Wanawake Kwenda Msikitini Kusali

Egypt's Dar Al-Ifta

Wanawake Kwenda Msikitini Kusali

Question

Ni rai ipi yenye kuzingatiwa kwa mujibu wa madhehebu ya Abu Hanifa kuhusu wanawake kuingia msikitini kwa ajili ya kusali? Kwa kuwa kuna baadhi ya wafuasi wa madhehebu ya Abu Hanifa huku London ambao wanasema: Inachukiza (inakatazwa) mkatazo unaokaribia kuwa wa uharamu kwa wanawake kwenda msikitini, na kwa ajili hiyo hawakujenga maeneo maalumu msikitini kwa ajili ya wanawake. Je, jambo hili linafaa? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Kuna Hadithi nyingi kutoka kwa Mtume (Rehma na amani zimshukie) kuhusu swala hili, kwa mfano Hadithi ya Ibn Umar –Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao- iliyo katika vitabu vya Bukhari na Muslim: "Msiwakataze vijakazi wa Mwenyezi Mungu Misikiti ya Mwenyezi Mungu" na katika mapokezi yao: "Pindi mmoja wenu akiombwa ruhusa na mkewe ya kwenda msikitini basi asimzuie". Na Abu Daudi amezidisha katika mapokezi yake: "Na nyumba zao ni bora kwao". Na jambo hili linapelekea kuwa, inafaa kwa mwanamke kwenda msikitini. Na kwa matazamo mwingine inajulisha kuwa inapasa (Inalazimu) kwa mwanamke kuomba ruhusa kwa mumewe pindi akitaka kwenda msikitini, isipokuwa wanazuoni wengi wamechukulia uombaji wa ruhusa ni kama jambo lenye kupendeza (na sio wajibu).
Na kauli nyingine kutoka kwa madhehebu ya Hanafi wametoa hukumu ya kuchukiza kwenda mwanamke msikitini kwa sababu ya kuenea ufisadi na kubadilika kwa zama (zama hizi sio za wacha Mungu). Na ushahidi wautumiao ni Hadithi ya Aisha –radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie – aliposema: "Lau kama Mtume –Rehma na amani zimshukie– angeliyaona yale waliyoyazusha wanawawake basi angeliwazuia kama walivyozuiwa wanawake wa bani Israel".
Na kuchukiza huku ambako baadhi ya wana madhehebu ya Hanafiy wasio wa zamani wanakuchukulia ni chukizo lililo karibu na uharamu, kwa mfano: Imam Al Hafidh Al Iyniy katika [Umdatul Qaari 6/156, chapa, Dar Ihyaa At Turath Al Arabiy). Isipokuwa kinachofahamika katika maelezo ya waliotangulia katika viongozi wa madhehebu ya Hanifa katika maswala haya ni chukizo la kujiepusha tu.
Kama alivyoelezea mwenye Madhehebu –Radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie- pale aliposema: (Haifai). Na mwenzake Imamu Muhammad –Mwenyezi Mungu amrehemu– aliposema: “Wanawake hawahitajiki kwenda Msikitini kwa kusali sala ya Eid”. Ikafahamika kuwa katazo ni la lazima na sio la kujuzu kwao.
Na chukizo hilo ni kwa wasichana tu pekee ama watu wazima (Wazee) wala haichukizi hata kidogo kwenda Msikitini kwa mujibu wa mtazamo wa wao (Hawa maimamu wawili). Na mwa mtazamo wa Abi Hanifa haichukizi kwenda msikitini kwa ajili ya sala ya Isha na Asubuhi na Eid mbili, na huchukiza kwenda kusali sala ya Adhuhuri, Alasiri na Ijumaa. Na pindi wakitoka kwa ajili ya Eid je, (kwa mujibu wa madhehebu ya Hanifa) watasali au watashuhudia tu sala pamoja na watu wengine? Kuna kauli (Rai) mbili:-
Imamu Muhammahd bin Al Hassan Al Shaybaniy rafiki wa imam Abi Hanifa anasema katika kitabu chake: [Al Hujatu ala Ahli Al Madinah 1/306, chapa Alamu Al Kitaab]: "Abu Hanifa amesema –radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie- kuhusu wanawake kutoka kwa ajili ya Eid mbili: Ilikuwa ikiruhusiwa, ama kwa sasa haifai (Haipasi) kwenda isipokuwa kwa vizee kwani wao hakuna tatizo." Mwisho.
Sheikh Burhan Din anasema katika {Al Muhit 2/208-209, chapa, Dar Ihyaal At turath Al Arabiy]: "Muhammad – Mwenyezi Mungu Amrehemu – Amesema: “… Haipasi kwa wanawake kutoka na kwenda katika (sala) ya Eid mbili, na walikuwa wakiruhusiwa kwa jambo hilo.” Akasema: Abu Hanifa amesema: “Siku hizi mimi ninachukiza jambo hilo kwao, na pia ninachukiza kwenda kushuhudia sala ya Ijumaa na sala za lazima (za rafadhi), isipokuwa ninaruhusu kwa vizee kushuhudia sala ya Isha, Alfajiri na Eid mbili. Na Abu Yusuf na Muhammad –Mwenyezi Mungu awarehemu- wamesema: “Inaruhusika kwa vizee kuhudhuria sala zote na za kupatwa kwa mwezi na kwa jua na sala za kuomba mvua." Mwisho
Pia amesema (2/211): "Na je, iwapo wakitoka kwa ajili ya sala ya Eid je watasali? Hassan amepokea kutoka kwa Abi Hanifa –Mwenyezi Mungu amrehemu- kuwa amesema, watasali; kwani lengo lao ni kutoka kwa ajili ya sala."
