Hukumu ya Kujinyima kwa Kufuata Madhehebu Maalumu
Question
Je, mtu anaweza kujinyima kwa kufuata madhehebu moja kati ya madhehebu manne? ni bora kwa mtu kufuata vibadala vingine?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Kuna tofauti katika suala hili baina ya kujifunza na kufuata: Kwa upande wa kufuata: Mtu wa kawaida halazimiki kushikamana na madhehebu maalumu katika matukio yote, bali ana haki ya kufuata maoni ya mwenye kujitahidi yeyote na hayo ndiyo ni maoni yaliyo sahihi; kwa hiyo, Maulamaa walikuwa na kauli mashuhuri: “Mtu wa kawaida hana madhehebu maalumu, bali madhehebu yake ni ya mwenye kumtolea fatwa”; hapa anakusudiwa aliyejulikana kwa elimu na uadilifu wake.
Hayo ndiyo maoni yaliyo sahihi kwa Wahanafi; Ibn A’bedin aliandika katika maelezo yake kutoka kwa Al Sharnablaly: “Mtu hawajibiki kushikamana na madhehebu maalumu, bali anaruhusika kwenda kinyume na vitendo alivyovifanya mwanzo kufuata madhehebu moja kwa kuiga mwenendo usio wa Imamu wake, tena ana haki ya kufuata hukumu mbili zisizolingana katika matukio mawili sharti yasihusiani, aidha havibatilishi vitendo aliyevitenda kwa kufuata Imamu mwengine”.
Linalosisitiza maoni haya ni kwamba Mwenyezi Mungu Amelazimisha kufuata Maulamaa bila ya kujinyima kwa kufuata mmoja, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui}[AN-NAHL 43], tena waliokuwa wanaomba fatwa katika zama za Masahaba na waliowafuata walikuwa hawashikamani na madhehebu maalumu, bali walikuwa wanauliza Imamu yeyote bila ya kujinyima na hakuna yeyote aliyewakataza hatika kitendo hicho.
Suala la kufuata mwenye kujitahidi yeyote ni la haki; kwani Maimamu wote wako katika njia ya haki; maana mtu huenda sambamba na ijitihadi yake, tena mwenye kufuata (kuiga) madhehbu maalumu hatakiwi kudhani kuwa wengine hawako hatika njia iliyo sahihi.
Kwa upande wa kujifunza: Suala la kufuata madhehebu katika wigo wa uchunguzi au kutafiti halina budi lipatikane wala halina kibadala; madhehebu haya manne yenye kufuatwa yalizingatiwa zaidi katika kuyanakili na kuyaandika maoni yake, pamoja na kujua maoni yaliyo sahihi zaidi na dalili zake licha ya kuwa Maimamu wake waliandikiwa ufasiri mpaka kila madhehebu kutokana madhehebu hizi zikawa ni shule peke zenye kujitegemea na zenye misingi iliyo maarufu na matawi yaliyoainishwa ambapo mwenye kutaka kujifundisha dini analazimika kushikamana nayo kwa kufaidika nayo ili aanze kutoka walipoishia.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote