ambapo mwanafalsafa anapotengeneza mtazamo fulani katika asili ya kuwepo au uhalisia wa maarifa hayo, anakuja mwanafalsafa mwingine kuthibitisha ubobeaji wake na kudhoofika mantiki yake. Kisha anakuja na mtazamo mwengine unaothibitika uwepo. Na hayo yote ni kutokana na vigezo alivyovitengeneza mwenyewe. Na upesi mtazamo huu unaanguka mbele ya uhakiki na kudhihiri udhaifu wake na kuwa mbali kabisa na ukweli.
Historia ya fikra ya binaadamu inatupa mapokeo kwamba wasomi wenyewe licha ya kutumia kwao akili zao hakuna hata mmoja aliefikia ukweli hata mmoja kwa yale yanayohusiana na msingi na asili ya vitu au ukweli wa kutokea au misingi yake ya mwanzo. Bali ni majaribio tu ya wanafalsafa na wasomi wakiwa wanabahatisha ambako hakujathibiti ukweli wake. Kama pia hakuna hata mmoja aliyeweza kwa kutumia vigezo vya kiakili ambavyo wamevitengeneza kama ndio njia ya kisomi au kifikra, kutengeneza njia au mtindo wenye kukubalika ambao utakwenda sambamba na uhakika wa kilimwengu. Na ilipokuwa wasomi wa kisasa wameshindwa kufikia ukweli japo mmoja tu kwa yale yanayohusiana na ukweli wa dini, na wakauzingatia kuwa ni wenye kupooza na kuzorotesha kazi za maendeleo ya akili ya mwanaadamu na harakati za ukuaji wa sayansi pamoja na kukashifu baadhi ya hadithi za Mtume Muhammad – rehema na amani zimshukie – huko ni kuikashifu asili ya dini.
Ilhali baadhi ya mielekeo ya kifikra za kimamboleo imeona kwamba isijitokeze kuishambulia dini moja kwa moja kwa sababu ya kutowasisimua waliowengi. Lakini wameelekea kwenye hali ya vigezo vipya kwa ajili ya harakati za kimaisha kama vibadala vya dini, kwa kisingizio kwamba ndivyo vilivyopo na vinalingana na binadamu wa kileo. Vigezo hivi wamedai vinatoa matokeo ya haraka na maendeleo yanayoonekanwa katika pande mbali mbali za maisha. Vigezo hivi ni aina ya ufikiri wa kifalsafa unaotarajiwa, ambao unahangaikia kuhimiza kujiengua kutokana na uongofu wa dini.
Vigezo hivi vya kimamboleo vimefungamana na tabia za kisayansi ya kimaisha bila ya kuzingatia undani ambao unahukumu tabia ya binaadamu ambayo inapelekea kwenda kinyume kitabia ambako kunakukabili jamii nyingi. Majaribio haya ya kibinaadamu yamefeli kuleta vibadala vya dini vinavyokusudia kumwongoa mwanadamu kuelekea katika dini ya haki.
Hakika kunyooka kifikira maana yake ni kutompelekea binadamu kuifanyia hila hukumu tukufu ya Mwenyezi Mungu. Wala asipingane na hoja zilizothabiti. Wala asimzulie Mwenyezi Mungu uongo. Wala binadamu huyo amwabudu Mwenyezi Mungu ukingoni (anaabudu nusunusu). Wala asiyakubali mambo fulani na kuyakataa mengine akidai kwamba hayatimizi uadilifu au hayakubaliani na wakati uliopo au hayamfikishi mwanadamu kwenye mafanikio.
Hakika mambo makubwa zaidi yanayosababisha raha na furaha kwa binaadamu duniani ni kufuata njia ya Mwenyezi Mungu na kuyafanyia kazi yale aliyoyaamrisha na kuyaacha aliyoyakataza. Na kwa vyovyote atavyofanyiakazi fikra zake mwenyewe binadamu na akajiweka katika vigezo vya kifikra vilivyobora kabisa au vigezo vya kimaada, basi hatohakikisha kheri katika uwepo wake na hatofikia mafanikio.
Hivyo, hakuna utatuzi kwa msomi wa kimamboleo isipokuwa kuongoka kwa amri za Mwenyezi Mungu na sharia yake, na awe na uyakinifu kwamba akili yake haiwezi kufahamu uhakika wa dini. Na kwamba mafanikio yake yanatimia kwa njia ya mafungamano ya akili na uongofu wa dini. Na hakuna kitakachopelekea hayo isipokuwa neno la kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Na inaipasa akili isiivuke sharia ya Mwenyezi Mungu, na wala isipingane na vitendo vya Mwenyezi Mungu mtukufu, na wala asitake ila au sababu, kwa sababu kumeshathibiti kwa dalili na hoja madhubuti kwamba Mwenyezi Mungu mtukufu ni Mfalme, Muweza na Mwenye Hekima. Basi ikifichikana hekima kwa binadamu kutokana na kitendo cha Mwenyezi Mungu, basi ni wajibu wake binadamu kufanya kushindwa kwake kuwa ni ujinga na ufinyu wa akili yake, na kutoweza kudirikia hikima ya Mwenyezi Mungu iliyodhahiri na iliyojificha. Basi hekima ya Mwenyezi Mungu mtukufu katika kukusanya vitendo hivyo vilivyofichikana kwa binadamu na sababu zake, hakuna anaezijua isipokuwa yeye Mwenyezi Mungu. Isipokuwa Mwenyezi Mungu akitaka kuziweka wazi baadhi ya hekima hizo kama alivyombainisha Nabii Mussa – amani iwe juu yake – hekima ya kuibomoa jahazi na kumuua kijana. Basi mwanaadamu mwenye akili timamu inampasa ajisalimishe kwa uweza wa Mwenyezi Mungu mtukufu na hekima yake iliyowazi na iliyojificha. Wala akili yake isivuke uweza wa Mwenyezi Mungu, wala hukumu yake na vitendo vyake Mola mtukufu katika ulimwengu na uumbaji na maisha; kinyume na hivyo atatumbukia katika ujinga, shirki na upotevu.

Marejeo: Profesa Daktari: Hassan el-Sharqaawy, Tabia za Kiisilamu, cairo: Taasisi ya Mukhtar ya Uchapishaji na Uenezi, toleo la kwanza 1988, (ukurasa wa 19 – 35).

Share this:

Related Fatwas