Na imepokewa na Al maaliy kutoka kwa Abi Yusuf -Mwenyezi Mungu amrehemu– Kutoka kwa Abi Hanifa –Mwenyezi Mungu amrehemu– “Kuwa hawatasali, lakini kutoka kwao ni kwa ajili ya kufanya wingi wa wavaaji wa nguo nyeusi katika waisilamu.” Mwisho.
Na rai ya kuchukiza –na sio ya kuharamishwa– ni kama alivyoeleza imamu Al Sarsakhiy katika kitabu cha: [Al Mabsut] Na imam Abu Hanifa Al kuduriy katika kitabu cha: [Al Mukhtaswar] na mwanazuoni Al Murghiyaniy katika kitabu cha: [Bidayatul Mubtadiy], na Abu Al Fadhli bin Mauduud Al Muswal katika kitabu cha: [Al Ikhtiyaar Lita`aliyl Al Mukhtaar", na Al khatib Attamartaashiy katika kitabu cha [Tanwiyru Al Abswaar] na kitabu cha: [Al Fatawaa Al Hindiyyah] na vitabu vingine vya madhehebu ya Hanifa vya waliotangulia (wasomi wa mwanzoni) na waliochelewa (na wa kisasa).
Na katika hoja zinazotiliwa nguvu sana na waliotangulia ya kuwa jambo hili linachukizo chukizo lisilo la uharamu ni: Wamezingatia hali tafauti za kwenda mwanamke msikitini, kwa mfano sala ya jamaa kwa wanawake, nia ya imamu ya kuwaongoza wanawake, na kusihi kufuata kwake sala ya Ijumaa na Eid mbili iwapo hajanuia kumfuata imamu na hukumu nyingine ambazo ni vigumu kusema kuwa ni haramu, (kwani mambo hayo si haramu).
Lakini kuna maelezo ya kuwa inafaa kwa mwanamke kukaa itikafu katika msikiti unaosaliwa sala ya pamoja. Na baadhi ya wanazuoni wa Hanafi wameendelea kusema: Inachukiza, na hii inamaanisha kuchukiza huko ni lile chukizo la kujiepusha na sio chukizo la kuharamisha, kwani jambo lenye kufaa huwa haliambatani na la kuharamishwa.
Imamu As Sarakhsiy anasema katika kitabu cha: [Al Mabsuut 3/216, chapa, Dar Al Fikr]: "Hasana amepokea kutoka kwa Abi Hanifa –Mwenyezi Mungu awarehemu- pindi mwanamke akikaa itikafu katika msikiti unaosaliwa sala ya pamoja basi itafaa. Ama kukaa itikafu katika msikiti ulio ndani ya nyumba yake ni bora zaidi, na kauli hii ndio sahihi." Mwisho.
Na imekuja katika kitabu cha: [Al Fatawa Al Hindiyyah 1/112, chapa, Dar Al Fikr]): "Lau mwanamke akikaa itikafu katika msikiti unaosaliwa jamaa inafaa na inachukiza, na hivi ndivyo katika Al Muhiit Al Sarakhsaniy." Mwisho.
Na jambo linaloonekana katika swala hili ni mabadiliko ya taratibu ya hukumu kwa mtazamo wa madhehebu ya Abu Hanifa kwa kutafautiana kwa zama, kama inavyodhihiri katika maneno ya Hafidh Al Ainiy katika kitabu cha: [Al Umdatul qariy 6/156] aliposema: "Wenzetu wamesema: Kwa sababu ya kutoka kwake inahofiwa fitina, nayo ndio sababu iliyopelekea kuharamishwa, na chochote chenye kusababisha uharamu basi nacho huwa ni haramu, kwa maana hiyo, waliposema (inachukiza) walimaanisha: Inaharamishwa, na hasa katika zama zetu hizi, kwa sababu ya kuenea kwa ufisadi wa watu wake." Mwisho.
Na waliotangulia wakatosheka kwa kusema “Inachukiza” na ufisadi ulipokuwa unazidi kuenea wale waliokuja baada yao wakatoa hukumu ya “Kuharamisha” kabisa.
Na maswala haya yanashikamana na desturi na mila za watu kwa mujibu wa wana madhehebu ya Abu Hanifa, kama alivyoeleza mwanachuoni Ibn Abidina katika anuani yake isemayo " Kuenea kwa desturi / ada hufanya (kuwepo) hukumu za kidesturi / ada." iliyochapishwa pamoja na kitabu cha [Maj Muatu Rasaailihi 2/126] kwani wameyaeleza maneno hayo na kuyajengea hoja za hitilafu –kwa uwazi zaidi na kwa upana mkubwa na kwa kutoa hoja zaidi – ya kuwa hukumu hubadilika kwa kubadilika desturi.
Na kwa kuitazama kwao Hadithi na kulinganisha na zama za Mtume –rehma na amani zimshukie – au kutafautiana kwao kati ya kuwa sala (kutoka na kwenda msikitini kusali) zao huwa zinachukiza kwa baadhi ya wanawake na hazichukizi kwa wengine, au kutafautiana kwao, je, kizee husali pamoja na watu aendapo kusali sala ya Eid au ataenda msikitini bila ya kusali. Au katika kutafautiana na wasomi wa madhehebu waliochelewa (wa kisasa) na kuchukua hukumu ya kuzuia katika hali zote, na maelezo yake ni kama yalivyotangulia.
