Uzuri katika Mtazamo wa Uislamu

Egypt's Dar Al-Ifta

Uzuri katika Mtazamo wa Uislamu

Question

Uzuri kama dhana ya kifalsafa una nafasi ya kipekee katika falsafa kwa ujumla, ni vipi fikra ya kiislamu ya kisasa inaweza kukabiliana nao?

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Waislamu waliufahamu vyema uzuri na rehma tokea zama zilizopita. Na uzuri kwa maana yake pana ambayo inavuka uzuri wa kifalsafa, ambao unaishia kwa yale yanayohusiana na jicho na muonekano kwa jicho, wakati ambapo waislamu wamekwenda mbali zaidi katika kuona na katika itikadi yao ya kwamba uzuri ni miongoni mwa sifa za Allah Mtukufu, katika Hadithi tukufu: “Hakika Mwenyezi Mungu ni mzuri na anapenda uzuri”([1]).

Na uzuri wa Madrasa ya Sultan Hassan na msikiti wake kimtazamo na uhalisia wake na madhumuni ya ujumbe wake alioutaka Sultan Hassan, ni mfano wa uzuri kwa Waislamu, na ni wajibu wetu kufahamu ni jinsi gani tutahuisha malengo haya matukufu katika zama zetu. Ustaarabu wa Kiislamu unaendelea haukufa na wala hautakufa, ingawa umekosa  uongozi, na umekosa  kuchangia katika manufaa, umekosa ushujaa na umakini, lakini kubakia kwa lugha yake, kitabu chake na urithi wake, pamoja na kuendelea kwa urithi wa Dini ambayo imejengeka juoitia kizazi hadi kizazi- inathibitisha kutokufa kwake bali kubakia kwake. Hiyo ni hali ya kulala inayotarajiwa  kuamka na wala haihitaji kuhuishwa  au kufufuliwa baada ya kufa.

     1-     Mwenyezi Mungu ameiumba nafsi ya binadamu kwa kupenda kila kitu kizuri, na kukichukia kila kibaya. Mwenyezi Mungu amemili upande wa uzuri. Hili ni jambo la kawaida katika maumbile yaliyokamilika. Tabia ya binadamu inachukia mandhari, tabia na sauti mbaya. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akaufanya uzuri kuwa ni jambo lililohimizwa katika Sheria yake tukufu. Katika uzuri kuna mkusanyiko wa mambo ya Ulimwengu na Mambo ya kisheria, na haya yamo  katika mshikamano wa hali ya juu.

Kwa ajili hiyo Uislamu umesisitizia juu ya mandhari nzuri, tabia nzuri, sauti na harufu nzuri. Na Mwislamu kwa tabia yake nzuri, na kumuabudu kwake Mungu vizuri, na kushikamana kwake na sheria nzuri, anakuwa mzuri na unaenea uzuri, raha na utulivu katika sehemu anayokuwapo Mwislamu huyo. Mwislamu ni kama mvua inaponyesha  huacha manufaa. Na tuangalie matini za Sheria tukufu ambazo zinaelezea uzuri.

Aya nyingi zinazouzungumzia uzuri na kuuhimiza zimo ndani ya Quraani. Miongoni mwa Aya hizo ni kauli yake Allah Mtukufu: {Na wanyama hao amekuumbieni. Katika hao mna vifaa vya kutia joto, na manufaa mengineyo, na baadhi yao mnawala. Na wanakupeni furaha pale mnapo warudisha jioni na mnapo wapeleka malishoni asubuhi. Na hubeba mizigo yenu kupeleka kwenye miji msiyo weza kuifikia ila kwa mashaka ya nafsi. Hakika Mola wenu Mlezi ni Mpole na Mwenye kurehemu. Na farasi, na nyumbu, na punda ili muwapande, na kuwa ni pambo. Na ataumba msivyo vijua} [AN NAH'L:5-8].

Katika aya hizi Mwenyezi Mungu anawahesabia viumbe wake uzuri na urembo aliouweka kwa wanyama. Na kauli yake Allah mtukufu: {Na hakika tumeweka katika mbingu vituo vya sayari, na tumezipamba kwa wenye kuangalia} [HIJR: 16].

Na huu ni muonekano mwingine wa uzuri ambao Mola wetu anatuitia ili tupate mazingatio ndani yake, nao ni uzuri wa mbingu na kupambika kwake kwa nyota. Kama ambavyo Allah Mtukufu alivyowahesabia viumbe wake uzuri wa bustani ya ardhini akasema aliyetukua: {AU NANI yule aliye ziumba mbingu na ardhi, na akakuteremshieni maji kutoka mbinguni, na kwa hayo tukaziotesha bustani zenye kupendeza? Nyinyi hamna uwezo wa kuiotesha miti yake. Je! Yupo Mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Bali hao ni watu walio potoka} [AN-NAML: 60].

Na Uislamu umehimiza kujipamba na kupendeza kwa ujumla – na hasa wakati wa kwenda misikitini - akasema Mola Mtukufu: {Enyi wanaadamu! Chukueni pambo lenu kwenye kila pahala wakati wa ibada} [AL-A'RAAF: 31].

Kama ulivyopokelewa msisitizo juu ya uzuri na kuutilia mkazo katika Sunna tukufu za Mtume, amesema Mtume S.A.W: “Hataingia peponi mtu ambaye ndani ya moyo wake kuna chembe ya kiburi. Mtu mmoja akasema: Hakika mtu anapenda nguo zake ziwe nzuri, na viatu vyake ni vizuri. Akasema Mtume: “Hakika Mwenyezi Mungu ni mzuri na anapenda uzuri; kiburi maana yake ni kukataa haki na kuwadharau watu”([2]).

Na kutoka kwa Muadh R.A alisema: Alikuja mtu mmoja kwa Mtume S.A.W, akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi napenda uzuri, na mimi napenda kusifiwa –kana kwamba anaihofia nafsi yake – akasema Mtume S.A.W: “Ni kipi kinachokuzuwia kuishi mwema na kufa mwenye furaha? Na hakika nimetumwa kukamilisha tabia njema”([3]).

Matini zote hizi za kisheria zinathibitisha thamani ya uzuri na athari yake katika nafsi ya Binadamu.  

Chanzo: kitabu cha “Simaat Al Asri, cha Mufti wa Zamani wa Misri Dk. Ali Juma.

 ([1])  Ameitoa Muslimu katika kitabu (Al Imaan) mlango (kuharamisha kibri na ubainifu wake) hadithi (91) katika hadithi ya Ibn Masoud R.A.

([2])  Ameitoa Muslimu katika kitabu (Al Imaan)) mlango (kuharamisha kibri na ubainifu wake) hadithi (91) katika hadithi ya Ibn Masoud R.A.

([3])  Ameitoa Al Bazzaar katika (musnad yake) 7/92, na Haarith Ibn Abi Usamah katika (Musnad yake) 2/841 hadithi (890), na Al Tabraaniy katika (Al Kabiyr) 20/65, na akaitaja Al Haythamiy katika (Majmaa Al Zawaaid) (8/23.)

Share this:

Related Fatwas