Imamu As Sarakhsaniy anasema katika kitabu cha: [Al Mabsuut 2/74]: "Na Abu Hanifa –radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie- amesema, kuhusu sala za usiku: Kizee atatoka hali ya kuwa amejihifadhi na hali ya kuwa kiza cha usiku kinamsitiri kati yake na kuangaliwa na wanaume, tafauti na sala za mchana na sala ya Ijumaa ambazo husaliwa mijini, kwani kutokana na msongamano huenda akaumwa na kichwa au kugongwa (kupigwa vikumbo), hali hiyo huwa ni fitina, na kizee ambaye atakuwa hatamaniwi na kijana basi atakuwa anatamaniwa na kizee mwenzake (kama yeye), na pengine huenda kijana akawa amemtamani na amezidiwa na hamu (ya kimapenzi) na akamgonga kwa makusudi. Ama sala ya Eid ataisali kando –mbali- na wanaume ili wasije wakamgonga." Mwisho.
Na mwanachuoni Al Marghinaniy anasema katika kitabu cha: "Al Hidayatu Sharhu Al Bidayati 1/57, chapa, Al Maktabatul Islmamiyyah]: "Na inachukizwa kwa wanawake kuhudhuria sala za jamaa." akikusudia wasichana, kwa kuogopea fitina, (na hakuna tatizo kwa kizee kutoka na kwenda kusali sala Alfajiri, Magharibi na Isha) na mtazamo huu ni kwa Abi Hanifa – Mwenyezi Mungu amrehemu- (na wakasema: Hutoka na kwenda kusali sala zote) kwani hakuna haja ya kuogopa fitina kwa kuwa hakuna atakayemtamani haitochukiza kama iwavyo katika Eid. Pia amesema: Akiwa na matamanio basi huenda pakawa na fitina, na ufuska hudhihiri sana nyakati za adhuhuri, alasiri na Ijumaa (nyakati za mchana, kuwepo kwa jua) lakini Alfajiri na Isha –wanaume –wengi- huwa wamelala, na nyakati za magharibi huwa wanajiandaa na chakula cha usiku, na maeneo ya kando yako mengi inawezekana kujiweka mbali na wanaume, hapo haitakuwa karaha (haitachukiza).
Na desturi hii ilipobadilika kutoka zama za Abi Hanifa ikawabidi wanazuoni waliokuja baadae nao wabadilishe maelezo juu ya maswala haya. Kwani ikawa –kwa wakati wao– kutoka mwanamke na kwenda msikitini ni fitina na uovu ukawa unaenea kila siku, kwa ajili hiyo waliokuja baadae wakatoa fatwa ya kuzuia hali zote, wakimaanisha kuwazuia wanawake kwenda kusali sala zote kwa nyakati zote, kama alivyoelezea Al Huswafkiy katika kitabu cha: "Al Daar Al Mukhtaar 1/566, chapa Dar Al Fikr]. Sipokuwa Al Kamal ametafautiana nao kwa kauli hiyo na kwa maelezo ya imam na wenzake wawili.
Mwanachuoni Al Kamal Bin Al Hamam –Mwenyezi Mungu amrehemu– anasema katika kitabu cha: [Sharhu Fathul Qadiry 1/366]: "Ufuska umeenea sana katika zama zetu hizi na hasa nyakati za usiku, kwa hivyo, inahitajika kwa Abi Hanifa kuzuia pia vizee, tafauti na wakati wa asubuhi mara nyingi huwa wamelala. Lakini waliokuja baadae wakaifanya hukumu hii ni kwa wote wasichana na vizee na katika sala zote na kwa nyakati zote kwa sababu ya kuenea kwa ufisadi kwa nyakati zote." Mwisho.
Na mwanachuoni Ibn Abidin anasema katika kitabu cha: [Radu Al Muhtaar Alaa Ad Dari Al Mukhtaar 2/307, chapa, Dar A`lam Al Kutub]: Amesema katika kitabu cha: [Al Bahr]: Na huenda ikasemwa kuwa fatwa hizi ambazo zimetolewa na waliokuja baadae zimekwenda kinyume na madhehebu ya imamu na wenzake. Kwani wao wamewafikiana kuwa msichana hukatazwa kabisa, ama kizee anaweza kuhudhuria sala ya jamaa kwa mtazamo ya imamu (Abu Hanifa) isipokuwa sala ya adhuhuri, alasiri na Ijumaa, bila ya kuzuiliwa.
Na kutoa fatwa ya kuwazuia vizee kwa hali zote na kwa nyakati zote hili linakwenda kinyume na mitazamo ya wanazuoni hao, lakini kauli inayozingatiwa ni ya imamu (Abu Hanifa). Mwisho.
Amesema katika kitabu cha: [An Nahr]: Na ndani yake kuna mtazamo uliotoka kwa imamu, nao ni kule kuwa na matamanio yaliyozidi mipaka, na kwa kuzingatia kuwa ufuska huwa hauenei wakati wa magharibi kwani wakati huo huwa wanajishughulisha na chakula, na wakati wa asubuhi na isha huwa wamelala, na iwapo ufuska huwa unaenea katika nyakati hizi –kama katika zama zetu hizi- basi makatazo yangelikubalika." Mwisho.
Na kupitia maelezo haya kuhusu maswala haya tunaelewa kuwa yamejengeka kwa kupitia desturi na faida (masilahi) zinazojitokeza ni: Kumhifadhi mwanamke kwa upande mmoja na kuondosha -kuzuia- ufisadi na fitina kwa upande wa pili, na jambo hili si kwa kutoka kwake na kwenda msikitini tu ila katika hali zote, kwa ajili hiyo haina maana kuhusisha utokaji kwa jili ya sala pekee. na kwa maana hiyo shekhe Burhan Ad din ameelezea katika kitabu cha: [Al Muhit 2/209], kuwa inachukiza kwa wanawake kwenda msikitini kusali sala ya jamaa kwa kuwa wameamrishwa kubakia majumbani mwao na wamekatazwa kutoka, na wameruhusiwa kutoka iwapo watakuwa katika kikundi, kisha wakazuiliwa baada ya hapo kwa kuwa kutoka kwao ni fitina.
Na wala haifichikani kwa mwenye akili ya kuwa desturi hizi zilizoelezewa kwa kina zaidi na kujengewa hukumu kuwa zimebadilika katika miji ya waislamu ukiachilia mbali miji ya wasiokuwa waislamu ambako suala hili limeulizwa, mwanamke wa sasa huwa hakai tena nyumbani lakini kutokana na mabadiliko ya zama imemlazimu kutoka na kwenda kutafuta elimu, kufanya kazi, na kutimiza majukumu ya uongozi na kutekeleza masilahi ya jamii, na kutokana na mazingira imembidi awepo katika nyanya za kisiasa, kitamaduni na kijamii, na wala hakuna kizuizi cha kumzuia iwapo kuna mikutano na kongamano.
Na haiwezekani kwa mumewe kumzuia asitoke iwapo wanaishi katika nchi zisizo za kiisilamu, lakini anaweza kwenda popote atakapo, basi inakuwaje – pamoja na haya yote- afungiwe milango ya msikiti na iwe ndio sehemu pekee ambayo mwanamke hawezi kuingia ndani!!
Kinachohofiwa kutoka na kwenda msikitini kwa mwanamke ni ile hali ya kuja kufikwa na matatizo au kuogopewa fitina zake au yeye kufitinishwa, na kwa ajili hiyo ikabidi kuhifadhiwa mwanamke ili asifikwe na hali kama hii. Na kubadilika kwa hali katika nchi za magharibi, na kubakia kumzuia kwenda msikitini na akawa na uwezo wa kwenda sehemu nyingine –katika kutafuta maisha na harakati nyenginezo– ni kama aina fulani ya mkanganyiko wa kutojielewa na ufinyu wa ufahamu na mgando wa mawazo jambo ambalo linakwenda kinyume na misingi ya madhehebu, na hasa ukizingatia wanazuoni wa madhehebu ya Abu Hanifa yametumika sana na waislamu kwa kuyatumia katika hukumu katika historia ndefu na kwa nchi nyingi kutokana na wepesi na upana na kuyazungumzia matukio na mambo mapya yanayojiri.
Lakini pia inaonekana kuwa mwanamke wa kiisilamu ndani ya nchi hizo na nyinginezo ana haja zaidi ya kwenda misikitini (kuliko wakati wote uliopita) kwa lengo la kujua hukumu za mambo ya dini yake na namna ya kufanya ibada zake na muamala wake. Na haja hizo ni zaidi kuliko awapo katika nchi za kiislamu, kiasi ambacho huenda ikafikia hukumu ya kuwa ni wajibu, kwa kuwa ndio njia pekee ya kuijua dini yake, na kwa kuwa misikiti katika nchi zisizo za kiisilamu si maeneo tu ya kusalia pekee bali ni vituo –pia- vya kukusanyika waislamu na kufundishia mambo ya dini yao na kujuliana hali zao na kusaidiana katika mema baina yao. Basi iweje isemwe kuwa: madhehebu ya Imamu Abu Hanifa yanamzuia mwanamke kuingia na wasitengewe sehemu maalumu kwa ajili yao?
Na kama ilivyokuwa kwa mwanamke wa kiislamu afanyaye kazi katika nchi za magharibi kuweza kusali imekuwa kama ni rehani –kwa mara nyingi– kusali msikitini, na pengine asipate sehemu –eneo- ya kutekeleza ibada ya sala yake, hivyo itamlazimu kuacha sala mpaka itakapotoka katika wakati wake. Na iwapo tunaelewa kuwa kukusanya sala ni jambo lisilokubalika katika madhehebu ya Hanafi, basi kutomtengea sehemu maalumu msikitini au kutomruhusu kuingia (msikitini) sala zake zitampita na kutoka katika wakati wake, na wala haifichikani kuwa sala yake katika mazingira kama haya ndani ya msikiti ni wajibu (ni lazima) hata kama kuna rai isemayo kuwa kutoka kwenda msikitini kwa mwanamke kunachukiza, kwani yakutanikapo makosa mawili ni wajibu kufanya kosa dogo ili iliepuke kosa kubwa, na kama wajibu hautimii isipokuwa kwa kuwepo jambo fulani, basi jambo hilo huwa ni wajibu.
Na lizungumzwalo hapa ni kule kupotea kwa sala yake na kuisali msikitini, basi iweje azuiliwe na jambo la lazima kisheria!? Lakini pia inaogopewa kwa atakayemzuia asisali akawa katika makemeo yaliyokuja katika aya hii {umemwona Yule anaye mkataza * mja anaposali?} [AL A'LAQ: 9-10].
Tukiongezea ya kuwa misikiti iliyopo katika nchi za magharibi ni kama mtazamo wa uislamu, na wala si sehemu ya madhehebu maalumu, lakini kutokana na mipango yake huwa ni kama kipimo na ishara ya kuwa mafunzo yake ni ya hali ya juu na wafuasi wake wana nidhamu na kujua namna ya kutaamali / kutendeana na wengine –kwani hilo litawafanya wapendezewe na uislamu na kuutamani– sasa kuendana na rai ambayo ipo kinyume na matukio tuliyonayo na huenda wasio waislamu waishio katika nchi hizo wakafahamu kimakosa ya kuwa uislamu unamdunisha mwanamke na wala haumpi umuhimu wowote ule hata katika Nyanja za ibada, hapo dini ya kiisilamu itatuhumiwa kuwa iko dhidi ya mwanamke hata katika mambo ya kisheria.
Hii ukiongezea hofu yao waliyonayo iliyosababishwa na waislamu wajinga au mambo yanayonasibishwa na uislamu kutoka kwa maadui zake na kuupaka matope kwa upande mwengine. Mambo kama hayo yatokezeayo katika wakati wetu huu hufanya ulinganio kuwa ni mgumu na ni namna mojawapo ya kujiweka mbali na njia ya Mwenyezi Mungu, kwani takuwa ni kuupaka matope uislamu na kuanzisha fitina kwa wasio waislamu ili wawakejeli waislamu. Na hapo haitajulikana kama maneno hayo ni ya madhehebu ya imamu Hanafi au imamu mwingine yule.
Bali itakuwa ni uzushi wa kusema neno ambalo Mwenyezi Mungu hakuliteremshia dalili yeyote katika zama zozote zile, bali hupata mwenye kuendeleza msimamo huwa hupata dhambi na mwisho wake hautakuwa mzuri (mwema).
Maulamaa wote kwa pamoja, pamoja na kutafautiana madhehebu yao wamekubaliana kuwa, hukumu ziendazo sambamba na desturi na ada zinaweza kuwepo au kutokuwepo, zitakuwepo kwa kuwepo kwa desturi na kutoweka kwa kutoweka kwa desturi.
Imamu Al Qurafiy anasema katika kitabu chake: [Al Furuuq 1/322-323, chapa Dar Al Kutub Al Elmiyyah]: "Hukumu zilizoambatana na desturi huwepo huwepo kwa kuwepo kwa desturi na hubatilika kwa kutokuwepo kwa desturi… na huu ni uhakiki uliowafikiwa na mkusanyiko wa maulamaa bila ya hitilafu.
Lakini tafauti inaweza kutokezea katika uhakika wake, nao ni, je, suala kama hili liliwahi kutokezea au hapana? Na kwa kanuni hii, fatwa zinazingatia kwa muda wote, desturi ikibadilika basi itazingatiwa na ikiondoka basi nayo -hukumu– itaondoka, na wala usikaushe wino kwenye daftari lako ndani ya maisha.
Na akujiapo mtu kutoka nchi za nje –si nchi yako– na kukuuliza maswala basi usimjibu pasi na kujua desturi za nchi yake, na mjibu kwa mujibu wa nchi yake na si kwa mujibu wa desturi za nchi yako, hii ndio haki na uwazi. Ama kung`ang`ania yaliyomo kwenye vitabu huu ni upotevu wa dini na ni ujinga wa kutofahamu makusudio ya wasomi wa kiislamu waliotangulia na wa kisasa." Mwisho.
Na amesema katika maeneo mengine [1/74]: "Hii ni kauli iliyothibiti ambayo ni lazima izingatiwe, na kwa kuijua kwa umakini Utafahamu kuwa maulamaa wenye kujibu maswali -kutoa fatwa- kwa yale yaliyoandikwa kwenye vitabu vya walimu wao kwenye miji yao na katika miji mingine iwapo wamefanya hivyo pamoja na kuwepo kwa desturi wakati wa kujibu maswali hayo basi watakuwa wamefanya makosa kwa kuwa wameenda kinyume na rai za wanazuoni wengi, na watakuwa wameasi kwa Mwenyezi Mungu na wala hawana udhuru kutokana na ujinga wao, kwa kule kujibu maswali wasiyoyajua na wala kutojua kinachoendelea na sharti zake na mabadiliko ya mazingira yake." Mwisho.
Na hata wana madhehebu ya Abu Hanifa wenyewe wameeleza jambo hili na kulitilia mkazo, mpaka katika mhakiki wa mwishoni wa madhehebu haya mwanachuoni Ibn Abdeen ameeleza katika kitabu chake: [Al Risalah]: "kuenea kwa desturi / ada hufanya (kuwepo) hukumu za kidesturi / ada. " iliyochapishwa pamoja na [Maj Muu Rasaail Ibn Abdeen], na akaeleza ndani yake aliyoyapokea kutoka kwa maulamaa wahakiki wa madhehebu ya Abu Hanifa, lau kuwa mtu atahifadhi vitabu vyote vya madhehebu ya Abu Hanifa, na maudhui zake, dalili zake na mapokezi yake basi haya yote haimtoshelezi kutoa jibu – fatwa – mpaka aelewe desturi za watu wa wakati ule na ada zao, na asipofanya hivyo basi hasara zake zitakuwa ni kubwa kuliko manufaa yake."
Na akafanya uhakiki katika kitabu cha cha: [Ar Risalah 2/116] "Desturi kwa mtazamo wa imamu Hanafi ina maelezo yake maalumu na huachwa kufanyiwa kazi mlinganisho (Qiyas)."
Na imepokewa kutoka kwa maimamu wa madhehebu ya Hanafiy [2/129] ya kwamba Mufti hana budi kuelewa wakati (zama) na hali za watu wake. Akasema: "Na hakuna budi awe amesoma na kupata ruhusa kutoka kwa mwalimu mtambuzi, na haitoshelezi kuhifadhi maudhui na dalili, kwani kwa mwenye kujitahidi hana budi kujua desturi za watu kama tulivyoelezea hapo kabla, na vile vile mufti, na kwa ajili hiyo amesema katika kitabu cha: [Maniyyatul Mufti]:
"Lau kama mtu atahifadhi vitabu vyote vya wasomi wa madhehebu yetu basi hana budi –pia- kusomea namna ya kujibu maswala ili aweze kujibu kwa usahihi. Kwani maudhui nyingi sana hujibika kwa mujibu wa desturi za watu pasi na kuhalifu sheria, mwisho. Na maneno yaliyokaribiana na haya yamenukuliwa katika kitabu cha: [Al Ash Baah] kutoka kwa Al Bazaziyyah, ya kuwa, mufti hujibu kwa yale yaliyomjia katika maswala… na kusema katika kitabu cha: [Fathu Al Qadiyr": Na uhakiki ni kuwa, mufti kiukweli hasa hana budi kufanya juhudi na kujua hali za watu." Mwisho.
Pia akasema [2/131]: "Hayo yote na mifano yake ni dalili tosha na ya wazi ya kuwa mufti hatakiwi kuwa mtu aliyetosheka na dalili zilizomo vitabuni bila ya kuchunga – kujua – nyakati na watu wake, na asipofanya hivyo atapoteza haki nyingi na hasara zake ni kubwa kuliko manufaa yake." Mwisho.
Na akasema pia [2/115]: Upambanuzi: Amesema katika kitabu cha: [Al Quniyah]: Si kwa mufti wala kwa kadhi kutoa hukumu tu bila ya kujua desturi. Na maudhui hii ikatajwa katika kitabu cha: "Khazanatul Riwayaat] kama alivyotaja Al Bayriy katika kitabu cha: [Sharhul Ash Baah". Mwisho.
Na kama alivyosisitiza kuwa utendaji utategemea na desturi nao ndio kiini cha hoja ya madhehebu, na akaelezea matawi mengi ya elimu ya kisheria ambayo yanapingana na mashehe wa madhehebu ya Abu Hanifa ambayo yameyatumia kutokana na zama zao, na kushikamana nayo katika mitaala na kauli zao, na sio kwa ajili ya maswala yao ambayo hubadilika kwa kubadilika kwa matukio hali ambayo hupelekea pia kubadilika kwa hukumu zinazoambatana na desturi, na kwa waliotangulia lau kama wangelikuwepo katika zama hizi za waliochelewa kuwepo basi wangelisema kama wasemavyo waliochelewa.
Pia anasema –Mwenyezi Mungu amrehemu– kuhusu maswala hayo [2/ 125/126]: "Elewa kuwa maudhui ya kisheria ima itakuwa imethibiti kwa kuwepo aya iliyo wazi kabisa, nayo ni upambanuzi wa mwanzo. Au itakuwa ni sehemu yenye kuhitaji jitihada na rai, na maudhui nyingi za hali kama hii huzingatia desturi na wakati kiasi ambacho ingelikuwa katika wakati ambao desturi ya jambo lile hutendeka basi wangelisema kinyume na vile wasemavyo katika nyakati nyengine (kwa kutafautiana nyakati na zama). Kwa ajili hiyo wakasema kuhusu sharti za kujitahidi: Kuwa hapana budi kujua desturi za watu, kwani hukumu nyingi hutafautiana kwa kutafautiana kwa zama kwa kubadilika desturi za watu au kwa kuwepo jambo la dharura au kuharibika kwa watu wa zama hizo, kiasi ambacho kama hukumu itabaki kama ilivyo zamani basi kutakuwa na mashaka na madhara kwa watu.
Na pia kwenda kinyume na kauli ya sheria iliyothibiti yenye kuwepesisha na ya kuondoa madhara na ufisadi, na kwa ajili ya kubakia ulimwengu katika hali ya nidhamu na mipango mizuri. Kwa ajili hiyo utawaona mashehe wa madhehebu wamekwenda kinyume na yale waliyoyaelewa waliojitahidi katika maudhui nyingi kwa kuzingatia zama zake, na kwa kuzingatia kuwa huyo wa mwanzo angelikuwepo katika zama hizi basi angelisema yanayokwenda sammbamba na zama hizi kwa mtazamo wa muundo wa sheria za madhehebu.
Kwa mfano: Wameruhusu kufaa kumuajiri mtu atakayefundisha kur`ani na mfano wake, kwa sababu ya kuacha kulipwa kwa walimu kama ilivyokuwa katika zama za mwanzo (nyakati zilizotangulia), na laukama walimu watafundisha bila ya kuchukua malipo wanafunzi na watoto wao watapotea. Na kama walimu watajishughulisha na ukulima na ujenzi basi kur`ani na elimu za dini zitapotea. Hiyo wakatoa fatwa ya kufaa kuchukua malipo ya kufundishia na vile vile kwa kazi ya uimamu na ya uadhini na mfano wake.
Pamoja na kuwa hayo yite ni kinyume na walivyowafikiana Abu Hanifa na Abu Yussuf na Muhammad kuwa haifai kumuajiri na kuchukua malipo kama ilivyo katika matendo mengine ya kumtii Mwenyezi Mungu kama kufunga, kusali, kuhiji na kusoma kur`ani na … na … kuna mifano mingi, kama; kuwazuia wanawake kama vile walivyokuwa wakati wa Mtume (Rehma na amani zimshukie) kwenda msikitini kwa ajili ya sala ya jamaa." Mwisho.
Pia akasema [2/128]: "Usemapo: Desturi hubadilika na hutafautiana kwa kutafautiana kwa nyakati, na kama kutakuwa na desturi mpya je, kwa mufti kwa mujibu wa zama zetu atatoa fatwa kwa mujibu wa utambuzi wake na kwenda kinyume na yaliyomo katika vitabu vya madhehebu, na namna hiyohiyo kwa hakimu?
Nitasema: pataangaliwa ujumbe uliopo –swali lililopo- na hali iliyopo, elewa kuwa, waliokuja baadae ambao wamekwenda kinyume na yaliyomo katika vitabu vya madhehebu katika maudhui iliyotangulia hawakutafautiana isipokuwa kwa kubadilika kwa wakati na desturi, uhakika ni kuwa hata mwenye madhehebu mwenyewe angelikuwepo basi angelisema kama walivyosema –waliokuja baadae. " Mwisho.
Na akasema katika maelezo: "Na tumekusikilizisha yanayotosha kuwa desturi na nyakati zikitafautiana basi na hukumu huwa tafauti, na juu ya mufti kwa sasa ajibu maswala kwa kujua desturi na watu wa zama zile hata kama atatafautiana na zama za waliotangulia, na vilevile kwa hakimu afanye kama hivyo tulivyosema kwani jambo hili si la kificho." Mwisho.
Kisha isemwapo kuwa inachukiza kwa wanawake kutoka na kwenda msikitini –sawa iwe machukizo yaliyo karibu na uharamu au machukizo ya kujiepusha– hii haimaanishi kuwa wasitengewe maeneo na sehemu maalumu kwa ajili yao ndani ya msikiti, kwa sababu zifuatazo:-
Kinachozingatiwa kwa baadhi ya wahakiki wa madhehebu ya Abu Hanifa kuwa haichukizi kwa vizee kwenda msikitini kwa nyakati zote au kwa baadhi ya nyakati, na hata kwa waliokuja baadae ukiachilia mbali Al kamal bin Al hammam- vizee sana. Na hili itapelekea kuwepo kwa sehemu zao za kusalia.
Na kauli isemayo inachukiza kwa wanawake kwenda kusali sala ya jamaa msikitini na kumzuia kufanya hivyo, hapa inakusudiwa kuwa haruhusiwi kutoka ndani ya nyumba yake kabisa, na katika jambo lijulikanalo katika sheria (fiqhi) ni kuwa, iwapo mwanamke yupo nje ya nyumba yake basi haitofaa kumzuia kuingia msikitini kwa namna yeyote ile na hili ni kwa madhehebu yote, kinyume chake itaogopewa kwa mzuiaji asije kuingia katika wale wenye kufanya dhuluma ambao wametajwa katika maneno yake Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema {Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko Yule anayezuia misikiti ya Mwenyezi Mungu kutajwa ndani yake jina lake} [AL BAQARAH: 114.]
Na kutenga sehemu maalumu ndani ya msikiti kwa ajili ya wanawake ni jambo linalokubalika kwa wasomi wa madhehebu ya Abu Hanifa ingawa wanasema inachukiza kutoka na kwenda kuhudhuria sala ya jamaa. Kwa kuwa wameeleza kwa uwazi kabisa –kama ilivyotangulia– kuwa inafaa kukaa itikafu ndani ya msikiti pamoja na kuwa wanasema, itikafu ndani ya nyumba zao ni bora. Na kupitia maelezo haya, inafaa kutengewa sehemu maalumu kwa ajili ya kukaa itikafu kwa mujibu wa madhehebu ya Abu Hanifa kama ilivyokuwa inaruhusika kuingia msikitini.
Kama ambavyo wamesema kuhusu sehemu ya kusimama wanawake katika sala ya jamaa msikitini. Na kutaja sehemu za kuwafanya wao kuwa ndio wenye kufuata (maamuma) basi itapelekea kutengewa eneo lao, na kama si hivyo basi kuna faida gani ya kuwaita wafuataji (maamuma)? Amesema katika kitabu cha: [Al Fatawa Al Hindiyyah 1/89, chapa, Al Maktbaatul Amiriyyah, Bulaq]: "Lau kama watakusanyika wanaume, watoto wadogo wa kiume, makhuntha, wanawake, na wasichana: wanaume watasimama baada ya imamu, kisha watoto wadogo wa kiume, kisha makhuntha, kisha wanawake, kisha wasichana, hivi pia imetajwa katika kitabu cha: "Sharhu Al Twahawiy" Mwisho.
Kuna tafauti baina ya maneno yaliyohaririwa katika madhehebu na baina ya maneno yaliyowekwa kufanyiwa kazi na kutolewa fatwa ambazo zinazingatia mabadiliko ya desturi, hali, zama na eneo.
Na kwa dalili za kivitendo ambazo huhukumu mafungamano ya kutendeana kati ya waislamu kwa kutafautiana mitazamo yao ya kimadhehebu ya kisheria (kifiqhi), kwa mfano wasemapo; haichukizi kwa walichotafautiana lakini huchukiza kwa walichokubaliana, na inafaa kwa muislamu kuchagua maneno ya madhehebu tafauti na kwa lile lililo karibu ili aende sambamba na makusudio ya sheria.
Na kujilazimisha kufuata madhehebu maalumu haimaanishi kuwa ni lazima ufuate kila kitu kilichosemwa katika madhehebu hayo hata kama jambo hilo lina hitilafu za masilaha au likawa na matatizo kwa mtu.
Mchukizo -ulio karibu na uharamu au unaohitajika kujiepusha– unawahusu wanawake na sio wengine, na jambo hili halilazimishi kuwazuia wasiingie msikitini pindi wakitoka majumbani mwao. Kwa namna hii ndio amejibu mwanachuoni Al Twahawiy katika kitabu cha: "Hashiyatuhu A`la Muraqiy Al Fallah Uk. 183, chapa, Bulaq]. Na kauli ya kusema kwamba, imamu ananuia kuwasalimia wanaume na malaika pekee pale atowapo salamu (asemapo) “Assalamu alaykum warahmatullah.” Hii haimaanishi kuwa inachukiza kuhudhuria wanawake kwa sababu imamu hakutia nia ya kuwatolea salamu, kwani itakuwa kuna upande haukufungamana –ama kwa upande wa imamu anachotakiwa ni kutia nia ya kuwaongoza pindi akiwa anawasalisha.
Madhehebu mengine mengi wamesema kuwa yafaa kwa mwanamke kutoka na kwenda msikitini, na msikiti ni nyumba ya Mwenyezi Mungu ambayo hukusanyika waja wake waislamu kusali basi na kuangalia madhehebu yao.
Ikimaanisha kuwa uislamu unatangulizwa kuliko madhehebu ya kifiqhi na tafauti zake zilizopo, haifai kwa wanaosimamia mambo ya waislamu wawe watu wasiobadilika katika maswala kama haya yenye upana mkubwa, na wala wasitie uzito katika jambo ambalo waislamu wametafautiana, lakini kinachohitajika ni kuwaweka pamoja ndugu zao waislamu wote na wa madhehebu yote. Na watafute mambo yenye kuwakusanya pamoja ambayo yatawaunga nyoyo zao na wala hayatawafarakisha, na ni lazima wafuate heshima na adabu za kutafautiana kama walivyokuwa maimamu –waliotangulia- Mwenyezi Mungu awarehemu.
Kwa mfano imamu Abu Hanifa na wenzake na imamu Shafi na wengineo walikuwa wakisali nyuma ya maimamu wa madhehebu ya imamu Malik pamoja na kuwa walikuwa hawasomi (hawatamki) “Bismillahi” si kwa siri wala kwa dhahiri.
Na mfano imamu Abu Yusuf alikuwa akisali nyuma ya Arashid aliyekuwa amepiga chuku na imamu Malik alitoa fatwa ya kuwa hana udhu, na wala hakuirudia sala pamoja na kuwa anaona kuwa kutokwa na damu kunatengua udhu.
Vilevile Imamu Ahmad bin Hanbali anaona hivyo hivyo, akaambiwa: Iwapo imamu wangu ametokwa na damu na wala hakutawadha je niswali nyuma yake? Akajibu: Iweje usisali nyuma ya Sayd Bin Al Musayab na Malik!!
Na mfano mwingine Imamu Shafi anaswali sala ya asubuhi bila ya kuomba dua ya Qunuti nchini Baghdad, karibu na kaburi la Abi Hanifa, akaulizwa kuhusu jambo hilo akasema: “Napingana naye na mimi nipo mbele yake!!
Vilevile amefanya Abu Abbas Ad Daghuliy Ashafii alipoacha dua ya Qunuti katika sala ya asubuhi nje ya nchi yake, na alipoulizwa juu ya jambo hilo akajibu: “Ili niupumzishe mwili, na kufuata desturi za watu wa mji, na kuchunga hali za wazee na watoto.” Na kama ilivyopokewa kutoka kwa Al Hafidh Adhahabiy katika kitabu cha: [Sayri Alami Anubalaa 14/559].
Na kwa mujibu wa swali lililoulizwa: Maelezo yaliyotajwa katika vitabu vya madhehebu ya Abu Hanifa kuhusu kumzuia mwanamke kutotoka na kwenda msikitini hii ilikuwa katika zama ambazo haja na desturi zilipelekea kuzuiliwa, na hii haimaanishi kwa namna yeyote ile kumzuia kuingia msikitini pindi iwapo ameshatoka nyumbani kwake, na kuzuiliwa msikitini, na inapasa kujengewa eneo maalumu ambalo watajisitiri mbali na wanaume.
Kwani kuchanganyika na wanaume ni uzushi ambao haukujulikana na waislamu pamoja na kutafautiana kwa zama na kwa miji yao, na pia jambo hili halina mfungamano na madhehebu ya imamu Hanifa –Mwenyezi Mungu amrehemu- kwa karibu au mbali. Na inapasa kumzuia kila anayetaka kufanya jambo hili (kuwakusanya pamoja wanawake na wanaume) kwa kuwa linakwenda kinyume na uislamu na kupotosha uislamu.
Na wasomi wa madhehebu ya Abu Hanifa wameieleza maudhui hii ya kutoka nyumbani kwa mwanamke na kwenda kusali sala ya jamaa msikitini kwa kuzingatia desturi / ada, na kuweka hukumu ndani yake kwa kutazama mabadiliko ya desturi kwa mtazamo wa undani, tafauti na zama za Mtume –rehma na amani zimshukie- na mtazamo ukazidi kuelezwa kuanzia kuzingatia nyakati za sala na kumalizikia kuzuia kwa waliokuja baadae kuwa asitoke kwa hali yeyote ile na kwa nyakati zozote kinyume na msimamo wa imamu na wenzake.
Na kwa kuendana sambamba na yote hayo pamoja na kubadilika kwa desturi na ada ambazo madhehebu ya Abu Hanifa yanazingatiwa, zama hizi itabidi hukumu irudi kama ilivyokuwa katika zama za Mtume – rehma na amani zimshukie – ya kuhalalisha kutoka kwa mwanamke kwenda msikitini bila kizuizi, na hasa katika nchi zisizo za kiisilamu, ili imani yao iwe mpya (kila siku) na kuweza kukutana na ndugu zao na kujifunza mambo ya dini yao.
Na hayo yote iwapo hakuna fitina yeyote kwao au kuogopewa isije ikawakuta, na kama hawapotezi haki za familia na haki za waume zao na watoto wao, kwani ukweli ni kuwa wanawake wengi wameshatoka majumbani mwao wanashirikiana na wanaume katika Nyanja nyingi tafauti za maisha, na ilivyokuwa washatoka basi hakuna faida ya kuwazuia kwenda katika nyumba za Mwenyezi Mungu Mtukufu wakitaka kufanya hivyo. Pamoja na kutanabahisha kuwa sala ya mwanamke ndani ya nyumba yake ni bora kuliko anayoisali msikitini isipokuwa kama ana malengo mengine –sio sala pekee – ambayo hayatatimia isipokuwa msikitini kama; kujifunza hukumu za mambo ya dini yake hatoyapata isipokuwa huko –msikitini- hivyo kwenda kwake msikitini itakuwa ni bora na si kwa sala pekee.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote
 

Share this:

Related Fatwas